Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge katika kuchangia hoja iliyo mbele yetu. Nianze kwa kusema naiunga mkono hoja hii asilimia mia moja lakini mniwie radhi kwa sauti yangu kidogo leo haijakaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili na mimi niseme, haya yanayoendelea pamoja na kwamba ni michezo ya kisiasa lakini isitukwaze. Sisi kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni za Bunge, akidi ya maamuzi tunayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kama kuna kitu Mbunge amekereka kanuni zina utaratibu. Mimi nawasihi wenzangu hawa tutumie Kanuni zetu, huo ndiyo utaratibu wa Kibunge na siyo kwenda kufanya vikao kantini na maeneo mengine. Mimi siko nyuma yako, bali niko bega kwa bega na wewe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Deni la Taifa, nimesikiasikia hata kwenye hotuba ya wenzetu wanalisemea hili, ndiyo linakua lakini Tanzania ya leo siyo ile ya mwaka 1960, 1970, 1980. Taifa hili linakua na mahitaji yake yanazidi kuwa makubwa na lazima Serikali kupitia bajeti yake iweze kuwahudumia wananchi katika sura hii. Hoja siyo deni la nchi hii kukua, hoja ni kwamba tunapochukua mikopo hii iwe ni mkopo wa muda wa kati au muda mrefu tunazielekeza wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika,tukizielekeza kwenye consumption ndiyo inakuwa tatizo, lakini tukizielekeza katika maeneo ya uzalishaji yanayotujengea uwezo ya uchumi wetu kukua kwa haraka deni letu litaendelea kuwa himilivu. Tulielewe hilo lakini kusema kwamba tunagawanya deni hilo kwa population haiendi hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa mkakati wetu wa kusimamia Deni la Taifa na Sheria yetu ya Mikopo, Dhamana na Misaada labda Waziri angeweza kutusaidia tu tukajua huwa tunafanya tathmini ya Deni la Taifa baada ya muda gani maana ni vizuri tukajua deni la kipindi cha muda wa kati au muda mrefu. Pia vile viashiria ambavyo vinatumika, maana ukichukua kwa mfano thamani ya sasa ya deni la Taifa uwiano wake na Pato la Taifa ni asilimia ngapi. Maana nadhani haya ndiyo yanapaswa sisi kama Wabunge Serikali iwe wazi ili kupunguza haya maneno. Unapolinganisha ukomo, ule ukomo ukisema ni asilimia 50 msingi wake ni nini au unaposema deni letu la Taifa kwa sasa thamani ni hii lakini ukilipima kwa mauzo yetu ya nje ya bidhaa zetu na huduma ni asilimia ngapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ndiyo masuala ya msingi. Nadhani Waziri wa Fedha anapokuja kuhitimisha atusaidie katika kuyasema haya ili nchi na Wabunge tuweze kulipata hili suala vizuri. Naamini deni hili linahimilika na tutaendelea kuwa nalo na tutaendelea kukopa lakini tukope kwa misingi ambayo inajenga Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili amelisema kwa sura tofauti Mheshimiwa Janet Mbene, nataka niulize tu tumekuwa na hili zoezi la nchi yetu kufanyiwa tathmini ili iweze kukopesheka nje, ile sovereign rating imesemwa sana humu. Mara ya mwisho nakumbuka katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014 Serikali ilisema wako advanced sana lakini sasa hivi hatusikii tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna faida zake kwenda route hiyo kwa sababu ndiyo unapata access kwa mikopo from masoko ya kimataifa ya masharti nafuu lakini pia na makampuni ya Kitanzania yanaweza pia na yenyewe kupata mitaji kutoka kwenye masoko ya Kimataifa. Sasa tungependa tuelezwe ni nini kimetukwamisha tena tunarudi nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni hili la Public Private Partnership. Kusema kweli visingizio vimekuwa vingi. Naiomba Serikali ile miradi 125, maana mwanzoni tuliambiwa sheria haijakaa vizuri, ni kweli maana mtu anakuja hapa na pesa zake umuambie afuate Sheria ya Manunuzi kulikuwa na mgongano, tukasema tuunyooshe na Bunge likafanya kazi yake. Wakasema kuna centers nyingi sana za maamuzi na kadhalika tukanyoosha sheria. Wakasema sasa imeleta miradi 125 inafanyiwa uchambuzi ili kuona kama inakidhi kuingia katika mfumo huo mpaka leo hatuoni kinachoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu unachochea uwekezaji lakini pia unapunguza mzigo wa Serikali kwenye bajeti ili tuelekeze nguvu katika maeneo ya afya na maji lakini barabara, miundombinu ya reli, bandari na kadhalika tunashirikiana na private sector kwa misingi tuliyojiwekea na hili mimi nasema linawezekana na linafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la nne limesemwa ni Benki ya Kilimo, inatia huruma sana kwa ahadi ya Serikali ya muda mrefu kutotekelezeka na mimi nasema there is more than one way of skinning a cat. Benki ya Rasilimali ya Tanzania Serikali ilipoianzisha miaka 1970 na ile iliyokuwa Tanzania Rural Development Bank kabla ya kuwa CRDB, Serikali ilichukua line of credit kutoka AIDA, European Investment Bank na Nordic Investment Bank kuweza ku-capitalize hizi benki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuwe wabunifu tukienda na lugha hii, kwanza Benki ya Maendeleo kwa Sheria ya Mabenki na Financial Institution unahitaji upate leseni minimum fifty billion, ten billion ndiyo fedha za kwenda kukopesha halafu tunasema ikopeshe kwa masharti nafuu maana yake ifanye hasara tangu day one haiwezekani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kweli kwa hili tu-capitalize the bank na tuone namna ya kufanya. Hizi hati fungani za mtaji zinawezekana zikatumika kwa sababu ukinitolea ni kama I owe you money, interest utakuwa unanilipa ndani ya miezi sita na principal mwisho wa mwezi, angalau una-clean up balance sheet yangu na wengine wanaoniangalia kama benki niweze kukopesheka, ndiyo tunaiomba Serikali ilione kwa mtazamo huo.
I owe you money, interest utakuwa unanilipa ndani ya miezi sita na principle mwisho wa mwezi ili kama benki niweze kukopesheka, ndiyo maana tunaiomba Serikali ilione kwa namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho. Hii Mifuko ya Hifadhi kwa principle hiyo hiyo, najua Serikali ime-underwrite Mifuko hii hasa PSPF; lakini kwa vile tumechukua pesa na tumezitumia kwa maendeleo yetu, nadhani tuwe wakweli tu, tunapowasema tutatoa a non cash bond kweli tuitoe. Tukisema tutatoa bilioni 80 mwaka huu kwenye bajeti zionekane kuliko kuzidi kuididimiza Mifuko hii halafu wafanyakazi waliostaafu kama mimi unakuta hawalipwi kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mimi nilikaa kwa kipindi cha miezi saba silipwi pensheni na, ni kweli eeh, lakini ndiyo haya mambo tunayosema, Serikali wasikasirike maana tumezitumia pesa hizi kwa nia njema, lakini tuje sasa na utaratibu utakaotusaidia kuyajibu hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa, Waheshimiwa Wabunge Kanuni za Bunge zinawaruhusu wala tusionekane kuwa ni wanyonge; hii Sheria ya Manunuzi kama Serikali hawataileta sisi wenyewe; hata mimi mmoja wao kwa sababu najua kuandika hizi sheria, tutaleta amendment ya sheria humu! Eee! Hilo tusiogope maana fursa hizi zipo tunaweza kuyafanya haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, amelisema vizuri sana Mheshimiwa Ritha, kwenye Sheria ya Micro-finance. Mimi nilikuwa consulted kufanya kazi hiyo na tulifanya kazi kubwa na akina Dunstan Kitandula. Sasa kwa kuiheshimu Serikali tukasema kwa sababu wanalifanya tukasema hebu waanze tutakuja ku-takeover baadaye, lakini naona sasa again halisemwi tena. Sasa tutayafanya hayo Waheshimiwa Wabunge tukitaka na ndio moja ya kazi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja hii mia kwa mia.