Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue nafasi hii niweze kukushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuleta Azimio hili ili tuweze kulipitisha. Umechelewa kwa sababu mimi ni mmojawapo wa wachezaji ambao wamecheza miaka ya nyuma, baadhi ya kizazi kimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi mabaya ya madawa haya. Kwenye timu zetu ni kitu cha kawaida, wachezaji walio wengi wamekuwa wakitumia bangi, lakini kabla ya kuendelea kuchangia tupeane pole kwa timu yetu ya Taifa kwa jinsi ambavyo tumefanya vibaya juzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili tumechelewa, niungane na wenzangu na wewe jinsi ambavyo umewasilisha hapa, kwamba sasa twende mbele, lakini kazi kubwa ambayo ipo ni kwamba tunafanyaje? Ni nani watahusika katika kulisimamia jambo hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyojua ni kwamba vikundi vingi vya michezo nchini kwetu vimesajiliwa. Ningependekeza kwamba, ukienda nchi nyingine zilizoendelea hamuwezi kuanza ligi mpaka wachezaji wamepimwa afya zao. Kwa hiyo aina ya Madaktari ambao wanakuwa kwenye vile vilabu wanakuwa waliosajiliwa, ni Madaktari wa kweli, ili pale linapotokea tatizo kwenye timu yake, amegundulika mtu ambaye anatumia zile dawa basi wa kwanza kuadhibiwa ni yule Daktari ambaye alimpima afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nachangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri nilipendekeza kwamba sasa hivi umefikia wakati ikiwezekana lile Baraza la Michezo tulivunje, tuanzishe Shirika la Michezo. Kwenye Shirika la Michezo itakuwa rahisi zaidi lenyewe kutafuta fedha au kupata kwa wahisani au kuchangia au hata katika harambee ili liweze kuendesha, kusimamia timu za Taifa kwa udhibiti na kudhibiti dawa za kulevya, ni kazi yao. Leo inawezekana tunapitisha hapa sina hakika kama tulikumbuka kuweka bajeti hii ambayo inakwenda kutusaidia kufanya kazi hii ya udhibiti huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nilizungumza pia, hatuwezi kuendelea kufanya vibaya kwenye timu yetu ya Taifa. Ukiangalia, kama tungewapima wale wachezaji baadhi ungewakuta wanatumia, aidha kwa kujua au kwa kutojua. Kwa sababu dawa hizi zinaweza kutumika hata kwa kula vyakula tu. Kuna baadhi ya vyakula ambavyo vinaweza vikawa vinasababisha mtu kupata nguvu, yaani vikasababisha kupatikana na viashiria vya dawa za kulevya, vyakula ambavyo tunatumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilipendekeza kwamba ili sasa timu zetu zifanye vizuri ni pamoja na kudhibiti matumizi mabaya ya madawa ya kulevya, sambamba na kuhakikisha kwamba wachezaji wanaotoka nje wanapunguzwa kwenye timu zetu. Kwa sababu wao wanakuwa bora tu pale vilabu vya Simba, Yanga, Azam vinapofanya vizuri na ukiangalia ndiyo wanaoongoza katika kufunga mabao, lakini unapokuja kutaka kuwatumia haiwezekani kwa sababu wao ni wa nje. Wachezaji wetu wa ndani tayari wanakuwa wamekata tamaa. Badala ya sasa kuitunza miili yao wanakwenda kwenye kuanza kutumia madawa ya kulevya ili wapate nguvu wafanane na wale wa nje, ambapo wenzetu lishe ndiyo bora kuliko kitu kingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Hafidh Ali amekuwa ni referee wa Kimataifa, amechezesha African Cup of Nations, amechezesha World Cup ya Vijana. Mchezaji kama Filbert Bayo mwanariadha, amekimbia Gidamis Shahanga na wengine wengi tu wamefanya vizuri kwa sababu walikuwa wanafuata zile ethics za michezo yenyewe. Leo hii itakuwa ni kazi kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu kiundwe chombo kizuri cha jopo la Madaktari kuweza kutusaidia kutupa ushauri na kuweza kuangalia jinsi gani tunaweza tukawa tunawapima wachezaji wetu wote kabla ya kushiriki kwenye michezo. Kabla ya kuanza ligi daraja la kwanza, la pili wanakuwa wamepimwa aki-qualify ndipo anaingia, asipo-qualify basi tunam-disqualify, anakuwa hayupo tena kwenye mashindano.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, nakutakia kila la kheri katika utekelezaji.