Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia tena siku ya leo. Naomba nianze kwa kutoa pongezi zangu za dhati kwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mpango na Naibu Waziri Mheshimiwa dada yangu Ashatu, kwa kuandaa na kuwasilisha bajeti hii elekezi kwa mwaka wa fedha 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ni ya kuungwa mkono kwa sababu kwa mara ya kwanza kabisa kama Waziri wa Fedha alivyosema asilimia 40 ya hii shilingi trilioni 29.53 inategemewa kujielekeza katika miradi ya maendeleo. Kama kweli bajeti hii itakwenda kama ilivyopangwa na kama kweli mipango na malengo tuliyoyaweka yatakwenda kama yalivyopangwa, basi Serikali hii ya Awamu ya Tano ina nafasi kubwa ya kubadilisha maisha ya Watanzania na kuwajengea tena imani ambapo tunatambua karibu watu milioni 10 wanaishi katika hali ya umaskini hususani wanawake, watoto na vijana wetu. Kwa hiyo, namuunga mkono sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niongelee suala la TRA, mimi binafsi naunga mkono TRA waende kwenye hizi Halmashauri zetu na kukusanya mapato haya. Naziomba Halmashauri za Mkoa wangu wa Iringa watoe ushirikiano wa kutosha na nina sababu zangu za msingi.
Moja, tunatambua kabisa Halmashauri zetu hazina watumishi na wataalam wa kutosha wa kuweza kukusanya mapato haya kwa wakati na kwa kiasi kinachotakiwa.
Pili, kama ripoti ya CAG inavyoonesha, kumekuwa na ubadhirifu mkubwa na ufisadi ambao unaendelea kwenye hizi Halmashauri zetu na tunajua miradi mikubwa ya maendeleo kama vile zahanati na maji inategemea sana kodi ambazo zinatoka ndani ya hii Halmashauri yetu. Kwa hiyo, kwa hili mimi namuunga mkono Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ombi, Serikali ihakikishe inapeleka hizi pesa kwenye hizi Halmashauri kwa wakati na kwa bajeti ambayo itakuwa imependekezwa na Kamati ya Bajeti kutoka kwenye hizi Halmashauri husika. Vilevile ningeomba hii Ofisi ya CAG ipewe pesa ya kutosha, kwa sababu hii ndiyo macho na masikio ya Serikali yetu, ndiyo itakayoweza kuhakikisha pesa hizi zilizotengwa zinakwenda kufanya yale malengo ambayo yamekusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niseme machache. Najua nia na lengo la Waziri ni zuri. Naomba nishauri machache ili tuweze kuiboresha hii bajeti yetu kwa sababu na mimi lengo na nia yangu ni kuhakikisha Watanzania wanaishi vizuri. Kwenye ukurasa wa 39 wa hotuba Waziri alikiri kabisa kuwa huduma za afya na maji bado ni changamoto na akaenda mbali zaidi akasema upatikanaji wa uhakika wa maji safi na salama bado ni changamoto hususani majumbani na viwandani. Naomba nimkumbushe alisahau eneo moja nyeti la hospitali kwani hospitali zetu nyingi bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tukubaliane na mapendekezo ya Kamati ya Bajeti, wao wameshauri tuongeze tozo ya Sh. 50 kwa kila lita ambayo itatusadia sisi kupata shilingi bilioni 250 na wakaenda mbali zaidi kusema shilingi bilioni 230 itakwenda kwenye miradi ya maji na shilingi bilioni 30 itakwenda kuboresha zahanati zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Waziri wa Afya hapa anasoma hotuba yake alieleza kabisa kuwa hali ya zahanati bado ni mbaya na vifo vya akinamama na watoto bado vinaendelea. Mwaka 2010 watu 454 walikuwa wanapoteza maisha wakati wa kujifungua, sasa hivi 2015 ni watu 398 bado wanaendelea kupoteza maisha. Sasa hili ni jambo la kusikitisha si jambo la kujivunia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri wakati nachangia kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii nilisema yafuatayo:-
Mkoa wa Iringa kuna hifadhi kubwa ya msitu wa Sao Hill. Serikali inapoteza takribani shilingi bilioni sita kwa mwaka na hii ni kuanzia mwaka 2007 na Mheshimiwa Cosato alilisemea hili pia. Kwa taarifa nilizopata jana, hawa wawekezaji wa RAI Group sasa hivi wanafanya lobbying Dar es Salaam kuhakikisha wanaendelea kulipa hiyo Sh.14,000 kwa cubic metre. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha ahakikishe hao watu wa RAI group wanalipa fair share sawa na Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna zahanati ziko katika hali mbaya, Wilaya yangu ya Kilolo hawana hata Hospitali ya Wilaya na wanahitaji shilingi bilioni 2.2 ili kuweza kukamilisha hospitali hii na nimesema tutapata shilingi bilioni sita kwa mwaka kutoka kwa hawa wawekezaji wa RAI group waweze kuchangia pato la Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wameweka imani kubwa kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano, wananchi wa Iringa wana matumaini makubwa sana kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano. Sasa kama tutaendelea kuwabeba hawa wawekezaji na kuwatwisha mzigo Watanzania wanyonge, wauza mitumba, waendesha bodaboda, tukawaacha hawa RAI Group waendelee kuvuna matunda ya nchi hii kweli itatusikitisha. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha afuatilie kuhakikisha hawa RAI Group wanalipa fair share. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.