Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Godfrey William Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia mchana wa leo katika hotuba hii nzuri ambayo imewasilishwa na Waziri wa Maji. Kwanza kabisa, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri na Naibu wake kwa kazi ambazo wameendelea kuzifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uwazi kabisa nachukua nafasi hii kuwashukuru na kwamba Mheshimiwa Waziri amekuwa bega kwa bega na mimi katika kuhakikisha kwamba Jimbo la Kalenga linapata maji ya kutosha. Vile vile Naibu wake ambaye tayari ameshatembelea Jimbo langu, napenda sana kuchukua nafasi hii kumshuru kwa kuwa ameonesha nia njema kwamba anawajua na ana nia nzuri na wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza tu, napenda sana kuipongeza hotuba nzuri ambayo imewasilishwa, hotuba ambayo imeleta matumaini mazuri kwa wananchi wote wa Tanzania, bila kusahau wananchi wangu wa Jimbo la Kalenga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni Kalenga tuna miradi mingi, lakini baadhi ya miradi ambayo wananchi wamekuwa wakiipigia makelele kwa muda mrefu, ni miradi ya umwagiliaji. Kwa uhalisia wa hali ya juu, napenda kutoa shukrani zangu kwa Serikali kwamba nimeona sasa scheme za umwagiliaji wa Mlambalasi na Cherehani zimeingizwa kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ni kilio kikubwa sana ambacho kilikuwa kimewakumba wananchi wa Jimbo la Kalenga lakini leo hii nawashukuru sana kwa sababu Jimbo litaenda sasa kunufaika; na wananchi ambao wanategemea kilimo kwa zaidi ya asilimia 95, wataona kwamba Serikali yao imewaangalia, vilevile kuona ni namna gani wanaweza wakasonga mbele katika masuala mazima ya kilimo na upatikanaji wa maji bora na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea tu, nimeangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri na nimeona kwa undani kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba wanapata maji kwa ajili ya wananchi wa Tanzania. Nami nachukua nafasi kwa sababu naona jukumu kubwa la Serikali na naona namna gani ambavyo Serikali inahangaika kupata pesa kwa ajili ya miradi ya maji katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii kwa sababu katika Jimbo langu la Kalenga bado tunasuasua kwenye miradi mbalimbali, lakini jitihada hizi ambazo zimeonyeshwa na Serikali naamini kabisa tutaweza kupata majibu katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kugusia tu, nina miradi mitatu ambayo inanisumbua Jimboni Kalenga. Nina mradi wa kwanza ambao ni Mradi wa Maji wa Mfyome, nina mradi wa pili ambao ni Mradi wa Weru, lakini mradi wa tatu unakusanya Vijiji vitatu; Kijiji cha Magunga, Itengulinyi na Isupilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kalenga lina zaidi ya watu 200,000, lakini upatikanaji wa maji katika Jimbo letu bado umekuwa ni mgumu. Nina imani kubwa kwamba kupitia Serikali ya Chama cha Mapinduzi, maji tutakwenda kuyapata lakini vilevile tutaenda kuwapa imani kubwa wananchi ili kufikia mwaka 2020 tuweze kupata kura nyingi na kukirudisha Chama cha Mapinduzi madarakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo moja katika upatikanaji wa fedha za miradi. Katika miradi hii mitatu niliyoitaja, kuna mradi mmoja unahitaji zaidi ya shilingi 1,100,000,000/=. Najua ni fedha nyingi lakini tuangalie ni vijiji vingapi vinavyokwenda kunufaika na mradi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ambao nimeutaja wa Magunga, Isupilo na Itengulinyi ni mradi mkubwa kwa sababu unawagusa wananchi wengi. Tatizo ni kwamba Wakandarasi wanapelekwa site, pesa hazilipwi; na Wakandarasi wanachukua nafasi ya kuwapeleka au kuipeleka Serikali Mahakamani ili pesa za miradi ziweze kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali na Wizara kwa ujumla tutakapokuwa tunapanga mikakati kwa ajili ya miradi, tuangalie miradi ambayo ina tija, miradi ambayo inawagusa wananchi wengi, inayowagusa akinamama ambao kwa namna moja au nyingine wanatumia muda wao mwingi kwenda kutafuta maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo moja ambalo linaingia kwenye jamii ni kwamba, akinamama wanavyoenda kuchota maji umbali mrefu na wanavyoamka asubuhi sana muda wa saa 10.00 au saa 11.00, wanahatarisha hata ndoa zao. Watakavyoenda kwa masaa matatu, manne huku nyumbani mwanaume anakuwa anapiga makelele kwamba mke wangu yuko wapi? Tuwaangalie wanawake ambao wanahangaika kule vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naunga mkono kwa hali na mali hotuba hii, lakini vilevile naunga mkono Wabunge wenzangu ambao wamechangia wakiomba kwamba Serikali iangalie kwa umakini namna gani tunavyoweza kupata maji. Kwa ujumla tu, nilikuwa nikiangalia bajeti nyingi zilizopita, nimeangalia bajeti ya Wizara ya Ujenzi, bajeti ya Wizara ya Maji na Wizara ya Elimu. Elimu imeenda zaidi ya shilingi trilioni moja; Ujenzi imeenda zaidi ya shilingi trilioni nne na Maji inagusa kwenye shilingi bilioni 900. (Makofi)
Ndugu zangu, naomba tuangalie kwa umakini, tatizo la maji linapigiwa kelele nchi nzima. Bajeti hii kama kutakuwa kuna uwezekano, basi tuiunge mkono na fedha zote ambazo zinaombwa ziweze kufika kwa wananchi na Serikali iweze kuwafikishia wananchi maji, kwa sababu maji ni uhai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mapendekezo kadhaa; wenzangu wameongea kuhusu Rural Water Agency; naunga mkono suala hili kwamba katika ile tozo ya sh. 50/= hebu tuongeze tufike sh. 100/= ili tuweze kupata maji ya uhakika. Tukifanya hivi tutapata maji hata kama tatizo bado ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi bado haijakamilika, naamini kuna miradi mingi bado haijakamilika, lakini kama tutaridhia na tutaweka utaratibu kwamba tuweze kuchangia sh. 100/= tofauti na kiwango cha sasa hivi cha sh. 50/=, basi tutakuwa tumejaribu kupata pesa za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimekuwa nikiangalia kwamba kuna tatizo lingine kwenye upambanuzi wa namna gani tunaweza tukainua mapato ya ndani ya nchi. Nilikuwa naangalia utaratibu wa watumiaji simu. Leo hii orodha ya watumiaji simu inaelekea kwenye milioni 39. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mahesabu madogo tu. Hivi kwa mfano, tukisema kila mtumiaji wa simu akachangia sh. 100/= kwa mwezi kwa watumiaji milioni 39 tulionao leo na hizo pesa zikaingia kwenye Mfuko wa Maji; tutapata zaidi ya shilingi bilioni 46 kwa mwaka. Kwa hiyo, hiyo itakuwa sehemu mojawapo ya kutatua tatizo hili na hizi pesa zote zikaenda kwenye miradi ya maji ambayo bado inasuasua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya namna hii, tukawatumia watalaam wa Wizara ya Fedha, tukawatumia wachumi ambao wapo, tukaona namna gani tutaweza kuweka mechanism ambayo tutaweza ku-charge at least sh. 100/= kwa kila mtumiaji wa simu pesa ikaenda kwenye maji, tutaweza kutatua tatizo kubwa la maji katika maeneo mengi ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naelewa nia nzuri ya Serikali ni kuhakikisha kwamba, tatizo la maji ambalo mpaka leo hii ni kubwa, tunakwenda kulitatua. Leo hii zaidi ya nusu ya wananchi Watanzania bado hawana maji safi na salama ya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni suala zuri na jema sana kuangalia na kumuunga mkono Mheshimiwa Waziri kwa kazi ambazo anaendelea kuzifanya. Tumuunge mkono bajeti yake ipite, wananchi waweze kupata maji lakini vilevile tuunge mkono jitihada zote zinazofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini tukiungana kwa pamoja tutapata maji, lakini vilevile miradi mbalimbali ambayo bado haijakamilika, itakwenda kukamilika bila kuwategemea wahisani wa nje, kwa sababu tunaenda na masharti ambayo wakati mwingine yanatuumiza sisi wenyewe kama Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, napenda sana kumshukuru Mheshimiwa Waziri, kukushukuru wewe na Serikali.