Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Naomba kwa namna ya pekee kabisa nikupe hongera sana Balozi Mahiga na Naibu wako. Na kweli tuwape hongera sana Mabalozi wetu wanaofanya kazi nchi za nje katika mazingira magumu. Wengine wanafanya kazi katika mazingira ambayo sio rafiki sana, hawana vitendea kazi, hawana staff wa kutosha, lakini wameendelea kufanya kazi kwa moyo mmoja, tunawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa naomba nianze na hili moja na Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba ulisikie hili. Lipo tatizo, nilikuwa nafikiri ni muhimu Wabunge wote wa Chama cha Mapinduzi, Wabunge wa Upinzani, tuwe na mafunzo maalum ya diplomasia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama ni ya siku mbili, siku tatu. Unajua Mheshimiwa Msigwa kuna mambo mengine hayasemwi hadharani. Kuna mambo mengine hayasemwi hadharani na kuna mambo mengine yanasemwa hadharani. Katika utamaduni wa diplomasia kuna mambo ambayo unaweza ukayasema tu hadharani na mengine yanazungumzwa ndani, under camera. Kwa hiyo, niombe, huko ndani nyuma kulikuwa na utamaduni huu kwamba Bunge linakaa, Balozi Mahiga na uzoefu wako unakuja na wenzako mnatupiga shule sawasawa, tunaelewa. Hata makatazo mnatueleza kwamba hiki usifanye na hiki ufanye. Maana haitoshi tu kwamba, wewe ni Mbunge unakwenda kukutana na Mabalozi, unakutana nao kuzungumza kitu gani? Kuna mambo mengine ambayo yanagusa uhai wa Taifa letu yana namna yake ya kuyazungumza na hata Bunge la mwaka 2005, Bunge la mwaka 2000 yote yalifanyika mafunzo yaliendeshwa na Wabunge walifundishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge kujifunza hakuishi, unaweza ukakaa unasema sema maneno hapa kwa sababu tu pengine hujui vizuri au unafikiri kila kitu lazima kisemwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Mheshimiwa Balozi nikurudishe kwenye kitabu chako ukurasa wa 118, nianze na kuzungumzia ujenzi wa Vituo vya Utoaji Huduma kwa Pamoja na pia nimeona imeambana na kipeperushi hiki hapa ambacho kinazungumzia Vituo vya Pamoja na Utoaji wa Huduma Mipakani. Naomba nikukumbushe tu, umeorodhesha vituo saba, lakini katika kipeperushi hiki umeongezea habari ya Vituo vya Kasumulu kule Songwe, Malawi na Mtambaswala na kwenye border ya Tanzania na Msumbiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba nikukumbushe kitu kimoja kwamba kuna vituo muhimu sana umevisahau. Kuna kituo muhimu sana cha forodha, kiko kwenye mpaka wetu wa Burundi, sehemu ya Manyovu na Burundi, ni border post ya muda mrefu sana na Serikali ya Tanzania kimkakati ilishajenga barabara ya lami kutoka bandari ya Kigoma mpaka kwenye border na wenzetu wamejenga barabara ya lami kuanzia border pale kwenda Bujumbura. Sasa kituo kile ni cha siku nyingi sana, sasa katika orodha hii sikioni. Nilikuwa nafikiri kama sio oversight basi mkiongeze na kiweze kupewa fedha kikarabatiwe vizuri. Mpaka wa Manyovu ni mpaka wa siku nyingi na ni mpaka wa kihistoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kingine cha forodha, ambacho umekisahau Mheshimiwa Waziri ni Kituo cha Forodha cha Mabamba na Burundi ni Kituo cha Forodha cha muda mrefu, kiko katika Wilaya ya Kibondo, hiyo Manyovu iko Wilaya ya Buhigwe. Nilikuwa naomba katika vituo vile ambavyo vinahitajiwa kufanyiwa ukarabati, Mheshimiwa Waziri ni vyema mkavitazama vituo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba, swali langu la pili Mheshimiwa Waziri, naomba Balozi unisaidie utakapokuwa unahitimisha, ni vigezo gani mnavitumia tunapoanzisha Ubalozi mpya? Ningependa kujua vigezo, ambavyo vinatumika kwa mfano, mimi mpaka leo sielewi ni kwa nini hatuna Ubalozi Seoul - Korea ya Kusini? (Makofi)
Mheshmiwa Mwenyekiti, nchi ya Burundi ina Ubalozi pale, nchi ya Zambia ina Ubalozi pale. Niliishi pale Seoul, kwa nini sisi Tanzania hatuna Ubalozi pale? Na mnajua wenzetu Wakorea hawa na katika diplomasia ya kiuchumi ndiyo wametujengea Daraja la Malagarasi.
Mheshmiwa Mwenyekiti, mtu akikuuliza moja ya vitu halisi vya kuonyesha ni kwamba Daraja la Mto Malagarasi na viunga vyake limejengwa kwa sababu ya ushirikiano ulioanzia Foreing Affairs kwa kweli na ni jitihada za Mheshimiwa Kikwete akiwa Waziri wa Foreign Affairs, ambaye alizungumza na wenzetu wale, hatimaye tukapa daraja lile. Sielewi kwa nini hatuna Ubalozi pale. Seoul - Korea ya Kusini mnajua ni nchi, ambayo imepiga hatua kubwa katika TEHAMA, katika ujenzi, katika kilimo, ni muhimu Mheshimiwa Waziri utakapohitimisha unieleze ni kwa nini hatuna ofisi pale Seoul?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, ambalo ningependa niliseme ni kuhusu Wakimbizi. Sisi Mkoa wa Kigoma tumepokea wakimbizi tangu uhuru, lakini bado wakimbizi wanaingia katika nchi zetu. Nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri kupitia ofisi yako pale ofisini kwako kwenye Foreign Services anzisheni kitengo cha wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kitengo cha wakimbizi kilichopo Mambo ya Ndani kina deal na usalama zaidi wa wakimbizi. Lakini sisi ambao tumeathirika na ujio wa wakimbizi, ambao Mabalozi wengi wanakuja Kigoma pale, Mabalozi wengi wanakuja Kasulu pale, Mabalozi wengi wanakwenda Kibondo pale hatuna namna ambayo tuna kiunganishi cha kwamba Mabalozi hawa sasa wanaokuja kuhudumia wakimbizi kuwe na jitihada maalum hasa ya kusaidia maeneo, ambayo yameathirika na ujio wa wakimbizi.
Mheshimiwa Balozi, mwezi Januari nilibahatika kukutana na Mabalozi sita waliokuja kutembelea kambi za wakimbizi, tumezungumza mengi sana nikahisi ni wakati sasa kwenye ofisi yako au ofisi yako muwe na uhusianao wa karibu kati ya Kitengo cha Wakimbizi Mambo ya Ndani na Kitengo cha Wakimbizi katika ofisi zako ambacho kitakuwa kina-raise masuala haya na hasa huduma kwa maeneo ambayo yameathirika na ujio wa wakimbizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nizungumzie suala la migogoro. Alisema ndugu yangu mmoja suala la Kongo, Mheshimiwa Balozi Mahiga, lazima tuilinde Kongo ya Mashariki, lazima tuilinde DRC kimkakati, wale ni partners wetu katika biashara. Kwa sababu tuna askari wetu kule ambao wanafanya kazi nzuri sana na nimwombe Waziri wa Ulinzi wale askari wasitoke Kongo wanatufanyia kazi nzuri sana, naomba tuilinde DRC kimkakati kama partners wetu wa kibiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naunga mkono kwamba wakati umefika pale Lubumbashi angalau tuwe na Ofisi ndogo ya Kibalozi kwa ajili ya kulinda maslahi yetu kama nchi. Ile ni nchi kubwa, nchi yenye utajiri mkubwa na kusema kweli tunaweza tukanufaika nayo kwa msingi huo, naomba uyazingatie hayo.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Nsanzugwanko.