Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mezani. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia napenda kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayofanya chini ya Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania wengi wana imani kubwa na Serikali hii ya Awamu ya Tano, lakini Watanzania wengi pia wana matumaini makubwa sana na bajeti ya kwanza ya Serikali hii ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikupongeze wewe pia kwa ujasiri ulionao. Nikuhakikishie kwamba Watanzania wote wanaona ni jinsi gani unavyokitendea haki Kiti hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika kuchangia hoja iliyopo mezani nikianza na sekta ya elimu. Kumekuwa na changamoto kubwa katika ugawaji wa fedha inayotengwa kwa ajili ya elimu. Mara nyingi tumekuwa tukiona kwamba fedha nyingi zimeelekezwa katika matumizi ya kawaida huku maendeleo ya elimu yakipata pesa ndogo na wakati tunajua kwamba maendeleo yamekuwa na changamoto kubwa na nyingi kama za ukosefu wa madawati, madarasa, vyoo, nyumba za Walimu, mabweni na maabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata tukirejea katika mwaka wa fedha wa 2015/2016, tunaona kwamba asilimia 84 ya fedha iliyotengwa kwa ajili ya elimu ilielekezwa katika matumizi ya kawaida huku asilimia 16 tu ikielekezwa katika fungu la maendeleo ambapo nusu yake ilielekezwa katika mikopo ya elimu ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii imeathiri sana elimu katika shule zetu za sekondari, primary lakini na vyuo vyetu vya VETA ambapo vimeshindwa hata kukidhi haja ya kuwa na teknolojia ya kisasa. Kwa mfano, mwanafunzi anayejifunza ushonaji katika Chuo cha VETA anatumia cherehani ya kawaida yaani ile ya kutumia miguu na mara nyingi wanafunzi hawa wamekuwa wakitamani kuajiriwa katika viwanda vikubwa let me say kama A to Z cha kule Arusha ambacho kina teknolojia ya kisasa na mashine zake ni za umeme. Ina maana tunawapa mzigo hawa wawekezaji kwa kuanza kuwa-train upya hawa wanafunzi kwa muda mrefu mpaka hapo watakapoanza kufikia ile quality ya ku-produce kile kinachohitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali katika ugawaji wa fungu la sekta katika mwaka wa fedha ujao itenge fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo ya elimu. Kwa kufanya hivi, maendeleo yetu yatasonge mbele, lakini pia tutapata nafasi kubwa ya kupata picha ya matumizi ya fedha ya maendeleo ya sekta ya elimu. Kama inawezekana hili fungu la mikopo ya elimu ya juu litolewe katika fungu la maendeleo lihamishiwe katika fungu la matumizi ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze katika kuchangia masuala yanayohusu Mkoa wangu wa Mwanza. Nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kututengea fedha kwa ajili ya meli mpya katika Ziwa Viktoria lakini nishukuru pia Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa daraja litakalounganisha Kigongo na Busisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea, napenda kutanguliza salamu zangu za masikitiko makubwa kwa Serikali juu ya Mkoa wa Mwanza kuwa mkoa unaoongoza kwa umaskini, kwa kweli ni suala la kushangaza sana na ukizingatia ripoti kutoka BOT inaonesha kwamba Mkoa wa Mwanza ni wa pili katika kuchangia mapato kwa Serikali. Je, hii inamaanisha kwamba Serikali haithamini watu wa Mkoa wa Mwanza? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda kwa kukutaarifu tu ni kwamba watu wa Mwanza ni watafutaji wazuri tu na wamekuwa wakijishughulisha na shughuli mbalimbali zikiwemo za kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji kule Sengerema na Misungwi, utalii pale Saa Nane Island, ukienda Magu utakutana na museum kubwa ya kabila la Wasukuma lakini ukienda Ukerewe pia utakutana na mawe yanayocheza. Nikuhakikishie kwamba shughuli zote hizi zimekuwa zikichangia mapato kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli Serikali ya Awamu ya Tano ina nia nzuri na Mkoa wa Mwanza, narudia kama kweli Serikali ya Awamu ya Tano ina nzuri na Mkoa wa Mwanza naiomba katika mwaka wa fedha ujao itenge fedha ya kutosha kwa ajili ya miradi ambayo tayari imekwishaainishwa ndani ya mkoa huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna miradi ambayo tayari ilikwishaanzishwa ila haijakamilika na mara nyingi tumekuwa tukipata majibu ya danadana. Naiomba Serikali iweze kuikamilisha miradi hii ili watu wa Mwanza waweze kunufaika na matunda ya michango yao katika pato la Taifa. Miradi hiyo ni kama ule wa maji wa Sengerema, Ukerewe, Misungwi na Magu pale Kisesa na Bujora na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kumekuwa na miradi mingine ya umeme ambayo bado haijakamilika mpaka hivi sasa. Ipo pia miradi ya barabara ambayo imekuwa ikiongelewa mara kwa mara kama mradi wa barabara ya kutoka Kamanga - Sengerema ambao pia upo ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi na mradi wa barabara kutoka Kisesa - Usagara na barabara nyingine nyingi ndani ya mkoa huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali imeweza kutoa maji Ziwa Viktoria ikayapeleka Shinyanga iweje leo mtuaminishe watu wa Mwanza kwamba Serikali imeshindwa kutoa maji Ziwa Viktoria kuyapeleka Sumve, Magu ama Sengerema, kwa kweli suala hili linatuweka katika hali ya sintofahamu. Serikali inaposema kwamba ina mradi wa maji vijijini imaanishe siyo tusikie kwamba miradi hii inapelekwa mijini kama ilivyokuwa huko nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina maji mengi sana, tukiachana na maji yaliyopo kwenye maziwa, mito na bahari yapo maji yanayotokana na mvua ambayo mara nyingi yamekuwa yakisababisha maafa ya mafuriko katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Napenda kutumia fursa hii kuishauri Serikali kuanza kufikiria kujikita katika miradi ya kuhifadhi maji katika mabwawa kwa ajili ya matumizi ya binadamu na matumizi mengine. Napenda kutumia fursa hii kuishauri Serikali kukubaliana na wazo la Kamati ya Bajeti la kuongeza Sh. 50 katika tozo ya mafuta ili tuweze kuiwezesha sekta hii ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta ya kilimo tunafahamu kwamba asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima na wengi wao wakiwa ni vijana na wanawake. Kwanza kabisa, napenda kuipongeza Serikali kwa dhamira yake ya kupunguza ama kuondoa kabisa ushuru mbalimbali katika mazao ya kilimo. Nimesoma hotuba iliyopo mezani inaonesha kwamba sekta ya kilimo imetengewa shilingi trilioni 1.56 ambayo ni sawasawa na asilimia 4.9 tu ya bajeti ya Serikali tukitoa deni la Taifa. Napenda kuishauri Serikali kuongeza fedha hii kwani haiendani na watu wanaotegemea kilimo. Kwa sababu Serikali…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.