Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuchangia bajeti ya Wizara hii muhimu. Pamoja na raha sana zilizotolewa na Mheshimiwa aliyemaliza kuzungumza na mimi basi nizungumze machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuchangia kidogo tu kuhusiana na mikakati ya Serikali kuhusiana na masuala ambayo yamezungumzwa na wenzetu wa Kambi ya Upinzani. Nikubaliane na taarifa ya Kambi ya Upinzani ukurasa wa nane na tisa kwamba yapo mambo ya msingi katika mgodi wetu wa Nyamongo kwamba wananchi hawahitaji kunyanyaswa, kudhulumiwa na Serikali kufumbia macho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufafanua kidogo, nikubaliane na Waheshimiwa Wabunge kwamba zipo sababu za makusudi za Serikali yetu kuchukua hatua dhidi ya unyonyaji unaoweza kujitokeza kwa wananchi wetu. Nikubaliane kwa kusema tu kwamba, Serikali imechukua hatua madhubuti na niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wa Tarime, Mheshimiwa Heche pamoja na Mheshimiwa Matiko wameshirikiana sana na Serikali hii kuhakikisha kwamba migogoro ya North Mara inamalizika mara moja. Hivi karibuni Serikali yetu imechukua hatua ambazo pia ni shirikishi kwa kuwashirikisha viongozi wa vitongoji wa North Mara kadhalika kuwashirikisha Waheshimiwa Wabunge wanaotoka karibu na mgodi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu inawezekana taarifa ya Kambi ya Upinzani ingekuwa nzuri sana kama ingeweza kutambua juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuondoa matatizo ya Nyamongo kuliko kuacha kama ilivyo. Nitambue tu kwamba Mheshimiwa Heche pamoja na Waheshimiwa Wabunge wameshirikishwa sana kwenye utatuzi wa migogoro hiyo. Wananchi wa Mara wana masuala ya msingi sana, ni kweli kuna masuala ya mazingira, kuna masuala ya mashimo, kuna masuala ya ajira na kadhalika lakini Serikali haijayafumbia macho. Nataka Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wajue kwamba Serikali inachukua hatua madhubuti za kuondokana na migogoro ya North Mara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hiyo haitoshi niseme tu kwamba ile timu iliyoundwa na Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini ambayo kwa sasa bado inakamilisha taarifa zake hatua zitakazochukuliwa pia zitakuwa ni shirikishi. Zitashirikisha Waheshimiwa Wabunge, Madiwani pamoja na Wenyeviti wa Vitongoji husika wa North Mara. Kwa hiyo, nilitaka kuliweka vizuri hilo siyo kweli kwamba Serikali imeyafumbia macho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mgogoro wa Bismarck na mgodi wa Acacia. Ni vizuri tukatambua Sera ya Uwekezaji pamoja na Sera zote za Nishati, Madini na za Mazingira zinahamasisha sana uwekezaji wa ndani na nje. Kwa kutambua hilo, nikubaliane kwamba kampuni ya Bismarck ni ya wazalendo na miaka ya 96 ilipewa leseni ya kutafuta madini kule Mgusu, lakini mwaka 2012 yenyewe ikaamua kuachia leseni zile. Hii ni kwa sababu za kiteknolojia za uchimbaji na mambo mengine. Baadaye sasa maeneo yale yakaombwa kumilikishwa na kampuni ya Pangea Minerals ambayo ni subsidiary company ya Barrick ambapo sasa wanaita Acacia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme sasa na ni jambo la msingi sana Waheshimiwa Wabunge tukitambua kuwa Bismarck ambayo pia ni kampuni ya Watanzania waliamua tu kufanya makubaliano ya kwao kabisa kimkataba na kampuni ya Acacia. Baada ya kutofautiana wakaamua kupelekana kwenye mahakama za usuluhishi za nje. Nitake tu kukubaliana na Waheshimiwa na niwaombe kwamba inapotokea mazingira ya namna hiyo watuletee taarifa Serikalini ili Serikali iyafanyie kazi kwa ufasaha. Sasa hivi suala linalozungumzwa la Bismarck na kampuni ya Acacia wala halipo hapa, wamepelekana wao kwenye usuluhishi wa kimataifa nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungependa sana Waheshimiwa Wabunge tuleteeni taarifa lakini kwa sasa hivi kulizungumza suala hilo lipo kwenye mahakama ya usuluhishi tutakuwa tunaingilia mhimili mwingine. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niwaombe sana tuvute subira kwenye masuala haya mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nichangie kidogo kuhusu ajira. Mheshimiwa aliyemaliza kuzungumza wa upande wa pili amesema kwamba wananchi wanaachiwa mashimo, hakuna ajira na wanaajiriwa kwenye kazi ndogo ndogo. Nitoe mfano kwa kampuni ya North Mara, ajira kwa Watanzania ni 968 ambapo wageni ni 57. Kwenye mgodi wa Bulyanhulu Watanzania walioajiriwa ni 1,755 na wageni wapo 71. Mgodi wa GGM Watanzania walioajiriwa ni 1,568 na wageni 68.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia uwiano ule bado Watanzania tunapata ajira lakini nikubaliane tuna haja ya kuongeza zaidi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niseme tu kwamba michango ya wawekezaji wa nje nayo ni mikubwa na inachangia kwenye pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja hii. Ahsante sana.