Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kusimama hapa kuchangia Wizara hii ya Maji. Pia naomba niunge mkono hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Mheshimiwa Bobali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wenzangu walivyotangulia kusema maji ni uhai, bila maji hatuwezi kuishi. Nianze na mradi wa Ziwa Victoria wa Shinyanga - Kahama, sisi Ziwa Victoria limetuzunguka lakini sikuona kama huo mradi unaweza kujumuisha hata Mkoa wetu wa Kagera au kugusagusa Bukoba Mjini ambayo ndiyo iko karibu kabisa na Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba Waziri atueleze kama mradi huo unagusa katika Wilaya hiyo ya Bukoba Mjini. Mkoa wetu wa Kagera una matatizo ya maji, wanawake wanapata shida ya maji na sisi tumezungukwa na vyanzo vingi vya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Mheshimiwa Rais alikuja kuzindua barabara ya Kyaka Bugeni, alitoa ahadi akawaeleza wananchi kwa sababu walimlilia wakapiga magoti, wakamwambia Mheshimiwa Rais tuna shida sana ya maji. Akawaahidi kwamba kuna mradi wa Omlukajunju, akawaeleza Omlukajunju huo mradi uishe haraka sana na Mheshimiwa Maghembe alikuwepo, lakini mpaka sasa hivi huo mradi haujaguswa wala haujasemwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende Bukoba Vijijini, ni matatizo makubwa sana, vijiji ambavyo unaweza ukaenda na hata ukawaonea huruma, wanawake wanaondoka saa kumi usiku wanarudi saa tano hawajapata maji, na maji wanayoyapata ni shida. Wakikuta tayari ng‟ombe ameshapita basi hawapati maji. Kuna Vijiji vya Kikomelo, Lubale, Kibirizi, Nyakibimbiri, Chaitoke, Izimbya, Luhunga na vijiji vingine vilivyopakana pale, vina shida ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanamke akienda kufuata maji anasahau kama nyumbani ameacha mtoto au anasahau kama kuna kula. Hawa watu ninaowasema ni wa kijiji ambacho kimezungukwa na vyanzo vingi vya mito. Kuna Ziwa ambalo linaitwa Ikimba, ni ziwa kubwa ambalo wanaweza waka-supply maji hata katika Vijiji vya Lubale kwenda mpaka Nyakibimbiri lakini tunashindwa kuelewa Serikali inashindwa nini kutenga fedha ambazo zitafanya vyanzo vidogo, kuliko kupanga miradi mikubwa ikashindwa kutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi inakuwa mikubwa naona li-book lilivyo kubwa, li-book ni kubwa lakini sasa utekelezaji unakuwa mdogo, afadhali kupunguza sehemu nyingine, maji, maji maji ni shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Misenye tumezungukwa na Mto Kagera, Mto Kagera unaweza uka-supply maji katika Mkoa mzima wa Kagera. Ukienda huko sehemu za Misenyi unakuta wanatumia maji ya kwenye mabwawa, wakichelewa watoto wakaenda kuchota watu wengine hawapati maji, yanavurugika yote yanakuwa matope. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni shida, hebu Mheshimiwa Waziri aangalie Mkoa wa Kagera, hivi ulikosa nini huo Mkoa, jamani kila tukisimama hapa watu wa Kagera tunalilia Kagera, afadhali mtusaidie maji na afadhali acha barabara tunazolilia kila siku, lakini maji, maji, maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda sehemu za Izimbya mtoto kuoga ni shida, watoto hawaogi, anaoga mara moja kwa wiki kwa sababu unamwambia mbona hujaenda kufua anasema mimi nafuaga Jumamosi peke yake ni kwa sababu ya maji, siyo kusema anapenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wageuze macho watuangalie, waangalie Karagwe wana shida ya maji, tuna mito, tuna mabwawa, tuna Ziwa Victoria hatuna hatuna maji, ni aibu. Wawaangalie hao akinamama, wawaangalie watoto, sisi ni watu wetu tunakwenda kuomba kura pale tunatoa ahadi za maji, tunatoa ahadi za barabara, na ahadi hazitekelezeki, itamalizika miaka mitano hata ahadi hizo tunazozisema hazijakwisha, tunazidi kuendelea kutoa ahadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba ni kwamba, sasa wakati umefika wa kutenga bajeti ambayo ni ndogo, ili kila mkoa angalau upate kitu ambacho ni muhimu. Kwa mfano, kama pale Bukoba unaweza ukatenga bajeti ya kusema kwamba halmashauri kwa sababu sisi, Idara ya Maji, sasa hivi wana mradi ambao tunaweza kusema hapa wanatumia vijiji vitano, vijiji vingine ni mwaka ujao, hivyo hivyo kila mwaka unatenga bajeti kidogo kidogo ili watu wote waweze kufikiwa na hayo maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyosema ni mkoa mzima hata ukienda Muleba, mama Tibaijuka yuko pale atakueleza ni matatizo yale yale ya maji hakuna sehemu ambako unasema kuna unafuu, labda wilaya fulani vijiji vitano vinapata maji, viwili havipati maji. Ukienda sehemu za Izimbya ninazozisema wanadanganywa wakati wa uchaguzi, kuna mwaka mmoja mwaka 2003 tulikuwa tuna uchaguzi mdogo, Mheshimiwa Karamagi alikuwa anagombea, Mheshimiwa Karamagi akawaahidi maji, akawaambia chimbeni mitaro, watu wakachimba mitaro wiki nzima, kumbe alikuwa anataka kura, alivyopata kura kwa heri, hawakupata maji mpaka leo hii. Wanasema angalau mtusaidie zile pump za kupiga za maji angalau tupate maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu za Kikomelo, twende Lubale, wanawake wakikuona tu, wanakwambia jamani sisi kura tunawapa lakini jamani maji, hakuna anayekwambia tupe pesa, ni maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana watu wa Kagera muangalie mikoa yao ina matatizo ya maji, hakuna kwenye unafuu na mito tunayo mingi, tuna Mto wa Kagera, tuna vyanzo vingi, Kalebe kuna vyanzo vingi, lakini hakuna maji. Kilimo cha umwagiliaji mmeshatunyima, kilimo ambacho kingesaidia vijana wapate ajira kwa kulima mbogamboga, huko pia hatuko, sasa si unaona kwamba tunasahaulika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende Dar es Salaam watendaji wako hapa, kuna vishoka wa maji, wanaitwa vishoka, ndiyo wanaosababaisha tupate na kipindupindu. Wale usiku kucha wanakata mabomba wanaiba maji usiku, mvua ikinyesha yale mabomba yanarudi tena kwenye matundu yale ya mabomba tayari kipindupindu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, waweke hapa, kuna mtu mmoja ameongea neno nimelipenda, nimependa neno la mawakala, tukiwa na mawakala, haya mengine tusingelalamika ingekuwa ni nafuu, mawakala wanazunguka kwa sababu nashangaa Dar es Salaam usiku kucha ukienda kwenye Mitaa ya Sinza, mimi huwa nafikia Sinza pale, usiku unaweza ukapita pakavu lakini ukirudi barabara imejaa maji, na wakishayakata hawajui tena kuyafunga yasiendelee kumwagika, tayari na yenyewe ni hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliangalie hili kama watendaji wa Dar es Salaam wako hapa wajue, kama wanatengeneza makundi au wanatengeneza timu za kuwa zina-supply kuangalia mitaa maji yanamwagika bure yanaingiliana na maji machafu, yanaingia na kwenye mabomba ya maji machafu tayari kipindupindu na hatutapona kama ni hivyo, tuwe tunaweka watu wa kwenda kuangalia na kuzunguka kuangalia watu wanaokata mabomba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende baharini, Ziwani, kuna uharibifu wa mazingira, tungekuwa tunasema watu watachota maji ziwani au baharini lakini huwezi kuyachota yale, ni machafu. Uchafuzi wa mazingira umekuwa mkubwa sana na ndiyo unasababisha wakati mwingine vyanzo vya maji vikauke. Unakuta watu wanalima kwenye vyanzo vya maji, wengine wanayatumia vibaya, kama mito hii kule Kalebe na wapi wanalima mle mle, wakishalima yale maji hata watu kusema labda wakinge ya kuweka kwenye visima hawawezi kwa sababu ni machafu na yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri akija kutujibu hapa, anijibu mradi huo nilimwambia wa kwanza wa Ziwa Victoria kama na sisi tumo Mkoa wa Kagera, atueleze ni lini watakuwa na mikakati ya kuweza kutuvutia maji kutoa Mto Kagera, angalau na Kalebe kupate vyanzo vya Kalebe vyanzo vya Kenyabasa ili watu waweze kupata maji yaliyoko salama kuliko kupata maji ya shida, kwa sababu nimefanya ziara kwa Mheshimiwa Mkuchika, wana matenki ya wakoloni mpaka sasa hivi yako pale, nikauliza hivi maji yanatoka mle wanasema humu hamna maji unaona mbwa wanakokanyaga na paka ndimo tunakochota maji, hiyo ni Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa kwenye kampeni nimeona Tandahimba, nimeona Newala watu wana shida ya maji, ni Tanzania nzima siyo kusema ni Kagera peke yake ni Tanzania nzima, watu wana shida. Nimeshindwa kunywa chai Tandahimba kwa Mheshimiwa Katani; nimekwenda kunywa chai, nilivyofika pale wanasema tumekwenda kuchota maji tumekuta mbwa wamekunywa mle tukashindwa kuyachota, sasa hiyo ni Tanzania ya wapi?. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ni Tanzania ya viwanda ianzie kwenye Tanzania ya maji, tuje twende kwenye viwanda kwa sababu bila maji hata viwanda hakuna. Sasa tunasema hapa kazi, hapa kazi tunataka kupata maji salama, tunataka kupata elimu, tunataka kupata barabara safi, ndiyo tutajua kwamba hii ni Tanzania ya hapa kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie maji mashuleni wamesema wengi…
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.