Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ESTHER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa naomba niunge mkono hoja. Tunafahamu kabisa michezo ni furaha, michezo ni elimu na michezo ni afya, niseme tu kama nchi ni kweli kwamba tumechelewa kukubaliana na Azimio hili. Kwa hiyo, kwa kuwa imeletwa sasa basi niwaombe na Wabunge wenzangu kwa pamoja tupitishe Azimio hili ili nchi yetu iweze kufaidika kama faida zilivyoorodheshwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme inafahamika kabisa kwamba madhara ya kutumia dawa hii ni makubwa kama yalivyoelezwa. Kama nchi sidhani kama tuna sababu ya kutokupitisha Azimio hili kwa sababu hatuna woga, tuna Watanzania wachezaji wazuri sana ambao wameiletea nchi hii heshima kwenye football, kwenye riadha na kadhalika. Kwa uchache tu nitambue heshima waliyoileta wanariadha hawa wafuatao:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna watu kama akina Simon Robert, John Stephen, John Bura, Nada Saktai, Focus Wilbroad Aweso, Francis Nada na Zebedayo Bayo, hawa watu wamefanya kazi kubwa katika nchi hii. Niseme tu tusiogope; tuwekeze kwenye michezo, tunao watu ambao bado wanaweza wakailetea nchi hii heshima.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia michezo inahitaji uwekezaji, tuendelee kuwekeza kama ilivyokuwa zamani kwenye UMISHUMTA na UMISETA tuendelee kutengeneza vijana wenye vipaji kuanzia katika utoto wao ili waweze kuiletea nchi yetu heshima na wakipata kuwekewa misingi na miundombinu mizuri nina hakika wala hatuhitaji kutumia madawa ya kuongeza nguvu maana vijana hawa watakuwa wameandaliwa vizuri na hatimaye wataweza kufanya vizuri katika michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kwamba hawa watu waliowahi kuiletea nchi yetu heshima hatukuona namna yoyote tukiwaenzi, namna yoyote ya kuona kwamba walileta mchango mkubwa wa fedha, wa heshima katika nchi yetu; hii inawakatisha tamaa wale wengine wadogo ambao wanaibuka katika tasnia hii ya michezo kama riadha, football na michezo mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiri kwamba juhudi za hawa watu zitambulike, kuwe na namna maalum ya kuhakikisha kwamba hawa watu wanakumbukwa. Sasa hivi hawa karibu wote niliowataja hapa ukiacha Filbert Bayi ambaye atleast yeye amejiingiza kwenye masuala ya elimu, wengine wote wanapata shida, wanakufa katika umaskini uliotopea kule vijijini, wengine wamejiingiza kwenye ulevi na maisha duni yanawaandama kama watu ambao hawakuwahi kuifanyia nchi hii kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme tu kwamba hakuna asiyefahamu kwamba Manyara kwa ujumla, mimi of course nimetoka Manyara, kwa ujumla Manyara imeiletea sana heshima Tanzania katika suala zima la riadha. Kwa hiyo naendelea kuiomba Serikali iendelee kuwekeza katika Mkoa wa Manyara tupate Sports Academy kule Manyara ambayo inaweza ikasaidia kuendelea kuibua vipaji. Bado tuna watoto hawa wa kifugaji wengi tu ambao kwa mazingira ya Manyara hayana tofauti na mazingira kama ya Ethiopia, wanaweza wakaibeba nchi hii na bado heshima ya nchi ikarudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashukuru tu kwa mchango huu na naunga mkono hoja.