Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda niwashukuru sana ndugu zangu mnaotutia moyo. Napenda niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wa Chama changu na Wabunge wa Upinzani. Tangu jana hapa hoja zilizotolewa, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, unaweza kuziita very constructive. Zilikuwa hoja nzuri sana za kujenga. Zilikuwepo chache ambazo zina miiba, miiba, ndiyo ubinadamu, lakini hoja ambazo zimetolewa hapa kwa kiasi kikubwa zimetujenga, nasi tunatoka hapa tukiwa tumejiamini zaidi katika kazi ambayo tunaifanya ya kuhakikisha kwamba nchi yetu inafaidika zaidi na maliasili ambazo tunazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge 90 wameleta michango yao kwa maandishi. Na mimi nawaheshimu na ninawashukuru sana. Nimesoma michango ile, kama ingesemwa hapa, pangekuwa na hewa nzuri zaidi, maana ilikuwa ni michango mizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, waliochangia kwa kuongea hapa Bungeni ni Waheshimiwa Wabunge 55; kwa kweli hii ni faraja kubwa sana na muda kama mlivyoelezwa, siyo rafiki sana. Nitajaribu kutoa majibu kwa upana na ninamshukuru sana Mheshimiwa Makamba, Mheshimiwa Profesa Muhongo, Mheshimiwa AG na wengine wote ambao mmetusaidia katika kujibu maswali kwa utangulizi mzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi, maliasili zetu na sisi wanadamu na wanyama na viumbe vingine vilivyo chini ya group kubwa la wanyama, tunaishi na mimea yetu kwa mtindo unaoweza kuuita symbiotic, yaani tunaishi kwa kusaidiana. Bila rasilimali zetu hizi za maliasili, tusingeweza kuishi na bila sisi, hizi rasilimali zisingekuwepo. Ninaposema sisi, nina maana ya sisi binadamu na viumbe wote ambao wapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maliasili zetu za misitu na nyuki, wanyamapori na utalii zinatuwekea mfumo wa ikolojia ambao ndiyo unakuwa muhimili mkubwa wa maisha yetu. Hewa tunayotoa sisi kama hewa chafu ili tuweze kuishi inavutwa na majani na kutumika kuzalisha chakula cha majani. Mimea yetu, miti na mimea mingine ndiyo chanzo kikubwa cha kurekebisha mvua yetu, kurekebisha joto katika dunia.
Katika Tanzania, Mwenyezi Mungu ametujalia, tumekuwa na aina tofauti sana, nyingi za mimea na viumbe wengine ambazo zinapatikana Tanzania peke yake na hazipatikani mahali pengine popote duniani na ndiyo maana tuna msingi mkubwa wa utalii kupita nchi zote duniani ukiacha Brazil. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ambayo ndiyo uhai wetu yanatoka kwenye misitu yetu na hifadhi zetu nyingine. Maji haya ndiyo tunayotumia nyumbani, ndiyo tunatumia kwa kilimo cha umwagiliaji, tunazalishia umeme kwa miaka mingi katika nchi yetu na ndiyo inaendesha viwanda vyetu. Maliasili hizi tumeelezwa hapa mara nyingi, ni msingi mkubwa wa pato letu la Taifa na zinatuletea asilimia 25 ya fedha zote za kigeni tunazopata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia hapa na Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu vizuri, kwamba tuna mradi wa zaidi ya dola milioni 200 wa kujenga misingi ya utalii Kusini mwa Tanzania. Tutaviboresha viwanja vya ndege, tutaboresha barabara kutoka kwenye viwanja hivyo mpaka kwenye hifadhi zetu na kwa sababu hiyo, wale ambao wamepisha Ruaha ili iwe mbuga yetu kubwa, waliopisha Kitulo, waliopisha Katavi wakae mkao wa kula, maana tunatengeneza mradi ambao utaboresha utalii katika maeneo haya ambayo yana sifa nzuri sawa sawa au hata kuzidi hizi mbuga nyingine ambazo tunazitumia kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya matatizo makubwa ambayo tunayo katika kuboresha utalii Kusini mwa Tanzania, ni bei ya tiketi za ndege. Kutoka Arusha mpaka Kigoma dola 1,800 kwenda na kurudi kwa dola 1,800 unaweza kutoka Dar es Salaam ukaenda New York na kurudi. Kutoka Dar es Salaam kwenda Mpanda; kutoka Dar es Salaam kwenda Iringa ni ajabu bei za ndege zilivyo kubwa.
Kwa hiyo, hatua ya kwanza ambayo tunachukua, tunaanzisha vituo vya kuzipa ndege mafuta katika viwanja hivyo vya ndege ili kuhakikisha kwamba hakuna kisingizio kwamba lazima tutue Tabora kwanza, tutue Dodoma kwanza ndipo twende, kwa hiyo, ni lazima bei ipande. Pia tumeishauri Serikali inunue ndege ndogo kama hizi Fokker Friendships ambazo zinaweza ku-service viwanja vyetu hivi ambavyo ndiko watalii wetu watakapokuwa wanakwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi zetu ndiyo kiini cha utalii wetu na zinalindwa kwa sheria kama ambavyo tumesema na kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge mmetueleza, mmerudia; Sheria ya Wanyamapori hasa sehemu ile ya 18(2), Sheria ya Misitu na Sheria ya Mazingira. Sheria hizi zinatutaka tulinde, tuhifadhi na tuendeleze maliasili zetu. Hizi siyo sheria za kwanza ambazo zinatulazimisha tuangalie shughuli zetu; wote tunajua watu ambao wamejenga kwenye hifadhi za barabara katika maeneo mengi nchini kwetu wameondewa na hata bila fidia kwa sababu wameingilia hifadhi ya barabara na watu ambao wamejenga kwenye mabonde. Kwa hiyo, siyo mara ya kwanza kuhakikisha kwamba tunasimamia Sheria za Uhifadhi kama ambavyo zimetungwa na Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niliambia Bunge lako Tukufu kwamba japo nchi nyingine za jirani zina sheria na zinavyozitekeleza zinakuwa za imla sana; kwa mfano, nchini Kenya ukiingia kwenye Hifadhi ya Taifa na huna sababu ya kuwa hapo, wanapiga risasi bila kukuuliza swali na nchini Botswana, hivyo hivyo. Nchini Tanzania hatuwezi kufanya hivyo, hata kama tunaingia kwenye matatizo ambayo wakati mwingine tunakuwa nayo.
Kwa hiyo, nimesikiliza kwa makini na nimesikia kwamba wafanyakazi wa wanyamapori, wafanyakazi wa misitu na walinzi wa hifadhi zetu wakati mwingine wanakuwa na roho mbaya sana. Wanapiga raia, hatukuwatuma kuwapiga raia; wanapiga mifugo risasi, hatukuwatuma kupiga mifugo risasi. Pia hatukuwatuma kuchoma nyumba za watu; hatukuwatuma kuwaumiza watu. Kwa hiyo, Wizara yangu itachukua hatua kali pale ambapo tutathibitisha kabisa kwamba askari alipiga watu, tutamchulia hatua kali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo, baada ya kikao hiki cha Bunge, tutawaita wahifadhi wote tuangaliane kwenye macho, tuelezane tabia nzuri ya kufuata huko kwenye hifadhi zetu na wale ambao hawatafikia kiwango cha weledi tunachokitaka, tutakapobadilisha hili Jeshi la Uhifadhi hatutawaingiza kwenye Paramilitary Force ambayo tunaijenga. Tutapeleka wale tu ambao wana weledi na uaminifu wa kutosha wa kuhakikisha kwamba Watanzania wamewaajiri ili walinde maliasili zetu, lakini hawakuwaajiri ili wawapige, wawaumize, wapige risasi ng‟ombe zao au wapasue nyumba zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mjadala ambao umeendelea hapa, nimeelewa kwamba katika maeneo mengi bado wakulima wanavuna mazao yao. Kwa sababu hiyo, ninawaomba wenzangu huko, Wakuu wa Mikoa kwamba wasiwabughudhi watu wakati wanapovuna mazao yao; na hivyo wawaache hao ng‟ombe kwanza mpaka watu wamalize kuvuna ndipo watekeleze agizo la Waziri Mkuu ambalo amelitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala ambalo lisememwa hapa la huyu mtu anayeitwa Green Miles Safari ambaye alifutiwa leseni, akafutiwa na vitalu vyake vyote; kwa nini Serikali imemrudishia leseni na kitalu chake?
Mheshimiwa Spika, ni vizuri Bunge lako Tukufu likajua kwamba katika eneo la Natron kabla ya mwaka 2011 kulikuwa na vitalu viwili; Natron North na Natron South; na kwamba baada ya kuweka tathmini katika vitalu hivi, vitalu vile vilionekana ni vikubwa sana na kwa hiyo, vikagawanywa tukatoa vitalu vinne. Majina yake siyo muhimu, lakini moja ya hicho kitalu kilipewa Green Miles na kingine akapewa Wengert Windrose Safaris. Green Miles Safari ni Mwarabu na Wengert Windrose ni Mmbarekani. Kwa hiyo, siasa za Kimarekani na Kiarabu zimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yule Mmarekani aliyekuwa na hicho kitalu chote kikubwa alisema eneo alilopewa Green Miles ndilo eneo zuri zaidi na yeye amewekeza zaidi hapo, kwa hiyo, hataki kuondoka. Anataka abaki na hicho kitalu chake hata kama hakupewa na Serikali. Idara ya Wanyamapori imejaribu kusuluhisha jambo hilo ikashindwa. Wengert Windrose akaenda Mahakamani kupinga jambo hilo kisheria. Kabla kesi hiyo haijamalizika, ikatolewa DVD hapa ambayo inaonesha watu waliokuwa wanawinda katika kitalu kimoja cha Green Miles huko Selous, siyo Lake Natron; huko Selous walifanya makosa na kuwinda kinyume na kanuni za uwindaji zilivyowekwa. Wale wote ambao mtapenda kuiona hiyo DVD tutakuwa tayari ku-share tuwaoneshe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ile DVD kuoneshwa hapa, Mheshimiwa Waziri aliongea na vyombo vya habari, akasimamisha leseni, akasimamisha na vitalu vyote vya Green Miles Safaris. Tarehe 30 Machi, 2015 Mahakama ikaamua, ikasema kitalu alichopewa Green Miles ni haki yake. Mahakama Kuu ya Tanzania sehemu ya biashara, ni haki yake, kwa hiyo, aruhusiwe kuendelea na kazi yake.
Kwa hiyo, ukiangalia ile Sheria ya Wanyamapori Kifungu cha 38(12)(c) ndiyo inayompa Waziri mamlaka ya kugawa vitalu, lakini pia mamlaka ya kumnyang‟anya mtu kitalu. Hata hivyo ukiangalia ile mamlaka ya kunyang‟anya kitalu inasema; “Waziri hatamnyang‟anya mtu kitalu kama mtu huyo hakuonekana ana hatia na Mahakama ya Tanzania.” Sasa huyu mtu hakuonekana ana hatia na Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulichofanya ni kutekeleza sheria na kutekeleza maamuzi ya Mahakama yetu. Kwa hiyo, hakuna jambo ambalo limefanyika hapa ambalo halikufanyika kwa utaratibu unaotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huyu bwana, alirudishiwa kitalu chake na amerudishiwa leseni ya kuwinda. Hata hivyo, wale wafanyakazi wa Serikali walioshiriki na wafanyakazi wa Green Mile Safaris na kuonekana kwenye ile DVD, tunaandaa utaratibu na charges tumeshapeleka kwa DPP ili waweze kufunguliwa mashitaka kwa kosa la kuwinda kinyume cha Kanuni. Sasa huwezi kwenda kumnyonga baba kama mtoto wake ndio ameua mtu. Kama mtoto wake amaeua mtu na ni mtu mzima, yule mtoto ana-face makosa yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia niongee kidogo kuhusu TANAPA. Nawashukuru sana wengi ambao mmewapongeza TANAPA kwa kazi nzuri ambayo wanafanya. Napenda pia niseme, sentensi moja moja kwanza kwamba, Serikali haichukui mapato ya TANAPA na kuyaweka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, kilichobadilishwa ni TANAPA na mashirika mengine yote ya umma, zile akaunti zake zote za makusanyo, zinafunguliwa Central Bank. Kwa hiyo, wakishapokea pesa kwenye Commercial Bank, ile Commercial Bank ina-transfer mapato yale kwenye Central Bank. Wakifanya matumizi, wanachukuwa fedha kule kwenye Central Bank na kutumia kama kawaida. Cha muhimu ni kutaka kujua kwa uhakika mashirika haya yote tulionayo, mapato yake ni kiasi gani, yanatumikaje na kwa wakati gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya madawati ya thamani ya shilingi bilioni moja, ambayo ni madawati 16,500, ambayo tulimkabidhi Mheshimiwa Makamu wa Rais wiki iliyopita, yametoka kwenye bajeti ya TANAPA ya Corporate Social Responsibility, siyo kwamba tumechukuwa fedha za mipango ya kazi ya TANAPA na kutengenezea madawati, hata kidogo!
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda at this juncture nieleze kidogo kuhusu haya madawati yote ambayo yatatolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii. Shirika la TANAPA limechangia madawati 16,500, katika Wilaya 55 na kila Wilaya itapata madawati 300 ambayo yatakaliwa na wanafunzi 300 mara tatu; na hizi ni zile Wilaya zinazozunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, imechangia madawati 2,000 katika Tarafa ya Ngorogoro yenye thamani ya shilingi milioni 140 na itatoa madawati mengine 10,000 kuchangia Mfuko wa Madawati wa Wizara; TFS itatoa madawati 20,000 na kutoa meta za ujazo za magogo 15,000 za misitu kama mgao maalum kwa kikosi cha Magereza na madawati mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zitaruhusiwa kuyanunua kutoka kwenye mashamba yetu mbalimbali bila kutoa mrahaba, lakini kulipa asilimia 25 ya mrahaba kwa ajili ya fedha zinazotakiwa katika kurudishia kupanda miti katika meneo hayo yatakayokatwa. Jumla ya madawati 168,500 yatatolewa na haya yana uwezo wa kukaliwa na wanafunzi 505,050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niende kwa haraka katika suala la concession fees. Ni kweli kwamba mwaka 2007 nilipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii tulitangaza concession fee ya kitanda dola 50. Baadaye watoa huduma wakakataa mchango huo, wakaenda Mahakamani mwaka 2007 na mwaka 2008 ndiyo Mahakama ikahamua. Kwa hiyo, kilichotokea hapo katikakati, Mahakama ilikuwa haijaamua. Sasa hivi tunangojea Bodi ya TANAPA ikamilike kuteuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya TANAPA ni tofauti kabisa katika kuunda Bodi na sheria nyingine. Wizara imefanya inayotakiwa kufanya na tunangojea hatua ya mwisho ya kukamilisha uteuzi huo na baada ya uteuzi huo, Bodi itapitia concession fee mpya na ikishapitia tutai-gazette na kuanza kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine lililosemwa hapa na nafuu niliseme linahusu lodge ya Mikumi. Tender ilishatangazwa, mjenzi ameshapatikana na tunangoja mjenzi huyo ajikusanye, aanze kujenga lodge hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wabeba mizigo, wapishi na waongoza misafara katika Mlima Kilimanjaro; Wizara ya Kazi, Wizara ya Maliasili tulikutana na Vyama hivi na wale wenyewe wanaohusika, wakatengenezeana mkataba wa malipo na tukaweka msimamo. Wale watoa huduma, lazima wawalipe wale wabeba mizigo, wapishi na waongoza misafara kabla hawajaanza kupanda mlimani na wasiwarushe pesa zao. Kwa hiyo, tunangoja tuone utekelezaji unavyokwenda na hivi sasa wana mikataba na bei ya kupanda ni dola 10 kila siku kwa mbeba mizigo; dola 15 kila siku kwa mpishi, nadhani na dola 30 kwa mwongoza msafara. Kwa hiyo, hilo liko vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mlima Kilimanjaro ni kweli kwamba kuna uchafu sana katika njia ya kupanda na njia zote zile. Suala la kutengeneza vyoo na maeneo mengine ya kupumzika liko mikononi. Tender ya Kimataifa ilitangazwa ili kupata vyoo ambavyo vinageuza kinyesi kiwe vumbi (powder) ili kupunguza uchafu kule juu ya mlima. Kwa sababu vyoo vyenyewe vinavyotakiwa ni vingi na bei ya kuvijenga vyote ni zaidi shilingi bilioni moja, ilitangazwa Kimataifa na tender ilikwishatolewa kwa Kampuni ya Korea ya Kusini, lakini Bodi ikija, Mwenyekiti ndio atasaini hiyo. Maana tender ya zaidi ya shilingi bilioni moja ni lazima isainiwe na Mwenyekiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kuliongelea hapa linahusu Watanzania wanaopewa ruhusa wenyewe au kampuni zao kufanya biashara ya wanyama hai. Wanyama hai wanaoruhusiwa kwa sasa, baada ya ile scandal ya kubeba twiga ndani ya ndege na kusafirisha nje ya nchi, wanyama wanaohurusiwa sasa ni primates hawa wadogo wadogo; nyani, tumbili na hawa wanyama wadogo, aina ya kenge, reptiles, ndege aina mbalimbali pamoja na wadudu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imeonekana kila siku tunapata taarifa ya Watanzania kusafirisha Wanyama nje ya nchi bila utaratibu; bila vibali, bila ruhusa, bila kitu chochote. Wanyama wanakamatwa Hong Kong, Thailand, Eastern Europe, wanakamtwa kila mahali! Hawa waliokamatwa na tumbili juzi, siwezi kusema jambo hilo kwa sababu liko mahakamani, lakini limefikishwa mahakamani kwa sababu kuna ushahidi kabisa kwamba walikuwa wanafanya michezo. Halafu wanyama hawa wanaosafirishwa nje, hata wale ambao wanakatazwa na conference of parties, wanapelekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuna jina chafu huko kwa sababu ya watu ambao wanapeleka wanyama hai bila utaratibu. Hakuna utaratibu mzuri uliowekwa kuhakikisha kwamba tunaweza kudhibiti biashara hata hii biashara hii ikaipatia Taifa pesa, wale tumbili walikuwa wanapelekwa for medical research.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anayekuja kupeleka wale wanyama wala hafanyi declaration ya aina yoyote kwamba wale wanyama wanakwenda kutumika kwa ajili gani? Kama wanaenda kutumika kwenye zoo, unaweza kuelewa; hawana faida kubwa sana ambayo unaweza kusimama imara ukasema hakuna ruhusa kupeleka; lakini wengine wanapelekwa kwa ajili ya utafiti wa dawa. Kwamba huyu nyani ni jamii ya mtu, tukitumia dawa ya namna hii kutibu hiki, inaweza kuponya au haiwezi kuponya? Tutumie kiasi gani? Tumtibu kwa muda gani ili huu ugonjwa upone? Dawa ikipatikana, ile kampuni inapata billions of dollars na sisi tunabaki na nyani aliyeuzwa kwa dola 15.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuanzia leo hivi nilivyosimama hapa, ninasimamisha kwa muda wa miaka mitatu usafirishaji wote wa wanyama hai kutoka Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba, wanyama wakubwa, swala, pundamilia, twiga, hawakubaliwi, lakini bado wanasafirishwa, bado wanaibiwa, kwa hiyo, tunasimamisha. Hata chawa wa Tanzania hatasafirishwa nje ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki cha miaka mitatu, Idara ya Wanyamapori itajipanga na kuweka utaratibu unaofaa ili Serikali ikiangalia na wenyewe unafaa, ndiyo biashara hiyo iweze kuruhusiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo la Sao hill. Muda hauko rafiki sana, lakini mradi wa misitu ya kupanda wa Sao Hill ulianzishwa kwa minajili ya kujenga kiwanda cha karatasi. Wakati umeanzishwa, ulianzishwa pia mradi wa kujenga kiwanda cha karatasi pale Ruvu, Kongowe. Kiwanda kilipangwa kijengwe Morogoro, unapoingilia Mto Ruvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi ule wa Ruvu ulikuwa umepangwa kwa pine ile ya Carribean ambayo haikuweza kukua katika mazingira yale. Pine iliyoanzishwa kule Sao Hill; pine ya Ellioti iliota na kukua vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya magogo kukua, kiwanda cha Sao Hill kikajengwa kama Kiwanda cha NDC, SU (Shirika la Umma). Tulipoendesha kikatushinda, tukakiuza kama ambavyo sasa kinamilikiwa na mtu binafsi. Sasa wakati tunacho kiwanda chetu, mi-pine ambayo tulikuwa tunatumia ya miaka 14, hiyo ndiyo inatumika kuzalisha paper, ndiyo kawaida, dunia nzima! Unaangalia ule mti, uone wakati ambao fiber ile ya kutengenezea paper ni ndefu kupita wakati wote; na kwetu hapa Tanzania, pale Sao Hill ni miaka 14.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, miti ile ya miaka 14, haifai kupasua mbao. Ndiyo maana wao walikuwa na mkataba na Serikali wa kuuziwa miti ile ambayo ni michanga na midogo ambayo huwezi kupasua mbao kwa shilingi 14,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, actually mwaka 2007, ukiangalia bajeti ambayo tulisoma hapa, yale magogo ya kutengenezea karatasi yalikuwa yanauzwa shilingi 1,700. Tuliyapandisha bei hapa mwaka 2007, ndiyo ilifika hapo; na magogo yale ya kupasua mbao yalikuwa shilingi 18,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mtu aliyenunua kiwanda hicho, naye alinunua kwa lengo lile lile, kutengeneza karatasi. Kile kiwanda ambacho kilijengwa pale na NDC, kilijengwa kutengeneza craft paper.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango iliyokuwepo ni kwamba kile ambacho kitajengwa pale Bagamoyo, ndiyo kitamalizia craft paper kuwa karatasi hii nyeupe ambayo tunatumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndiyo maana unaona yanayotokea pale. Kwanza wamepewa bei ile ya chini ya pulp na bei hiyo ni tofauti na wale ambao wanatengeneza mbao. Kwa sababu bei ya paper na mbao ni tofauti kabisa. Ukiwa na kiwanda cha karatasi kinachonunua magogo kwa bei ya timber, hakiwezi kuuza karatasi barabarani, ndiyo jambo muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilichotufikisha pale ambapo wanatumia magogo makubwa kama wale wanaopasua mbao, ni ule muda uliotumika kuanzia tuliposhindwa kukiendesha mpaka tulipopata mwekezaji. Ile miti yote ambayo ilikuwa kwa ajili ya kuzalisha paper, ikawa imekuwa magogo makubwa, lakini hakuna eneo kubwa zaidi ambalo lilipandwa.
Kwa hiyo, ile yote ikawa lazima igawanywe, nyingine itengenezwe paper kwa bei ya paper and pulp na nyingine itengeneze mbao na ndiyo sad story ya pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa cha muhimu wananchi wa Mufindi, Njombe, Mbeya na Morogoro mpande miti kwenye mashamba yenu. Pale Sao Hill penyewe kuna four thousand hectors ambazo wananchi wanaweza kupanda miti yao. Mpande miti ile, ikiwa midogo, mnaweza kuiuza kama pulp and paper, lakini mkiacha ikiwa mikubwa mnaweza kujikwamua kiuchumi kama Mheshimiwa Mbunge wangu wa Viti Maalum alivyosema kwa uchungu sana na mimi namuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu itaendelea kuwapa miche bure ili muweze kupanda miti katika eneo lote hilo na mjitegemee hapo badaye, mjikwamuwe kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niseme kwamba suala hili la migao ambalo limelalamikiwa hapa, na mimi nimelalamikiwa. Nimesema mgao mpaka kwanza tuupitie ule utaratibu wake na ndiyo tutatoa mgao. Mwaka huu hakuna mgao mwezi wa sita na labda hata mwezi wa saba hautatoka mpaka tumejua namna ya kuugawa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa bado nina karatasi nyingi hapa, lakini muda ndiyo umekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.