Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nikupe pole kwa yaliyotokea maana mimi nipo karibu nao hapa, nilisikia minong‟ono yao tangu mapema. Tunakushukuru kwa uvumilivu wako mkubwa maana kwa kweli waliamua kufanya vurugu ambayo wala haikuwa na msingi wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna moja nilitaka kulisema lakini lingenoga kama wangekuwepo. Nataka niwakumbushe Wabunge wa CCM kwamba hii Serikali ni yetu sisi na sisi ndiyo wenye ajenda, wao hawana cha kupoteza hawa. Nilikuwa nafikiri ni vyema na sisi tukalifahamu vizuri jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kuna Mbunge mmoja amezungumza ningependa angekuwepo rafiki yangu yule kwamba Wabunge wanajikombakomba, jambo hili limenikera sana. Hatuwezi kujikomba Serikali ni ya kwetu sisi. Rais huyu anatokana na Chama cha Mapinduzi ndiye anakuwa ni Rais wa Watanzania wote. Kwa hiyo, Serikali hii ni ya Chama cha Mapinduzi of course inafanya kazi kwa wananchi wote. Ndugu zangu Mawaziri mlioteuliwa na Mheshimiwa Magufuli msonge mbele kwani ajenda iliyopo mbele yetu ni kubwa na tusipepese macho. Twende kwa malengo yetu ili tuwe na cha kusema mwaka 2020 vinginevyo wenzetu hawa kwa msingi mkubwa hawana cha kupoteza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee naomba niwashukuru wananchi wa Kasulu Mjini kwa kuniamini, kwa kunituma kuja hapa na kwa kunirudisha Bungeni. Walinipeleka likizo lakini wameamua wao wenyewe kwa mapenzi yao nirudi hapa. Nami nawahakikishia kwamba sitawaangusha na nawashukuru wananchi wa Kasulu kwa kuchagua Madiwani wengi wa CCM na kura nyingi za Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hotuba hii kwa maoni yangu, ningeshauri sana hotuba hii iwe ni input kwenye Mpango wetu wa Maendeleo kwa sababu imegusa kila kitu ambacho wananchi wanakilalamikia. Ukurasa wa 6 Mheshimiwa Rais amezungumzia vitendo vya rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Ukienda ukurasa 12 anazungumza hayo hayo lakini anahitimisha ukurasa wa 25 ana-quote maneno ya Mwalimu Nyerere miaka ya 1980 ambaye alisema hivi:- “Rushwa na ufisadi havina budi kushughulikiwa bila huruma kwa sababu naamini wakati wa amani, rushwa na ufisadi ni adui mkubwa wa ustawi wa jamii na ni adui mkubwa kuliko hata wakati wa vita.” Hayo ni maneno ya Mwalimu Nyerere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 6, 11, 12 na 25, Mheshimiwa Rais ameonekana kukerwa sana na vitendo vya rushwa na wizi. Lazima tumsaidie kwa nguvu zetu zote kupiga vita rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nitoe mfano tu, katika kipindi cha mwaka 2012 - 2015, miaka mitatu tu, sisi wenzenu wa Halmashauri ya Kasulu, kwa mujibu wa ripoti ya CAG, tuliibiwa fedha shilingi bilioni 5.9 na wakati huo, ndiyo nataka na rafiki zangu wangesikiliza, waliokuwa Wabunge wa Majimbo yote mawili, Jimbo la Kasulu Mjini na Jimbo la Vijijini walikuwa ni wapinzani hawa. Wizi uliopitiliza, wizi uliotamalaki umetokea wakati wapinzani hawa wanasimamia Halmashauri yetu ila kule tumewashinda, tumewashughulikia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona Waziri wa TAMISEMI simuoni hapa, niombe kwa Waziri Mkuu, yale majizi yaliyotuibia kule Kasulu bado yapo. Wengine wamehamishwa, wengine wamestaafu na wengine eti wamepewa likizo za kustaafu. Tunaomba sana, Waziri Mkuu na Waziri wa TAMISEMI, bahati nzuri tumepata nyaraka muhimu sana za wote waliohusika, nitazipeleka kwa Waziri Mkuu ili majizi haya yashughulikiwe na mkondo wa sheria uchukue nafasi yake na yale yatakayotiwa hatiani hakika tuyapeleke jela pengine kule magereza ndipo ambapo wanastahili kuishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nimefarijika Mwanasheria Mkuu wa Serikali amenidokeza kwamba kumbe sheria ya kufilisi mali bado iko, haya majizi yanayotuibia nafikiri wakati sasa umefika, kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali sheria hiyo isimamiwe vizuri haya majizi tuyafilisi jamani haya. Wanaiba, wanafungwa wanarudi, tuyafilisi majizi haya ili nchi yetu iendelee kuwa na ustawi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Mheshimiwa Rais amelizungumza na aliliona kama ni kero kote alikopita ni tatizo la maji. Maana ni ukweli usiopingika kwamba wanawake wa nchi hii ndiyo wametupa utawala huu na wanawake hawa ndiyo wanateka maji. Nafikiri wakati umefika kwa kweli wanawake hawa tuwape faraja ya kuwaondolea mzigo wa kuteka maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kule kwetu Kasulu sisi hatuna shida ya vyanzo vya maji na Waziri wa Maji analijua hili. Vyanzo tunavyo, shida ni kuviendeleza tu ili kuongeza mtandao wa maji katika Mji wa Kasulu ili hatimaye katika kata zinazozunguka Mji wa Kasulu ziweze kupata maji ya kutosha. Vyanzo tunavyo, tunahitaji fedha wala si nyingi sana ili tuweze kuwa na mtandao mkubwa wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 11 Mheshimiwa Rais amezungumzia na ametukumbusha juu ya nia na sera za CCM za kujenga barabara za lami kuunganisha mkoa na mkoa. Hili jambo ni la kisera wala siyo la utashi wa mtu, barabara ya kuunganisha mkoa na mkoa ni kipaumbele cha Serikali ya CCM. Waziri wa Fedha unalijua suala hili vizuri, sisi barabara ya Kigoma – Nyakanazi haina mbadala kwa sababu inatuunganisha na Mkoa wa Kagera, Geita, Mwanza na Shinyanga. Barabara hii kwetu haina mbadala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilidokeze kidogo tu ni suala hili la ujenzi wa reli, tumeshalizungumza sana.
Mimi ni muumini katika uchumi wa reli, bila nchi kuwa na reli hakuna kitu kinachoitwa kukuza uchumi. Huwezi kukuza uchumi au ukafikiria kuingia katika uchumi wa kati kama huna railway system. Hilo naliamini kabisa kwa nguvu zangu zote na Waziri wa Fedha bila shaka na yeye anaamini hivyo. Tutizame reli ya kati kwa jicho la kwenda kubeba mzigo ulioko Kongo ya Mashariki. Kule Kongo ya Mashariki kuna tani milioni tatu za shaba zinataka kwenda Ulaya na njia muafaka na nyepesi ni kupita reli ya kati, bandari ya Dar es Salaam na mwisho kwenye masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni wakimbizi. Jambo la wakimbizi sisi kwetu ni jambo kubwa na sisi wenzenu wa Mkoa wa Kigoma tumebeba dhamana ya kubeba wakimbizi hawa. Tuna wakimbizi kutoka Kongo, Rwanda, Burundi na kusema kweli tuna wakimbizi kutoka Somalia. Wote hawa wako katika Mkoa wa Kigoma. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Rais kwa asilimia mia moja kwa mia moja. Nashukuru sana. (Makofi)