Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Awamu ya Tano ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mungu kwa kunipa uhai na leo nachangia hoja kwa mara ya kwanza kwa hii bajeti ya Serikali mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais mwenyewe kwa kazi nzuri anazozifanya na juhudi anazozionesha kwa kunyanyua maisha ya Watanzania. Napenda nikupongeze wewe mwenyewe kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Philip Mpango na Naibu wake Mheshimiwa Ashatu kwa kazi nzuri wanazozifanya. Napenda niwaambie Wabunge wenzangu kwamba, Jimbo la Mheshimiwa Philip Mpango ni Tanzania nzima si kwamba Mheshimiwa Philip Mpango hana Jimbo, Jimbo lake ni mipaka ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwapongeze akinamama wenzangu, Wabunge wa Viti Maalum na niwaambie kwamba ninyi akinamama Wabunge wa Viti Maalum Majimbo yenu ni makubwa kuliko Wabunge wa Jimbo kwa sababu mipaka yenu ni mkoa mzima, kwa mfano wewe unatoka Mkoa wa Kigoma, ina maana wewe ni Mbunge wa Jimbo la Mkoa wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo napenda kuchangia bajeti hii ya Serikali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nianze kwenye elimu. Nashukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano imetenga pesa nzuri kuboresha elimu mpaka tunaweza kupata elimu bure ambayo itashughulikia vitabu bure mashuleni, chakula bure, gharama zote za mitihani zitakuwa zinashughulikiwa na Wizara ya Elimu. Napenda niipongeze sana Serikali kwa hilo. Hata hivyo, napenda kutoa angalizo kwa maneno machache kuhusu elimu ambayo wanafunzi wanaipata ndani ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara ya Elimu ingeangalia utaratibu wa kujenga shule za kindergarten kwenye shule zetu za primary ili watoto kabla hawajaingia darasa la kwanza waweze kujifundisha, kwa sababu unakuta uelewa wa mtoto Mtanzania ambaye ana miaka mitatu ni wa chini ukilinganisha na mtoto wa miaka mitatu wa kindergarten kutoka nchi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba shule zetu za primary zijengewe darasa kwa ajili ya kindergarten ili watoto wawe wanapita pale kindergarten kabla hawajaingia kwenye elimu ya primary school.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naomba kuchangia juu ya tatizo la wasichana wadogo wa umri wa miaka 15 mpaka 19, ambapo imeainishwa kwenye kitabu ukurasa wa 10 kwamba, kuna ongezeko, kutoka asilimia 23 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 27 mwaka 2015; ambapo watoto wenye umri mdogo wa miaka 15 mpaka 19 wamekuwa wakipata mimba za utotoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iliangalie hili suala kwa makini kwa sababu baada ya miaka mitano tutajikuta tuna watoto wengi sana, Serikali itakuwa na mzigo wa kuhudumia hawa watoto, pia Serikali inakuwa na mzigo wa kuwasomesha kwa sababu watoto wengi wa aina hii wanaishia mitaani na Serikali yenyewe na nchi yetu yenyewe kama tunavyojua hatuna nyumba nyingi za kulelea hawa watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo natoa ushauri kwamba, Serikali ingezifuatilia shule za sekondari ambazo zinajengwa, hasa shule za watu binafsi, iangalie kwamba, zile shule ziwe na mabweni ya kulala wasichana. Kwa sababu unakuta shule nyingine inajengwa haina mabweni, matokeo yake wasichana wanapanga kwenye nyumba za watu binafsi, hii inapelekea kupata matatizo ya upataji mimba za utotoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia napenda Serikali iangalie suala la kubadilisha sheria ili hawa watu ambao huwa wanakatisha masomo ya watoto waweze kupewa adhabu kali. Pia naomba Serikali ingeangalia suala la kurekebisha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ambayo inamruhusu mtoto kuolewa akiwa na umri wa miaka 15; kwa sababu vyote hivyo ni vitu ambavyo vinamfanya yule mtoto aone kwamba yuko tayari kuingia katika majukumu hayo kwa sababu hata sheria za nchi zinamruhusu kwa upande mmoja aolewe na miaka 15 na upande mwingine zinamwita mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali ijaribu kuzileta zile sheria zijadiliwe na wadau na kubadilishwa hasa sheria ya ndoa ya mwaka 1971, kwa sababu hatuwezi tukawa na sheria mbili ambazo zinakimbizana; sheria ya mtoto ya mwaka 2009 na sheria ya ndoa ya mwaka 1971. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba niende kwenye suala la Mkoa wangu wa Katavi. Katika Mkoa wangu wa Katavi tunayo matatizo kwa sababu mkoa ni mpya na Halmashauri nyingi ndiyo zinaanza kujengwa na Wilaya zile ambazo zimepitishwa kuwa Wilaya kwa mfano kama Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda hawajatengewa fedha kujenga zile ofisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba Serikali ijaribu kuangalia utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya kujenga ofisi za Halmashauri ili ziweze kujiendesha. Kwa sasa mkoa una Halmashauri mpya za Wilaya tatu. Awali mkoa ulikuwa na Halmashauri mbili na sasa hivi una Halmashauri tatu mpya ambazo hazina ofisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Katavi tunao wageni (waliokuwa wakimbizi) ambao sasa hivi ni Watanzania wenzetu, wako kule mishamo na Katumba. Wageni hawa walijengewa shule na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo zile shule hazitoshi kwa sababu wale tangu walipokuja wakiwa wakimbizi ni siku nyingi na kwamba sasa wameongezeka kwa idadi yao, hivyo, unakuta wengine wanasomea chini. Kwa hiyo naomba Serikali iangalie utaratibu wa kuangalia suala hilo na kuweza kuongeza shule kwenye Mkoa wangu wa Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la mitumba. Nchi yetu ya Tanzania hatujawa na viwanda vingi vya nguo, naomba hiyo mitumba iachwe kwa sababu ndiyo nguo ambazo zinatumika kule vijijini kwetu na nyingine zilizopo ni za ghali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie suala la kukatwa kodi kwa kiinua mgongo cha Wabunge. Naomba kuzungumzia hili suala kwa sababu Mbunge ndiye kiunganishi cha Serikali na wananchi. Mwananchi wa kawaida anapopata matatizo anampigia simu Mbunge, hawezi kumpigia simu Waziri wala hawezi kuipigia simu Serikali. Kwa hiyo, naomba suala hili liangaliwe kwa sababu mishahara yetu inakatwa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba suala la kiinua mgongo cha Mbunge lijaribu kuangaliwa ili ile kodi isikatwe kwa sababu Mbunge mshahara wake au kitu chake anachokipata si kitu ambacho anatumia peke yake, mshahara wake anatumia na watu wengi na kusaidia wananchi na yeye ndiyo kiunganishi cha Serikali pamoja na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwananchi anapomwomba Mbunge kitu chochote amsaidie, Mbunge kama hajamsaidia anachukulia kwamba, Serikali ndiyo haijamsaidia. Naomba suala hili liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwatetea watu wa bodaboda, kwamba kodi hiyo kutoka 45,000 kwenda 90,000 ni kubwa sana. Ukiangalia vijana wengi hawana kazi, wamemaliza shule na vijana wengi wanajihusisha na biashara ya bodaboda kuwapa tozo la sh. 90,000 kulipa kodi ni hela kwa kijana na unaweza kukuta ile bodaboda amekopeshwa anatakiwa arudishe zile pesa kwa mwenye bodaboda. Sasa si sawa kumwambia alipe 90,000 akasajili ile bodaboda, na pesa yenyewe amechukua kwa mkopo na hiyo pesa ni kubwa sana naomba tuangalie vyanzo vingine vya mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushauri; kwa mfano Mkoa wetu wa Katavi tunao utalii mzuri, tunaye twiga mweupe ambaye hapatikani mahali popote. Naomba Waziri wa utalii amtangaze huyo twiga ili watalii waje kumwangalia yule twiga kule na waweze kuleta mapato nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watalii wanakuja kuangalia vivutio vyetu vingi, lakini kama tutazidisha kodi watalii wanaweza wakakimbia wakaenda Kenya. Pia naomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ijaribu kuutangaza sana Mlima Kilimanjaro kwa sababu mara nyingi unakuta Mlima Kilimanjaro unatangazwa kwamba upo Kenya. Kwa hiyo, watalii wengi wanapokuja wanashuka Kenya na wanapakizwa kwenye mabasi kupitia Namanga kuja Tanzania...
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.