Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa madhumuni ya kuchangia hoja, wakati nikifanya hivyo niweze pia kama Naibu Waziri kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakishiriki katika majadiliano ya hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema wake na kwa fadhili zake kutujalia afya njema ya kuwa hapa kwenye Bunge lako Tukufu kutekeleza wajibu wetu kwa Taifa. Aidha, nachukua fursa hii muhimu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano ya Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Nampongeza pia Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Mbunge, kwa kuteuliwa na kuthibitishwa na Bunge lako Tukufu kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa kuchaguliwa kuliongoza Bunge letu la Kumi na Moja katika Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu, nawapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa au kuteuliwa kubeba dhamana ya kuwakilisha wananchi na kutenda kazi katika Bunge hili kwa maslahi mapana ya Taifa letu. Nawapongeza pia Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kuchaguliwa na kuendelea kulisaidia Bunge kupitia Kamati zao, Bunge kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba na ya Kikanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee naomba kuipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii chini ya Mwenyekiti wake Mhandisi Atashasta Justice Nditie, Makamu wake Mheshimiwa Kemilembe Julius Lwota na Waheshimiwa Wajumbe wote kwa namna ambavyo wameendelea kuishauri Wizara yetu ili kuifanya sekta ya maliasili na utalii ifikie malengo yake ya kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi, kuwaongezea wananchi kipato, kuongeza fursa za ajira na kuboresha huduma za kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumshukuru kwa namna ya pekee Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kuniteua kubeba dhamana hii kubwa ya kumsaidia Waziri wangu kuisimamia sekta hii ya maliasili na utalii nchini. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa nitamsaidia Waziri wangu kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika eneo la sekta ya maliasili na utalii ili kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali itakayokuwa inatolewa mara kwa mara kuyafikia malengo yake. (Makofi)
Mwisho lakini siyo kwa umuhimu nawashukuru wapiga kura na wananchi kwa ujumla wa Jimbo la Tunduru Kaskazini kwa kunichagua kuwa Mbunge wao na kwamba nipo njiani, mara tu baada ya kukamilisha jukumu hili la Kitaifa tutaungana pamoja katika kuendeleza utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa Jimbo na kwa Wilaya nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze katika ufafanuzi wa hoja. Napenda nianze kwanza kabisa kwa kusema kwamba michango yote iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge ilikuwa ni yenye afya na ni michango yenye malengo mazuri ukiacha kasoro za hapa na pale, lakini kwa ujumla wake ni michango ambayo kweli tunaipokea na mingi tutaifanyia kazi ili iweze kuongeza tija katika mafanikio ya Wizara. Jukumu letu kama Wizara au jukumu letu kama Serikali katika sekta hii ni kupokea na kuyafanyia kazi maoni hayo na ushauri wote tulioupokea kwa sababu huko ndiko kukubali kushauriwa na kusimamiwa kwa mujibu wa Katiba hiyo ndio kazi ya Bunge.
Maliasili na utalii ajenda yake kubwa ni uhifadhi. Napenda nirudie katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii ajenda kubwa ni uhifadhi. Tunapaswa kuhifadhi tulichonacho, tunapaswa kukilinda tulichonacho kinachotutofautisha sisi na nchi zingine au na maeneo mengine ambayo ni nje ya Tanzania na hilo ndilo linalotufanya sasa hata tuzungumzie utalii kwa sababu wanaokuja hapa wanakuja kuona vitu ambavyo kwao havipo na vinaweza vikaendelea kuwepo na kuboreshwa ili tuweze sasa kuweza kufikia malengo ya kukidhi haja ya watalii.
Sasa wakati tukiwa tunajipanga upya kwenye maeneo ambayo yana kasoro na mapungufu ya hapa na pale, kwa sababu haiwezekani kuwa hakuna maeneo ambayo yanahitaji kufanywa vizuri zaidi. Mimi nina msemo wangu siku zote huwa naurudia mara kwa mara, huwa nasema hakuna mwisho wa kufanya vizuri, kila wakati utakapodhani umefanya vizuri bado kuna namna bora zaidi ya kufanya vizuri zaidi. Sasa kwa sababu hiyo, tunataka tubaki pale pale kwenye lengo la kwamba kwa sababu sekta hii ina husisha makundi mbalimbali kama ambavyo yamekuwa yakijadiliwa tangu pale mwanzoni. Ustawi wa sekta hii unahitaji wafugaji, ustawi wa sekta hii unahitaji pia wakulima wa mazao, ustawi wa sekta hii unahitaji pia wavuvi na watu wengine wote ambao wataweza kuorodheshwa kulingana na shughuli zao mbalimbali wanazofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati tukiwa tunazingatia maslahi ya kila kundi, lakini maslahi ya Taifa ndiyo yatayotakiwa kupewa nafasi kubwa zaidi. Kwa hiyo, tunajipanga katika kuzingatia zaidi maslahi ya Taifa kwa sababu maslahi ya Taifa yanazidi au yanavuka ukomo wa umuhimu kwa mahitaji ya makundi moja moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unayafikiaje maslahi ya Taifa? Sisi kama nchi tunayo vision, tuna dira; dira yetu ni dira ya 2025. Ukisoma dira utakutana na masuala yote yanayohusiana na uhifadhi, utakutana na masuala yote yanayohusiana na tabianchi kwenye dira ile, tuna kawaida ya kusoma kwa kwenda kwenye search engines na kusoma mambo ya mataifa mengine lakini natoa wito tusome pia na nyaraka ambazo ni za kwetu tulizoziandaa wenyewe na nyingine tumeziandaa humu Bungeni au kuziidhinisha, tusome vision lakini pia tuangalie namna ambavyo tunaweza tukasoma mipango tuliyojiwekea kwa mfano, tuna mipango ya miaka mitano mitano, tuna mipango ya kila mwaka, lakini pia tunayo Katiba yetu, tunazo sheria, tunazo kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa tumeshakubaliana juu ya yote hayo na hasa tunapokubaliana juu ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo, basi wajibu wetu baada ya pale hatuna uchaguzi isipokuwa ni kufuata na kutii. Pale ambapo tunaona kwamba kuna sababu yoyote ile ya msingi ya kuweza kubadilisha au kufanya marekebisho kulingana na wakati au kwa sababu nyingine yoyote tutakayoona inafaa, basi tunapaswa kufuata utaratibu ule ule na kuweza kufanya marekebisho ya sheria au hata kufuta kabisa sheria kwa sababu taratibu zipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kubwa ambayo imebeba mjadala au imefanya mjadala wa Bunge jana na leo uweze kuwa mzito zaidi, watu wamechangia kwa hisia mbalimbali, watu wamechangia wengine baadhi yao kwa jazba tunawasemehe, lakini nataka nisisitize tu kwamba suala la migogoro ya ardhi, migogoro ya mipaka limebeba uzito mkubwa. Napenda niseme kwamba Wizara kwa kuzingatia pia andiko ambalo limeandikwa na Wizara ya Ardhi na ambapo nimekwenda kuchukua takwimu kama ifuatavyo tunaweza kutoa jibu moja tu hapa ambalo ni la mwelekeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba kwanza tuna jumla ya migogoro 281 kwa kadri ambavyo takwimu zimekusanywa na Wizara ya Ardhi, lakini miongoni mwa migogoro hiyo; migogoro ambayo inahusu hifadhi ni migogoro 35 tu ambayo hii ni asilimia 12.5. Mikoa inayoongoza kwa migogoro ambayo inahusiana na hifadhi na Mikoa yote inayoongoza kwa migogoro yote kwa ujumla ni Kagera, Mara, Tanga na Tabora ambayo inabeba karibu asilimia 50 ya migogoro yote. Mkoa wa Tabora ambao wenyewe ni wa nne kwa idadi ya migogoro kwa ujumla yenyewe migogoro yake asilimia 40 ni migogoro ya hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nirudie hapa sasa baada ya takwimu hizi hoja ya Mheshimiwa Profesa Muhongo kwamba tatizo siyo eneo, tatizo siyo ukubwa wa ardhi na mimi tayari nilikwishaliona hilo kupitia takwimu hizi zilizokusanywa na Wizara ya Ardhi kwamba Mkoa wa Tabora ambao ni miongoni mwa mikoa minne yenye maeneo makubwa lakini ambao una asilimia 40 ya migogoro inayohusiana na hifadhi ndiyo unaoongoza kwa kuwa na eneo kubwa nchini. Tabora wana kilometa za mraba 760,151.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwanzoni tutakachofanya sasa hivi ni kuhakikisha kwamba migogoro yote hii sasa Wizara zote zinazohusika zinakwenda kukaa kwa sababu tayari tuna agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusiana na kushughulikia migogoro hii. Wizara zote sita ambazo naweza kuzitaja hapa haraka haraka ni Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili na Utalii, TAMISEMI, Wizara ya Maji, Wizara ya Nishati na Madini lakini pia Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) wote tunakwenda kukaa pamoja kwa ajili ya kwenda kushugulikia migogoro yote kwa ujumla. (Makofi)
Kuhusu migogoro ya ardhi nimekwishamaliza kwa namna hiyo. Lakini nizungumzie ujangili kidogo kwa sababu muda umeshakimbia sana. Masuala yote yaliyotajwa kuhusu ujangili kwanza tumeunda chombo kipya kinachoitwa TAWA (Tanzania Wildlife Authorty), Mamlaka ambayo inakwenda kuchukua maeneo ambayo yanahusiana na uhifadhi wa mbuga za wanyama zile ambazo zipo nje ya zile zilizopo chini ya TANAPA na Ngorongoro. TAWA inakwenda kuboresha zile mbuga ambazo zilikuwa hazina uongozi wa pamoja kama ilivyokuwa TANAPA na Ngorongoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla wake sasa sekta ndogo ya wanyamapori inakwenda kuwa bora zaidi, inakwenda kuboreshwa zaidi baada hasa kuhusiana na masuala ya uhifadhi mambo yanayohusiana na askari wa hifadhi, tunaanzisha chombo kinaitwa Jeshi Usu ambalo ni Paramilitary kwa namna ile sasa tunakwenda kukusanya kwa namna bora zaidi ya kuweza kuboresha mapato ili tuweze kushughulikia zaidi maadili ya askari hawa, mmetaja mambo mengi yanayohusiana na matendo ambayo yasiyofaa ya ukosefu wa maadili, kuyataja moja moja muda hautoshi kama mnavyoona, lakini kwa kuanzisha Jeshi Usu tunakwenda kuimarisha zaidi maadili, nidhamu lakini pia tunakwenda kushughulikia zaidi pia maslahi ya hawa askari, incentives zao, lakini pia tunakwenda kuwafanya waweze kuwa manageable zaidi kuliko ilivyo sasa. Kwa hiyo, kwa njia hii tunaweza kuondoa changamoto nyingi zaidi zinazohusiana na ujangili kwa maana ya eneo hili. Yapo mengine mengi lakini kwa sababu muda hautoshi labda pengine naweza kuishia hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utalii, kila mmoja amezungumza hapa juu ya mapungufu kwenye sekta ya utalii na kwamba kunahitajika uboreshaji. Wanazungumzia vivutio vipya, kwanza kuboresha vivutio vilivyopo pia kwa kubuni vivutio vipya, lakini pia kutangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba katika ziara zangu nilizofanya kwenye baadhi ya Wilaya nimetoa maelekezo na huu ndiyo msimamo wa Wizara kwamba vivutio vyote vinavyoweza kuorodheshwa kwenye vivutio vya utalii nchini, Wilaya zote tunakwenda kuziagiza ziweze kuorodhesha kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wanasema hapa, waende wakashirikiane na Halmashauri zinazohusika waorodheshe kwa sababu tunakwenda kuandaa directory ya vivutio vyote vinavyoweza kuwa na sifa ya utalii nchini na ambavyo sasa tutaweza kuvi-market kwa maana ya kuvifanyia utangazaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia miundombinu mbalimbali kwenye maeneo ya utalii. Ni kweli lipo suala la miundombinu ndani ya hifadhi zenyewe kwa maana jinsi ya kuweza kutembelea hifadhi, masuala ya hotels mle ndani lakini pia kuna suala la miundombinu ambayo inakufikisha kwenye hifadhi yenyewe kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Sasa huku upande ambako tunazungumzia miundombinu ambayo inakufikisha kwenye hifadhi, kama barabara, Wizara hii haifanyi kazi peke yake, tunakwenda kushirikiana na Wizara inayohusika, inayoshughulika na mambo ya ujenzi pamoja na mawasilIano na mambo yanayohusiana na hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la Southern Circuit, (Utalii wa Kusini). Tuna mradi mkubwa sana unaitwa REGROW (Mradi wa Kuboresha Utalii Kusini) wa makusudi kabisa chini ya Benki ya Dunia wenye dola za Kimarekani zaidi ya milioni 210. Tunakwenda kufanya vitu vingi sana. Kwanza kuboresha vivutio vyenyewe, lakini pia kwenda kuzitambua mbuga, hifadhi na vivutio vingine vyote vilivyo katika ukanda wa kusini ili kuwe na maana ya circuit kweli kweli, kwa sababu mtalii akifika sehemu moja aweze kupata value for money, kwa sababu anaweza kutembelea zaidi ya kivutio kimoja kwa wakati mmoja kwa sababu ya ukaribu na vitu kama hivyo. Ndani kuna viwanja vya ndege vya ndani ya hifadhi na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema muda hautoshi, nakwenda mbio lakini nataka kusema kwamba wote ambao wameguswa na suala la kuimarisha utalii ukanda wa kusini, nataka kuwaambia kwamba Serikali tayari ina mpango mahsusi kwa ajili ya hilo.
Pia hata kuhusiana na vivutio, tumekuwa na vivutio vya aina iliyozoeleka, wanyama; na Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema hapa. Ukweli ni kwamba tunakwenda sasa kuimarisha utalii wa kihistoria, utalii wa kiutamaduni, utalii wa starehe labda (leissure tourism), zote hizi ni aina tofauti za utalii ambazo tunakwenda kuziboresha kwa kutekeleza miradi mbalimbali, lakini kwa mipango mbalimbali ambayo kulingana na wakati na kulingana na jinsi fedha zitakavyopatikana tunaweza kwenda kuufanya utalii ukawa bora zaidi kuliko hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.