Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutenga fedha kiasi cha shilingi bilioni sita point nane kwa ajili ya Miradi ya Maji iliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Niseme wazi kwamba kwa kipindi kirefu fedha zilikuwa zikitengwa kwa ajili ya kuongeza na kupanua miundombinu katika shirika letu linalogawa maji kule kwetu ambao ni MANAWASA.
lakini kwa bahati mbaya sana hazikufika. Mwaka huu tena tunaona wametengewa pale shilingi bilioni moja, sasa tunaomba hizi fedha zifike ili waweze kupeleka maji katika Vijiji vya Mpohora, Nangoo, Mbemba, Mbaju, Chigugu, Chikundi, Liloya na Makongwa pamoja na Njenga maeneo ambayo yanapitiwa na bomba kubwa kabisa la maji yanayotokea Mto Mbwinji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Ndanda tuna neema kubwa sana ya maji na maji mengine sisi tunayauza, maana yake kwamba yanatutosha. Tatizo kubwa tulilonalo ni miundombinu katika maeneo yetu, tukiweza kusaidiwa fedha za kuweza kuweka miundombinu maji haya tutahakisha yanafika katika Vijiji vya Lilala, kwa sababu kuna mradi unaoishia pale unaoelekea Vijiji vya Chiwale. Lakini tuna maji mengi sana maeneo ya Namajani ambayo yanatumiwa na askari magereza pale, tatizo tu pale ni kupata umeme ili transfoma ishushwe pale waweze kupampu maji yale yatumike maeneo ya Kata ya Namajani, yanaweza kufika pia Kata ya Mlingula pamoja na Chilolo kwa sababu eneo hili pia kuna wakazi wengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata msaada wa JICA kwa ajili ya utengenezaji wa kisima katika Kijiji cha Nambaya, lakini kwa bahati mbaya sana kisima kile hakijamaliziwa na wananchi wanahitaji yale maji. Tunaomba waangalie ni jinsi gani wanaweza kutusaidia kumalizia kile kisima ili wananchi waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tuseme tunatamani sana kuona watu wa MANAWASA wanapewa fedha ya kutosha kwa sababu sasa hivi pamoja na kudai fedha nyingi katika Idara mbalimbali za Serikali, lakini wamekuwa hawana fedha za kutosha kwa ajili ya kuweza kujipanua kufikia maeneo mengi sana waweze kuendesha miradi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini wakiwawezesha MANAWASA kutakuwa hamna shida ya maji katika maeneo yetu na tutaacha kufanya kampeni kwa kutumia shida za wananchi hasa zaidi maji kwa sababu watu hawa wote wana uwezo wa kupata maji katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, atakapokuja kuhitimisha hapa atatuambia ni jinsi gani anataka kuwapa nguvu MANAWASA pamoja na Mheshimiwa Meneja yule ili sasa aache kuaibika kwa sababu anashindwa kupeleka maji katika vijiji vilivyopo karibu sana na eneo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, hasa zaidi ukiangalia Kijiji cha Chikunja na Kijiji cha Lukuledi ambako hivi karibuni tulikuwa na mradi wetu wa maji lakini ulikuwa unaendeshwa kifisadi, tuliurudisha mikononi mwa wananchi tunaomba pia nao mtusaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, japokuwa wale watu wanafikiri kuna fidia watakuja kupata, lakini hata hivyo kwa sababu hawakusoma ripoti ya mapato na matumizi hakuna fidia yoyote tunawaambia watakayoweza kupata pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata msaada sisi kutoka TASAF, lakini kumefanyika ubadhirifu wa fedha shilingi milioni 378. Waliofanya ubadhirifu huu tunawafahamu, tumejaribu kufuatilia hili jambo polisi kwa muda mrefu sana limekuwa likisumbua lakini tusingepata shida ya maji katika baadhi ya vijiji kwa sababu tayari kulikuwa kumeshatengwa fedha ya kuchimbwa mabwawa katika Vijiji vya Masonga, Mraushi na vijiji vingine vinavyozunguka ambavyo vingeweza kuhudumia Kata tano katika maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI japokuwa Waziri nimempa taarifa kuhusu jambo hili amesema analishughulikia kwa ukaribu sana. Hivyo, tunataka atakapokuja hapa kuhitimisha, basi atuambie wazi jinsi gani anaweza akasaidia watu wa Wilaya ya Masasi kuweza kupata maji kiurahisi kwa sababu maji ni mengi, tatizo kubwa tulilonalo ni miundombinu ili iweze kuwafikia watu mbalimbali katika maeneo yale. Vile vile na kuwaongezea nguvu MANAWASA ili waweze kugawanya maji haya kwa uhakika zaidi katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivi tutakuwa tumemaliza tatizo la maji katika maeneo yetu kwa sababu maji tunayo ya kutosha, shida kubwa tuliyonayo sisi ni miundombinu, kiasi watu wale wanaopitiwa na bomba kubwa la Mto Mbwinju wanashindwa kupata maji ya kutosha na maji yale ni safi na salama yanayokwenda Nachingwea. Kwa hiyo tunaomba atakapokuja …
MWENYEKITI: Ahsante.