Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Fedha. Kwa dhati kabisa nakupongeza kwa umahiri na uhodari wako kwa jinsi unavyoliongoza Bunge hili na hivyo ndivyo tunavyotegemea, hutishwi wala hubabaishwi. Mimi ikiwezekana nataka ukae asubuhi na jioni uoneshe kama wewe uko fit kweli kweli. Maana hapa tuko katika sehemu ya kutunga sheria na kuondolea wananchi dhiki zao waliotutuma halafu tunakuja kufanya michezo ya kuigiza hapa kuingia na kutoka kama biharusi aliyekuwa hana kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo niseme kwanza naunga mkono hotuba hii ya Waziri wa Fedha kwa asilimia mia moja. Naamini kwa kupitisha bajeti hii basi yale mambo yote yaliyokuwa yanapata utatanishi au ugumu kidogo chini ya Mheshimiwa Dkt. Mpango yatakwenda sawa kwa sababu ni mchumi mahiri na anaweza kuongoza Wizara hii na naamini atafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme katika kusimamia uchumi wa nchi yetu hii basi ni lazima uchumi huu uwe na udhibiti mkubwa, tutengeneze mikakati ya kudhibiti uchumi wetu. Kwa mfano, kwenye nchi hii sasa hivi mtu anatumia currency yoyote anayotaka na kwa sehemu yoyote anayotaka, hapa udhibiti unaonekana umekuwa hafifu. Unaenda sehemu saa nyingine unaambiwa ulipe kwa dola na wewe Mtanzania uko hapa, kwa nini? Kwa nini kule tunakokwenda kuwakilisha ukitaka kununua chochote kama kule South Africa, hata kama unayo hiyo dola au Euro unatakiwa ukanunue kwa pesa za kule ambazo ni rand. Sasa na sisi tuudhibiti uchumi wetu, Wizara ya Fedha ifanye kazi hiyo, shughuli ya kudhibiti currency yetu ifanywe kwa bidii zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango ya maendeleo inasema kwamba uchumi wetu kama sikosei umekua kwa 7% lakini ni kwa kiasi gani mtu wa kawaida anaweza kupata reflection hiyo? Unamfaidia vipi au mtu wa kawaida anaonekana vipi hali yake kunyanyuka kiuchumi? Kwa sababu haya maelezo tunayopewa hapa ni ya kisomi zaidi lakini tunataka aje chini hata yule mtu wa chini ajue anafaidika nini na ukuaji wa uchumi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nalotaka kuzungumzia ni hili la ukusanyaji wa kodi. Tunapongeza hatua zilizofikiwa za kuweka mashine za electronic sehemu nyingi lakini bado kuna uvujaji katika ukusanyaji huo, hii efficiency iko kwa kiasi gani? Kwa mfano, inawezekana na imeshatokea unakamatwa na traffic njiani anakwambia mashine ya kutolea risiti haifanyi kazi, sasa unamlipa nani au ile pesa ukiitoa inakwenda kwa nani? Hapa inaonekana ni vema udhibiti uzidishwe pamoja na kwamba tunakuwa na digital lakini udhibiti kwenye hivi vifaa vya kukusanyia kodi uwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la kukuza sekta binafsi. Sekta binafsi tumeambiwa inachangia uchumi kwa kiasi kikubwa na tunaunga mkono, jambo hili ni zuri. Hapa hapa inaonekana wadau wazalendo ambao wanashiriki kwenye hii sekta binafsi wanapata vikwazo kwa sababu wageni wanaleta bidhaa zao japokuwa hafifu, sisemi kama zote lakini nyingi ni hafifu, kwa bei ndogo ambayo wanaiuza hapa; mzawa na mwekezaji wa sekta binafsi anashindwa ku-compete. Hii binafsi na holela sana haifai, uwepo udhibiti wa bidhaa na tuwaunge mkono kweli kweli hawa wawekezaji wa binafsi ili waweze kushamiri. Kwa sababu nchi hii itajengwa na wenyewe wazawa, hao wengine wanakuja kuchuma kisha wanaenda zao. Itakuwa kama hii hadithi ya kudai mjusi, mjusi kachukuliwa tunadai hapa kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, naamini bado kuna kazi kubwa ambayo inatakiwa ifanywe na hii Wizara yetu ya Fedha na ninaamini itawezekana. Sina maneno zaidi kwa sababu mimi si mtaalamu wa fedha lakini kidogo mwanga ninao na naamini kwa kupitia Waziri wetu huyu kazi kubwa sana itafanyika. Nawapongeza wote na naunga mkono hoja.