Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dimani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAFIDH ALI TAHIR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nami niishukuru Serikali na nimshukuru Waziri wa Habari, ambaye leo hii ametuletea hotuba yake inayozungumzia kuhusu kuridhIa mkataba ya Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu katika Michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania naona tumechelewa kidogo, tumechelewa hasa kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri jinsi gani vitendo kama hivyo vimetokea katika kipindi kirefu kilichopita. Tanzania ni moja katika nchi ambazo zimefanya vizuri katika michezo miaka mingi ya nyuma, tusisahau kwamba Tanzania ni moja katika nchi za Afrika ya Mashariki ambayo imeweza kutoa wakimbiaji wa ridhaa wa Kimataifa ambao wamechukua medali ya dunia na bado mpaka hivi sasa historia ya Tanzania kupitia mkimbiaji Filbert Bayi bado inatamkwa katika ulimwengu wa michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ilikuwa tuanze mapema katika suala hili lakini pamoja na hayo nakubaliana na Azimio hili na naridhia yale yote ambayo yamo katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri, hali kadhalika pale ambapo alipotoa yale maelezo na maazimio yanayohusiana na misaada na mambo mengine kutoka UNESCO.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina michezo mingi na pale ambapo tunasema sasa tueleke katika kuridhia Azimio hili basi pia tunatakiwa tujiandae na masharti ambayo yamo katika Azimio hili, lakini pia tuwaandae wanamichezo wetu katika kufuatilia na kutimiza Kanuni na Sheria za Azimio hili. Kwa sababu bila kufanya hivyo, Tanzania tutakuwa tunaadhibiwa kila siku au wanamichezo wetu watakuwa wanaadhibiwa kila siku kutokana na masharti yaliyomo katika Azimio hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi nyingi ulimwenguni wanariadhaa wake, wanamichezo wake wa baiskeli, lakini wale ambao vilevile wanatumia michezo ya ngalawa na mambo mengine wamekuwa wakiadhibiwa kutokana na vitendo vya kutumia madawa haya ya kuongeza nguvu katika michezo. Hapa kubwa ambalo nataka nilitilie mkazo ni kuhusu wale wanamichezo ambao bado hawajafikiria kama jambo hili linaweza likaja Tanzania. Mheshimiwa Waziri hapa pamoja na Mwenyekiti aliyekuja kusoma hotuba yake waligusia mambo mengi, lakini mwisho wamegusia suala la kutumia vilevi vya kawaida Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi ni mwalimu wa michezo na michezo yangu mara nyingi ni mpira wa miguu. Katika mpira wa miguu wanamichezo na wachezaji wakati fulani ili uweze kucheza vizuri basi lazima uvute bangi, siyo kweli kwamba ukivuta bangi ndiyo utacheza vizuri au watu wengine wanasema lazima apate pegi kidogo ya bia ndiyo aweze kucheza vizuri, siyo kweli! Haya ni mawazo tu ambayo mtu anajiweka mwenyewe na anahisi kwamba nikivuta bangi basi nitakuwa mchezaji mzuri kumbe siyo kweli isipokuwa anajiharibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika historia yangu ya kuwa mwamuzi wa Kimataifa wa mpira wa miguu nimeona baadhi ya waamuzi nao wanaingia katika harakati hizi. Sasa hapa nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri ambaye anashughulika na michezo, kwamba ni lazima tuwe na kitu maalum hivi sasa mbali na Kimataifa lakini Kitaifa tuwe na Kamati inayochunguza yale mambo ambayo yanafanywa ama na wachezaji ama na waamuzi ama na watu wengine hasa katika mpira wa miguu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpira wa miguu Tanzania tunasema kila siku unadidimia lakini pia tunasema mpira wa miguu wa Tanzania haukui. Mpira unakua lakini sasa kuna mambo madogo madogo ambayo yanarudisha nyuma maendeleo haya. Kwa hiyo, hapa Mheshimiwa Waziri namwomba sana azungumze na taasisi zinazohusika kwa sababu ya Azimio hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wakati umebadilika,ukiangalia ligi zetu hizi za Tanzania wachezaji wetu kwa sababu mchezaji mpira kuna wakati unatakiwa uwe basi huchezi, mimi naingiwa wasiwasi kuna wachezaji sasa hivi wanakaribia miaka 40, miaka 42 bado wanacheza ligi kuu ya Tanzania hizi nguvu kazipata wapi? Mimi nina wasiwasi kuna mambo hapa yanafanyika!
Sasa lazima tuwe na kitu hapa cha kuchunguza mbali na Kamati zetu mbalimbali. Kwa hiyo, tuwe tunachunguza lakini tuwe tunaona wapi tunaelekea katika kuliunga mkono Azimio ambalo limewasilishwa hivi leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina mengi isipokuwa naunga mkono hoja iliyoletwa na Mheshimiwa Waziri. Ahsante.