Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nichukue nafasi hii kuweza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha na mimi kuwa Mbunge ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mhe
shimiwa Mwenyekiti, vilevile niungane na Watanzania wote kuonyesha masikitiko makubwa sana kwa hiki ambacho kimetokea leo ndani ya Bunge letu. Nakumbuka huko nyuma nilishasema na kuwaambia Watanzania kwamba hawa wenzetu hawana ajenda yoyote ya kutaka kumkomboa Mtanzania wa leo, ajenda yao kubwa ni vurugu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Waheshimiwa Wabunge ambao tuko ndani ya Bunge hili tutakumbuka siku ya tarehe 20 Novemba, 2015 wakati Mheshimiwa Rais amekuja kufungua Bunge hili, wenzetu hawa walikuwa mstari wa mbele kupinga na hatimaye kutoka nje ya Bunge hili. Kwa kweli mimi jana tulipoanza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais nilishangaa kuona wao wanakuwa mstari wa mbele kuchangia na kukosoa hotuba hii adhimu ya Mheshimiwa Rais. Nashangaa ujasiri huo waliutoa wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hizi vurugu ambazo zimetokea humu ndani, ni imani yangu Watanzania wameona ukweli wa yale tunayoyazungumza kila siku kwamba hawa wenzetu hawana ajenda yoyote zaidi ya kutaka kuvuruga. Sisi kama Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, tunatambua kwamba Mheshimiwa wetu Rais ana kazi kubwa sana, ana ajenda nzuri ya kutaka kuwakomboa Watanzania lakini vilevile kuhakikisha kwamba Tanzania inaenda kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajikita kwenye mchango wangu napenda nitoe elimu ya uraia kidogo hata kama hawapo narusha jiwe gizani najua huko waliko litawakuta. Tunakumbuka kabisa kwamba baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na Chama cha Mapinduzi kuibuka kidedea kutokana na kuwa na Ilani ambayo kwanza inatekelezeka lakini wenzetu wale waliwaambia Watanzania kwamba Ilani yao inapatikana kwenye tovuti wakati Watanzania wa leo hawajui tovuti ni kitu gani na wengi wanaishi vijijini. Kutokana na kuwa na Ilani ambayo haieleweki Watanzania waliweza kukichagua Chama cha Mapinduzi hatimaye Rais wetu mpenzi, Dkt. John Pombe Magufuli kuweza kuibuka kidedea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo kumekuwa na upotoshaji mkubwa sana juu ya utendaji kazi wa Rais wetu Magufuli. Wenzetu hawa kama kawaida yao ya kukurupuka kama ambavyo leo wamekurupuka katika Bunge hili, wameendelea kupotosha umma na kusema kwamba Mheshimiwa Pombe Magufuli anatekeleza Ilani ya UKAWA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nisikitike sana kwa sababu sisi sote ni mashahidi wakati wakizindua kampeni zao pale Jangwani walitaja vipaumbele vyao ambavyo vilitajwa na mgombea wao wa Urais ambapo cha kwanza kilikuwa ni kumtoa Babu Seya ndani, kipaumbele kingine wakatuambia wao wakipata ridhaa ya kuweza kuongoza Taifa hili watajenga reli kiwango cha lami. Mimi niseme kwamba, kabla mgombea wao hajatangaza kwamba ana mpango wa kwenda kugombea Urais mwaka 2020, ni vema angejua kwamba reli hazijengwi kiwango cha lami. Vilevile wakasema kwamba wao wana mpango wa kuwatoa wafungwa wa Uamsho. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ndivyo vilikuwa vipaumbele vyao ambavyo waliwaambia Watanzania na ndio maana leo hata wanapokuja katika Bunge hili wanafanya fujo sishangai kwa sababu nawajua, ndiyo tabia zao na hawana ajenda yoyote na Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Rais alijikita zaidi katika kubana matumizi, kuhakikisha kwamba Watanzania wanakuwa na maisha ya kiwango cha kati lakini vilevile kufungua Mahakama ya Mafisadi vitu ambavyo kwao wala hatukuvipata kuvisikia. Niwatoe hofu Watanzania kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Rais wetu John Pombe Magufuli, imejipanga vya kutosha kuhakikisha kwamba Tanzania inaenda kufikia uchumi wa kiwango cha kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijikite katika kuchangia hotuba hii adhimu ya Mheshimiwa Magufuli. Mimi natoka katika Mkoa wa Songwe na kama tunavyojua ni mkoa mpya ambao una changamoto nyingi za kiuchumi. Vilevile mimi kama mwakilishi wa wanawake wa Mkoa wa Songwe hapa Bungeni, nina ombi moja na napenda nijikite katika kuchangia kwenye masuala ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Songwe kabla hawajaugawa ulipokuwa katika Mkoa wa Mbeya tulikuwa na hospitali kubwa kabisa ya rufaa lakini vilevile kulikuwa na hospitali kubwa kabisa ya mkoa. Baada ya sisi kuwa Mkoa wa Songwe tumebaki kama yatima, Mkoa wetu hauna huduma za afya, hatuna hospitali ya rufaa wala ya mkoa. Akina mama wa mkoa ule wanapata shida sana linapokuja suala la uzazi. Nikitolea mfano kwenye Wilaya yangu ya Mbozi inakabiliwa na changamoto kubwa sana kwa sababu wodi ya akina mama ni ndogo haikidhi mahitaji na hospitali ile imekuwa ikihudumia akina mama wanaotoka katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wetu wa Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitolea mfano wa Wilaya yetu ya Momba, pale Tunduma kuna hospitali moja tu. Hospitali ile ni ndogo, haikidhi mahitaji, haina madaktari wa kutosha, haina vifaa vya kujifungulia hata inapokuja suala la operation hawana theatre inabidi wasafirishwe kutoka Tunduma, Wilaya ya Momba kuja Wilaya ya Mbozi na ukizingatia pia hospitali liyopo Mbozi haina jengo la kuwatosha akina mama wale. Kama ambavyo Mheshimiwa Rais ameeleza katika hotuba yake kwamba atahakikisha Watanzania wanakuwa na afya, atahakikisha akina mama wanapata sehemu bora za kujifungulia, napenda nichukue nafasi hii kuweza kumuomba Rais wetu John Pombe Magufuli aufikirie mkoa wangu mpya wa Songwe tuweze kupatiwa hospitali za kutosha. Katika hotuba yake ukurasa wa 22 amesema atahakikisha kila mkoa unakuwa na hospitali, kila kata inakuwa na zahanati, tunaomba sana Mheshimiwa Rais aweze kuufikiria mkoa wangu wa Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia pia katika hotuba yake ukurasa wa 24, Mheshimiwa Rais alitueleza kabisa kwamba ana mpango madhubuti wa kuhakikisha Watanzania tunatoka kuishi gizani na tunakuwa na umeme wa uhakika.
Niseme jambo moja kwamba Mkoa wangu wa Songwe tatizo la umeme limekuwa kubwa sana, umeme ukishakatika saa tano unakuja kuwaka kesho yake saa kumi na mbili alfajiri. Unaweza kuona mazingira hayo yalivyo magumu, akina mama wanaofanya kazi kwa kutegemea umeme hawawezi kufanya kazi zao. Vilevile hata vijana wanaokaa Mkoa wa Songwe ambao wanategemea umeme kufanya shughuli mbalimbali ili kuweza kujiingizia kipato hawapati nafasi ya kufanya shughuli hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru sana Serikali ya Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu ni hivi karibuni Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo alikuja kwenye Mkoa wangu wa Songwe. Naamini kabisa aliona changamoto ambazo zipo katika mkoa ule na ni ishara tosha kwamba sasa wananchi wa Songwe wataenda kupata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)