Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue fursa hii kukushukuru sana, lakini nikupongeze kwa ukakamavu ambao unauonesha hapa Bungeni, Mungu akubariki sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri na ama hakika Watanzania sasa wanasubiri kuona mabadiliko ambayo tumewaahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye hoja, nianze na reli ya kati. Tunajenga reli ya kati kwa standard gauge lakini liwe jambo jema sana tuzingatie vituo vyote. Nafahamu pale Singida itapita Manyoni, Itigi na kuendelea mbele, lakini reli ya kati ilikuwa inakwenda mpaka Singida Mjini. Sehemu pekee ambayo ndiyo sehemu ya kibiashara iko pale mjini. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri katika vituo vyake asiache kituo cha Singida Mjini, almaarufu reli yetu ile tulikuwa tunaiita Kamnyampaa maana yake ndiye mzee mwenyewe yule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili, kwenye bajeti tumezungumzia ongezeko la kodi ya mitumba kutoa 0.2 mpaka 0.4. Ni lazima tuwe wakweli, Watanzania bado hatujawa na maandalizi ya kutumia viwanda vyetu vya ndani, ya kutumia nguo zilizoko ndani badala ya kutumia mitumba ambayo ni bei rahisi. Leo hii ukitazama vizuri sisi wote tunatumia sana mitumba kuliko nguo za dukani. Tukiongeza kodi maana yake tunaongeza thamani ya mitumba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Waziri amezungumza kuna tatizo la kiafya na mambo mengine. Mpaka tunafikia umri huu kwa kweli wajibu wa Serikali ni kuwaelimisha Watanzania juu ya afya kuliko kuongeza kodi. Kama hiyo haitoshi, tumezungumzia ngozi, kwamba Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itakuja na mpango madhubuti wa ku-deal na sekta ya ngozi, ni mpango gani huu? Tunazungumzia sekta ya ngozi wakati hatuna viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda hivi vinavyozungumzwa hapa vyote hivi vinatengeneza wet blue, ni temporary turning, ndivyo viwanda tulivyo navyo. Viwanda vinavyofanya finishing, utazungumzia Himo na Moshi Tanneries kule, viwanda viwili haviwezi kukidhi haja ya kutengeneza bidhaa kwa Watanzania wote milioni 50. Tunazungumzia sekta ya ngozi ambayo leo ngozi inaoza kwenye ma-godown, tuna tani karibu 5,000 zinaoza, halafu tunasema tutakuwa na mpango madhubuti. Nilitarajia mpango madhubuti ni kufungua milango, tuondoe ile kodi ya zaidi ya asilimia 80 ya exportation ili hawa watu waweze kuuza ngozi yao East Africa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeua kiwanda cha Mwanza Tanneries kwa sababu ya ukaribu wa ziwa, kitu ambacho siyo kweli. Hebu twende tukaangalie ile Jinja Tannery, ni mita 200 tu pale lakini kiwanda kinafanya kazi, leo tunaendelea kuua viwanda. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri, kwenye suala hili la ngozi, huu mkakati madhubuti unaozungumzwa ni vizuri ungeletwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara na nimeshiriki kwenye kikao cha wadau, wachuuzi wa ngozi na wale wenye viwanda vya ngozi, hakuna majibu thabiti yaliyotolewa ni namna gani tuna-deal na viwanda vya ngozi. Leo hii ngozi inaoza, ngozi imeshuka bei imefika mpaka Sh.100, inatupwa, lakini tunasema tumempa Waziri sasa aje na mkakati. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hakuna mkakati na kama upo uletwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la mafuta, tumeweka asilimia 10 kwenye importation ya crude palm oil, lakini mafuta yaliyoko ndani leo bado VAT inatutesa. Nilitarajia kuiona Serikali sasa inaondoa VAT katika bidhaa inayosindikwa. Tumendoa VAT katika bidhaa ambayo haisindikwi lakini mkulima yule yule ambaye analima alizeti, anaipeleka kiwandani, ikishatoka pale inalipiwa kodi asilimia 18, maana yake utakuwa hujamsaidia. Kwa hiyo, niombe sana tuondoe VAT pia kwenye mafuta yetu haya ya alizeti ambayo tunayatumia sasa, tutakuwa tumemsaidia mkulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa Kenya kwenye mashudu wameondoa VAT na sisi tunategemea sana haya mashudu yatusaidie. Niombe na sisi tuondoe VAT kwenye mashudu. Hii nayo itasaidia wakulima wetu wadogo wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini na mimi nichangie kwenye zile shilingi milioni 50 ambazo Serikali inazitoa vijijini. Kuna mambo mawili hapa, tunazungumzia shilingi milioni 50 vijijini lakini hatuzungumzii shilingi milioni 50 kwenye mitaa. Kama sababu kwamba vijiji vina mamlaka ya kisheria, yawezekana mnatutofautisha hapo, mimi nina mitaa 50 na vijiji 20, sasa tunakwenda kuleta mgawanyiko katika jamii ambayo inaongozwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Kama sababu ni kwa sababu vijiji vina mamlaka ya kisheria, basi ni vizuri sasa na mitaa hii ipewe mamlaka hayo hayo na wenyewe wapewe mgawanyo huo sawa, unless otherwise tuzungumzie shilingi milioni 50 vijijini kwenye vijiji na mitaa, hapo tutaelewana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini shilingi milioni 50 hii, wenzangu wamejaribu kuchangia nami naomba nishauri, tujifunze katika yale mabilioni ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, tusije tukazalisha mgogoro ambao hatukuutarajia. Tumekwenda na nia njema ya kuwakomboa Watanzania, lakini namna ya kwenda kusimamia zoezi hili la shilingi milioni 50 linaweza likawa mwiba mchungu sana kwetu hapo kesho.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niombe, kama tutashindwa kuanzisha Community Bank basi ni vizuri tutumie NMB kwa maana iko kila halmashauri, tuweke dawati litakalo-deal na hii shilingi milioni 50 li-act kama Community Bank. Tukiweka dawati pale NMB tayari usimamizi wa fedha zile utakuwa uko salama. Sisi wanasiasa tuwe sehemu ya kuwahamasisha watu wetu kuanzisha vikundi na kwenda kufungua akaunti, lakini watakaotoa elimu hiyo wawe ni watu wanao-deal na fedha, jambo hili litakuwa limetuokoa na tunaweza kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie usajili wa pikipiki. Asilimia 50 ya Watanzania leo wanatumia usafiri wa pikipiki. Vijana wetu leo wote unaowaona wamejiajiri kwenye usafiri wa pikipiki. Wanaolipa kodi na wanaochangia matibabu leo ni hao hao waendesha boda boda lakini tumeongeza thamani ya usajili wake kutoka Sh. 45,000 mpaka Sh. 95,000. Nilitarajia kuona utapungua badala ya kuongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia Watanzania kupata ajira, wako ambao tayari wamejiajiri. Ni lazima tuwatengenezee mazingira bora ili waweze kuboresha sehemu zao hizo za kazi. Naomba jambo hili pia nalo tulitafakari kwa kina tuone ni namna gani tunaweza kuwasaidia hawa waendesha boda boda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na property tax. Nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa hatua madhubuti ambazo wameamua kuchukua kwenye property tax. Yawezekana tukalitazama kwamba halmashauri zetu sasa zinakwenda kufa kwa sababu sehemu hii maalum imechukuliwa na TRA, la hasha! Ule mpango ambao tumejiwekea, kwenye Halmashauri yetu katika zile bilioni tatu ambazo tutakusanya ndani ni pamoja na property tax.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyofahamu kwenye mpango huu kile kiasi ambacho tumekipanga TRA kwa maana Serikali itatuletea kama kilivyo, sasa silioni tatizo la property tax hapa, kwa sababu kama tumekubali kukusanya shilingi milioni 100 kwenye property tax Serikali inatuletea zile shilingi milioni 100, imetupunguzia mzigo. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kuipongeza kwa dhati Serikali kwa hatua hii ambayo wamechukua kwa kweli property tax itatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze sehemu nyingine, tumeweka kodi ya asilimia 10 kwenye importation ya karatasi. Awali wakati nachangia kwenye viwanda nilisema, Mufindi Paper Mills walipewa jukumu la kutengeneza karatasi na si mifuko, lakini wamekuwa wakisafirisha pulp na kupeleka Kenya badala yake karatasi huku kwetu inaingia bure. Leo Serikali imeweke asilimia 10, naipongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana.