Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Godbless Jonathan Lema

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza kabisa na mimi namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba hii ni awamu yangu ya pili kuwa ndani ya Bunge hili na ninawashukuru sana wananchi wa Arusha, kwa sasa nina Madiwani 34 na Chama cha Mapinduzi kina Diwani mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili niwashangae wenzangu wapinzani wanapowalaumu sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, sijui wanategemea nini? Mimi sijawahi kutegemea kitu bora kutoka huko upande huo.
Kwa hiyo, ninavyoona wanatarajia kitu bora kutoka upande huo, nawashangaa. Tutakaa tutaongea ili badala ya kuwalaumu sana, waanze kuwaombea, kwa sababu lawama ikizidi inakuwa laana. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoongelea maendeleo ya nchi ni lazima uongelee stability ya nchi. Suala la Zanzibar mnafanya nalo mzaha. Aliongea Mheshimiwa Mbunge mmoja kutoka Chama cha CUF na akasema kwamba demokrasia inapokandamizwa na watu wanaposhuhudia uonevu, wakaona hawawezi kujitetea, ugaidi na ujasusi utazaliwa katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uliomba na mlimpiga miongozo mingi sana, lakini maneno haya alisema Mandela wakati anakwenda jela. Alisema mtu mnyonge anapozalilishwa na kuteswa, hafundishwi uoga, anafundishwa njia ya kutafuta utetezi. Makundi mengi ya ugaidi duniani ukisoma historia, mwende mkasome, yametokana na ukandamizaji uliofanywa na Serikali zilizoko madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnafanya mzaha na Zanzibar, mtashinda uchaguzi, mtafanya uchaguzi bila uwepo wa vyama vingine, mtapeleka polisi kutoka Bara, mnaweza mkaazima polisi na Kongo, lakini mtakuwa mmeshinda uchaguzi na mtakuwa mmeharibu the next generation ya Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, anayetakiwa kuongoza Zanzibar aliyeshinda uchaguzi siyo Msudani, ni Mtanzania na ameshafanya kazi kubwa katika Taifa hili na ni Makamu Kwanza wa Rais wa Taifa hili, hamtaki kumpa nchi kwa sababu mna bunduki, mna majeshi na mnaweza mkawazuia watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliambiwa miaka ya nyuma iliyopita huko na nilisema hapa Bungeni; unaweza ukazini kwa siri, lakini huwezi kuugua UKIMWI kwa siri. Hiki mnachokifanya Zanzibar kitaleta madhara Tanzania Bara huku. Uchaguzi ulikuwa halali na Rais akapatikana. Mnafikiri kumnyang’anya Maalim Seif ushindi wake ni kutunza Muungano, mnachokifanya sasa, ndio mnabomoa Muungano. Hakuna Jeshi lenye nguvu ya kuzuia umma uliochukia kwenye nafsi. Watu wataanza kutafuta mabomu, kutengeneza mabomu, wataanza kufikiria kujilipua. Taifa hili litakuwa mahali pabaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyoongea, Wazungu ambao ni wafadhili wakubwa wa Taifa hili, watalii ambao wanaingia katika Taifa hili, wakizuia watalii kuingia Zanzibar, Arusha itaathirika, Serengeti itaathirika, mtaua uchumi wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Zanzibar ni suala la msingi sana na tunapojadili Mpango wa Taifa, stability ya Taifa hili ni muhimu kuliko Mpango wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa juzi mmezima matangazo ya TBC1 na mna mkakati wa kuzima matangazo mengine; mtafanikiwa, mko wengi sana! Mtafanikiwa kila dhambi, lakini mshahara wa dhambi ni mauti. Kila dhambi mnayoipanga mtafanikiwa, lakini mshahara wake ni mauti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashauri Waheshimiwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi; tunapotengeza Sheria ndani ya Bunge, tunapo-set precedent za nchi yetu ndani ya Bunge, leo nyie ni Mawaziri, watoto wenu hawatakuwa Mawaziri. Leo ninyi mna ndugu ma-IGP, watoto wenu hawatakuwa ma-IGP. Mheshimiwa Mama Mary Nagu alikuwa ni Waziri leo anauliza maswali ya nyongeza. Mtoto wake huko mtaani atakuwa wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnapotaka kutengeneza Taifa lenye misingi bora, ni vyema ninyi Wabunge mliopo leo, mkajua nchi hii ina kesho, ambapo hamtakuwa na influence. Shangazi zenu hawana influence mlizonazo, wengine hapa mlitokea kwenye matembe, mkaenda university mmekuwa Wabunge. Tunapokaa Bungeni kuongelea Taifa hili, tunaongelea ndugu zetu, jamaa zetu ambao hawana influence tuliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mnazuia matangazo live! Wananchi wanapoona hawatetewi, watatafuta utetezi! Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania linapokuwa live… (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Godbles Lema, umejenga hoja yako, sasa twende kwenye Mpango usaidie nchi. (Kicheko)
MHE. GODBLESS J. LEMA: Huu ndiyo Mpango. Tulia! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuongoea mpango bila kuongea stability ya nchi. Tulia Mzee, tulia!
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmezima matangazo hapa ya TBC1, leo wananchi nje hawajui kinachoendelea humu ndani. Ninyi mnafikiri tukiwasema sana nyie, mnafikiri chama chetu ama vyama vya upinzani vinajenga umaarufu, lakini kimsingi kabisa, vyama vingi vimeleta amani katika Taifa hili, kwa sababu ni alternative ya peace. Wananchi wanapoona tunasuguana ndani ya Bunge, wanakuwa na uhakika wa kesho, wanajua wana watetezi na Serikali ya tender.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mmeondoa matangazo, mnafikiri mko salama? Mmeondoa maangazo tukisema tusisike, mnaweza mkafanya kila kitu. Yesu alisema, watu hawa wasipopiga kelele, mawe haya yataimba. (Makofi)
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huko tunakoelekea watu hawataongea tena, hiki mnachokifanya hamtakifanya tena! Wakishindwa kuandamana, zitaanza assassination; wakishindwa kuandamana, nyumba zitaanza kuchomwa moto. Haki itatafutwa kwa gharama yoyote ile! (Kicheko/Makofi)
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashauri sana, mkikaa humu ndani, nawe ukikaa hapo juu, unajiona kama ni mdogo wake Mungu, mnakandamiza demokrasia, mnaleta polisi humu ndani, mnadhalilisha watu wanaodai haki! Ipo siku itafika! (Makofi)
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumekuwa ni alternative ya amani. Wanachama wenu wakichukia, wanakuja kwetu. Siku wakichukia wakaona huku hakuna msaada, wataenda porini. Vijana wenu wakichukia… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)