Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba pia nitumie nafasi kukupongeza kwa namna ambavyo unaendesha Bunge letu na niwape pole wenzetu ambao wanasubiri siku ambapo utalegeza msimamo. Nadhani hii ndio namna bora ya watu kuheshimu taratibu na sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kuchangia kwa hoja ya Mkoa wa Mwanza, Geita na Kagera kuonekana ni mikoa maskini zaidi Tanzania. Mwanzo ni kweli na nilikuwa napata shida, na nilikuwa sielewi mantiki ya suala hili linatoka wapi? Lakini nimekuja kugundua sababu za msingi ni kama ambazo wenzangu wamezieleza. Yapo mazao na kazi za msingi ambazo zilikuwa zinafanya maeneo haya yaonekane maeneo ambayo uchumi wake uko juu, yanaenda yanakufa polepole.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukizungumzia Mkoa wa Mwanza na Mkoa wa Geita, ambao miaka yote tulikuwa tunajivunia pamba, sasa hivi pamba imekufa hakuna dalili kuna mkakati maalum wa Serikali wa kurudisha zao hili kwenye chati na ukiangalia trend yake ya uzalishaji kwa miaka mitano, mwaka jana ilikuwa even worse. (Makofi)
Kwa hiyo, nadhani kwamba, hatuna sababu kwa nini tusiwe maskini. Mkoa wa Kagera walikuwa kahawa inakosa soko, walikuwa na migomba, migomba inaugua, ndivyo ilivyo katika mikoa mingine mingine ya Mwanza na Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaanza msimu wa pamba, lakini nataka kukuambia mpaka leo bei haijulikani na wananchi wana pamba iko ndani na ni haya haya ambayo mwakani zikija takwimu hapa itaonekana mikoa hii ni maskini sana. Kwa hiyo, nilikuwa nasema, Serikali pamoja na kutoa takwimu hizi bado ina kazi ya kufanya ili kuhakikisha kwamba, ina-coordinate mazao haya na kazi hizi za wananchi ziweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiangalia katika Mkoa wa Geita, ambao una dhahabu katika kila Wilaya, haijulikani mpaka leo wale wachimbaji wenyewe wa dhahabu wanauza wapi? Wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu haijulikani wanauza wapi? Wanaojulikana ni wanunuzi wa dhahabu wakubwa wakubwa. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba uchumi huu mdogo katika level ya chini hauko coordinated, haujulikani. Lazima wananchi hawa waonekane ni maskini, lakini influx inayosababishwa na machimbo katika Mikoa ya Geita na Mwanza na wapi ni kubwa sana na watu wote hawa wako bize kwenye kazi za kiuchumi. Nilikuwa nadhani watu wa uchumi wanatakiwa wafanye kazi vizuri zaidi hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye pendekezo la kuondoa msamaha wa kodi kwenye bidhaa ambazo walikuwa wanauziwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Naweza nikaunga mkono suala hili, lakini naomba nitoe mapendekezo yangu kwamba bidhaa hizi zinaweza zikalipiwa kodi, lakini uwekwe utaratibu ambao utavifanya vyombo yetu vya ulinzi na usalama viwe na credit card wakati wa kufanya manunuzi. Kwa mfano kama askari hawa wataweza kwenda kwenye duka lolote bila kujali duka hili ni lile ambalo limetengwa, wakiwa na credit card au debit card na wakaweza kupata punguzo la kodi pale pale, mantiki ya maduka haya itaendelea kuwa ile ile na mantiki ya kuwapa huduma nyepesi wanajeshi watu itakuwa ile ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, unapoongeza mshahara au ukaongeza pesa kwenye mshahara wake haijulikani huyu mtu atanunua nini kwa mwezi, nina uhakika kwamba tutaendelea kufanya maisha ya vyombo hivi kuwa vigumu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na naomba nichangie pia kwenye suala la kufutwa kwa misamaha kwenye taasisi mbalimbali. Ni kweli kwamba, Serikali ilikuwa inapoteza karibu shilingi trilioni mbili kwenye kodi kwa sababu ya misamaha, lakini ninataka tu kutoa hoja hapa kwamba kama vyombo hivi vitalipa kodi, urasimu wa namna ya kurejeshewa kodi hii lazima Serikali ijipange vizuri. Kwa sababu nitapa wasiwasi namna wanavyokwenda kugagua na kujiridhisha kwamba, bidhaa hizi zilizoingizwa zimetumika kwa mujibu wa malengo yaliokusudiwa na matokeo yake tuta-demoralize hawa waliokuwa wanasaidia. Maana yake ni lazima tukubaliane nchi yetu mpaka leo, sehemu kubwa ya Hospitali zilizo kwenye Wilaya, sehemu kubwa ya taasisi ziliko hapa, shule pamoja na nini zinamilikuwa na taasisi mbalimbali. Kama watu hawa watakatishwa tamaa na wataacha tutakuwa tunarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kwa hiyo, lazima Serikali iangalie namna ya kulifanya hili ili lisije likatela usumbufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, yamefanyika marekebisho mbalimbali kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri, nampongeza sana Waziri kwa kuondoa baadhi ya tozo kero kwenye maeneo mbalimbali. Lakini nilitaka kusema bado mazingira ya kufanya biashara kwenye nchi yetu ni magumu sana. Nitoe mfano sehemu moja tu. Sehemu ya hoteli, mtu akiwa na hoteli leo pamoja na kupata leseni, pamoja na kupata tax clearance kutoka TRA itaanza kulipa OSHA, atalipa Fire, atalipa hotel levy, ana aina ya tozo pale karibu kumi, ambazo zote hizi zinafanya mzunguko wa pesa kwa wananchi kuwa mdogo. Sasa inaonekana Serikali inajiaanda tu kukamata pesa kila kona na kuzirudisha kwake.
Mheshmiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nadhani kwamba bado kuna haja ya kuangalia vizuri, kwenye hoteli hapo utakuna na mtu wa afya, utakutana na mtu wa TFDA, utakutana na kila aina ya ushuru na wote hawa ni vyanzo vya mapato, nilikuwa nadhani kuna haja nzuri ya kuliangalia vizuri upya hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kodi za majengo, naweza kusema kwamba nilikuwa naunga mkono watu wa Halmashauri waendelee kutoza hizi, lakini nitaunga mkono TRA iwapo Mheshimiwa Waziri, utatuambia ni kwa namna gani pesa zilizokadiriwa kwenye Halmashauri atahakikisha zinapatikana kama zilivyo kwenye bajeti, vinginevyo tutajikuta kwamba, wakishindwa kukusanya TRA madhara yakuwa makubwa sana kwenye Halmashauri zetu za Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu makato kwenye gratuity ya Mbunge; nilitaka tu nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, sisi Wabunge wa Bunge la Tanzania kwanza ni Wabunge tunaolipwa kidogo zaidi kuliko Mabunge yote Afrika Mashariki. Nataka nitoe takwimu hapa, ukichukua salary na allowance, Bunge la Kenya walipwa dola 11,000, Rwanda dola 9,000, Uganda dola 8,000, South Sudan dola 7,000, Burundi dola 6,000, Tanzania ni least pay dola 5,000, hii ni salary na allowance. Sasa atuambie baada ya kuingiza haya makato anakwenda kuboreha wapi ili tufanane na nchi zingine? Kama hilo halifanyiki nataka kumshawishi Mheshimiwa Waziri afikirie namna mpya ya kutanua hii tax base kwa sababu kinachomsumbua sasa ni kufikiri kwenye base ile ile wakati unaongeza projection. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na njia rahisi ya kutanua tax base, akumbuke kati mwaka 2007 na 2010, Serikali iliweka stimuli kwenye baadhi ya viwanda na mazao ili kuwa inalinda visife ili Serikali isipoteze walipa kodi. Sasa ushauri wangu hapa tunavyo viwanda vingi vimesimama, kama tunataka kuongeza kukusanya mapato tupeleke pesa huko viwanda vifufuke tuanze kukusanya kodi vinginevyo leo wataanza kukata kodi kwenye gratuity, kesho watakuja kwenye allowance, atakuja kwenye per diem baadaye pataisha pa kukata kodi wakati huo anaendelea kupanua projection. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninaomba pia suala la polisi ambao wamewekwa kwenye chanzo cha mapato. Unapo-commercial raise service ukawambia polisi wakae barabarani ukawapa malengo ya kukusanaya shilingi bilioni moja, maana yake unawambia wakamate sana watu barabarani na kwa tabia ya polisi hawa-negotiate na wateja tutaanza kupata migogoro mingi kwa sababu watajielekeza kwenye kufikia malengo ya kukusanya shilingi bilioni moja kwa mwezi. Nilikuwa nadhani hawa wangeachwa watoe huduma na inapotekea wanatoa faini iwe ni faini ya kawaida, lakini wanapowekwa kwenye kikapu cha kuanza kukusanya pesa na kwamba lazima walete shilingi bilioni fulani lazima tunatengeneza mgogoro mkubwa kati ya watumiaji wa barabara na poilisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na lingine ni kuhusu kodi kwenye withdraw mbalimbali M-pesa na benki. Nataka tu kufahamu kwamba Serikali imejiandaaje kuweka regulatory board ambayo ita-control sasa wasipandishe hovyo hovyo. Walizoea hizi pesa zote kuzichukua wao, sasa tumepeleka kodi pale matokeo yake wataongeza, tutajikuta watu wanaogopa kupeleka fedha benki.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nashukuru sana.