Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia katika huu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2017/2018 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri kwa maelezo yake mazuri na mipango mizuri niliyoiona katika maelezo yake na hotuba yake. Vilevile naipongeza Kamati husika nao wametoa mapendekezo mazuri tunawapa pongezi sana kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kwamba Serikali inakwenda kuongeza kiwango cha Bajeti kutoka trilioni 29.5 kwenda kwenye trilioni 32.9. Nawapongeza sana kwa mawazo mazuri na mipango hii mizuri, kwa sababu hii ni ishara kwamba Serikali ya CCM imejipanga sawasawa kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi wake ikiwa ni pamoja na kutoa elimu bure bila malipo, umeme vijijini, barabara za vijijini, maji safi na salama na huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi na changamoto nyingi ambazo zimeonekana katika Bajeti ambayo imepita, hivyo tunavyo-focus kwenda kwenye Bajeti hiyo kubwa ni lazima basi Serikali iwe na mikakati mizuri na mipango ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na vyanzo vizuri vya kuweza kupata pesa ili tuweze kukamilisha yale malengo tunayoyahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama katika Bajeti ya Mwaka 2016/2017, ambayo ndiyo tunaendelea nayo sasa hivi tuko katika quarter ya pili, kwa maana ya kwamba quarter ya kwanza tumeimaliza tunakwenda kwenye quarter ya pili leo ni tarehe moja ina maana tuna mwezi mmoja wa quarter ya pili. Tukitazama ni kwamba pesa za maendeleo zimekwenda kidogo sana, hii ni kwa sababu pengine kuna mikakati fulani haikukaa sawa, basi hili tunaomba lisijitokeze tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokwena kwenye mwaka mpya wa fedha na tumeweka makadirio makubwa ya kiasi hicho cha shilingi 32.9 trilioni inabidi tujifunge kibwebwe kwelikweli kuhakikisha kwamba tunaongeza mapato ambayo yataweza kuwezesha bajeti hii kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kuchangia kwenye masuala ya fedha. Pamoja na kwamba tunakwenda katika mkakati na mpango huu, kuna tatizo kubwa limejionesha katika taasisi mbalimbali za kifedha. Kulikuwa kuna tatizo la kupeleka pesa ambalo Mheshimiwa Mpango naye ni shahidi, ni kwamba waliamua kupeleka pesa kwenda BOT yaani Central Bank kutoka kwenye taasisi kubwa za kifedha, kwa mfano NSSF na taasisi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa mabwana walikuwa wanapeleka pesa kwenye hizi commercial banks mara ya kwanza, kwa mfano, NSSF walikuwa wanapeleka mabilioni mengi kwenye hizi commercial banks na kule commercial banks walikuwa wanalipa interest kwa maana ya kwamba walikuwa wanawalipa kila mwezi kiasi fulani cha fedha ambazo hawa NSSF walikuwa wanaweza na wao sasa kutumia pesa zile za interest kuweza kuwalipa wateja wao, kwa maana ya zile benefits wanapojiondoa kwenye mafao. Sasa unapoziondoa zile pesa kupeleka Central Bank ina maana kwamba ile biashara umeiondoa kwa hawa wahusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kunakuwa na impact nyingine kwenye commercial bank kwa sababu wanakuwa wamekosa pesa, sasa hivi na wao nao wanakosa pesa ya kuwakopesha wateja wao. Unapowakosesha pesa ya kuwakopesha wateja wao yaani wafanyabiashara, hizo benki na zenyewe zinakufa kwa sababu zinashindwa kupata interest kutoka kwa wafanyabiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mtindo huu naomba Serikali itazame kwa macho mawili huu mpango, iweze kubadilisha, kurudisha zile pesa kwenye commercial banks. Unavyoziondoa ina maana kwamba hizi benki za kibiashara unaziua na kwamba zisiwe na uwezo tena wa kukopesha wateja wao. Hivyo basi tunaomba Serikali itazame upya, kwa sababu kwa kupeleka pesa kule ina maana kwamba benki isingekufa na Serikali ingeendelea kupata pesa pale inapohitaji pesa, lakini mnapopeleka Central Bank ina maana kwamba mnakwenda kuziweka kwenye shelf hizi pesa, zinakosa mzunguko, hakuna anayelipa interest na mwisho wa siku tunashindwa kupeleka pesa kwenye maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la bandari. Suala la bandari tunalipigia kelele kwenye mambo makubwa mawili tu. Jambo la kwanza ni VAT kwenye auxiliary services on transit goods. Sisi Tanzania tumesaini mkataba wa Vienna, tulisaini mkataba wa World Trade Organisation (WTC), mteja anayepita Tanzania au raia wa nchi nyingine anayepita Tanzania anapopewa huduma au anaponunua kitu, unapokwenda nchi nyingine yoyote wewe kama ni mgeni ukinunua hata shati, unapotoka kama ulilipa VAT unarudishiwa! Kwa nini tunaweka VAT kwenye mizigo ya watu wanaokwenda nje? Kwa nini tunakwenda kinyume na mikataba? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kukosa hivi ni kwamba tunaweka mazingira magumu, hawa wafanyabiashara wa Congo na sehemu zingine tunawa-charge hizi VAT, matokeo yake ile VAT inakwenda kwa wateja wao. Mwisho wa siku wanakwenda kwenye bandari zingine, wanaamua kwenda Mombasa, wanakwenda Beira kwa sababu kuna charge kubwa inayochajiwa katika Bandari yetu. Tunaomba hiyo VAT iondolewe. Tuliyazungumza kwenye mpango wa mwaka 2016/2017 na nalirudia leo katika huu Mpango wa 2017/2018, ondoeni! Tunazidiwa na bandari za majirani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine katika bandari tumezunguka tumeliona, kuna kitu kinaitwa single customer territory, huo mkataba ni tatizo. Tulioingia mkataba ni nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Congo haipo kwenye huu mkataba. Sisi tumesaini, tumewahi, tumeingia kwenye huu mkataba leo Wakongo wanachajiwa kodi kwenye bandari ya Dar es Salaam, risk ya mteja anapochajiwa mzigo wake Dar es Salaam, mfano mafuta amechajiwa Dar es Salaam, akatembea katikati gari likapata ajali, mafuta yakamwagika yule mteja anapata hasara mara mbili kwa sababu anakuwa amenunua, hasara na amelipa kodi, hasara mara ya pili, tuna kiherehere gani cha kwenda kusaini hiyo mikataba? Matokeo yake hawa wateja wanahama wanakwenda Beira, wanakwenda Mombasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari iji-assess upya, Serikali iangalie bandari ina matatizo yapi na isitoshe bandari iwe na kitengo cha marketing, waweze kufanya research na kugundua ni nini tatizo limewafanya wateja wa Congo na sehemu zingine waondoke? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo mawili yamefanya wale watu wanaofanya biashara ya copper badala ya ku-export mzigo katika bandari ya Dar es Salaam wana-export kupitia bandari ya Beira. Meli kubwa hawawezi wakaja Dar es Salaam kama hawana uhakika wa kushusha mzigo na kupakia mzigo. Hizi shipping zinataka uhakika wa kushusha mzigo na kupakia mzigo, wasipokuwa na uhakika wa kupakia mzigo wa ku-export maana yake ni kwamba wataleta mizigo mingine kwa gharama kubwa kufidia ile mizigo wanayoikosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ondoeni hizi sheria tuziangalie upya. Kwa kufanya hivi tumeondoa wafanyabiashara wakubwa. TATOA wana magari 26,000; magari asilimia 60 yamepaki ambayo ni magari 15,000 ina maana kuna madereva 15,000 wamesimama hawana kazi, utingo 15,000 wamesimama hawana kazi, vipuri hawauzi, wenye matairi hawauzi, ina maana wale wafanyabiashara wa mafuta hawauzi mafuta, mama ntilie anakosa biashara, mwenye guest anakosa biashara, mwenye M-PESA anakosa biashara. Maana yake tumedhibiti mapato ya milioni 600 halafu tukazuia circulation ya bilioni sita, what are we doing? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye kilimo na hasa kilimo cha pamba, kuna mpango wa C2C naomba uzingatiwe, tuna soko kubwa sana la nguo Afrika Mashariki, tuna nchi tano, Tanzania yenyewe tu ina watu karibu milioni 50 sasa, ukienda na nchi zingine tuna watu zaidi ya milioni 100, hawa watu wote wanavaa nguo kutoka China, wanavaa nguo kutoka India na sehemu zingine, Tanzania tuna uwezo wa kulima pamba ya kutosha, tuna uwezo wa kufungua viwanda vya nguo na hivi viwanda vya nguo vikaweza kuzalisha nguo za kutosha kuuza soko la East Africa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tusitegemee mtu binafsi atajenga kiwanda cha nguo. Kiwanda cha nguo ni jambo ambalo Serikali inatakiwa i-intervene iingie kwenye ku-invest kwenye viwanda vikubwa kwa kufanya spinning, kutengeneza vifungo, kutengeneza ribbons, kutengeneza vitu mbalimbali ambavyo vinaunda nguo, pawe na industry ya textile maalum kwa soko la Afrika Mashariki, tuende huko. Tukishafanya vile ina maana kwamba tutakuwa na soko la uhakika na kuweza ku-export nguo zetu katika soko la East Africa na mkulima wa pamba, pamba yake itauzika na mkulima wa pamba atapata soko la uhakika kuliko sasa hivi mnavyotuendesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa viwanda napenda kumalizia, kuna watu wanaitwa TEMDO. TEMDO wana teknolojia ya kutengeneza mitambo midogomidogo ambayo inaweza ikamsaidia mwananchi wa kawaida, tukawa na viwanda vidogovidogo hata vya ndani, mtu akawa na kiwanda kidogo cha kukamua alizeti, kiwanda kidogo cha kutengeneza soksi, kiwanda kidogo cha kutengeneza bidhaa ndogondogo ambazo ni highly consumed katika market yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ina maana kwamba, tukiwawezesha hawa ndiyo tutaweza kupata uchumi wa viwanda, lakini leo TEMDO hawapewi hela, leo tumekwenda kwenye quarter ya pili, TEMDO hata senti tano hawajapewa, wakati wanatakiwa wanunue vipuri, wanunue spare mbalimbali waweze kuvumbua zile teknolojia na kuwauzia watu wengine waweze kufyatua mashine mbalimbali ndogondogo kwa ajili ya viwanda vidogovidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tuwabebe akinamama, tubebe vijana, tunataka kwenda kuwapa milioni 50 ya mitaji, lakini kama tutawapa mitaji kwa maana ya kuchuuza, kuchukua bidhaa moja iliyotengenezwa yaani finished product kwenda kwenye soko lingine kila mtu anafanya, tunataka twende kwenye uchumi wa uzalishaji, uchumi wa kila mtu aweze kuzalisha kuondoa state moja ya bidhaa ya kilimo, kwenda kwenye new state, haya ndiyo yanayoweza yakatuondoa, bila hivyo hatuwezi kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho, tuangalie kodi hizi ndogondogo ambazo ni kero zimezungumzwa katika bajeti iliyopita, lakini bado kodi ndogondogo ni kero. Tumehesabu kodi zinazochajiwa ndogondogo ziko kodi zaidi ya 41 tumeziona ziko wazi, tuziondoe hizi kodi zinawafanya watu waweze kurudi nyuma, zinawafanya watu wasiweze kwenda mbele. Tunaomba hizi kodi ziangaliwe upya, tunapokwenda katika mkakati huu na mpango wa mwakani ina maana tuhakikishe kwamba tunaziondoa kodi ambazo ni kero, tunakwenda kwenye kodi chache zinazoweza kumwinua mwananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wananchi wa kawaida wapewe mikopo midogomidogo ili waweze kujinasua pale walipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.