Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. George Mcheche Masaju

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kupata fursa ya kuchangia jioni hii kwenye hoja hii muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nikushukuru kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia. Nichukue fursa hii pia kukupongeza kwa kazi nzuri unayofanya ndani ya Bunge hili, ili kuwezesha chombo hiki muhimu ambacho kimepewa jukumu kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali kitekeleze majukumu yake ya Kikatiba ipasavyo, kiweze kufanya majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Katiba na Kanuni kilichojiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku moja niliwahi kushauri hapa kwamba, chombo kama hiki, ambacho kinafikia maamuzi yake kwa majadiliano ni lazima kiheshimu Katiba, Kanuni na Sheria zinazotawala katika uendeshaji wa shughuli za chombo hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja iliyoko mbele ya meza yako Tukufu na nampongeza Mheshimiwa Waziri na Wizara nzima kwa kuleta hoja hii mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeombwa kuchangia ili kueleza mambo machache ya Kikatiba na Kisheria, ambayo yamejili katika michango ya Waheshimiwa Wabunge, ambao nao nawapongeza kwa michango yao ya kuboresha Hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni hili linalohusu Sheria za Mifuko ya Hifadhi za Jamii, kuhusu mapendekezo ya kurejesha au kuwa na fao la kujitoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema tu kwamba, mafao ya wafanyakazi yanasimamiwa na Sheria za Mifuko ya Jamii na Sheria hizo ni Sheria ya Mfuko wa Mafao ya Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Sheria ya Mfuko wa Mafao ya Serikali za Mitaa (LAPF), Sheria ya Mfuko wa Mafao ya Mashirika ya Umma (PPF), Sheria ya Mfuko wa Mafao ya Utumishi wa Umma (PSPF) na Sheria ya Mfuko wa Mafao wa GEPF.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa msingi wa mafao haya ya watumishi wa umma ni katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ibara ya 11 ya Katiba hii, Mheshimiwa naomba uniruhusu niisome, hii ndiyo inaweka msingi wa mafao hayo ya watumishi wa umma na yenyewe inasema hivi:-
Mamlaka ya Nchi itaweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu kufanya kazi, haki ya kujipatia elimu na haki ya kupata msaada kutoka kwa jamii wakati wa uzee, maradhi au hali ya ulemavu na katika hali nyinginezo ambazo mtu huwa hajiwezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndio msingi wa mafao haya ya wafanyakazi hawa. Sasa sheria tulizonazo zimegawanyika kwenye makundi mawili; Sheria ya LAPF na Sheria ya PSPF, zenyewe bado zinalo fao la kujitoa, lakini Sheria ya NSSF, Sheria ya PPF na Sheria ya GEPF haina fao la kujitoa. Sasa kumekuwa na hoja kwamba, labda kama kuondolewa kwa fao hilo la kujitoa kunavunja Katiba ya nchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusema kwamba, kwanza hizi Sheria, ambazo hazina fao la kujitoa ndizo zinazozingatia matakwa ya Katiba ya nchi, lakini pia suala hili liliwahi kufikishwa mahakamani. Mahakama ya Rufaa katika shauri la rufaa namba 105 (consolidated civil appeal) namba 105 na 81 za mwaka 2006, kati ya Nassoro Athuman Gogo na James William Lugiana, wakiwakilisha wenzao 2,487 liliamua kwamba, Sheria ya PPF iliyokuwa haina fao hilo la kujitoa ilikuwa haivunji Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huu ndiyo ushauri wangu, ndiyo msimamo wa Katiba, ndiyo msimamo wa Sheria kwenye masuala haya. Lakini Bunge linaweza kufanya maamuzi, maamuzi ambayo lakini pia linapoyafanya lazima lizingatie Katiba na maamuzi ya Mahakama ya Rufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni hili ambalo limezungumzwa kuhusu suala la kampuni moja inaitwa Quality Plaza, kwa sababu nimeliona hapa, halikuzungumzwa hadharani. Mashauri yako mahakamani yanayohusu masuala haya na yameshasikilizwa na inasubiriwa tu sasa kutolewa hukumu. Kulikuwa na mashauri mengi na vyema niyataje tu mashauri haya, lakini sitaenda ndani kwa sababu suala liko mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kulikuwa na shauri namba 33 la mwaka 2009 Mahakama Kuu, shauri namba 40 la mwaka 2011 Mahakama Kuu, shauri namba 59 la mwaka 2012 Mahakama Kuu, shauri namba 77 la mwaka 2012 Mahakama Kuu. Hata hivyo, baadaye mashauri yote haya yaliunganishwa kwa pamoja yakawa consolidated kwamba ni shauri namba 33 la mwaka 2009 kwa sababu yote ni ya migogoro ya upangaji. Shauri hili limesikilizwa, linasubiriwa tu kutolewa hukumu na kwa sababu hiyo hatuwezi kulijadili hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata hivyo, Quality Plaza walifungua shauri namba 97 la mwaka 2015 walipotakiwa kuhama na liko mahakamani, hatuwezi kuyaongelea hapa. Kwa hiyo, ndiyo niliona kwamba, niyaseme hivi, lakini ukweli ni kwamba, PSPF imekuwa ikichukua hatua za kuhakikisha kwamba, inalinda maslahi kwenye pango hili isipokuwa kama tu kwa sababu ya technicalities za mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, ambalo naomba kuliongea ni hili suala la chombo kinachoitwa Financial Intelligence Unit. Naomba kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba, mwaka 2014 ndugu George Mcheche Masaju, wakati huo akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Taasisi moja ya masuala ya kifedha duniani inaitwa Financial Action Task Force. Tanzania ilikuwa imekuwa blacklisted for almost five years, kwamba tuna mifumo dhaifu ya kupambana na utakatishaji wa fedha haramu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi Januari, mwaka 2014, nikatumwa Paris kwenye Financial Action Tax Force, nikaitetea wale wakubwa wakaridhika. Mwezi wa Nne wakaja kufanya On site visit Inspection, wajiridhishe na mifumo yetu ya Sheria, wakaridhika. Mwezi wa Saba, 2014, Tanzania ikaondolewa katika lile kundi la nchi ambazo zina mifumo dhaifu ya udhibiti wa fedha haramu na vitendo vya ugaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Tanzania ina mifumo imara ya kisheria ya kudhibiti vitendo vya utakatishaji wa fedha na ugaidi. Na ni kwa sababu hiyo pia, imejiunga na Egmont Group, ambayo ni jumuiya ya Taasisi hizi za Financial Intelligence Unit, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kumekuwa na hoja kwamba, Financial Intellegence Unit ya Tanzania ilipaswa iwe na mamlaka ya kuchunguza kama zilivyo mamlaka nyingine. Haiwezekani! Yenyewe hii, kuna makundi matatu ya hizi Financial Intelligence Unit.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ni Administrative kama ya kwetu hii, ya kiutawala. Yenyewe inapata taarifa hizi, inazipeleka kwenye vyombo vya uchunguzi kama Polisi, PCCB na Taasisi nyingine halafu na Vyombo vya mashtaka. Pia, kuna kundi la pili linaitwa Investigative Financial Intelligence Unit, hii inakuwa na mamlaka yenyewe ya kuchunguza, inachunguza tu, lakini inapeleka kwenye vyombo vingine vya mashtaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kundi la tatu ambalo ni Hybrid lenyewe linachunguza na kushtaki. Mifumo yote hii mitatu imekubaliwa katika kundi hili la Egmont Group na ndiyo maana sisi tulijiunga mwaka jana kwenye hii Egmont Group kwamba tuna sifa zote za kutekeleza hayo. Kinachozingatiwa zaidi kwenye hizi financial intelligence ni kwamba; je, hizi Taasisi ni huru? Hilo la kwanza. La pili, zina uwezo wa kuchunguza na kujiridhisha kufanya focused investigation ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Taasisi nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kushauri tu kwamba, hii Taasisi ya Financial Intelligence Unit iliyopo hapa kwetu, kwa sababu tu yenyewe haichunguzi au kwamba, haipeleki mashtaka mahakamani kwamba, basi ni dhaifu, hapana. Ndivyo ilivyo na ni utaratibu katika dunia kwa haya makundi matatu na sisi tunaingia kwenye kundi hilo, hakuna matatizo mengine yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niseme tu kwamba, naunga mkono hoja kama ambavyo nilishaongea tokea mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.