Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Dkt. Nagu fujo hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nichangie katika Wizara hii inayoshughulikia maji. Inasikitisha sana kuona kwamba tunatengeneza madaraja kwa namna ambavyo tunapata maji katika nchi hii. Sisi kwenye Jimbo la Temeke tunaonekana kama watu wa daraja la tatu ambao hatustahili kuwekwa kwenye mpango wa kutumia maji matamu maji ya bomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote mipango ambayo inaigusa Temeke ni ile ya visima, maji ya visima ni yale ambayo yanakuwa na asili ya chumvi chumvi na haya ndiyo maji ambayo watu wa Temeke tunakunywa. Ukipikia chai ile chai inakuwa ina utamu wa chumvi na sukari, kwa hiyo lazima utumie sukari nyingi zaidi ili upate utamu wa chai. Ni vizuri Wizara ikaangalia mgawanyo ulio sahihi wa watu wote Dar es Salaam kupata maji ya bomba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii mipango zikitajwa hapa Kata za Jimbo la Temeke zinatajwa zile ambazo pengine zinapakana pakana na Ilala hivi, ndio labda ziingizwe kwenye huo mpango. Inatajwa hapa Kurasini, inatajwa Keko, inatajwa Chang‟ombe, lakini tunaacha eneo kubwa lenye watu wengi ambalo limejikita katika kutumia maji ya visima, tena siyo vile visima virefu, Visima vingi ni hivi vya watu binafsi, vinavyomilikiwa na watu binafsi ni visima vifupi havijachimbwa kiutalaam, unakuta hapa ni choo, hapa kimechimbwa kisima, ndiyo maana kila siku kipindupindu kikiingia Dar es salaam lazima kitafikia Temeke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Mheshimiwa Waziri akatuangalia kwa jicho lingine, atuangalie kwa jicho la huruma, basi aje hata na mpango tu mzuri kwamba kwa sababu visima vingi ni vifupi ambavyo maji haya si salama basi kuwe na utaratibu wa kuwekea dawa visima hivi, utaratibu ambao hautotugharimu sisi wanywaji. Serikali hilo ni jukumu lao kuhakikisha haya maji yanakuwa treated ili wananchi wao waweze kunywa maji yaliyo salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hayo, lakini bado tunahitaji kuwe na mpango maalum wa kupata maji ya bomba, amezungumza hapa Mbunge wa Rufiji, kama Serikali kweli ina nia ya kufikisha maji Dar es Salaam iweke fedha kwa ajili ya huu mradi, kutoka Rufiji kuja Dar es Salaam sio mbali na tutapata maji ambayo yatatumika Rufiji, Mkuranga, Kisarawe, Dar es Salaam. Kwa Dar es Salaam si kwa maana ya Temeke peke yake, hata maeneo ya Kinondoni, maeneo ya Ubungo wanaweza kutumia maji haya kutoka Rufiji na yakawa mazuri zaidi na mengi kuliko haya ambayo tunahangaika nayo kutoka Ruvu, kwa nini Serikali haijikiti uko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa Wizara hii itoe kipaumbele sana kuhakikisha kila mtu anapata maji na yaliyo safi na salama kwa wingi. Ukikatika umeme tu Dar es Salaam, ukikatika umeme Temeke basi ujue siku hiyo hakuna maji kwa sababu ili watu wapampu maji lazima wanahitaji ule umeme. Kwa kuwa maji yenyewe ni visima vimechimbwa na watu binafsi hawana matenki makubwa ni matenki ya lita 2,000, lita 5,000, kwa hiyo, ukikatika umeme hatuna maji, tunasubiri huku tumepanga foleni mpaka usiku umeme ukirudi kama tuko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Temeke pia tunataka tuishi maisha ya kimjini jamani, tunaomba tupatie maji. Haya ndiyo mambo wanayoyataka wananchi, tena wale wananchi wa kawaida kabisa wakati wa kampeni tunawapelekea tisheti na kapero. Shida yao siyo hivyo, shida yao ni maji haya, basi Serikali iweke fedha za kutosha kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji, lita elfu moja kwa Temeke tunazinunua kwa sh. 3,500. Maana yake familia ya watu wawili tu kwa mwezi mnalipa maji zaidi ya shilingi…
MWENYEKITI: Ahsante.