Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Emmanuel Papian John

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nampongeza Waziri wa Fedha kwa hotuba nzuri ya bajeti ambayo inatupa matumaini ya huko tunakokwenda kwa kipindi hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ninalotaka kuzungumzia ni kushukuru kwa bajeti hii kwa sababu hii bajeti itafanya Watanzania waweze kufanya kazi. Naomba na kushauri sana wabane, watafute vyanzo vingine, hata hivi ni kidogo, pesa zishindikane kupatikana Watanzania waanze kufanya kazi kwa sababu hawataki kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona speech ya Rais akizungumza juu ya vijana ambao wanazunguka, watu hawataki kufanya kazi. Naomba Mheshimiwa Waziri Mpango na Naibu Waziri wajitahidi wahangaike kiasi kwamba pesa iwe ngumu ili watu waamke wanatafuta pesa badala ya kufikiri kuangalia runinga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna msamaha wa kodi kwenye makanisa na mashirika ambayo yanatakiwa kusamehewa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi hiki ni kipindi ambacho watu wengi wamekuwa wana diverge kodi wanakwepa kwa sababu siyo waaminifu kama zamani. Mtu anaweza kuleta kontena nne anasema hii tunajenga kanisa, ni tiles, ni vioo, kontena moja ndio inayofanya kazi, kontena tatu zinapigwa mtaani, halafu mkimaliza mnasema tunakwenda kusali kumbe kodi imepotea. Hiyo usibadilishe yeyote anayesema kodi ilipwe kwanza, watakapomaliza kulipa kodi atakaporejesha zile risiti kwamba hivi vitu vimetumika, basi wewe mrudishie kilicho chake lakini msamaha usiondoe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo na mifugo. Na-declare interest kwamba, mimi ni mkulima na ni mfugaji, si mdogo ni mkubwa. Naomba na kuzidi kusisitiza ili Watanzania watoke kwenye huu umaskini waende kufanya kazi, wafanye kazi kwa bidii watafute maisha ni lazima Benki ya Kilimo iongezewe mtaji ili tuweze kuondoa wale watu wanaosongana mijini, wanashinda vijana wenye vifua wanatembeza nguo za akinamama za elfu mbili mbili. Ili warudi vijijini ni lazima hii benki iweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la matrekta. Hebu tuingizieni matrekta ya kutosha watu wetu wakope waende mashambani maana hawatalima Dar es Salaam. Tusaidieni ruzuku za pembejeo, hakikisha kwamba tunainua mashamba yote ya kilimo ambayo yanaweza kuzalisha mbegu ili mbegu tunayo-import zaidi ya asilimia 80, zaidi ya bilioni kadhaa zinazotoka nje zibaki hapa ndani ili kuwe na creation ya employment na watu wao watafanya kazi mashambani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na kitengo cha kilimo-anga. Zamani tulikuwa na wataalam wazuri wa kilimo-anga ambao ma-pilot wetu ndio wa kwanza East Africa na Central kwa kuendesha ndege za kumwaga madawa, lakini leo hatuna pilots, hatuna ndege, na kesho kutwa mwezi wa tisa Kondoa inaomba chakula cha msaada. Naomba msikie hapa, tukirudi Bungeni Waziri wa chakula ataombwa chakula kupeleka Kondoa, ndege wamemaliza chakula. Niwaombe, kwenye bajeti yao wafikirie kununua ndege ya kilimo, wapelekeni vijana wetu wakasomee kuendesha ndege za kumwaga madawa Uingeza badala ya kukodi wataalam wa kuja kumwaga dawa hapa, huo ndio ushauri wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ATC. Tunanunua ndege tunapongeza kwa mpango huo ndege na zije Watanzania wafanye kazi na shirika lifanye kazi. Naomba kushauri tangazeni nafasi ya Chief Executive Officer wa ATC ambaye atasimamia. Atoke nje hatutaki ubabaishaji kwenye hili shirika tena. Madeni yote yanayodaiwa weka pembeni wataendelea kudaiana na Serikali, wataendelea kudai mishahara huko huko shirika lianze upya, akaunti mpya, CO mpya, watendaji wapya, tusonge mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Mazingira. Nchi ya Tanzania ni chafu sana. Niombe kushauri wametenga pesa kwa ajili ya kupanda miti milioni kadhaa nchi nzima. Kwa nini wasifikirie ni namna gani tunaweza kufuta mifuko ya plastic nchi nzima ili tuokoe kwanza udongo, tuokoe ardhi, tuondoe uchafu, tuokoe magonjwa, tuokoe uhai kabla ya kupanda miti? Maana hizi plastic bag zimesambaa na ni nyingi sana madhara yake ni makubwa hatuwezi kuyaona leo lakini ukiangalia nchi yetu kwa uchafu huu ni mara mia tutumie disposable paper ambayo inaweza kwisha na udongo wetu ukabaki salama, huo ndio ushauri wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, CAG tunaomba aongezewe pesa, ndilo jicho letu, ndilo jicho la Mheshimiwa Rais, ndilo jicho la Mheshimiwa Waziri Mkuu, ndilo jicho la Mheshimiwa Waziri wa Fedha; hiki kitengo kipewe pesa. Lakini naomba kushauri jambo, kumekuwa na mrundikano wa madeni; mara tunaangalia yalienda wapi, yakaenda wapi miaka kumi bado CAG anakagua haviishi vilipanda vilishuka. Hebu mshaurini CAG afute haya matakataka yaliyoliwa huko nyuma, maana yameliwa na Watanzania hawa hawa wamemaliza, ayafute ili hiki kitengo kiweze kufanya kazi vizuri na kwa ufanisi. Ni kwamba kipunguziwe mzigo wa ku-audit. Ana-audit miaka kumi ishirini iliyopita huku mbele vinaliwa, huku nyuma ameshindwa kuzuia sasa afanye nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu wafute hivi vitu, Mheshimiwa Waziri afute haya matakataka yote haya yaishe tuanze upya mafaili mapya, tukamatane kwa upya, CAG aweze kufanya kazi kwa ukaribu vinginevyo unamfanya ana-audit vitu wiki mbili tatu hawezi ku-cover nchi kumbe ana audit vitu vya 2013, 2012 huko, badala yake tungekuwa tunakwenda mbele ili aweze kukabiliana na uovu ambao umetokea kwa wakati huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo nataka kushauri, hawa auditors wa CAG wangeweza hata kukabiliana na watendaji wetu wahalifu kwa wakati. Sasa otherwise ni kwamba anapokwenda ku-audit anakuta mtumishi alihama aliiba, akapandishwa cheo, akaua zaidi badala ya kuokoa pale. Watu wakamatwe kwa wakati kwa sababu tunahitaji hawa watu tuweze kuwakamata kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TRA. Tunaomba isaidiwe watumishi wengi wa TRA wanapata vitisho kutokana na walipa kodi, kudai kodi siyo kazi rahisi wamefunga roho. Hawa watumishi wetu wa TRA wasaidieni ili waweze kulindwa na usalama wao, otherwise wanaweza kuyumbishwa na wafanyabiashara na viongozi wanasiasa watendaji, mwisho wa siku wakafanya uhalifu wa kuhujumu nchi bila wao kutaka. Naomba wasaidiwe maana wanakutana na shida nyingi na maamuzi mengine wanayafanya bila wao kutaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, watakapofanya hivyo itatusaidia sisi kujua na kukagua vitu vyetu ambavyo vyote vinawezekana na makusanyo mengi yatakuwa makubwa kiasi kwamba, tutakuwa tumeweza kukusanya kiasi ambacho sisi tulikuwa tunakitarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati. Kiteto tumepewa zahanati tatu, sasa wale Wamasai wangu wa kule porini naenda kilomita 150 watakutana lini na dawa? Simangilo zahanati moja watakutana lini na dawa, clinic watakutana nayo wapi, sasa Mheshimiwa Waziri tunaomba hili suala mliangalie…
Mheshimiwa Naibu Spika, muda umekwisha? Yesu wangu! Naunga mkono hoja.