Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi na ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ameniwezesha kusimama kwenye Bunge lako hili. Pia nishukuru kwa dhati Wizara hii ni Wizara ambayo mimi nimefanya kazi nikitumika katika Ofisi ya Taifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kwa hiyo, kufika kwangu hapa kwa moyo wa dhati naamini uko mchango mkubwa wa Wizara hii.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwamba Wizara hii inasimamia mafungu mengi na kama tulivyoona kwenye report hii kuna mambo mengi ambayo ameyaonyesha Mheshimiwa Waziri niwashukuru kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niende moja kwa moja kwenye kuchangia hoja hii. La kwanza nilitaka nijue tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Rais hapa aliahidi kwamba Sheria ya Manunuzi italetwa katika Bunge hili. Nilikuwa nikipitia report, sijaona kwamba tumejiandaa namna gani ili sheria hii ambayo ni mwiba inakuja kwenye Bunge hili ili tuweze kuipitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nilitaka nizungumze juu ya hizi idara chache tu ambazo ziko chini ya Wizara hii nikianza na hii ya Ofisi ya Msajili wa Hazina. Utaona kabisa kwamba inalo jukumu kubwa sana la kusimamia taasisi nyingi ambazo ziko chini yake na hizi taasisi tunategemea zikisimamiwa vizuri ili ziweze kutoa mchango mkubwa wa mapato katika Serikali. Niko kwenye Kamati ya Uwekezaji ya Mitaji ya Umma, utaona kabisa kwamba mashirika yaliyoko huko na taasisi ziko 215 lakini tunahitaji tuwe na watumishi wengi sasa utaona kabisa hata bajeti ta TR iko ndogo sana na bado tumeona hapa, tumesikia kutoka kwenye taarifa ya Kamati wamepata asilimia nane ya kilichokuwa kimebajetiwa kipindi kilichopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji kuangalia mambo mengi sana katika taasisi hizi ili ziweze kutoa mchango mkubwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali. Capital structure ya mashirika haya haiko vizuri, lakini utaona mashirika yaliyo mengi hata investment plan hayana, kwa hiyo, utaona tunahitaji watu wenye weledi tofauti katika ofisi ya TR ili iweze kuweka msukumo mzuri na mwisho wa safari tuone mchango mkubwa unakwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ukiangalia kwenye kiasi ambacho kitachangiwa na non-tax revenue bado kiasi hiki ni kidogo lakini ukienda kuangalia kwa undani kabisa nafasi ipo kama tutasimamia vizuri Mashirika haya naamini kwamba mchango mkubwa utakuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nilitaka nichangie tu kwenye hii Wizara, kwamba nilikuwa nafikiria Mheshimiwa Waziri atasema hii kada ya wahasibu. Kada ya wahasibu bado inatoa tu taarifa, msukumo haujawekwa vizuri nilikuwa nafikiria labda tungeweza kuzipandisha hadhi angalau ziwe katika hadhi ya Ukurugenzi ili waweze kutoa mchango mkubwa wa uchambuzi lakini pia kushiriki katika maamuzi kwenye Wizara. Kwa hiyo, utaona tumeendelea kuwa na unit, lakini umeona kabisa katika Wizara kuna fedha nyingi sana ambazo Wahasibu wanasimamia nilikuwa nafikiri Mheshimiwa Waziri alitazame. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine nilitaka nizungumze juu ya uandaaji wa hesabu. Serikali imefanya uamuzi mzuri utayarishaji wa hesabu kwa viwango hivi vya Kimataifa kwenye Accrual Basis, utaona sasa karibu kile kipindi cha mpito karibu kinakwisha, hatutakuja kuwa na hesabu nzuri. Tunahitaji tupate hesabu ambazo zitaonyesha ile National Wealth tuone majengo yanaonekana kwenye hesabu, jumuifu tuone madaraja gharama zake, tuone ardhi, tuone madeni na mali mbalimbali, utaona sasa tangu tulivyoingia kwenye mfumo huu ikifika mwaka 2017 itakuwa kile kipindi cha mpito kinaisha, tutategemea kuwa na hesabu ambazo zinaweza zisipate hati safi kama ilivyokuwa kwenye Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa liko jambo la kufanya Mheshimiwa Waziri, uliangalie hili, kikubwa zaidi kwenye kufanya uthamini wa mali utaona kwamba hata Kwenye Halmashauri za kwetu tunao ma-valuer lakini hawafanyi kazi ya kutathmini mali hizi za Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nafikiri nimshauri Mheshimiwa Waziri kwamba hili suala la kuthamini mali lichukuliwe kama ni National issue ili tuwe na frame work nzuri ya kuhakikisha kwamba tuna muda wa haraka kukamilisha uthamini wa mali ili hesabu zetu siku za usoni ziweze kuwa nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliombe kupitia Wizara yako Mheshimiwa Waziri, mafunzo ya IPSAS kwa sababu update zipo kila wakati, tuweke msukumo ili tuweze kuwa na hesabu nzuri ambazo zitatusaidia kufanya maamuzi mbalimbali tunahitaji kuwa na kuhasibu oil and gas, tunahitaji kuhasibu shares na investment, kwa hiyo kila wakati kuna update zinakuja nilikuwa najaribu kuangalia kwenye bajeti ninaona kwamba saa nyingine upande wa mafunzo bado kidogo tunahitaji tuweze kusukuma tuweze kuweka mafungu ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nilitaka nizungumze juu ya accountability (uwajibikaji). Nilikuwa najaribu kuzitazama hizi ofisi za Internal Auditor General lakini naangalia pia na ofisi ya CAG. Nilivyokuwa nikiangalia kule naona kwamba tutakuwa na shida kubwa kwa sababu pamoja na kuwa kulikuwa na utaratibu ule wa kupunguza matumizi kwenye OC lakini utakuja kuona kabisa kuna kazi hazitafanyika. Mheshimiwa Waziri alitazame hili, Internal Auditor General ofisi yake ikiwezeshwa, itamuwezesha CAG iwe nyepesi na saa nyingine hata gharama za ukaguzi zinaweza zikapungua lakini bado naona hapa msukumo upo mdogo, hivi kwa nini Mheshimiwa Waziri ofisi ya Internal Auditor General isipewe full vote ili uwajibikaji uweze kuongezeka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia bajeti ya CAG imepungua sana na ukija kuiangalia kwa undani nilikuwa naangalia kitabu Volume II, utaona kabisa kwamba hizi kaguzi kwenye Serikali za Mitaa hazitafanyika Mheshimiwa Waziri hebu litazame kwa sababu utaona kwamba imetengewa kwenye ule upande tu wa kwenda kutembelea Halmashauri, kwa mfano, ziko shilingi milioni 332 kwenye kile kifungu ukiangalia. Sasa hii ni wastani tu labda wa mtu mmoja siku 20 kila Halmashauri ataenda kufanya kazi haitawezekana, kwa hiyo utaona kabisa kwamba hii funding iliyokuwepo kwenye ofisi hii Mheshimiwa Waziri itazame vizuri lakini vinginevyo hatutategemea kuwa na report nyingi kama ulivyozionyesha kwenye report hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna report nyingi sana mwaka huu tumezipokea, kwa hiyo tutegemee siku za usoni hatutakuwa na report za ukaguzi nyingi kama ilivyokuwa kwa sababu hali iliyopo hapa siyo nzuri. Utaona kabisa sehemu ambayo ilikuwa imetengewa kwa mwaka uliotangulia shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya ukaguzi wa Wizara, ziko shilingi milioni 280, sasa hii inatuonyesha nini? Inaonyesha kwamba hii kazi ya ukaguzi haijapewa msukumo wa kutosha ili kuhakikisha kwamba tunapata report lakini mwisho wa safari tunaweza kufanya maamuzi mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka pia nimalizie kwa kutoa ushauri tu kwamba kama tulivyosikia kwenye report ya Kamati pia kwamba kiasi ambacho kilikuwa kimetengewa kwenye bajeti ni kiasi kidogo, kwa hiyo, wakati msukumo mkubwa unakwenda kufanya makusanyo ya kutosha basi tuhakikishe kwamba kiasi ambacho kinatengwa kwenye Bunge lako hili Tukufu kinapelekwa na kwa wakati ili kama kiasi chote kitatolewa basi itakuwa ni wakati mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo kuweza kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati huo huo tuendelee kuangalia maeneo mengine ambayo yataweza kuongeza mapato ya Serikali na hasa hasa hii non-tax revenue yako maeneo mengi ambayo tukiweza kuweka msukumo mkubwa tutaweza kuona kwamba tunapata fedha za kutosha na mwisho wa safari utaona kwamba angalau hata ule mtiririko wa fedha kwenda kwenye Halmashauri utakuwa unakwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusisitiza tena suala la asset valuation ni suala muhimu sana ili national accounts ziweze kuficha vizuri ili mali zetu kwenye Halmashauri zetu ziweze kuonekana vizuri, lakini pia hati safi ziweze kuongezeka. Utakuja kuona kwamba kwenye Halmashauri zetu kwa mwaka huu uliokwisha saa nyingine tunaweza tusiwe tumefanya vizuri sana lakini kutokana na hili tatizo kubwa la asset evaluation imekuwa ni tatizo kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimia Naibu Spika nashukuru sana kwa nafasi hii naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.