Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nami napenda kuipongeza Wizara hii ya Mambo Nchi za Nje kwa juhudi kubwa inayofanya pamoja na Mabalozi wetu walioko nchi za nje wanaoiwakilisha Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Balozi zetu zilizoko nchi za nje zinafanya kazi kubwa wakati fedha zinazopelekwa ni chache ukiachilia mbali kucheleweshwa kwa baadhi ya mahitaji yao. Pia Balozi zinafanya kazi kubwa kuwapokea Watanzania wanaopata matatizo wakiwa nje ya nchi mfano kama Oman, India, Marekani, Uingereza ambapo wengi wao huenda kwa sababu zao binafsi kama kutafuta ajira baadaye kutelekezwa na waajiri wao, wengine wanakwenda kwa matibabu wanaishiwa fedha na wanakimbilia kwenye Balozi zetu za Tanzania na Balozi zinafanya kila jitihada kuhakikisha wananchi hao wanarejea Tanzania. Napenda kuzipongeza sana Balozi zetu zilizoko nchi za nje kwa uvumilivu wao huu na upendo kwa Watanzania wenzao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri tumearifiwa kwamba Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki imehamia rasmi Zanzibar. Mimi napenda tu kusisitiza kwamba Kamisheni hii ipewe kipaumbele cha vitendea kazi ili iweze kufanya kazi zake vizuri. Kwa sababu kwa kutumia lugha yetu ya Kiswahili tutaongeza ajira kwa vijana wetu, pato la Taifa na tutaitangaza nchi yetu Tanzania duniani kote. Kwa hivyo, kuamua Kiswahili makao makuu yake kuwa ndani ya nchi yetu ya Tanzania ni fahari kwetu sote Watanzania katika umoja huu wa Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kuliongelea sasa hivi ni elimu juu ya fursa za kiuchumi na biashara katika masoko ya Afrika Mashariki. Wananchi wetu wa Tanzania wengi hawaelewi ni mbinu gani na njia gani za kufanya biashara katika masoko hayo ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kulizungumza hapa kwa mashirikiano ya pamoja kwa Wizara hii ya Mambo ya Nje na Wizara ya Mambo ya Ndani kuhakikisha wanadhibiti wasafiri Watanzania na abiria wengine wanaopitia Tanzania kupitia viwanja vyetu vya ndege kwa usafirishaji wa madawa ya kulevya. Tatizo hili linalipa aibu sana Taifa letu wanapokwenda nchi za nje tukaambiwa watu hawa wametokea Tanzania au ni raia wa Tanzania. Udhibiti ufanyike pale kwenye viwanja vyetu vya ndege, madawa haya ya kulevya yasitokee nchini kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba kwa Mabalozi wetu walioko nchi za nje watumie fursa hiyo kuitangaza Tazania na kutafuta mialiko mbalimbali kama matamasha ya kiutamaduni na biashara yanayokuweko katika nchi hizo wawalete Tanzania ili wananchi wetu waweze kufika huko. Hili nina ushahidi nalo kwa sababu mimi mwenyewe nilishawahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Utamaduni na Mambo ya Sanaa nilikuwa natafuta mwenyewe mialiko kwa viongozi na wasanii kutoka Zanzibar kwenda kuitangaza Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapofika katika baadhi ya Balozi na vikundi vyangu vya utamaduni hata wao wanakuwa hawaelewi kwamba kuna fursa za namna hiyo katika nchi zao. Kwa hiyo, ninachoomba wafanye utafiti na wawe wanatafuta mialiko kama hiyo ya maonesho mbalimbali ili Watanzania waweze kushiriki na kuitangaza nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.