Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hotuba ya Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kukupongeza kwa kazi nzuri unayoifanya ambayo Watanzania wote na Wabunge wa CCM tunaamini kazi yako ni nzuri sana, kama jina lako lilivyo Tulia, uendelee kutulia kama ulivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza ku-declare interest kwenye upande wa viwanda. Nianze kusema tunapozungumza katika Serikali yetu ya Awamu ya Tano kuhusiana na suala la viwanda kwa ujumla. Tunavyo viwanda, tulikuwa navyo vingi vya pamba pamoja na viwanda vya nyuzi. Katika Bajeti ya Waziri wa Fedha, ukiitafakari na kuifuatilia ni nzuri sana imeonesha maeneo mbalimbali. Nizungumzie suala la pamba na wafugaji pamoja na samaki katika Kanda yetu ya Ziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kodi iliyopunguzwa ni shilingi 450,000 ukurasa wa 89 na shilingi 250,000, lakini vilevile tunategemea sisi watu wa pamba bei ya soko liko nje, tunajaribu kuangalia mali ambayo iko hapa nchini ambayo wanunuzi wake wako hapa, tayari moja kwa moja panakuwa na kodi kubwa. Mfano mashudu unapoyapa kodi tayari unaongeza gharama kubwa na anayefanya hii biashara ya mashudu ni mtu mdogo wa kawaida, muuza kuku na wafugaji wadogo wadogo, tayari wanaongeza bei ya pamba inaongezeka kupata bei nzuri angalau mkulima, ni kwa sababu control hatuna ya bei ya soko la pamba. Niiombe Serikali ijaribu kuangalia sana kwa mapana zaidi kuhusiana na suala zima la viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye upande wa alizeti, ukipita barabara ya kutoka Singida unaenda Shinyanga utakuta wananchi wameshaji-organise pale wanauza mafuta yale. Lakini Serikali lazima ifike mahali itazame ni namna gani iwasaidie na hawa wakulima wadogo wadogo ili ile mali iweze kuzalishwa vizuri zaidi, iingizwe kwenye soko, i-compete na masoko mengine, lakini hivi sasa inaangaliwa tu, hakuna jitihada ambazo naona kama zinafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile lazima tujipange kuangalia viwanda vyetu vidogo vidogo; mfano viwanda vya SIDO, mimi kwangu kule kwenye Jimbo langu la Itilima ninalo eneo kubwa la SIDO, lakini sijawahi kuona Serikali imekuja kutembelea na kupata mawazo katika eneo lile husika lakini kila siku tu tunakutana tunazungumzia viwanda. Niombe sana Serikali ya Awamu ya Tano iweze kufanya kazi hiyo ili iwafikie wahusika tuweze kuboresha viwanda vyetu na wananchi waweze kupata bei nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia habari ya viwanda na vingine. Wenzetu wanaoendelea kwa kasi sana mfano kama Wachina, ziko Benki za Maendeleo ambazo zina-finance wawekezaji, lakini leo nchi yetu hii ukiitazama vizuri sana utakuta gharama ziko kubwa, mtu akitaka kuingiza kiwanda lazima atachajiwa kodi na anaenda kuwekeza zaidi ya miaka miwili, mitatu ndiyo ataanza kupata profit. Moja kwa moja inakuwa ni gharama kubwa katika uendeshaji na hawezi kuendesha kiwanda hicho husika kwa asilimia 100, matokeo yake ni hasara hata fit katika competition ya biashara katika nchi zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia kuimarisha uwekezaji wetu wa ndani, mimi niiombe Serikali iweze kujua na kufuatilia ni kwa nini wawekezaji wetu wa ndani kila mwaka wanashuka chini, lazima kuna sababu za msingi ambazo zinasababisha. Ukiangalia nchi yetu wakati inapata uhuru, Mwalimu Nyerere yuko nayo kuna vitu vingi ambavyo viliachwa katika nchi hii. Kulikuwa na Musoma, kulikuwa na Mwanza MWATEX, kulikuwa na Tabora, kulikuwa na Urafiki, kulikuwa na Mbeya; zote zile hazifanyi kazi lakini kila mwaka tunapokutana tunaposikia bajeti, tupo wadogo mpaka tumeingia humu Bungeni tunasikiliza mipango, mipango. Ningeomba sasa kwa sababu Waziri wa Fedha ni Mpango, mipango hii sasa ifanane na jina lake, aweke mipango mizuri ili tutoke hapa tulipo tusonge mbele kuleta maendeleo katika nchi yetu na Taifa letu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie suala la Benki ya Kilimo. Serikali imefanya jambo jema la kuhakikisha inaweka Benki ya Kilimo, sasa tuiombe nayo hii Benki pamoja na msimamizi wa Serikali ambaye ni Waziri wa Fedha awahamasishe sasa watoke mjini waende vijijini. Waende kwenye mikoa ambayo inazalisha siyo kuja kuendelea kulalamika na kuomba fedha hata zile ambazo Serikali imeshatenga bado hazijafanyiwa kazi. Tukifanya hivyo tutakuwa tunawajenga wakulima wetu kuweza kujua jinsi ya matumizi mazuri ya benki na vitu vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie katika suala zima la ufugaji. Lazima tufika mahali tutambue kwamba ufugaji ni nini na unaingizaje pato katika nchi yetu. Tunapozungumzia ufugaji nao wanahitaji watengenezewe mazingira ambayo ni mazuri na ni salama ya kuweza kunufaika na maeneo yetu.
Tunatambua kabisa katika nchi yetu tunaamini kabisa kwamba tunahitaji hifadhi na kadhalika, juzi Mheshimiwa Waziri wa Maliasili alikuwa anajibu swali langu alisema vijiji vinavyopakana na kandokando ya hifadhi zinapata asilimia 25 ya fedha zinazotozwa, siamini kama zile fedha kweli zinaenda tofauti na hela tu ndogo, nitaomba Mheshimiwa Waziri nitamtafuta kwa muda wake anielekeze ni jinsi gani kwa sababu naamini hela zinazokuja ni kidogo sana wala haziwezi kuwasaidia wananchi katika maeneo hayo wanayoishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze Benki ya Maendeleo. Benki ya Maendeleo ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu. Kama tunataka tujenge viwanda na kama tunahitaji tuwekeze katika maeneo mbalimbali, hii benki ikiwezeshwa na ina wataalam inaweza ikafanya kazi kubwa, nzuri ya kuingiza fedha nyingi bila kutegemea kodi tu kwa sababu itazungusha na wale watu wawekezaji watakuja kukopa katika benki yetu hii na itaweza kuzalisha fedha nyingi katika kuleta uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niishauri Serikali, hii kodi ambayo imewekwa kwenye mabenki, ninavyoiona inaweza ni nzuri kwa sababu tunahitaji tupate kodi, lakini kwa mtazamo wangu na muono wangu na kuishauri Serikali tunaweza tukajikuta tunapoteza deposite nyingi kwenye mabenki kwa sababu kodi itakayotozwa ni hela nyingi sana. Sasa hivi kama una wafanyakazi 300, ukipeleka kwenda kufanyiwa malipo kila mfanyakazi mmoja ni shilingi 3,000 kwa hiyo utakuta watu hawaweki hela kwenye benki wataamua kutumia njia zingine, tayari nchi itaanza kuyumba katika hali ya kiuchumi. Niombe hilo nalo waweze kuliangalia ni jinsi gani ili waliboreshe vizuri zaidi na lengo letu ni kupata mapato mengi ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie katika Kanda, mfano Kanda ya Ziwa iangalie ni viwanda gani vinavyohitajika katika maeneo yetu. Leo hivi sasa tunazungumza bei ya pamba haieleweki na wakulima nao wanasubiri wauze waweze kupata fedha zile, lakini kila mwaka zao hili linadorora, ukifuatilia zaidi zao hili linaingiza fedha nyingi sana kwa mwaka, mwaka jana tumepata dola bilioni 6.4, lakini hakuna kipaumbele kinachowekwa na Serikali kuhakikisha kwamba hawa wakulima wa zao la pamba tunawasiadiaje kuongeza hizi gharama, matokeo yake zinaongezwa tu kodi katika maeneo husika na imefika mahali Serikali hata ruzuku ya pembejeo haipeleki, kwa mwaka wa jana haikupeleka hata senti moja, wakulima wenyewe wanaendelea kujiendesha. Niiombe Serikali ijaribu kuangalia namna gani kuhakikisha inatatua tatizo la bei ya pamba katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho tukitaka tuende vizuri, zao hili la pamba linaweza likajiendesha vizuri sana, zikipungua kodi ambazo hazina msingi, ambazo zinazosababisha kuongezeka kwa bei, kwa sababu hatuwezi tukasema kwamba tuzuie kodi, lakini lazima tuangalie kwamba inaingiza kiasi gani kwenye nchi dola za kigeni na asilimia kubwa nchi inatumia fedha za kigeni nyingi, kwa sababu mahitaji mengi hatunayo hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie ni jinsi gani itasaidia katika eneo hili ili tupunguze malalamiko katika maeneo na ipunguze hizi kodi ambazo hazima maana. Kweli naiomba Serikali suala kabisa la mashudu watoe kodi haina sababu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia 100.