Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia Hotuba ya Waziri wa Maji kwa Wizara yetu hii muhimu ambayo ni nyeti sana kwa viumbe vyote ambavyo vimeumbwa duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kusema kwamba, maji ni uhai. Maji ni uhai kwa viumbe vyote vilivyoko hapa duniani. Maji ni uhai kwa maana ya kwamba, bila maji vifo vinaweza kutokea. Ukiugua kitu cha kwanza unapewa maji kwa drip, hayo ni maji. Bila maji mtakuwa na njaa kali sana nchini, ndiyo maana ya kusema ni uhai. Pia bila maji hutakuwa na viwanda vyovyote wala hutakuwa na maendeleo yoyote ya kutengeneza barabara wala hutakuwa na maendeleo ya aina yoyote endapo maji hayatatiliwa mkazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wetu Engineer anajua na nimeshamsumbua mara nyingi safari iliyopita kuhusu suala la maji, lakini kwa kweli, walikuwa wanajaribu kujitahidi, lakini nahisi kwamba, Waziri wewe kama Waziri hutaweza kuleta hizi hela za bajeti! Bajeti uliyotenga bilioni 915 haina kazi yoyote kwa sababu, hata bajeti iliyopita, safari iliyopita haikufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani sasa ifike mahali Wizara ya Maji, Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, TAMISEMI kwa sababu nao wanapitishiwa fedha, nendeni kwa Rais mkaombe hela. Hatuna haja ya sisi kuzungumza habari ya bilioni mia tisa hapa kwa sababu, haitoshelezi! Sasa kama haitoshelezi tunaongelea nini? Nadhani tuache, nendeni kwanza mkafanye hiyo kazi, halafu mrejeshe hapa kwamba, hela tumeongezewa! Uchukuzi wanapewa trilioni mbili! Mahali ambako uhai tunautegemea, bilioni 900! Tunazungumza nini sasa hapo? Naona tunapoteza muda tu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara haiwezi kutengenezwa bila maji, hakuna kiwanda kinatengenezwa hamna maji pale. Sasa kama barabara haiwezi kutengenezwa hawa wanapewa hela kubwa halafu maji wanapewa hela ndogo! Hii ni dharau kubwa kwa kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, kuhusu suala la uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini. Ukweli ni kwamba, wakala huyu atafanya kazi na wewe Wizara utakuwa na mahali pa kukamata; fedha zote zinazokwenda vijijini hutumika vibaya. Maafisa Masuuli wameona kwamba, fedha za maji sasa ndio duka lao! Ndiyo mahali pao pa kupata mitaji kwa sababu, kuna Wizara mbili! Wizara ya Maji inazungumza habari ya mradi wao kutoka Wizarani, TAMISEMI nayo ina mradi wa maji unakwenda pale kwenye Halmashauri D-by-D, lakini nao hawafuatilii. Kwa hiyo, imeonekana lile ndio duka lao ambalo wanafanya matumizi makubwa yasiyofaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza hivi kwa sababu, kwa Wilaya ya Hanang naomba kuzungumzia masuala ya Programu ya Usafi wa Maji na Mazingira. Mpaka sasa hivi ninapozungumza hapa zaidi ya 4,000,757,000/= zimekwenda pale, lakini ukiambiwa miradi ile ya vijiji 10, Mheshimiwa Waziri ambayo anasema ni asilimia 80 kwenye taarifa yao, ni vijiji saba tu ambavyo vimepata maji kati ya vijiji 96!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Hanang ina vijiji 96, vijiji saba tu! Hiyo ni asilimia 70 kweli au mnawadanganya Watanzania kwa asilimia? Hakuna maji! Siyo kwamba, ile Wilaya haikuwa na Waziri, ilikuwa na Waziri! Mimi nina mashaka Mawaziri hamuwezi hilo! Twendeni kwa Rais atupe maji, ndiye anayeweza, hakuna mtu mwingine! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Kambi ya Upinzani kuhusu uanzishwaji wa Wakala kwa maana ya kwamba, fedha zetu zisimamiwe vizuri. Kwenye maandishi utaambiwa kwamba, wamechagua vijiji 15, lakini vijiji havina maji! Saa hizi ukiondoka Waziri nenda Hanang, utakuta hata pampu za maji hazipo hata hivyo vijiji saba! Mwananchi hana maji, pampu za maji mbovu! Ni hali mbaya kabisa. Kwa hiyo, ni lazima kuangalia ni jinsi gani tuweze kuokoa hela za Watanzania na hela zinazotokana na misaada mbalimbali kutoka nchi za wenzetu wanaotusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Hanang, Ishponga ilipewa milioni 209 hawana maji ya kutosha! Ukiangalia value for money hakuna kilichofanyika! Waziri wa TAMISEMI msaidie Waziri wa Maji kwamba, hela kule zinaliwa bure. Garawja ilipewa bilioni moja na point moja ya kutengeneza mradi wa maji, hayo maji bado hayajakamilika mpaka leo! Kwenye vitabu vyao vimeonesha maji yamekamilika, kumbe bado, hela zote zimetumika! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha nyingine Mogitu, mradi wa Kateshi na Mogitu ni mradi mmoja, lakini utakuta wanasema mradi wa Mogitu umetumia milioni 578,000/= halafu mradi wa Kateshi umetumia milioni 867; sasa mradi wa Kateshi na mradi wa Mogitu ni mmoja ambapo kuna hela za Rais pale pia, milioni 390! Huo mradi mpaka sasa hivi bado haujakamilika, watu wa Kateshi hawajapata haya maji ambayo yanatokea Mogitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaambiwa kupitisha kalavati tu, zimetumika milioni mia mbili sijui na kitu! Eti kuchimba barabara halafu kupitisha bomba chini, milioni mia mbili na kitu! Tunataka Mheshimiwa Waziri aende akahakikishe kwamba, hizi fedha pia, zinatumika vibaya ndiyo maana tunakosa maji; watu wa Hanang hawana maji, ni vijiji vichache tu vilivyopata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakwenda, Basotu tunatumia maji ya ziwa, ni chanzo cha maji kizuri, lakini yale maji hayako salama. Hayako salama kwa sababu mashamba ya ngano yanayolimwa yanapigwa dawa ya kuua wadudu, maji yote yanaelekea kwenye hilo ziwa, wananchi wanatumia yale maji hayako kwa njia ya bomba. Ni Wizara ipi inayoweza kuwasaidia wale wananchi wa Basotu, Hanang waweze kupata maji safi na salama ambayo hawapati kansa kama inavyofanyika sasa hivi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia suala la Hanang, suala la irrigation; scheme ya irrigation imepelekwa Hanang, iko kweli kwenye Kijiji cha Endagau, lakini fedha zake zote pia zimetumika! Milioni 410 zimetumika vibaya na tunahitaji irrigation kwa hali ya juu. Saa hizi ni kweli umetupitishia hela kuja kule, lakini nani msimamizi kama hakuna wakala? Ndiyo maana tunasema kuwe na wakala wa kusimamia miradi ya maji kwenye vijiji kwa sababu ya upotevu wa fedha nyingi sana za Serikali. Sasa sisi tutalia! Waziri analia! Kila mtu analia kwa ajili ya maji kumbe ni fedha zinatumika vibaya pia kwa asilimia100. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunaomba hili aliangalie sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la irrigation ukweli ni kwamba, fedha mlizotenga bilioni 35 ni ndogo sana. Mnategemea kutengeneza mradi wa irrigation wa hekta laki nne, hekta laki nne utazipataje kama hela ni hizi bilioni 35! Hazitatosha kwa ajili ya irrigation. Kwa hiyo, hatuna budi kuongeza kwa sababu, tuna mabonde mengi sana, ili kuondoa njaa nchi hii hatuna budi kutenga hela za kutosha kwa ajili ya irrigation ili kuondokana na njaa. Leo tunakosa sukari wakati kuna irrigation ya kutosha, tuna mabonde ya kutosha! Peleka hela ya kutosha wananchi walime miwa, ili waweze kutengeneza sukari yao, hakuna haja ya kuagiza nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mabonde. Mabonde nchi hii yameelekezwa Kusini zaidi, lakini wamesahau pia Kaskazini zinahitajika sana fedha za kutosha. Tunaomba muelekeze kule pia, kwa ajili ya irrigation kuweza kupeleka hela za kutosha, sio lazima kupata hizi, naomba sana hili liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia suala hasa la upotevu wa fedha. Nimejaribu kwenda TAMISEMI mara nyingi, nimejaribu kwenda ofisini kwa Mheshimiwa Waziri, lakini hakuna anayesaidia kuhusu upotevu wa hela za Hanang! Milioni 540 za maji mpaka sasa hivi hazionekani zimeelekea wapi! Atatusaidiaje Watanzania Wanahanang ili milioni 540 za maji zionekane zimeelekea wapi? Tunataka taarifa hizi anapo-wind up atwambie kwamba, tutapata wapi hizo hela zilizopotea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba sana kumwomba Mheshimiwa Waziri u…
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango wako.