Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikushukuru sana kwa kuliongoza vizuri sana Bunge toka asubuhi na mchana huu. Niungane na waliotangulia kusema kwamba haya wanayofanya upande mwingine yasikukatishe tamaa. Chapa kazi, fanya kazi ambayo Bunge hili lilikuchagua kufanya na hakika Watanzania wanajua umahiri wako na matunda ya kazi yako njema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango mizuri sana na ushauri wao na naahidi kabisa kwamba ushauri ambao mmetupatia tutaufanyia kazi na tutauzingatia katika kutekeleza bajeti ijayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya Waheshimiwa Wabunge 36 wamechangia hotuba yangu; waliochangia kwa kuzungumza ni 24 na waliochangia kwa maandishi ni 12. Kwa kuwa baadhi ya michango ni ushauri lakini hata hoja hizi si haba, kwa muda ambao ninao sitaweza kujibu zote, lakini naomba kuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba tutawasilisha majibu ya hoja zote kwa maandishi ili Bunge liwe na rejea na kumbukumbu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo machache ya utangulizi, basi naomba nitoe maelezo kwa baadhi ya hoja ambazo zimejitokeza wakati Waheshimiwa Wabunge wakijadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango na taasisi zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nianze na hoja ambayo ilijielekeza kusema kwamba ni vizuri kama Serikali tuangalie tutakavyoweza kuzuia athari zinazoweza kujitokeza katika kukopa na kutumia instrument mbalimbali za masoko ya fedha kama vile hedging na swaps.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hili labda tu niseme kwamba, Wizara ya Fedha na Mipango katika ukopaji tunazingatia Mkakati wa Kati wa Usimamizi wa Madeni, kwa Kiingereza inaitwa Medium Term Debt Strategy, lakini pia Sheria ya Madeni. Mkakati huu unaelekeza tukope wapi, sarafu zipi, riba gani, kama ni fixed rates au variable rates, lakini kubwa ni kwamba tuhakikishe Serikali inakopa kwa gharama nafuu na zenye athari ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika ukopaji wa deni la nje kuna athari nyingi ambazo zinaweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya riba (Interest Rate Risk) lakini pia mabadiliko ya viwango vya kubadilisha fedha (Exchange Rate Risk). Tunaweza tukatumia vyombo mbalimbali ikiwa ni pamoja na instruments ambazo aliyetoa swali alipendekeza, ikiwa ni pamoja na hedging na Interest Rate Swaps. Hivi ni vyombo ambavyo hata hivyo vina gharama kuvitumia na pia vinahitaji utaalam wa hali ya juu katika kuotea viwango vya riba katika masoko ya fedha ya Kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba, kimsingi hizi instruments kwa sasa zinatumika zaidi kwa nchi ambazo ziko kwenye mikopo ya kibiashara na ambazo zina viwango vya riba vinavyobadilika mara kwa mara, lakini mahali pia ambapo madeni yako katika sarafu moja. Kwa hiyo, tunavyoendelea huko mbele tutaangalia tukiongozwa na, kama nilivyosema, Medium Term Debt Strategy ili kuona polepole na sisi tunavyoweza kutumia hizi instruments zikatusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nisemee kidogo suala la deni la Taifa na nimshukuru sana Mheshimiwa Mtemi Andrew Chenge kwa ufafanuzi wake mzuri alipolielezea kwa nini linaongezeka. Naomba tu nisisitize kwamba kwa kweli kwa Taifa kama letu ambalo lina mahitaji makubwa sana ya maendeleo, ni lazima tuendelee kukopa na ukikopa maana yake unaingia kwenye deni. Tuna mahitaji makubwa sana ya miundombinu, kwa hiyo lazima tukope. Kwa sasa hatuna vyanzo vya fedha vya kutosha kuweza kukidhi hayo mahitaji yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kikubwa Mheshimiwa Chenge amekieleza, ni kwamba tunakopa kwa masharti gani? Hili ni jambo la kuangalia. Kwa hiyo riba kiasi gani, tutalipa kwa muda gani, grace period na masharti mengine, haya lazima kuyachambua kwa umakini. La muhimu zaidi, tunakopa hizi fedha kufanyia nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mara huwa nasisitiza nchi inavyokopa haina tofauti na mtu binafsi. Kama unakopa ukaenda kustarehe ukalewea pombe na kadhalika basi unajua kabisa huo mkopo hauna faida kwako wewe na familia yako na Taifa ni hivyo hivyo. Kama unakopa na unazitumia kuongeza uwezo wako wa kuzalisha, unaongeza uwezo wako wa miundombinu bora ambayo inawasaidia wawekezaji na wananchi kuweza ku-move goods and services, hilo ndilo jambo jema.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kinachotakiwa ni umakini, kwamba mikopo hiyo tunaifanyia jambo gani. Kwa nchi yetu, kikubwa tumeelekeza mikopo hiyo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. Ni wazi kabisa miundombinu kama umeme Kinyerezi, barabara nyingi ambazo zimejengwa nchini, madaraja na kadhalika, yote haya kwa fedha za ndani peke yake tusingeweza, kwa hiyo ilitulazimu kwenda kukopa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa upande wa tathmini ya deni la Taifa, kwa kweli hapa tunafanya tathmini mara nyingi. Kila mwaka tunafanya tathmini chini ya ushirikiano wetu na Shirika la Fedha la Kimataifa na wao wanashiriki, hatufanyi peke yetu. Kwa hiyo hizi estimates, tunapoangalia uhimilivu wa deni la Taifa kulinganisha na vigezo vya Kimataifa, kwa kweli hakuna uchakachuaji. Kwa hiyo, moja tunatazama uwiano kati ya deni na pato la Taifa (debt to GDP ratio) na Kimataifa ni kwamba debt to GDP ratio inatakiwa isizidi asilimia 50, ndiyo viwango vya Kimataifa na kwa Tanzania hivi sasa tuko asilimia 19.9.
Mheshimiwa Naibu Spika, kigezo kingine ni deni la nje kwa uwiano wake na uwezo wetu wa kuuza bidhaa nje (export) na hapa ulimwenguni ukomo wastani ni asilimia 200, Tanzania sasa hivi tuko asilimia 97.7. Pia tunaangalia uwiano kati ya deni la nje na mapato yetu ya ndani na ukomo wa Kimataifa ni asilimia 300, sisi bado tuko asilimia 145.3 kwa hiyo tunaangalia vigezo kama hivi na zaidi ya hapa na kimsingi vigezo vyote vinatuonesha kwamba deni letu ni himilivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kidogo kuhusu Serikali kutoa non-cash bond. Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ilishaamua kutoa cash bond na tumechelewa kidogo kwa sababu tumekuja kupata taarifa kwamba baadhi ya madai ya Mifuko yana maswali mengi. Kwa hiyo, kwa maana kwamba sasa tunatoa cash bond kwa kuzingatia madai yapi ilikuwa ni tete na ilikuwa ni muhimu sana kufanya uhakiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu ilashamuagiza Internal Auditor General kufanya uhakiki na bahati nzuri hivi ninavyozungumza amekamilisha uhakiki, anamalizia tu ku-polish ile ripoti yake ili tuweze kufanya uamuzi na kuendelea kutekeleza uamuzi wa Serikali wa kutoa cash bond.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulishauriwa na nafikiri alikuwa Mheshimiwa Prosper Mbena, kwamba tuangalie upya mwenendo wa benki kwa sababu kwa kweli hali ya interest rates si nzuri na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, nithibitishe tu kwamba Serikali tumeanza kufanya hivyo. Mtakumbuka kwamba katika kikao kilichopita cha Bunge lako nililieleza Bunge lako uamuzi wa Serikali, kwa mfano kuagiza kwamba fedha ambazo zinashikiliwa na Benki za Biashara, fedha za Serikali za taasisi ambazo zinashikiliwa kwenye benki za biashara zifunguliwe akaunti Benki Kuu ili tuweze kuona fedha hizo ni kiasi gani na zinatumika kufanya nini badala ya benki za biashara kuzitumia kufanya biashara, ikiwa ni pamoja na kufanya biashara za hati fungani za Serikali hiyo hiyo. Kwa hiyo hatua kama hii ni moja ya hatua ambayo inazilazimisha sasa hizi benki ziondoe too focus kwenye makampuni makubwa na kwenye miji ili sasa ziangalie na kwenda kutafuta wateja hata vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaangalia pia sababu nyingine ambazo zinasababisha interest rate katika benki kuwa kubwa na hii ni pamoja na kutoa elimu ili wananchi wa Tanzania wawe na hakika kabisa kwamba unapokwenda kukopa lazima urudishe na lazima utaratibu huu uendelee kujengwa siyo unakwenda kukopa halafu unaingia mitini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima kuchukua hatua za makusudi kabisa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba Mtanzania anajulikana alipo anafanya shughuli gani, mali zake ni zipi ambazo amekopea na kadhalika. Hizi zote ndizo zinazochangia kwenye gharama za mikopo, kwa hiyo, lazima hizi tushughulike nazo ili riba hatimaye ziweze kuteremka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ilikuwepo hoja ya pia kwamba wafadhili kupunguza ahadi zao ni kweli haikubaliki na kwamba ni vizuri Serikali ijulishe dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tu kwamba kwenye hotuba yangu nimeeleza baadhi ya hatua ambazo tumechukua ili kukabiliana na tatizo hili. Moja kubwa ni kuendelea na mazungumzo na wadau wetu wa maendeleo. Kama nilivyoeleza asubuhi tumekwishafikia uamuzi kwamba tunatafuta, tumepata mtaalam elekezi ambaye ni third part na yeye ataangalia pande zote mbili ili kuona changamoto ambazo zinajitokeza (concerns) kwa pande zote ili tuweze sasa kuandaa utaratibu mzuri zaidi wa hii misaada ya wafadhili na kuhakikisha kwamba ahadi zao zinatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ilitolewa observation kwamba pana upotevu mkubwa sana wa mapato bandarini ikiwa ni pamoja na bandari bubu. Hili halina ubishi na Serikali na Wizara inafanya jitihada za makusudi kabisa kuimarisha ulinzi na kuhakikisha kwamba tuna patrol team ambayo inakagua baadhi ya hizi bandari zikiwemo bubu na kufuatilia pale ambapo tunakuwa tumepata taarifa za kiintelijensia juu ya watu ambao kwa makusudi wanatumia bandari zetu kuikosesha Serikali mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli pia kwamba nchi yetu ni kubwa na mipaka yetu ni mirefu, kwa hiyo, njia za panya bado ni nyingi. Wito wangu kwa Watanzania ni kuendelea kutupatia taarifa kutoka sehemu mbalimbali za nchi yetu ili tuweze kwa kadri inavyowezekana kudhibiti mipaka yetu na bandari zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulishauriwa hapa kwamba Tume ya pamoja ya fedha ifanye kazi yake. Mheshimiwa Waziri anayesimamia masuala ya Muungano alilieleza vizuri kwamba kwa kweli waraka ulishaandaliwa ambao ni pamoja na kuhakikisha kwamba, kwa mfano mgawanyo wa mapato baina ya Serikali zetu mbili, unafanyika vizuri na kwa makubaliano ya pande zote na tume ya pamoja ya fedha kwa kweli ni interest ya kila mtu kwamba ifanye kazi yake vizuri ili Muungano wetu uendelee kuimarika.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulisemea ni hili la malipo ya wazabuni kwamba watalipwa lini? Niseme tu kwamba Wizara ya Fedha na Serikali kwa ujumla imedhamiria kuongeza kasi ya kumaliza malimbikizo halali, nirudie tena malimbikizo halali ya madai ya wazabuni. Bahati nzuri kwa kuwa sasa makusanyo ya Serikali yanaimarika kwa kweli ni dhamira ya dhati kabisa ya Serikali kwamba tuyamalize haya mapema inavyowezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nitumie nafasi hii kusisitiza kwa wazabuni, wote ni muhimu sana wanapowasilisha madai yao yakawa ni ya kweli. Pawepo uaminifu katika madai ambayo yanawasilishwa kwa sababu kila mara Ofisi ya Internal Audit General inapofanya kaguzi zake, inapofanya uhakiki tumegundua kuna madai mengi hewa. Kwa hiyo, nao watusaidie, ni sehemu ya kufanya machelewesho kwa sababu ni lazima tuhakikishe kwamba tunalipa madai halali na siyo kutumia fedha za umma isivyo sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulipokea maoni kwamba utumbuaji wa majipu mamlaka ya mapato umezaa mapato zaidi. Ni kweli na napenda nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba kwa hili tutaendelea tutawatumbua Watumishi wasio waadilifu, tutawashughulikia kikamilifu. Wakati huo huo niwapongeze sana watumishi wema wa Mamlaka ya Mapato ambao wameendeelea kufanya kazi yao nzuri sana na kwa sasa tuna zaidi ya trilioni moja kama mapato ya Serikali ya kodi kila mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Shirika la Bima la Taifa, kama mpango wa kulifufua na kuliongezea uwezo uko wapi? Hata bodi kwamba iko na walio wengi kwenye management wanakaimu. Napenda niseme tu kwamba, Wizara yangu imefikia hatua nzuri kuteua Wajumbe wa Bodi na ninavyozungumza Wajumbe wanaopendekezwa wanafanyiwa upekuzi na mara baada ya bodi kuundwa basi bodi hiyo nayo tutaielekeza mara moja ishughulikie suala la Maafisa Waandamizi ambao bado wanakaimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ndani ya Serikali tumekwishatoa maelekezo kwamba kwa kadri inavyowezekana Taasisi za Umma na Mashirika yake zitumie National Insurance Corporation ili tuweze kuhakikisha kwamba tunaliongezea mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja juu ya Mfuko wa Mahakama lakini pia ukweli kwamba kuna upungufu wa Mahakimu lakini hata hali yenyewe ya Mahakama zetu, Mahakama za Mwanzo hairidhishi na inahitaji kuboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo la msingi kabisa na Serikali inatambua hili, ndiyo maana mapema mwaka huu Mheshimiwa Rais, aliagiza Mfuko wa Mahakama uongezewe fedha na tulifanya hivyo, tuliwaongezea fedha za maendeleo Shilingi bilioni 12.6 na moja ya kazi ya fedha hizi ni kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu ya Mahakama inajengwa na Serikali itaendelea kufanya hivyo kwa kuwa tunatambua umuhimu wa Mhimili wa Mahakama katika kutoa haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nilisemee suala la tuhuma ambazo zimetolewa kuhusu Benki Kuu kufungua makampuni na watumishi wanachukua tenda za Benki Kuu ambazo zinajumuisha kazi za siri. Naomba tu nikiri hapa kwamba taarifa hii nimeisikia hapa mbele ya Bunge lako Tukufu na namwomba Mheshimiwa aliyetoa hoja hii atupatie taarifa kamili niko radhi kabisa tuzungumze tupate hizo taarifa na tutazifanyia kazi tuhuma hizi mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nilisemee hili la kwamba Serikali haijasaidia kukuza sekta binafsi na hususani baadhi ya kodi na sheria ambazo zinakuwa ni kero kwa Waajiri na pengine na baadhi yao hazina tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niseme kwamba namwombaMheshimiwa Mbunge aliyetoa hoja hii asubiri na asikilize hotuba yangu ya bajeti ya Serikali Kuu Jumatano ijayo kwa hamu baadhi ya mambo haya tutayashughulikia. Hata hivyo, niseme tu kwamba ni kweli baadhi ya vipengele vya sheria yetu ya kazi vimekuwa vinalalamikiwa na wawekezaji na kwamba pengine haitoi fursa kwa waajiri kuchukua hatua ingawa pia kuna upande mwingine kwamba baadhi ya waajiri nao wanawanyanyasa wafanyakazi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Serikali ni sikivu, imesikia na inaendelea kusikia na ndiyo maana Mheshimiwa Rais, kati ya makundi ya kwanza aliyokutana nayo mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni wawakilishi wa wafanyabiashara na kusikiliza kero zao ili kuweza kuhakikisha kwamba mazingira ya kuwekeza na kufanya biashara ikiwa ni pamoja na marekebisho yanayotakiwa kwenye hizi sheria yanafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nilifuata hatua za Mheshimiwa Rais wetu na nimeshafanya mikutano na wafanyabiashara Dar es Salaam na Arusha lakini lengo ilikuwa ni hilo hilo, kwamba tuzielewe vizuri changamoto ambazo wanakabiliana nazo ili tuweze kuzifanyia kazi na kupata suluhisho mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nisisitize kwamba wakati nawasilisha mpango wa maendeleo wa miaka mitano hapa nilisema wazi kabisa kwamba Serikali ya Awamu ya Tano moja ya msisitizo mkubwa ni kuhakikisha kwamba mazingira ya biashara na uwekezaji haya tutayawekea mkazo zaidi katika awamu hii maana hatutaweza kujenga viwanda katika nchi yetu kama mazingira ya wawekezaji na waajiri hayako sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja pia kwamba kwa nini Serikali isiingie katika uwekezaji mkubwa na hususan wa miundombinu kupitia PPP. Niseme tu kwamba kwa kweli hii ndiyo njia nzuri na njia mbadala ya kuhakikisha kwamba nchi changa kama yetu basi itakuwa na uwezo wa kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo na hasa ile ambayo inagharimu fedha nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niseme mawili. Bahati mbaya ni kwamba experience ya nchi yetu katika PPP haikuwa nzuri sana. Mtakumbuka kwa mfano tulipopeleka utaratibu wa PPP kwenye sekta ya maji na kwenye sekta ya umeme matokeo yake yalikuwa si mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli pia ni kwamba PPP bado ni mfumo mgeni na unahitaji ujuzi ikiwa ni pamoja na negotiation katika kuingia ubia. Kwa hiyo tumeanza sasa, ndiyo maana tunacho kitengo pale ndani ya Wizara ya Fedha kwa ajili hii, ambacho bado kinajengwa. Tumeanza na miradi michache, ni matumaini yangu kwamba tutapiga hatua nzuri na kwa haraka kutumia mfumo huu kwa haraka zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nimalizie kwa kusema juu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina. Ofisi ya Msajili wa Hazina ni chombo muhimu sana maana hili ndio hasa jicho la Serikali kwa ajili ya kumiliki mali ambazo tumewekeza kwenye taasisi mbalimbali za umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Ofisi hii imefanyiwa maboresho makubwa ikiwa ni pamoja na marekebisho ya sheria inayoongoza chombo hiki, lakini pia tumebadilisha uongozi ikiwa ni pamoja na kupata Treasury Registrar mpya ambaye ana uzoefu kutoka sekta binafsi lakini pia tunaendelea na jitihada za kuiongezea taasisi hii watumishi wenye weledi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niseme tu kwamba uzuri katika kipindi kifupi ambacho mabadiliko haya yamefanyika tumeanza kuona matunda kwa maana ya kuongezeka kwa mapato, lakini dividend kutoka kwenye Mashirika haya. Kwa hiyo, nafikiri ni hatua nzuri, Waheshimiwa Wabunge naomba tuendelee kuiunga mkono ofisi hii ili ifanye kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwezo wa Mashirika kama TTCL kwa nini nashindwa kuingia kwenye ushindani naomba niseme tu kwamba tumekuwa na changamoto toka tulipo anza kuingia kwenye ubinafsishaji na management ya TTCL kwa kweli bado ni mpya inaendelea kujipanga. Naamini ndani ya muda mfupi tutaona mabadiliko.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini haya Mashirika kwa kweli hatuwezi kusema tu kwamba kwa sababu kwa sasa hivi yanaonekana ni mzigo basi tuyatupe. Ni muhimu ni sisitize kwamba baadhi ya haya mashirika ikiwa ni pamoja na TTCL ni mashirika ambayo ni ya kimkakati, very strategic kwa ajili ya usalama wa nchi lakini pia kwa maana ya contribution yake kwenye uchumi wa Taifa. Kwa hiyo, hatuwezi kuyatupa tu, ni lazima tuyafanyie kazi ili tuweze kuyafufua.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa kumalizia nichukue nafasi hii kuwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri na ushauri wao. Kama nilivyosema naahidi kuwa ushauri mliotupatia tutaufanyia kazi na tutauzingatia vizuri kwa umakini katika utekelezaji wa bajeti hii na bajeti zijazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tutakapoingia kwenye hatua zinazofuata Waheshimiwa Wabunge waunge mkono hoja yangu ili tuweze kuendelea kutekeleza haya ambayo tumewaelezeni toka asubuhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.