Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kutoa shukrani kwa kuweza kunipatia nafasi hii. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunipatia afya njema na leo hii kuweza kusimama tena mbele ya Bunge lako Tukufu kuzungumza haya nitakayozungumza muda si mrefu. Nakutakia kila la kheri, Mwenyezi Mungu akupatie afya njema, akupatie wepesi kutokana na kazi nzito unayoifanya. Ujue ya kwamba tunakuombea na tunaendelea kukuombea upate afya hiyo mpaka mwisho wa Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia kuhusu bajeti ya Serikali. Nadhani wataalam tuliokuwa nao waliweza kujifunza katika kipindi kilichopita cha Awamu ya Nne na kufuatana na kasi ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa John Pombe Magufuli kuhitaji kuweka asilimia 40 ya fedha kwenye maendeleo ya wananchi wake basi itawekwa msingi madhubuti kuweza kumhakikishia Rais huyu kusimama kwa miguu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya nimeona kila Mbunge anayesimama hapa hayuko rafiki na bajeti hii, sijui hii Wizara haikuwa makini kufikiria na kuona hii kasi ya Mheshimiwa Rais itakwendaje ama itaanzaanza vipi katika kuhakikisha kwamba asilimia 40 inapatikana na maendeleo ya wananchi yanapatikana. Kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu Wizara hii imekwenda tofauti na Kamati ya Bajeti jinsi ilivyotoa mapendekezo yake, hii inaashiria wazi kwamba Wizara haikuona umuhimu wa Kamati hii kufanya kazi kwa niaba yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nastaajabu kwa nini ameileta bajeti hii kwetu na sisi Wabunge wenzetu walikataa mapendekezo yao? Kama kweli aliona thamani ya Wabunge kwamba lazima wapitishe bajeti hii basi angehakikisha mapendekezo ya Kamati ya Bajeti yanazingatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia suala la afya. Tunafahamu wazi kabisa kwamba afya ya mtoto mama ndiye anayesimamia siyo hilo tu mama ndiye anayesimamia hata malezi ya baba. Baba akiugua ndani ya nyumba mama ndiye mwajibikaji wa kuhakikisha afya ya baba inakuwa katika usalama na hali kadhalika ya mtoto. Sasa mama huyu tunamwekea mazingira ambayo siyo mazuri kwake, tunaendelea kumuongezea mzigo juu ya mzigo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia nini? Nazungumzia zahanati. Ukichukulia mfano wa Wilaya ya Sumbawanga Mjini kuna kata saba zinazozunguka mji ule lakini hazina kituo cha afya, zina zahanati lakini baadhi ya zahanati kwenye vijiji ni maboma ambayo bado hayajakamilika. Halafu Waziri wa Fedha anasema hakuna fedha ambazo zimewekwa kwa ajili ya kukamilisha zahanati hizi, kwa ajili ya kukamilisha vituo hivi ili huyu mwanamama awe na huduma ya afya karibu na yeye mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Wizara hii kwa sababu inafahamu wazi kanuni sijui sheria ya 106 inayosema kwamba sisi kama Bunge hatuwezi kubadilisha kifungu chochote labda ndiyo maana amekuwa na kichwa cha kusema kwamba hata wakisema hayawezi kubadilika kwa wakati huu. Sisi tunasema ni vyema Wizara ikawa na ushauri mzuri ama ikawa na maelekezo mazuri na kutukubali sisi Wabunge kama ndiyo tunaosimamia Serikali katika kuiongoza nchi hii. Waziri akienda kinyume na ukweli huo hatakuwa rafiki wa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, kama amekosea kipindi hiki tunaomba kipindi kinachokuja aje na fungu maalum la kuhakikisha miundombinu ya zahanati, miundombinu ya vituo vya afya inakamilika kwa maana ya theater ili akina mama waweze kufanyiwa upasuaji wakati wa zoezi la kuongeza idadi ya wananchi wa Tanzania hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu shilingi milioni 50 kwa vijiji ambapo shilingi bilioni 59 zimetengwa. Imesemwa hapa kwamba hazitasambazwa nchi nzima bali watachukua maeneo maalum kama pilot program. Mimi nasema Mheshimiwa Rais alisema ni kwa nchi nzima leo hii tukisema tunachukua baadhi ya mikoa iwe ndiyo shamba darasa la hizi shilingi milioni 50 ndani ya vijiji vyao tutakuwa hatujawatendea haki wengine. Ushauri wangu kama ni kutafuta mashamba darasa ya kuona hii shilingi milioni 50 itakwendaje basi ni vyema hizi shilingi bilioni 59 zigawanywe ili kila Jimbo waweze kupata vijiji viwili ama vijiji vitatu viwe ni pilot program katika maeneo hayo ili na wale ambao wanawazunguka waweze kujifunza nini makosa ya wenzao kuliko ukisema kwamba pilot program inakuwa Tanga mimi niko Rukwa wapi na wapi? Tunaomba tuweke kwa kila Jimbo ili tuweze kupata pilot area ya kujifunza sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la asilimia 10 halikuweza kutekelezeka kwa sababu ndani ya Kamati ya Bajeti ama Kamati ya Fedha ya Halmashauri hakuna anayelizungumzia wala hakuna anayelifuatilia wala hakuna mwenye uchungu nalo. Kwa nini? Ni kwa sababu Wabunge wa Viti Maalum ama Waheshimiwa Madiwani wa Viti Maalum kwenye ile Kamati hawamo na ndiyo wenye uchungu na vijana na akina mama wenzao. Naomba Wizara inayohusika isiwe na kigugumizi itoe tamko rasmi kwamba hawa Madiwani wa Viti Maalum na Waheshimiwa Wabunge waingie kwenye Kamati ya Fedha za Halmashauri wakazungumzie na kufuatilia asilimia yao 10. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya bajeti yetu tumesema Wizara ya Utalii ndiyo ambayo inaleta fedha za kutosha takribani asilimia 25 lakini mazingira yanayotengenezwa kwa huu utalii si rafiki. Badala ya kupata zaidi ya asilimia 25 ni dhahiri katika kipindi kifupi tutapata chini ya asilimia 25 na kwa maana hiyo uchumi wetu utaanguka. Nasema hivyo kwa sababu wenzetu wa Kenya katika bajeti ya mwaka 2016/2017 wametenga shilingi bilioni 90 sisi tumeweka shilingi bilioni 135 lakini si kwa utalii peke yake ni pamoja na Maliasili na Utalii. Kama wakigawana pasu hawa kila mmoja anapata shilingi bilioni 67.
Hii saa inasema uongo sasa. Naomba kuunga mkono hoja.