Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigamboni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia katika Azimio hili, kuhusiana na Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Madawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba huu umekuja umechelewa lakini ni mkataba ambao ni muhimu sana. Kama walivyotangulia kusema wenzangu michezo ni afya, michezo ni ajira, michezo ni mahusiano na michezo inajenga undugu na amani. Katika dhana hii ya michezo kumekuwa na tatizo kubwa tena kubwa sana kuhusiana na baadhi ya washindani kutaka kupata ubora ama ushindi katika njia za mkato.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi katika dunia ambao wanafuatilia vyombo vya habari watakuwa wanajua wanariadha wa Kenya ambao wamekuwa wanasifika sana duniani wamepata kashfa ya matumizi ya madawa ya kulevya. Vilevile kwa upande wa Urusi maabara ambazo zimekuwa zinapima matumizi ya madawa ya kulevya nazo zimeingia matatani. Mara nyingi nchi ambazo zinapata matatizo haya huwa zinakosa sifa na zile ambazo zimekuwa zimejengeka kwa muda mrefu kuhusiana na washindani wao na inatia mashaka kuhusiana na wanariadha wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama Daktari athari za madawa ya kulevya ni kubwa sana, wachangiaji waliopita wamezisema, siyo tu kwa kipindi kile ambapo wanariadha wanashiriki katika michezo lakini hata baada ya miaka kumi, ishirini, thelathini baada ya kuacha kutumia madawa haya watu bado wana athari za kimwili, kisaikolojia na kiakili. Kwa hiyo, mkataba huu umechelewa na naunga mkono tuuridhie na nitawaomba Waheshimiwa Wabunge wote na sisi tuukubali kwa sababu una manufaa makubwa sana katika suala zima la michezo katika nchi yetu. Hata hivyo, wakati tunaelekea kuuridhia mkataba huu nitaomba tu vile vile tuangalie katika mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, moja; tuhakikishe kwamba tunatoa elimu ya kutosha kuhusiana na hivi vitu ambavyo ama madawa ama zile njia ambazo zimedhibitiwa katika mkataba huu; sio kila mwanamichezo anaelewa hili na siyo mamlaka zote zinaelewa hili. Kwa hiyo, tujikite zaidi kupitia Wizara husika kuhakikisha kwamba tunajenga, tunatoa elimu ya kutosha kwa wanamichezo vilevile katika mamlaka mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili; tujenge uwezo wetu wa ndani wa kuweza kubaini matumizi ya madawa haya; maana yake ni kwamba sasa tuwe na maabara zetu, zitasajiliwa na ambazo zitakuwa zinatumika katika mashindano yetu ya ndani tuwe na uwezo wa kuweza kubaini baadhi ya matumizi haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo naliomba ni kutoa elimu vilevile kwa Madaktari wa michezo. Inawezekana mtu akapewa dawa pasipo kujua dawa hii inakuwa na athari ama inaweza kuwa ni stimulants ama ikawa na madhara ama ikawa ni sehemu ya yale madawa yasiyoruhusiwa na mtu ameitoa tu. Kuna madawa kwa mfano, kuna dawa zingine tu za mafua ambazo mtu akipewa zinakatazwa kwa mujibu wa mkataba huo. Kwa hiyo, nataka tutoe hii elimu kwa Madaktari wa michezo, lakini sasa tuwe na mtatibu wa kusajili Madaktari wa michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, nami naunga mkono hoja hii ya kuridhia Mkataba huu, umechelewa kuja, lakini ni Mkataba muhimu sana katika ushiriki wa Tanzania katika masuala ya michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.