Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Kwa jina naitwa Engineer Nditiye, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua nafasi hii kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniteua kugombea nafasi hii. Vilevile nawashukuru wananchi wa Jimbo la Muhambwe kwa kuniamini na kuona sasa maneno maneno Bungeni hayatakiwi, inatakiwa Kazi tu! Nawaahidi kwa moyo wa dhati kabisa kwamba Engineer Nditiye, nimekuja kufanya kazi wala siwezi kuwa na maneno maneno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, ndugu yangu Mheshimiwa Mpango. Kwanza namsifu sana kwa hotuba yake nzuri sana na mipango yake mizuri sana. Vile vile nashukuru hotuba ya Mheshimiwa Rais, ambayo Mheshimiwa Dkt. Mpango mipango yake mingi ime-base kwenye hotuba ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na suala la elimu; ili tuingize nchi yetu katika uchumi wa viwanda, tunahitaji tuboreshe sana suala letu la elimu. Ni lazima tujikite sana katika kuhakikisha kuanzia shule za msingi, wanafunzi wanapenda masomo kama hesabu na sayansi ili hata hivyo viwanda vitakapoanzishwa tuweze kupata watu sahihi, kwa ajili ya kuviongoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimkubushe Waziri wangu wa Nishati, Profesa Muhongo kwamba ili ku-achieve mipango yetu, tunahitaji tupate umeme kwa sababu, Serikali yetu ilitushauri kwamba kila Kata iwe na sekondari, na wananchi waliitikia huo mwito, kila Kata ina sekondari.
Vilevile Serikali yetu ilituambia kwamba kila sekondari ya Kata sasa iwe na maabara. Nikuhakikishie kwamba katika Jimbo langu la Muhambwe, karibu sekondari zote za Kata zimekwisha jenga maabara na tumekwishafikia asilimia 80, tunasubiri tu hatua ndogo ndogo ili maabara zianze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyoko ni kwamba, katika Jimbo langu lenye Kata 19, ni Kata tatu tu ambazo zina umeme; na maabara yoyote ile sidhani kama inaweza kuendeshwa kama hakuna umeme. Kwa hiyo, ndugu yangu Mheshimiwa Profesa Muhongo pamoja na kazi nzuri unayoifanya, nakuomba sana ufikirie hilo Jimbo la Muhambwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la reli. Sidhani kama kuna Mbunge yeyote ambaye atasimama hapa aache kuizungumzia reli ya kati, kwa sababu inahudumia mikoa zaidi ya 13.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile reli ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. Hilo liko wazi, tunaomba sana, kwenye mipango yako utueleze in detail. Siyo kueleza juu juu tu kwamba kilometa ngapi zitakarabatiwa; tunataka utueleze za wapi na wapi na kivipi? Tunataka reli yote ikarabatiwe kwa sababu umuhimu wa reli hiyo hauna maswali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa ni Mbunge wa kutoka Mkoa wa Kigoma siwezi kumaliza bila kuzungumzia barabara ya kutoka Nyakanazi mpaka Kigoma, nimeiona hapa kwenye ukurasa wa 11 imewekwa, naomba sana na tutakuwa makini kweli kuhakikisha hiyo barabara ambayo kwetu sisi ni ya muhimu kutuunganisha na Mikoa mingine inapewa kipaumbele na ijengwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la miundombinu ya maji. Kama nilivyozungumza hapo awali, Wilaya yangu ya Kibondo ina Kata 19, lakini Kibondo Mjini kwenyewe hatuna maji ya uhakika wala hayako salama haya yanayotoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba Wizara ya Maji ihakikishe inatafuta chanzo kingine, kwa sababu chanzo kilichokuwepo kimeshavamiwa na shughuli za kibinadamu na hakifai tena; hakitoa maji; na kama Wilaya unaweza ukakaa hata siku nne bila kuwa na maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Waziri wa Maji katika mipango yetu hii ahakikishe kwamba wananchi wanapata maji safi na salama ili waweze kuendelea na shughuli zao za ujenzi wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la maliasili. Katika Jimbo langu nina Kata zaidi ya sita ambazo zinapakana na Hifadhi ya Moyowose, Kata za Busunzu, Busagara, Lusohoko, Kitahana, Kata ya Mulungu na vijiji vyake. Kwa muda mrefu sana tumekuwa tukiomba Serikali irekebishe mpaka ili wananchi wapate sehemu ya Kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba Vijiji hivi ni vya muda mrefu na wakati huo wananchi hawakuwa wengi, sasa wameshaongezeka na wanahitaji sehemu zaidi ya kulima.
Kwa hiyo, nashukuru sana kwa waraka uliopitishwa na Mheshimiwa Waziri wa Ardhi kuorodhesha vijiji vyote ambavyo vinapakana na mpaka ili waweze kuongezewa sehemu ya kulima. Nashukuru sana, nami nitashirikiana na wewe kwa karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa haraka haraka. Kwenye kampeni za Mheshimiwa Rais, alipopita Jimboni kwangu pale, aliahidi kuhusu suala la pensheni kwa wazee wote, awe mtumishi, mkulima au mfugaji na wavuvi aliahidi pensheni kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba hilo suala litekelezwe na liwekwe kwenye mpango imara ambao utatekelezeka ikiwezekana kuanzia mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, michezo. Nimefurahi sana kwamba hivi karibuni tumetoa product moja Tanzania ambayo imesikika moja kwa moja. Huyu anaitwa Mbwana Samatta. Tukumbuke kwamba michezo ni chanzo kizuri sana cha mapato kwa nchi. Angalia nchi kama Brazil, asilimia kadhaa ya uchumi wake wanategemea sana wanamichezo ambao wanaenda kucheza nchi za nje, wanaleta uchumi nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhakikishe sasa tunaanza kuwekeza hasa kwenye Mikoa ile ambayo ni vyanzo vya sanaa na michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia Mkoa wa Kigoma, Tanga kidogo na Morogoro kwenye football huwezi ku-doubt. Vilevile kwenye sanaa ya muziki, hata maigizo; Mkoa wa Kigoma una mchango mkubwa sana.
Naomba sana Serikali ijikite sana katika kuwekeza katika Mkoa wetu kuhusu suala la michezo na sanaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo, naunga mkono hoja.