Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii. Kwa kuwa siku ya leo ni siku yangu ya kwanza kuzungumza ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kuipata nafasi hii ya kuwawakilisha akina mama wanawake wa Mkoa wa Rukwa. Mwenyezi Mungu, nakushukuru sana.
Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, awali ya yote, napenda kuwakumbusha kuhusu hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Magufuli. Kwa kweli hotuba ile ilikuwa ni hotuba ambayo imesheheni kila upande wa Tanzania hii na kila Jimbo la Tanzania hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba niwakumbushe ndugu zangu wa Chama cha Mapinduzi kwamba, daima mtoto huwa anapiga madongo ya kila aina kwenye mti wenye matunda au mti wenye neema kwao. Mtoto hawezi kutupa madongo yoyote kwenye mti ambao hauna kitu. Kwa hiyo, haya madongo tunayoyapata kutoka upande wa pili, ni ashirio tosha kwamba mti wa Chama cha Mapinduzi na Serikali yake imefanya kazi. Hivyo sasa tunahitajika tukaze buti ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)
Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, katika hotuba ya Rais iliweza kugusa kila eneo ambalo kwa namna moja au nyingine limegusia hatua ambazo zinahitajika kufikiwa kwa wananchi wetu wa Tanzania. Sasa basi, kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshabainisha nini ambacho anachotakiwa kufanya kwa wananchi wa Tanzania ili waweze kupata uchumi wa kati; kwa hiyo, hatuna budi kumuunga mkono na kuifanya kazi hii ili iwe na maendeleo kwa wananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)
Ndugu zangu, leo tuna shughuli ya kuzungumzia juu ya Mpango wetu wa kazi ambayo tunahitajika kuifanya ndani ya mwaka 2016/2017. Mpango huu ni mzuri, ni Mpango ambao umeainisha nini ambacho Chama cha Mapinduzi imesema itafanya ndani ya miaka yake mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, Mpango huu umeona tatizo ni nini? Mbona maendeleo yetu hayakamiliki? Imebainika kwamba tatizo ni mapato. Sasa Serikali imeelekeza kukusanya mapato na hatimaye kuyarejesha mapato hayo kwa wananchi kwa maendeleo yao. Hilo ni jambo zuri na tunaomba tuliunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulizungumzia suala la afya. Tuliamua ndani ya Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010/2015 kuweka zahanati katika vijiji vyote na kazi hiyo wananchi wameweza kuunga mkono na kujenga hizo zahanati. Tatizo, zahanati hizi haziko katika ramani inayofahamika, kila kijiji wamejaribu kutengeneza zahanati kufuatana na nguvu ya mapato waliyokuwanayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake tumepata tatizo kubwa katika zahanati hizi kwa sababu eneo la kujifungulia limewekwa karibu na eneo la OPD, limewekwa karibu na eneo ambalo watu wa kawaida wanasubiri madaktari, ndipo palipo na chumba cha kuweka akina mama waende kujifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Waziri wa Wizara inayohusika, kazi ile ya kujifungua akina mama wana kazi pevu na bora iwe usiku kuliko ikiwa mchana. Mifano tunayo, zahanati ya Kisumba, kwa kweli ile ramani siyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawaomba katika Mpango wetu uainishe dhahiri nini watafanya katika suala zima la kuhakikisha wanatembelea ama wanaweka mpango mkakati wa kuhakikisha ramani zilizotengenezwa hivi sasa ziboreshwe ili akina mama tupate eneo la kuifadhiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, zahanati nyingi hazina vitanda vya kuzalia, hakuna vyumba vya kupumzikia, kwa maana ya kwamba hakuna vitanda vya kupumzikia. Tunaomba tupate vitanda hivyo. Siyo hilo tu ndani ya afya, zahanati zetu nyingi hazina umeme. Pamoja na kwamba kuna umeme wa REA, lakini bado hawajaunganisha kwenye zahanati zetu. Solar zilizopo zimeharibika na hakuna mtu tena wa kutengeneza zile solar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tuunganishwe na umeme wa REA, katika zahanati zetu zote. Siyo hilo tu, maji hakuna kwenye zahanati zetu. Tunaomba Mpango Mkakati wa kuhakikisha kwamba zahanati zetu zinapata huduma ili akina mama waweze kujihifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kuhusu suala la elimu. Tumeamua kuboresha elimu yetu na iwe elimu bora, lakini kuna maeneo ambayo tumeanza kuweka utaratibu wa watoto wetu waweze kujifunza teknolojia ya kisasa, kwa maana ya kwamba wamepeleka computers katika shule zetu za sekondari. Naomba mipango iwekwe ya kutosheleza mahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kushangaza, mfano Sekondari, darasa lina watoto 40, lakini kuna mikondo miwili; na mikondo hiyo miwili ni watoto 80, zinapelekwa computer 10 ambazo hazitoshelezi. Naomba tuliangalie hilo katika utaratibu. Mifano tunayo, pale Sumbawanga kuna shule za sekondari za Kizito na Mazu wana computer 10 na watoto wako 80, watafanya nini wakati wa mitihani yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni barabara. Maendeleo ya huduma za jamii katika Mikoa ya pembezoni tumekuwa nyuma. Mimi nasikitishwa sana ninaposikia wenzetu wenye barabara, wanaongezewa barabara za juu, wanaongezewa barabara ziwe sita, wapite barabara watu sita. Kwa kweli mimi nasikitishwa sana kwa suala hilo. Maadamu tumeamua kwanza tuunganishe Wilaya, tuunganishe Mikoa, zoezi hili ndugu zangu bado halijakamilika. Sasa kama halijakamilika, huyu aliyekamilika kuongezwa na katika Wilaya zake zimeunganika, Mikoa ya jirani ameunganika; nchi za jirani ameunganika; kwa nini aongezewe tena mradi wa barabara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tuelekeze Mkoa wa Rukwa. Hatujaungana na Katavi, hatujaungana na Kigoma wala na Tabora. Nawaomba ndugu zangu, huo Mpango uje ukionyesha mikakati, tunajitengeneza vipi kuhusu hizi barabara kuweza kuunganika? Vilevile Mkoa wa Rukwa, tumeungana na nchi ya Zambia barabara haijakamilika, nchi ya Zaire bado barabara haijakamilika. Tunaomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji, tuna mradi mkubwa sana pale Mkoa wa Rukwa karibia shilingi bilioni 30, lakini mradi ule bado haujakamilika, bado pale mjini watu wanahangaika na maji; bado vijijini vya jirani vinahangaika na maji, tuanomba Mpango unaokuja, huo mwezi wa tatu, uwe umekamilika ili na sisi tuweze kupata maji katika Mkoa wetu wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ardhi, tunaomba wataalam wa upimaji wa vijiji, hawapo wa kutosheleza na hata vifaa vyake havipo vya kutosheleza. Tunaomba tuhesabu ili tuweze kukamilisha.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja.