Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa jioni ya leo kuchangia Bajeti hii ya Serikali, na nianze kusema naunga mkono hoja. Pia niungane na Waheshimiwa Wabunge wengi kukupongeza wewe binafsi na kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara ya Fedha walioandaa bajeti hii nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kujielekeza kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa saba. Hotuba hii alinukuu hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akifungua Bunge. Naomba ninukuu, kwenye ukurasa wa nane Hotuba ya Mheshimiwa Rais ilijielekeza katika kusema kwamba huduma zisizoridhisha za upatikanaji wa maji, elimu bora na afya ni mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano. Nimejielekeza kwenye hotuba yake, naunga mkono wazo la maombi ya kuongeza tozo ya Sh. 50 kwenye bei ya mafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunamalizia bajeti ya mwaka ambao Bunge lilipendekeza tozo ya Sh. 50 kwenye lita moja ya mafuta, bei ya mafuta ilikuwa sh. 2,100 mpaka 2,400. Hapa katikati bei ya mafuta imeshuka lakini hatukuona athari yoyote, hazikushuka bei za usafiri, hazikushuka bei za vyakula, hazikushuka bei za aina yoyote, lakini mpaka sasa bei ya mafuta ni 1,700 hadi 1,900 bado Watanzania wana uwezo wa kuhimili ongezeko la Sh. 50. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini naomba niunge mkono pendekezo hilo ambalo limetokana na Kamati yetu? Ni kutokana na hotuba hii ambayo Awamu ya Tano inajielekeza kutatua kero hizi kubwa za Watanzania. Ukiangalia hotuba yetu kero kubwa ya Watanzania ukiacha maji inayofuatia ni upungufu wa zahanati na vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka mmoja takribani akina mama 15,000 wanapoteza maisha, akina mama 42 wanapoteza maisha kwa siku, lakini sababu kubwa inayochangiwa kupoteza maisha kwa akinamama hawa ambao ni nguvu kazi ni uhaba wa vituo vya afya, uhaba wa zahanati na uhaba wa vifaa tiba. Pamoja na Serikali kuwa na nia nzuri, bajeti hii ninavyoiona hakuna kifungu cha moja kwa moja kinachoonesha ujenzi wa zahanati, ukarabati au kumalizia majengo yaliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika kwa nini nasema hivyo? Tuliwasilishiwa mkeka na Wizara ya TAMISEMI ambayo ilikuwa inaonesha takribani bilioni 32 zimetengwa na Halmashauri zetu, lakini ukiangalia vyanzo vya Halmashauri zetu ni own source, Local Government capital grant ambavyo vyote havina uhakika. Ndiyo kusema hata huu mkeka unaoonesha kwamba kuna vituo vya afya vitakarabatiwa, kuna zahanati zitajengwa, kuna wodi zitaongezeka, hauna uhakika kwa sababu chanzo chake hakina uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, sisi wote Wawakilishi wa wananchi ndio tunaowasemea wananchi wetu kama walikubali tozo ya Sh. 50 wakati bei iko 2,100 hebu tuwaongezee tozo na kiasi kikubwa itahimiliwa na sisi wenyewe ili tuweze kutenga kiasi cha pesa kuziongezea hizi bilioni 32 ili hali ya vituo vya afya na zahanati zetu iboreke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wa viwanda unategemea afya bora ya Mtanzania, lakini wanawake wakiwa ni moja ya nguvu kazi; tunategemea kuanzisha viwanda vya nguo, viwanda vya kubangua korosho; asilimia kubwa ya wafanyakazi ni wanawake, ambao wanahitaji kupata afya bora wakafanye kazi kwenye viwanda hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana na nasema hivyo naunga mkono hoja kwa sababu hata nikiangalia kwenye Mkoa wa Pwani kwenye orodha hii ya mkeka ulioletwa ni wilaya mbili tu; Kisarawe na Mafia. Wakati ninaposimama namkumbuka Daktari wa Zahanati ya Kijiji cha Kitomondo Kibaha Vijijini analala kwenye gari ndogo, hana nyumba na tulimwombea milioni 25 kumalizia nyumba. Tunapochangia Wabunge wanawake sekta ya afya inatuuma, inatugusa. Naomba Serikali ilitazame hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kama nilivyosema kwa sababu hata sasa tuna vituo vya afya 716 kati ya Kata 3,800 ni asilimia 18 tu, maendeleo ni mchakato lakini kama shilingi bilioni 30 katika shilingi bilioni 250 ambazo zitaongezwa kwenye miradi ya maji kwenda kwenye sekta ya afya, kupanga ni kuchagua. Naomba Bunge lako Tukufu kupitia Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tupange mipango hii vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningeomba kujielekeza ni suala zima linalohusu mfuko wa CAG, na mimi naomba niingie kwenye rekodi na naomba kwa sababu naamini Hansard itatumika vizazi vijavyo na ninawapongeza Wabunge wote waliochangia kuomba Serikali itazame jicho la huruma ofisi hii ni wazalendo, tunaliomba hilo kwa sababu tunaamini ni mmojawapo ya nguvu itakayomsaidia Mheshimiwa Rais wetu ambaye amejipambanua wazi wazi kwenye hotuba yake atapambana na ubadhilifu, atapambana na ufisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ina shilingi trilioni 29, matumizi ya kawaida shilingi trilioni 17, matumizi ya maendeleo shilingi trilioni 11, Ofisi ya CAG kufuatilia hizo hela, shilingi bilioni 18, kwenye matumizi mengineyo. Tuna Halmashauri 168 na mimi nayasema hayo kwa sababu nilishawahi kuwa Mkaguzi miaka kumi, najua adha ya ukaguzi! Najua utaratibu na kukagua unakagua kutokana na Tanzania Auditing Standards na International Auditing Standards, zipo taratibu. Leo tunapopeleka hela mpaka kwenye kijiji CAG anafikaje? Tunapopeleka hela kwenye zahanati, kwenye vituo vya afya, CAG anafikaje? Tunapopeleka hela kwenye pembejeo? (Makofi)
Kwa kuwa kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali, ushauri inategemea, lakini kazi yetu kubwa ni kuisimamia na tunaisimamia kupitia oversight committee. Nikuombe kwa kulinda hadhi ya Bunge lako na kwa kuwa kuisimamia Serikali ni kupitia oversight committee isije tunakuja Bunge lijalo Kamati zako PAC na LAAC zinakosa kazi ya kufanya. Hela hizi nyingi. Naomba sana itazame. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika nimemsikia Mheshimiwa Waziri wa Fedha anasema ataangalia, ameji-commit lakini mwezi wa 12 mapitio ya bajeti CAG anatakiwa amalize kazi zake, tunaende kwenye kufunga mwaka wa fedha za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliona na mimi niingie kwenye Hansard kwamba nimeisemea ofisi hii ili vizazi vijavyo viweze kuona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nimeona nia njema ya Serikali ya kuleta usawa kwenye masuala ya pensheni, nami naunga mkono. Lakini naomba usawa huu ubainishwe kinagaubaga ni makundi gani? Kwa sababu tunayo Sheria ya Retirement Benefits za Viongozi wa Kisiasa walitajwa pale! Lakini ieleweke wazi hata Wabunge wanalipa kodi shilingi 1,200,000 kwa mwezi; kwa mwaka shilingi milioni 15, kwa miaka mitano ni shilingi milioni 75. Wabunge hawa pia wanachangia shughuli mbalimbali za maendeleo. Hata kuzika, madawati tumeunga mkono, vituo vya afya tunaunga mkono, lakini isionekane Watanzania msikubali kuamini kwamba Wabunge eti ni kundi linalojipendelea, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ingekuwa mimi ningewaombea pia wafanyakazi wa Tanzania msamaha kwenye kiinua mgongo chao. Mfanyakazi anafanya miaka 40, miaka 30, anavyostaafu kwanini asipewe kiinua mgongo chake? Kwa kuwa kundi la wafanyakazi, kundi la wanasiasa ni kundi ambalo liko loyal kulipa kodi, kwa nini nisiwatetee? Kwa nini isifike wakati nao wasamehewe? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naunga mkono. Najua kuwa kweli kuna changamoto katika misamaha ya kodi, zimetajwa taasisi…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.