Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana lakini pia niungane na wenzangu kutoa pongezi kwako pamoja na Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha bajeti kuu ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo imani kubwa sana na utendaji wa kazi ambao unafanywa na Serikali yetu ya Awamu ya Tano, hivyo mambo mengi ambayo yamewasilisha katika bajeti yetu hii nimekuwa na imani nayo kubwa sana juu ya utekelezaji wake na hii ni kwa sababu yako mambo yaliahidiwa mwaka jana wakati wa kampeni na mwaka huu tumeshuhudia tayari yameshaanza kutekelezwa. Kwa hiyo, nitajielekeza zaidi kwenye kushauri yale mambo ya msingi ambayo lengo likae katika kuboresha ili Serikali yetu iweze kutoa huduma kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila Mbunge aliyesimama hapa katika Bunge hili amesimama kuzungumzia changamoto zilizoko katika majimbo yetu. Wengi tumezungumzia masuala ya maji, barabara, viwanda, lakini pia tumezungumzia suala la uboreshaji wa huduma. Hizi huduma zote hatuwezi kuzileta na Serikali yetu haiwezi kufanikiwa kama haiwezi kukusanya kodi, Serikali yetu lazima ikusanye kodi na hizi kodi zinakusanywa katika vyanzo mbalimbali. Sasa nimuunge mkono Mheshimiwa Waziri wetu kwa yale aliyotuletea ambayo yanaakisi na yana lengo la kutaka kuonesha namna gani ambavyo tumedhamiria kwenda kuwaletea wananchi wetu maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo ninaunga mkono kwanza katika eneo la kukata kodi kwa Wabunge, jambo hili lazima tulipe nguvu na sisi lazima tuwe mfano hata kama limekuja kwa wakati huu nafikiri katika hitimisho Mheshimiwa Waziri atakwenda kufafanua zaidi kwa nini amelileta kwenye bajeti hii wakati anajua suala hili la posho za Wabunge kwa maana ya kile kiinua mgongo kinaenda kupatikana ndani ya miaka mitano au minne ijayo.
Kwa hiyo, mimi ninaunga mkono katika hili na tutakuwa wa kwanza katika kuhakikisha Serikali yetu inatimiza malengo yake ya kuwatumikia wananchi kama ambavyo wafanyakazi wengine, wananchi wa kawaida na wao tunavyowahimiza kulipa kodi na sisi lazima tuonyeshe mfano katika hilo eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo ningependa nalo pia kulizungumzia ni eneo la ukataji wa tozo katika mazao ya biashara ahadi hii ilitolewa na Mheshimiwa Rais wakati anafanya kampeni, aliahidi mara atakapoingia madarakani ataondoa kodi au tozo zote ambazo ni kero. Kwa sisi watu wa Mikoa ya Kusini tunapongeza na naomba nitoe salamu za wananchi wa Jimbo la Nachingwea, wananchi wa Jimbo la Ruangwa jirani zetu pale kwa sababu ni wadau wakubwa wa zao la korosho wamefurahishwa sana na kitendo cha Serikali kuondoa tozo hizi tano ambazo zilikuwa ni tatizo na kwa kiasi kikubwa ziliwarudisha nyuma wakulima wa Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Kwa hiyo, sisi tunaunga mkono muhimu na ambacho tungependa kushauri ni namna bora na haraka kwa sababu sasa hivi tuko kwenye msimu basi waraka utoke mapema ili Vyama vyetu vya Msingi na Ushirika viweze sasa kupkea maagizo haya na tuanze kutekeleza wakati tunakusudia kwenda kuimarisha na kuwainua wananchi wetu kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo ningependa kulizungumzia ni eneo la shilingi milioni 50 kwa kila kijiji, hili ni jambo zuri na tayari tumeona kwenye bajeti kiasi cha pesa ambacho kimetengwa. Ushauri ambao ningependa kuutoa kwa Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha ni kwamba kwa Jimbo kama Nachingwea nina jumla ya vijiji 127 nikipiga hesabu kwa shilingi milioni 50 kwa vijiji hivi maana yake Nachingwea pekeyake tunaweza kupata zaidi ya shilingi bilioni sita karibu na milioni 300. Nachingwea imejaliwa kuwa na ardhi kubwa sana sijajua ni mfumo gani tunakwenda kuutumia ingawaje tayari tumeshaanza kuona suala la kuundwa kwa SACCOS mbalimbali bado nina mashaka namna ambavyo fedha hizi zitakavyokwenda kuwanufaisha Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa yale maeneo ambayo yamejaaliwa kuwa na rasilimali kama ardhi na wananchi wake wanautashi wa kushiriki kwenye kilimo nilifikiri Serikali ingefikiria mara mbili namna ya kuweza kuzigawanya fedha hizi ili ziweze kuleta tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ushauri huu narudia kwa mara ya pili kuutoa hata kama hauwezi kufanyiwa kazi. Nilikuwa nashauri kwa yale maeneo ambayo yana interest ya kilimo ni bora hizi pesa zikaletwa tukanunua matrekta. Kwa Wilaya yangu kwa idadi ya vijiji nilivyokutajia tukipata matrekta 127 sasa hivi Wilaya nzima matrekta hata kumi hayazidi, wananchi wakati huu wakuandaa mashamba wanapata shida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo pesa hii badala ya kupelekea vikundi tungepeleka katika vyama vyetu vya Ushirika au utaratibu mwingine wowote ili waweze kununua matrekta ambayo yatarahisisha wananchi kutibulisha maeneo yao kwa gharama nafuu na hivyo tunaweza kuongeza kipato kwa wazalishaji wa kilimo na pia tunaweza sasa kuongeza jitihada na kutimiza ndoto zetu katika lile lengo la kuwa na viwanda ambavyo kwa sehemu kubwa vinategemea malighafi kutoka kwenye eneo la kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ambalo ningependa kulizungumzia ni eneo la nishati, nimesoma kitabu cha mpango wa uchumi, nimeangalia kanda mbalimbali namna ambavyo zimejipanga katika kuboresha uchumi wa maeneo husika. Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Mtwara sasa hivi ndio unaongoza kwa kutoa gesi ile ya Songosongo lakini gesi ya Mnazi Bay, lakini kwa sehemu kubwa bado nimeangalia kanda za madini ambazo zimetajwa katika Taifa letu, katika kanda hizi kwa bahati mbaya sijaona kanda hata moja kutoka Mikoa ya Kusini wakati sasa hivi kuna gypsum inapatikana maeneo ya Lindi, kuna madini yanapatikana maeneo ya Nachingwea, kuna madini yanapatikana ukanda mzima wa gesi kwa maana ya pale Lindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado katika kanda hizi za Kitaifa bado Mikoa ya Lindi na Mtwara hajatambulika, ingawa kuna hii LNG plant ambayo nimeona nayo pia Serikali imeweka mkakati wa kwenda kuboresha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakati unakuja kutoa hitimisho tunaomba ufafanuzi wa kuona namna gani katika kuboresha uchumi wa Taifa letu watu wa Mikoa ya Lindi na Mtwara ni kwa kiasi gani wanakwenda kunufaika na rasilimali hii ambayo imekuwa inatoa huduma Tanzania nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo uchumi wetu hauwezi kwenda vizuri katika Mikoa ya Lindi na Mtwara kama hatuwezi kuboresha huduma ya nishati ya umeme. Bado tuna tatizo la umeme katika Mikoa yetu pamoja na kwamba gesi inatoka katika Mikoa hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Wizara ya Nishati tunampongeza Mheshimiwa Profesa Muhongo kwa jitihada anazozifanya, lakini tunaomba kupitia bajeti yetu hii basi vijiji vyetu viende kupata umeme wa uhakika lakini pia viende kuboresha viwanda ambavyo tumeshaanza kuwa navyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunacho kiwanda cha Dangote pale Mtwara lakini bado wakazi wa Mikoa ya Lindi naMtwara hawajanufaika kwa sehemu kubwa na kiwanda hiki kutokana na bei kuwa kubwa ya cement ambayo inazalishwa pale. Sasa bado wananchi wetu wako chini kiuchumi na hatuwezi kuwasaidia kama tunawauzia kwa bei kubwa wakati Dar es salaam na maeneo mengine wanapata kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumza hayo naomba niunge mkono hoja.