Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa mara ya pili nawashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Ndanda baada ya kuamua kuondokana na boya wa Chama cha Mapinduzi walisema nije kuwawakilisha hapa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa nichangie katika huu mpango, kwanza kabisa kwa kumpa pole Mheshimiwa Magufuli kwa sababu amepokea Serikali iliyorithi matatizo mengi sana katika mfumo wetu wa uongozi, lakini hata hivyo namwamini kwa sababu naamini ataweza kutatua mgogoro wa UDA, lakini pia hapa ndani tunategemea kusikia mgogoro wa Home Shopping Center umetatuliwa, lakini pia tutasikia issue ya makontena nayo imekamilika na waliohusika katika hujuma hizo wanachukuliwa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite moja kwa moja katika hoja, lakini pia nikiwapa pole familia mbili za ma-suppliers ambao wamefariki katika eneo langu, kuna mmoja anaitwa Muwa Gereji na mwingine Ndelemule, hawa watu walikuwa wanaidai Serikali kwa ajili ya kutoa huduma katika Chuo cha Wauguzi cha Masasi mpaka wamefariki Serikali haijaweza kuwalipa fedha zao na kilichowaua ni presha baada ya kuambiwa mali zao zinauzwa walizokuwa wamewekea bondi wakati huo. Tunaomba sasa Mpango huu uoneshe wazi mpango wa waziwazi kabisa wa kutaka kusaidia kuwalipa Suppliers pamoja na Wakandarasi wengine katika maeneo mbalimbali tusije tukawaletea matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara tunaomba kama ingewezekana basi ungeingizwa ikawa ni ajabu nane katika yale maajabu ya dunia. Kwa sababu Mtwara ndiko ambako sisi kwa kipindi kirefu wakati huo nilikuwa naona hapa akina Mzee Nandonde na wengine wakiwakilisha Mikoa ya Mtwara mengi walikuwa wanayasema lakini yalikuwa hayatekelezwi. Siku za hivi karibuni pamegundulika gesi kule pamoja na vitu vingine, Serikali iliyopita ikaamua kuondoa gesi ile tena kwa gharama kubwa sana na kuipeleka kwenda kuzalishia umeme maeneo ya Kinyereze megawati 150 bila kuangalia kwamba tunategemea lini kurudisha ghrama za uzalishaji ule ili wananchi waweze kunufaika nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lLakini pia Mkoa wa Mtwara ndiyo Mkoa pekee ambao una chanzo kikubwa cha uzalishaji wa umeme lakini maeneo mengi ya Mkoa ule hakuna hata umeme. Hata yale maeneo ambayo yamepitiwa na umeme kwa nguzo juu ya maeneo yale, kwa mfano ukienda Kijiji cha Chipite, ukipita Kijiji cha Mumbulu, ukipita Kijiji cha Liputu na Majani, lakini pia ukienda katika Kijiji cha Rahaleo pamoja na Liloya, maeneo haya nguzo zinapita juu ya vichwa vya watu. Watu wale waliambiwa wakate mikorosho yao, watu wale waliambiwa wakate miembe katika maeneo yale wakiamini kwamba siku moja watapata umeme lakini hata hivyo watu wale hawana umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu Waziri wa Nishati na Madini, asipoviingiza vijiji hivi katika Mpango wa kupatia umeme nitakuwa wa kwanza kushika fungu ili bajeti yake isipite katika Bunge lijalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme wazi, kule kwetu kuna utaratibu wa kitu kinaitwa stakabadhi ghalani. Ule utaratibu siyo mzuri sana kwa mwanzo, lakini kwa sababu upo na upo pale kisheria ninawashauri watu wa Mtwara tuendelee kuutumia, isipokuwa tunataka marekebisho makubwa sana katika utaratibu ule. Wanakijiji wa Kijiji cha Ujamaa Nagoo, walipotelewa Korosho zao tani 103 mwaka jana, lakini sheria ya stakabadhi ghalani inasema wazi na nitaomba nii-qoute hapa, kwenye section 18 sub-section (d), lakini pia ukienda kwenye section 22 sub-section 3 inamtaka mmliki wa ghala, utakapotokea upotevu wa mali yeyote ya mtu aliyetunza katika ghala lake ndani ya siku kumi aweze kulipa na kufidia vile vitu vilivyopotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo sasa hivi lina mwaka mmoja, waliyosababisha ule upotevu wanajulikana, akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho ambaye tunamwambia kabisa Waziri wa Kilimo kwamba atakapokuja kwetu Mwenyekiti huyo akiendelea kumuacha hatutampa ushirikiano kwa sababu siyo mtu anayetaka kutusaidia kuliendeleza zao la korosho, isipokuwa amekwenda pale kwa ajili ya hujuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nikueleze wazi, Masasi ndiko ambako kulikuwa kuna viwanda vikubwa vya korosho, viwanda vile sasa hivi vimegeuzwa kuwa maghala ya kutunzia choroko na mbaazi, havifanyi kazi iliyokusudiwa ya awali. Tunasema hatutaki, mtakapokuwa mnapanga mpango wenu, mkiamua kifikiria viwanda katika maeneo yetu basi tungependa sana muanzie katika viwanda vile ambavyo sisi tulivizoea, msituletee viwanda vya ajabu, halafu mkaja kutujazia watu kutoka maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani kwanza tushughulike na korosho yetu kwa kuanzia, baadaye mtutafutie viwanda vingine vitakavyokuwa na tija, lakini tunafahamu ujenzi wa viwanda vipya ni wa muda mrefu tena wenye gharama kubwa, kwa hiyo kwanza mturudishie vile viwanda vyetu vya asili ambavyo ni Viwanda vya Korosho katika eneo letu visitumike kama maghala kama ilivyo sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nikuambie, Msimamizi Mkuu wa Bodi ya leseni za maghala, amekua akihusika kwa kiasi kikubwa kwa kupokea rushwa lakini pia kuto kutenda haki kwenye utoaji wa leseni za maghala. Namtaka pia Waziri wa Kilimo atakapokuja hapa na mpango wake naye atueleze anataka kufanya nini katika eneo hili, kwa sababu sasa hivi kupata leseni za maghala kule kwetu ni sawa na mbingu na dunia kitu ambacho tunasema hatutataka kiendelee na tusingependa iendelee kufanyika hivi, utuondolee yule Mkurugenzi katika eneo lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nirudi katika eneo lingine katika huu utaratibu wa korosho kuna mchango kule unaitwa export levy, madhumuni ya awali kabisa ya export levy ni kwa ajili ya kuwagharamia wakulima kuweza kupata pembejeo lakini pamoja na mafunzo. Hizi fedha zinaishia Dar es Salaam ambako hakuna mikorosho, sisi kule tunaoishi na mikorosho fedha hizi hatuzioni. Hata hivyo pembejeo zile hazifiki kwa wakati, tunashauri sasa export levy ikishakusanywa ile fedha ipelekwe katika kila Halmashauri na Halmashauri zile zitaamua zenyewe kwa sababu Halmashari zote zinazolima korosho zinatofautiana katika misimu ya ulimaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri asituletee sisi pembejeo Masasi akatufananisha sisi na watu wa Mkuranga kwa sababu misimu yetu inakuwa tofauti katika maeneo haya. Kwa hiyo, nishauri kabisa export levy iende moja kwa moja kwa Mkurugenzi kwa ajili ya kupanga mikakati na wakulima wake waweze kununua pembejeo kwa wakati ziweze kuwafikia wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia pia kitabu cha Mpango, Mpango mzuri sana mmeweka humu ndani, lakini niseme, nina maslahi katika eneo hili. Tuje kwenye suala la usafiri na usafirishaji. Imeguswa hapa katika eneo moja kuhusu reli ya kati, niwapongeze sana Wabunge wanaotoka katika reli ya kati na naiomba Serikali ihakikishe inatekeleza hili kwa sababu reli ya kati ni sehemu kubwa sana ya uchumi wetu sisi wote Tanzania hakuna asiyetambua hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niunganishe, mwaka huu naona hapa tuna bahati tumechajiwa kuhusu reli pia ya Mtwara kwenda Mbambabay imetajwa humu kwenye huu mpango. Tusipoiona katika utekelezaji nitakuwa wa kwanza kushika kifungu ili kwanza hili litekelezwe kwa ajili ya maslahi ya watu wa Mtwara na watu wa Kusini kwa ujumla ndipo tuangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ningetaka kuwaangaliza jambo moja, unapokuja Mtwara, unaposema unakwenda kwenye barabara ya uchumi, ile barabara ni ndefu sana inaanzia Mtwara Mjini inakwenda mpaka Newala lakini pia inatokea mpaka Masasi. Inaendelea Mpaka Nachingwea, Liwale, Ruangwa anakotokea Waziri Mkuu ambako leo nimepata taarifa kwa sababu na mimi ndugu zangu wanaishi kule kwamba ukitaka kwenda kijijini kwa Waziri Mkuu hakupitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tuseme na yeye anahitaji kupata barabara, ile barabara inakuja kutokea Nanganga, nimeona pale kuna daraja limetajwa na Nanganga Two, ningependa siku moja na Waziri tufuatane tukaangalie vizuri huu mpango tuone kama kweli unatekelezeka hasa maeneo ya Kata za Lukuledi na Kata nyingine hapa katikati watu wengi walichorewa nyumba zao X, sasa waliniagiza nije kuuliza lakini pia kutoa taarifa kwa Waziri wa Ujenzi na Miundombinu kwamba X zile kama hamna matumizi nazo basi tunaomba tukazifute, tutatafuta wenyewe rangi ya kufutia kwa sababu zinawapa watu presha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi waliyo na X katika maeneo ya Dar es Salaam wamekuwa wakivunjiwa nyumba zao. Kule kwetu sisi kuna X, hatuambiwi kama barabara ya Masasi kwenda Nachingwea - Liwale, kwenda Ruangwa mpaka Nanganga itajengwa lini? Haya maneno ya upembuzi yakinifu ninaomba mtakapokuwa mnataja miradi yote inayohusika katika eneo langu lisitumike kwa sababu nitakuja niondoe kifungu, nataka mnipe tarehe mahsusi tutaanza siku fulani, tutamaliza siku fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu nimesikia hili neno toka nikiwa mdogo na maeneo mengi yaliyokuwa yanatumika eneo hili vile vitu pale havitekelezwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa namna ya pekee niseme kule kwetu tuna madhila mengi sana, ukija kwenye masuala ya kiafya sasa hivi kuna mgogoro mkubwa sana unaendelea katika Hospitali ya Wilaya ya Masasi, ningemtaka Waziri tukutane halafu baada ya hapo nimwelekeze nini pale kinaendelea kwa sababu wakubwa waliopo pale hawataki kuambiwa ukweli na watu walioko chini yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Daktari mmoja pale anafanyiwa figisu, anataka kufukuzwa na hii inashirikisha Mkurugenzi wa Wilaya pamoja na Daktari Mfawidhi wa pale, amekuwa akiwanyanyasa wafanyakazi wale kimapenzi, kwa hiyo, naomba Waziri nikuletee taarifa hii rasmi na nitaomba nikae na wewe ili tuliweke hili sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Waziri wa Ardhi sasa hivi Wilaya ya Masasi imeanza kuwa na migogoro mikubwa ya ardhi kuhusu upimaji na mambo mengine, Mheshimiwa Lukuvi hili tutaliongea na bahati nzuri uliniambia ulishawahi kuishi maeneo yale sasa umetaka kuanza kutugombanisha kwa ajili ya udongo wetu hasa zaidi katika Kijiji cha Mtandi na hivi ninavyokwambia hapa ninaomba tafadhali tukae nikufahamishe zaidi nayafahamu matatizo ya lile eneo kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwisho kabisa niseme kwamba, Tanzania ni nchi kubwa sana tena ni nchi pana, kwa hiyo tunatamani patakapokuwa panafanyika mikakati na mipango ya maendeleo basi mipango hii ingekuwa inagawanywa kwa mtambuka ili kila eneo angalau kidogo watu waguswe nalo, lakini siyo maeneo mengine yanasahaulika moja kwa moja yatakuja kutuletea shida katika utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia kwamba katika maeneo haya kuna shida kubwa sana ya maji, lakini cha kushangaza kuna bomba kubwa la maji linaloelekea katika Wilaya ya Nachingwea likitokea Ndanda kupitia pale Mwinji. Sasa niseme wazi tunaomba utueleze na mpango wako uje utuambie wananchi wanaokaa juu ya bomba lile kuna mpango gani wa kuwapatia maji katika maeneo yao, kama hili halitafanyika nitawahamasisha tutoboe na tuanze kunywa pale katika eneo letu. Hata hivyo, siungi mkono pale nitakapopatiwa maelezo mazuri kuhusu maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. (Makofi)