Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nikupongeze, nimpongeze Waziri wa Fedha na watendaji wote na nashukuru kwa nafasi hii uliyonipatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumwomba Waziri wa Fedha. Rais alipokuja Kigoma moja ya jambo ambalo alituahidi ni suala la tozo kwenye zao la kahawa ambalo lina tozo 26. Alisema hizi tozo lazima ziondoke. Namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu, atuambie kwa nini hakuona umuhimu wa kutoa tozo hizi kwenye zao la kahawa? Ni kwa nini tunaomba tozo hii zipunguzwe? Ni kwa sababu bei ya soko la kahawa imepungua duniani. Namna ya kuwasaidia wakulima wetu ni kupunguza tozo hizo ili waweze kufaidika na zao la kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni suala la maji kwenye Jimbo la Kigoma Kaskazini. Tatizo la maji ni kubwa sana, lakini tuna Lake Tanganyika. Namwomba sasa Waziri wa Fedha aje na mipango atuambie lini tutaanza kuyatumia maji ya Lake Tanganyika; siyo kwa Kigoma Mjini, ni kwa ajili ya Jimbo la Kigoma Kaskazini pamoja na Mkoa mzima wa Kigoma? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpongeze Waziri wa Fedha, anapeleka asilimia 40 kwenye maendeleo. Kwa vyovyote vile haya ni mageuzi makubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimetafakari sana asilimia 40 maana yake nini? Asilimia 40 Mheshimiwa Waziri wa Fedha, maana yake unaenda kutengeneza umeme, majenereta utayanunua nje, kwa hiyo, tuta-save fedha zetu, tutatoa dola kupeleka nje kupata umeme. Tutatoa dola kutengeneza reli, maana itabidi tuchukue kwanza shilingi, tutawalipa wakandarasi, kwa vyovyote vile watakuwa wa nje. Kwa hiyo, hela itakwenda nje; tunanunua ndege, fedha itakwenda nje. Maana yake ni nini? Tuna-save kama nchi kwa shilingi yetu; itabidi tununue dola kununua hizi services. Ili tuweze ku-strike a balance lazima na sisi tuwe na eneo ambalo litatuingizia dola nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ndipo ambapo wachumi wetu tungewaomba watusaidie. Ninayo maeneo makubwa matatu ambayo nataka niwashauri watu wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni suala la tourism. Wanaoshindana na sisi kwenye utalii ni Kenya, Uganda, Rwanda, Mauritius na South Africa. Wenzetu hawajaweka VAT kwenye utalii, maana yake tunaifanya Tanzania iwe destination ambayo ni gharama na utalii mtu hawezi kuja.
Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tukiweka VAT uwe na uhakika katika watu ambao wataumia zaidi ni Wazanzibar na uchumi wa Zanzibar. Kwa sababu uchumi wa Zanzibar unategemea tourism na tourism ya Zanzibar iko packed pamoja na utalii wa Kaskazini. Mtu angependa aende Zanzibar, aende na Serengeti; aende Mikumi aende na Zanzibar. Naombeni hili jambo tuliangalie kwa umakini mkubwa sana.
Sehemu ya pili ambayo itatuingizia dola ambayo lazima wachumi wetu tukubaliane, ni suala la kwenye masoko ya mitaji. Dar es Salaam Stock Exchange tuliamua kuwapa incentive kwenye capital gain ili watu wengi wapeleke, waende waka-list pale. Waki-list kwenye DSE maana yake ni nini? Maana yake ni mitaji tutapata liquidity, maana yake ni job, ndiyo tutafanya uchumi uchangamke.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Gavana wa BOT, ame-liberalize account ya nje ndiyo maana sasa DSE kuna watu wanatoka nje wanakuja kununua share; lakini ukiweka hiyo kodi maana yake watu wataondoka Dar es Salaam Stock Exchange. Hata anachotaka kukipata, hakitafanikiwa.
Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, walioamua kuweka zile incentives kwa ajili ya soko letu lichangamke, naamini walifikiri vizuri. Haiwezekani tuziondoe leo sisi, nakuomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hiyo tu, hata kukusanya hiyo kodi ni ngumu sana; maana capital gain tax ni wakati gani? Mimi nina share 200 nimeuza, pale nikizidisha ndiyo unakuja unakata, kwa sababu watu wote hatuuzi share at a time. Kwa hiyo, unachotaka kukipata unaweza usikipate mwisho wa siku. Kwa hiyo, suala hilo litakuwa ni gumu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu, jana Mbunge mwenzangu wa Kahama amelisema, sijui kama nitafanikiwa kulieleza kama alivyolieleza. Ametuambia jambo jipya, lakini limekuwepo, mwaka 2011 Kamati ya Madini na Nishati walilisema kwamba umefika wakati tufungue soko la dhahabu Tanzania. Tunalifunguaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuweke mazingira kwamba kila anayekuja na madini yoyote Tanzania, halipi hata shilingi moja. Halipi kodi yoyote, lakini atakayetaka kuyatoa madini hapa Tanzania, tusichukue kiasi kikubwa, unaya-export 1% tu.
Mheshimiwa Waziri wa Fedha ngoja nikwambie kitakachopatikana; tukiamua kufanya hivyo, unayo hakika kwa mwezi tutapata siyo chini ya tani 20 za dhahabu peke yake. Watu watakaokuja kununua hapa, ile dhahabu moja kilo moja ni dola 40,000. Maana yake ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, unapozi-export maana yake unachukua dola 40,000 unazidisha kwa hizo kilo 20,000 utapata karibia dola milioni 800; ukizidisha kwa hela ya Tanzania ni 1.6 trillion. Maana yake ni nini? Asilimia moja ni shilingi bilioni 16. Kwa hiyo, kwa mwaka una hakika utapata shilingi bilioni 200. Shilingi bilioni 200 ni Wizara ngapi umezipa fedha? Ni nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu watakaokuja hapa, watanunua vyakula vyetu, tutapata kwenye VAT, tutapata kwenye hoteli zetu, watanunua kwenye masoko yetu. Naombeni wachumi wetu wakati wa kutumia mambo ya kwenye vitabu, tuanze na mambo ambayo ni practical, tuyasimamie, tutabadilisha nchi yetu. Ndiyo maana tunataka kuweka kodi kila eneo kwa sababu tunataka kufikiria maeneo yale yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nasema ile 48% ambayo tutaipeleka kwenye maendeleo, tutafute namna ya kuirudisha ndani. Namna ya kuirudisha ndani Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tunaomba twende kwenye tourism, tuanzishe soko la dhahabu, lakini pia tuwe na incentive kwenye Dar es Salaam Stock Exchange ili watu wengi waweze kuja hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa nichangie baada ya kutoka hapa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ni suala la viwanda. Bajeti yako inaimba neno “viwanda.” Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ukisoma historia ya watu ambao wameendelea juzi tu kwenye viwanda, kuna mambo lazima tukubali kuyakosa. Ni aidha upate viwanda ama upate kodi. Ukianza na kodi hatuna viwanda; tukubaliane! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leather industry, kwa maana ya Leather Industry in Ethiopia. Wanasema imefanikiwa kwa sababu one, hakuna kodi kwenye capital goods; hakuna kodi kwenye construction materials; kuna cheap electricity; kuna cheap labour. Wamepewa miaka sita kutolipa income tax. Wamepewa holiday! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unachotafuta kwenye viwanda, kitu cha kwanza ni ajira. Watu wetu wakishakuwa na ajira watakuwa na purchasing power. Kwa hiyo, kodi yako utaipata, ni indirect tax, utaipata tu! Cha pili, ni bidhaa ziwepo sokoni. Kodi ni sehemu ya tatu unapoongelea kwenye ule mnyororo wa viwanda. Target ya kwanza ni ajira, bidhaa, ndiyo unakuja kodi na unakuja kuangalia GDP yako.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Wizara ya Fedha, tuliangalie hili eneo. Kama hatujajiandaa, tutasema sana kwenye vitabu, lakini tunaweza tusifanikiwe na nia yetu ni kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la sunflower. Sunflower imeongezeka, ilianza kidogo, sasa hivi imefika tani 180,000; maana yake industry inakua. Sasa tukiweka kodi kwenye crude oil maana yake unasema hakuna haja nilete crude oil, acha nilete refined oil ili nilipe 25% niuze; lakini utakuwa umepoteza ajira za watu wangapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vitu vingine tunavifanya ili kulinda viwanda, ili kulinda ajira, hili ndiyo la msingi kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nilitaka niongelee suala la PPP. Suala hili linasemwa sana kwenye vitabu, lakini kwenye matendo halionekani. Namwomba sana Waziri wa Fedha, sheria ipo, kanuni zipo, tuanze. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaulize Waheshimiwa Wabunge wenzangu, hivi kweli karne hii leo tunaweka bajeti kununua ma-generator ya umeme, wakati ukitangaza, utapata watu wengi tu wa kununua majenereta ya umeme. Kwa nini tuweke hela ambayo tungeipeleka kwenye afya, elimu na maji? Ni jambo ambalo ukiwaita wawekezaji watakuja, unachotakiwa kuweka ni tarrifs ambazo watu wako watafaidi kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuweke mazingira ya kusema, unataka kuja kuleta umeme Tanzania? Eeh, lazima uwe na Mtanzania mwenye 30% mpaka 40%. Haya tukiyafanya, tutaenda mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Mashirika ya Serikali, mimi nitatoa mfano wa shirika moja tu. Mafuta ya ndege Tanzania, Puma ndiyo wana-manage 90%, lakini eti tunampa mtu mwingine aagize ndiyo amletee Puma na sisi tuna share kule 50%. Hivi nani ambaye hajipendi? Lazima tufike maeneo mengine tufanye maamuzi kwa sababu tuna interest kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tumemwona Waziri wa Fedha anapokea dividends. Maana yake ni nini? Kwamba, tukiwapa biashara kubwa, tutapata fedha nyingi kama Taifa. Tukipata fedha nyingi, tutachangia kwenye uchumi wa nchi, tutachangia kwenye maendeleo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba watu wa Serikali, tusaidieni. Yale maeneo ambayo tuna interest kama Taifa, tusione aibu kutumia makampuni yetu. Tusione aibu hata kidogo, kwa sababu tukiogopa tunafanya nini? Tutakuwa tunaongea huku, mkono huu tunafanya kitu cha ajabu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, cha mwisho nataka niongee suala la Kurasini Logistic Centre. Nimesoma hapa suala la Kurasini. Suala hili ni jema sana, lakini nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, ukisoma kwenye Mpango wa Miaka Mitano, Waziri wa Fedha anasema kwenye mpango ule kwamba kuna kampuni za Kichina zitakuja kufanya biashara pale Kurasini; jambo jema, tutapata bidhaa za bei rahisi; lakini mnajua maana yake? Maana yake tumewaua Wakinga, tumeua Wachaga, Kariakoo tumeiua. Maana yake hawawezi ku-compete.
Mheshimiwa Naibu Spika, wale watakaoleta mizigo yao kutoka kule China watapewa export guarantee, watapewa incentive na nchi zao, anakuja anauza bei ambazo umeweka wewe; wewe utakuwa na gharama. Sisi tutakuwa ni expensive; watu wote watakwenda pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najua argument ya baadhi ya watu wanasema, ukifungua Logistic Centre ile kitakachotokea nchi zote zilizotuzunguka zitakuja kununua Tanzania. Sawa nakubali, lakini zikinunua Tanzania, yule anayeuza ni Mchina, sio Mtanzania! Maana yake fedha zile zinakwenda China. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukubaliane jamani, moja ya mambo ambayo tusipokuwa waangalifu tukiwaondoa hawa wafanyabiashara wa katikati, tunaua economy yetu. Tukubaliane, hatuwezi kuendelea bila Watanzania wengi kuwa matajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii habari ya kufikiria Watanzania wakiwa maskini ndio tutaendelea, haiwezekani. Tutapata kodi nyingi wakiweko wafanyabiashara wengi zaidi. Tuweke mazingira ya kukusanya kodi, lakini tuweke mazingira ya kulinda biashara za watu wetu. Tulete mazingira ambayo kule ambako tunafanya biashara kama Serikali, tuhakikishe tunawapa biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tusipofanya hivyo, Mungu ametupa jiografia nzuri sana Tanzania; maeneo haya tuliyopewa kama nchi tuyatumie kibiashara. Tanzania tuna amani, Tanzania tuna mvua, Tanzania tuna maji, tuna mito, tuna lakes, tuna everything! Sasa kwa nini tusitumie jiografia yetu hii kwa ajili ya maendeleo yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba wachumi wetu wakae tufikiri; tusidhani tutakuwa tunafanya mambo kama tunavyofanya miaka yote, mambo yamebadilika sana. Naiomba sana Wizara ya Fedha itusaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho na mimi niliseme, nimesikitika kidogo. Mheshimiwa Waziri wa Fedha anasema, katika mikoa maskini ni Kigoma, Mwanza na mingine aliyoisema. Hapa tuulizane Waheshimiwa Wabunge; hivi kweli jamani Mwanza ni maskini kuliko Katavi? Mwanza ni maskini kuliko Lindi? Mwanza kweli kuliko Pwani! Maana Pwani ni nchi katika nchi ambazo zimefanya vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Mheshimiwa Waziri wa Fedha, atuambie vigezo vyake vya kupima umasikini ni vipi? Ni idadi ya watu au ni nyumba? Ni kitu gani kinapima umaskini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwanza ambako wana ng‟ombe; Mwanza ni wavuvi; Mwanza kuna dhahabu; inawezekanaje wawe maskini kuliko watu wa Lindi? Inawezekanaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiniambia Kigoma, Mwanza, nitaelewa. Kigoma maskini nakubali; lakini hata mimi ukiniambia Kigoma ni maskini sikubali sana; ndiyo Mkoa pekee hatujawahi kupewa chakula toka uhuru wa nchi hii. Halafu watu hawa eti ndio maskini. Tunakuwaje maskini? Kwa hiyo, naomba data zetu tuziangalie upya. Naamini liko tatizo kwenye kuandaa hizi data zetu za watu wa Mipango. Kabisa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ni suala la pensheni. Nimwombe Waziri wa Fedha, suala la pensheni…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Peter Serukamba, dakika zako 15 zimeisha na zile ulizokuwa umepewa pia umeshazimaliza.