Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Konde
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami kabla ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kusimama hapa na pia napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwajalia Wabunge wenzangu wote ambao tuko hapa, tupo katika hali ya afya njema na salama kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza kabla ya kutoa mchango wangu wa mpango huu kuitakia heri Kamati ya Uongozi ya Chama cha CUF chini ya Jenerali Julius Mtatiro. Pili nimtakie kheri kipenzi cha Wazanzibari, Maalim Seif Sharrif Hamad nikimwambia zidisha uzi huo huo na kwa niaba ya Wabunge wa Chama cha Upinzani cha CUF, wote wako pamoja na wewe na Kamati ya Uongozi wa CUF na hawatayumba na hawatayumbishwa, wale wote wenye dhana kwamba CUF itakufa, watakufa wao kabla CUF haijafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Stanslaus Nyongo aliongelea suala la mdororo wa mizigo katika bandari yetu. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Nyongo ni Mjumbe mwenzangu tuko katika Kamati moja inayoongozwa na Mwenyekiti shupavu Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango kama huu mwaka uliopita mimi ni miongoni mwa waliosimama hapa kwa mdomo huu huu, kiti hiki hiki, kipaza sauti hiki hiki nikatahadharisha juu ya mpango wa Serikali kuingia kwenye mfumo mmoja wa himaya hii ambao utawafanya Wakongo walipie mizigo yao kabla ya kuondoka katika bandari ya Dar-es-Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitahadharisha kwa kujua kwamba, athari zake wafanyabiashara wa Congo wana mbinu zao ambazo hazihusishi nchi yetu na nikatahadharisha sana kwamba, tutahadhari na mpango ule tusijiingize katika jambo lile ambalo limekuwa ni source moja kubwa ya mdororo wa mizigo katika bandari ya Dar-es-Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri sana tulipopata bahati ya kwenda katika Bandari ya Dar-es-Salaam Kamati yetu kutembelea na kuona uhalisia wa mambo ulivyo na taarifa tulizopewa na Watendaji wa Bandari, tuliporudi na kuiambia Serikali ukweli wa tulichokiona, zilikuja tafsiri tofauti tofauti ambazo tulionekana sisi ni waongo na hatuna ukweli katika tunayoyaeleza, au tumetumwa au tunatumiwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bunge yenye mchanganyiko wa Vyama vyote inakwenda kufanya kazi kwa ajili ya maslahi ya kuisaidia nchi hii, leo tunapoeleza ukweli, tunapokuwa tofauti na Watendaji wa Serikali ambao wanaogopa kumwambia Rais ukweli, huu ni ukweli! Wanaogopa kumwambia Mheshimiwa Magufuli ukweli uko hivi, wakadharau na wakasema waliyoyasema, lakini namshukuru Mwenyezi Mungu kitu cha ukweli kitaonekana tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Waziri wa Biashara na Viwanda, Mheshimiwa Charles Mwijage, akikutana na Taasisi ya Wafanyabiashara Wasafirishaji (TATOA), kauli aliyosema ni ushahidi Watanzania nyote mmeisikia. Amekaa na wenye ma-truck anawaambia kwa muda waliofikia mizigo katika bandari yetu imepungua na sasa kinachofuata ni malori yenu mtafute parking myaweke na ikiwezekana wekeni vilainishi (grease), ili msubiri, hatujui ni mwaka huu au mwaka ujao. Nani mkweli na nani mwongo? Kamati kweli au Waziri mwongo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu mhukumuni kwa matendo yake, msimhukumu kwa dhana hafifu. Tuliyasema yale, leo Waziri amekuja kumthibitishia Rais kwa mlango wa nyuma kama ni kweli Kamati iliyoyasema, mdororo wa mizigo Bandari ya Dar-es-Salaam umekithiri na umeathiri sekta nyingi sana. Umeathiri uuzaji wa mafuta katika ma-truck, umeathiri huduma za mahoteli, umeathiri hata wale madereva, dereva yule wa truck kutoka Tanzania hadi Congo ana vituo chungu nzima, humo si ajabu wengine wameshazaa na watoto! Watu wale leo hawapiti, mashaka yameongezeka, uchumi umedorora, mahoteli yamefungwa! Sisi tunasema ukweli, ule mpango haufai na tunaiomba Serikali izingatie hili na iuondoe mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi katika huduma za mizigo ya transit ni kigezo cha pili ambacho kimesababisha wafanyabiashara wa Congo wakimbie! Naomba Mheshimiwa Waziri, jambo hili pia walizingatie kwa makini ili bandari yetu irudi katika hali yake, wafanyabiashara warudi na sekta za uchumi za nchi hii ziweze kupanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingi duniani ndani ya siku 100 za utawala wao huwa wanatoa taswira ya hali za uchumi za nchi zao zinavyoendelea, leo tuna mwaka mmoja wa utawala huu wa Chama kizee bado hatujajua hasa Watanzania wanaelekea wapi katika mfumo wa uchumi wa nchi hii. Hili ni jambo la kusikitisha sana! Sasa tunapowaambia hapa siyo kwamba, tunawaambia tunawachukia, tunawaambia ili mjue kama ni wajibu wetu kuwawakilisha wananchi na kuwaambia yale yaliyo ya kweli na hakuna budi myafuate, kwa sababu, sisi pamoja na kwamba ni washauri, lakini mshauri anayemalizia na kuwa na azimio huyo ni mshauri tofauti na washauri wa ngoma za mtaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie Kituo cha Uwekezaji ambacho kimeandikwa katika taarifa ya Kamati, Kituo cha Uwekezaji cha Biashara cha Kurasini; mradi huu mkubwa wa Kituo cha Uwekezaji cha Kurasini ni jambo lililoanza mwaka 2010 na Bunge lililopita kwa mara ya mwanzo walitakiwa kulipa bilioni 45 Tanzania shillings ili kuuwezesha mradi ule mkubwa wa uwekezaji uwepo ndani ya nchi yetu. Matokeo yake mradi ule ulisuasua kutoka shilingi 45 bilioni ukaenda mpaka shilingi bilioni 60 ni mwaka wa pili, ukaenda mpaka shilingi bilioni 90 mwaka wa tatu, ukaenda mpaka shilingi bilioni 120, ndiyo matokeo yake umemaliza kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha leo katika taarifa hii nimeona wanasema kama wale wafadhili ambao walikusudia kuendeleza mradi ule kuutekeleza wameondoka na haijulikani hatima yake. Tukumbuke kwamba, pesa za Watanzania zilizotumika, Watanzania walioondolewa maeneo yale kupisha mradi ule ni gharama kubwa ambayo imepatikana na maslahi hayaonekani yako wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo ni nini? Tatizo ni kuchelewa kwetu kufanya maamuzi katika mambo ya msingi ya nchi hii. Tunachelewa, ni hodari sana wa kuandika kwenye karatasi, lakini ni wazito sana wa kutekeleza yale ambayo tunadhani yanaleta tija kwa nchi hii. Leo mradi ule ambao ulikuwa unagombaniwa na nchi zote za Kiafrika, Tanzania ikapata bahati ikachaguliwa na China kuletewa mradi ule mkubwa tumekaa hapa tumebabaika-babaika mpaka tayari mradi ule, leo nimeona kwenye taarifa umeondolewa wakati Tanzania ikiwa imeshalipa mabilioni ya shilingi kupata lile eneo na Watanzania waliokuwa wakiendesha maisha yao pale wametupwa hata hatujui wametupwa wapi! Leo matokeo yake tunakuja kuona hapa kwenye taarifa kama wafadhili wale wamejiondoa. Hiyo ni hasara nyingine kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huku kusuasua kwa kutekeleza miradi ambayo ni fursa kwa nchi inatueletea shida sana. Leo ni mwaka karibu wa 10 tunazungumza ndani ya nchi hii kuna chuma pale Liganga na Mchuchuma na kwenye mpango huu, kila mpango unaokuja tunaambiwa, tunasadikishwa kwamba, mradi wa chuma Liganga na Mchuchuma utafanyika, lakini matokeo yake tunaishia kusoma vitabu! Laiti mradi ule ungekuwa uko Kenya au Uganda au Burundi, leo tayari nchi zile zingekuwa zinazalisha chuma kile kwa wingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana Mwenyezi Mungu akishawapa anawapa, lakini kwa ugoigoi ambao tuko nao hata kama ingekuwa Mwenyezi Mungu anafikiria kuuondoa, bora angeuondolea mbali kwa sababu anatupa riziki tuzitumie kwa niaba ya watu wetu, lakini hatuwezi kutumia zile fursa, badala yake tunaandika kwenye makaratasi tu hatuwezi kufanya chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu tena leo nimeona nia ya Serikali juu ya kufufua viwanda. Imezungumzwa hapa General Tyre ya Arusha na viwanda vingine, TEMDO na kadhalika. Mheshimiwa nyimbo hizi hebu sasa Waheshimiwa Mawaziri, Serikali, wawe tayari kile wanachotusadikisha kinaweza kufanyika waweze kukifanya kwa muda unaowezekana. Leo hakuna asiyejua kwamba nchi ina demand kubwa ya matairi ya magari, biashara ya matairi ya magari ni biashara kubwa sana duniani, leo fursa ipo, mipira ndani ya nchi hii inazalishwa, lakini bado tunaimba wimbo tunafufua General Tyre kwenye vitabu, kwenye utekelezaji hakuna kinachotekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Maprofesa wengi wabobezi wa uchumi, wabobezi wa uchumi chungu nzima kwenye nchi wa kuisaidia Serikali kuandaa mipango mizuri ya uchumi, leo badala yake kupata wachumi wakatoa ushauri wao na kukaa na Serikali, leo wachumi mnawapeleka kuzoa taka mkiwapiga picha na wheelbarrow Mheshimiwa Mwenyekiti, Wachumi wa kuisaidia nchi hii mnawapiga picha wakizoa taka na ma-wheel barrow! What? Tutakwenda wapi? Wachumi wetu tunawageuza vituko tukitegemea nchi itakwenda mbele! Hasara yao. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie lile Shirika la TEMDO. TEMDO ile taasisi imeanzishwa kwa ajili ya kusaidia uvumbuzi wa viwanda vidogovidogo na mashine ambazo zinaweza kuwasaidia Watanzania kuanzia wa viwango vya chini kabisa, lakini cha kusikitisha Mheshimiwa Serikali imeanzisha taasisi ile kwa kujua umuhimu na faida zake, lakini taasisi ile imetupwa kama yatima. Wamekuwa wakilazimisha waonekane wapo kwa kutenda mambo ambayo hata Serikali haiwasaidii hata senti tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunafanyaje? tunaanzisha kitu kwa nia ya kusaidia Taifa, lakini leo mnakitelekeza mnakifanya yatima! Matatizo ni yapi, hakuna kinachofanyika pale wakati wana uwezo mkubwa wa kusaidia kama vile viwanda amesema mwenzangu, viwanda vidogo-vidogo vya soksi, viwanda vya juice, viwanda vya kuteketeza taka kwenye mahospitali, ni watu ambao wana ujuzi mkubwa na wamesomeshwa na Taifa hili, lakini badala yake wametelekezwa. Naomba Mheshimiwa Waziri waiangalie hii taasisi, hakuna nchi zilizoendelea bila kuwa na taasisi za uvumbuzi kama hizi, taasisi za utafiti kama hizi ambazo zinaweza kusaidia nchi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itakuwa ni nchi ya ajabu sana kwamba, leo tunapozungumzia suala la uimarishaji wa viwanda, lakini wawekezaji wanapotoka nje ya nchi kuja hapa kutaka kuwezeshwa kuwekeza katika maeneo wanapata usumbufu sana kuanzia kwenye ardhi na watu wa NEMC wanakuwa ni vikwazo vikubwa vya uwekezaji katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uko ushahidi wamekuja wawekezaji hapa, Mwekezaji anatumia mpaka mwaka mmoja kuhangaikia vibali vya kuweza kuwekeza miradi ambayo italeta tija kwa nchi hii, italeta ajira kwa nchi hii. Wako wawekezaji wamekuja na wamehangaika mwisho wameondoka kwa kuona kwamba sisi ni Taifa ambalo hatuko tayari. Hawakufanya kosa Rais Museveni na mwenzie Rais Kagame siku zile walipoamua wakasema katika East Africa kuna nchi zilizo tayari kimaendeleo na kuna nchi kama Tanzania tuziache kwa sababu wao hawako tayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwanza tuwe tayari kusikiliza ushauri unaotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Pili, tuwe tayari kumshauri na kumwambia ukweli Mtukufu Rais kwamba, hali halisi ilivyo ni hii. Yule tunatakiwa ni Rais wetu tumheshimu na nawaahidi watu wa CCM tunamheshimu Rais Magufuli, lakini niwaambie hatutamwogopa katika kumwambia ukweli utakaosaidia kulijenga Taifa hili. Tutamheshimu ni Rais wa Tanzania, ni Rais wetu, lakini muwe tayari kumweleza ukweli, mnapoendelea kumfichaficha hamumsaidii! Mficha maradhi kifo humuumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa Tanzania ukikua kwa kumshauri na kumwambia ukweli Rais, sifa na maendeleo ya nchi yetu ndio itakayotufanya sisi tujione ni Wabunge bora ni Mawaziri bora ni Serikali bora, lakini kuendelea kuona kila mmoja aah! Bwana mkubwa hafikiki! Itatuletea dhara na sisi tunawaambia haya, kama sisi tungekuwa na nia mbaya sana na Chama cha Mapinduzi tusingeyasema haya, tungekaa tu kwa sababu tunajua mnaharibikiwa. Watanzania sasa hivi wote wanalia hali ilivyo! Watanzania walikuwa hawajawahi kulia kwa ukosefu wa dawa katika nchi hii, mara hii mnasikia kilio!
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wetu wanalia na mabegi barabarani wanarudishwa makwao hawana pesa katika mikopo! Leo huduma nyingine zote zimedorora, lakini akishuka hapa Mheshimiwa Waziri wa Fedha atasema uchumi wetu umekua! Uchumi umekua mabenki yanaeleza kabisa, draft imetolewa mabenki yote yame-collapse! Hasara tupu ambayo ipo katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuwe pamoja katika hili, tumshauri Mheshimiwa Rais Magufuli. Mtukufu Rais sio Mungu ni mwanadamu akiambiwa atasikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.