Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami nitoe mawazo yangu kwenye Mpango ulioko mbele yetu, hoja iliyoko mbele ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa siha njema ya kusimama kwenye Bunge hili. Nawashukuru wapigakura wa Jimbo la Vunjo walionichagua kwa zaidi ya asilimia 72 ya kura zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango uliopo mbele yetu unatakiwa ujibu yafuatayo:-
(1) Unakuzaje uchumi wa Taifa letu?
(2) Unasaidiaje vijana wetu kupata ajira?
(3) Ujasiriamali wa Taifa hili utaongezeka kwa kiasi gani?
(4) Sekta mbalimbali katika Taifa letu na hasa sekta binafsi Mpango huu utaishirikisha kwa kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza na hilo kwa sababu Taifa letu hapa tulipofikia sasa Serikali ya Awamu ya Tano siyo kwamba imeanza sifuri. Serikali zilikuwepo za tangu Awamu ya Kwanza mpaka sasa, lakini Taifa letu limekosa itikadi. Leo hii hatuna itikadi ya Taifa ya kutuonesha kwamba itikadi yetu ni nini na malengo yapo namna gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano nieleweke vizuri, wakati wa Mwalimu Nyerere tulikuwa na itikadi ya ujamaa, lengo likiwa ni kujitegemea na mifumo yetu yote, sekta zetu zote zilikuwa zinatekeleza itikadi ya ujamaa, lengo likiwa ni kujitegemea, lakini leo hii ukiangalia Mpango huu una-address au unatoa mwelekeo gani wa kuonyesha itikadi ya Taifa letu ni ipi kama ipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme itikadi ya Awamu ya Tatu ilikuwa ni uwazi na ukweli, ndiyo itikadi au ya Awamu ya Nne labda maisha bora kwa kila Mtanzania au ya Awamu ya Tano useme hapa kazi tu je, hiyo ndiyo itikadi. Tunatakiwa tuwe na itikadi ya Taifa, vyama vishindane kwenye msingi ile ambayo tumekubaliana ya Kitaifa. Kwa mfano, kwenye sekta ya elimu, siyo kwenye sekta ya elimuWaziri aliyekuwepo ndiyo aamue namna ya kuindesha sekta hiyo, tuwe tumekubaliana Kitaifa, sekta ya elimuinaongozwa hivi kwa miaka kumi au ishirini ijayo. Kwa hiyo, yeyote atakayeingia pale ataongoza kwa misingi ambayo imewekwa. Lakini hebu tuangalie muda tunaoupoteza kwenye kugombana, akiingia huyu anabadilisha, akiingia huyu anabadilisha na ni kuvuruga tu Taifa la Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuwe na maono ya miaka ishirini au thelathini ijayo, lakini siyo kwamba tunakosa mifumo na hasa ile mifumo inayolinda utu wa mwanadamu, inayokuza utu wa mwanadamu, mifumo hiyo ni ya elimu, mifumo hiyo ni ya kiutamaduni, mifumo hiyo ni yetu sisi kama Taifa ambayo inakuza zaidi utu wa mwanadamu, thamani ya utu wa mwanadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasoma Netherlands miaka ya 2007/2008, Bishop Acronson anakwambia maendeleo ya Netherlands yamepatikana kwa kasi kwa miaka 64 kwa sababu ya maelewano ya Kitaifa na kutambua utu wa mwanadamu upo namna gani, kutambua uhai wa mwanadamu upo namna gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii hapa Watanzania sisi sote ni watoto wa mama Tanzania, lakini kama sisi sote ni watoto wa mama Tanzania kwa nini tunabaguana? Kwa nini tunajenga misingi ya kulipasua pasua Taifa la Tanzania? Kwa nini tunajenga misingi leo hii Tanzania ni moja, anasema huyu wa Kusini, huyu wa Kaskazini, huyu wa Mashariki huyu wa Magharibi, ni kwamba tumekosa mifumo inayojali utu kwamba huyu Mtanzania ana haki kama Mtanzania mwingine, kama ni mifumo ya utawala bora, mifumo ya utawala wa kidemokrasia inalinda haki za wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesomea mambo ya majanga, yapo majanga ya aina kuu tatu na zaidi ya asilimia 95 ya majanga yote yanasababishwa na binadamu. Kuna known knowns risk, known unknowns risk and unknown unknowns risk ambazo ni acts of God, lakini hizi known known risk tunazisababisha sisi binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majanga kusipokuwa na utulivu kwenye Taifa, kwa mfano, mwaka 2013 Taifa lilikuwa limekwishaanza kupasuka misingi ya udini, waislamu na wakristo, Taifa litaongozwaje, kuuawa kwa viongozi wa dini, Taifa litaongozwaje, mipango itatekelezwaje, lakini tulipokaa watu ambao ni chini ya 100 Taifa lilitulia, Mheshimiwa Lukuvi alikuwepo kwenye mazungumzo yale tuliyojifungia watu chini ya 100 Taifa likatulia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi tukiwa na meza ya maridhiano, uundwaji wa dola siku zote duniani ni meza ya maridhiano, sisi sote ni Watanzania tuheshimiane na tukubaliane. Yanayotokea Zanzibar tusione kwamba ni mambo madogo, la hasha, ni mambo makubwa sana, yanayotokea Zanzibar leo hii tujue kwamba Tanzania tunaihitaji dunia kuliko dunia inavyoihitaji Tanzania. Narudia, Tanzania inaihitaji dunia kuliko dunia inavyoihitaji Tanzania. Leo hii Tanzania hatuwezi tukawa ni kisiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mipango tunayopanga hapa ni lazima tu-address suala la utawala bora na kwa kuwa tumekubaliana kwenye mfumo huu na Tanzania sisi siyo kisiwa je, duniani, let us think globally but act locally. Kama hatuwezi tuka-address kwamba dunia hii ambayo imeshakuwa leo hii ni kijiji, akili zetu zinajishusha kwamba dunia imekuwa ni kijiji kwa kasi ya maendeleo ya kasi ya sayansi lakini leo hii tunarudi hapa kuanza kuulizana wewe wa Kaskazini, wewe wa Kusini, wewe wa Mashariki, wewe wa Magharibi, wewe Mzanzibari, wewe Mbara tunaliua Taifa la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipokubali kwamba umoja wa Taifa la Tanzania ndiyo utakaoweza kulea kizazi hiki na vizazi vijavyo, tutakuwa tunajimaliza wenyewe. Sisi Wabunge majukumu yetu ya kwanza kwa Taifa tunalileaje Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo rasilimali nyingi tu za Taifa hili, nendeni kwenye ripoti ya kutekeleza Mpango huu na hili nitoe nasaha kwa Mawaziri, kuna baadhi ya Mawaziri wanasema tu sijui ili waonekane kwenye runinga, wanasema ohh, tunaweza tukajitegemea kwa rasilimali zetu sisi wenyewe, mtapata wapi fedha Serikali ya kujenga reli ya kati kwa standard gauge kwa rasilimali zetu sisi wenyewe humu ndani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kabisa kujenga reli ya kati na matawi yake yote kwa kuwa ndiyo langu kuu la uchumi wa Taifa la Tanzania. Tuimarishe Bandari ya Dar es Salaam, tuunganishe na mitandao ya reli, Taifa hili uchumi wake utakwenda kwa kasi kubwa sana. Tusianze kugombana na Kagame na Uhuru Kenyatta wametuamsha, tuwachukulie positively katika kujenga Taifa letu. Tusianze kulalamika lalamika tu hapa ohh, Kagame anatuzidi kete, Kenyatta, kwanza hata lugha hizo ni kwamba umeshindwa kufikiria. Nimeshawahi kusema kuna nguzo kuu sita za umaskini wa fikra ambazo ni ya kwanza, majungu; ya pili fitna; ya tatu umbea; ya nne kusema uongo; ya tano kujenga chuki na ya sita uvivu wa kufikiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, let us think big positively Taifa letu hili tutalipeleka mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Vunjo tunategemea sana sekta ya utalii, Tanzania ni ya pili kwa vivutio vya utalii duniani lakini Tanzania inashika nafasi ya 110 kati ya nchi 133 kwa…
Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.