Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nianze kwenye kitabu hiki cha Mpango, ukurasa wa saba ambapo anasema, mwenendo wa uchumi unaashiria kuendelea kuimarika kwa uchumi na utoaji wa huduma za jamii unaboreka. Ndiyo maana kukawa na hoja kwamba ingelazimika tukapata tathmini ya kipindi kilichopita kwa muda huu tulionao ili tuweze kujua mwelekeo. Hii kauli inachanganya sana wananchi wa kawaida na hata mimi mwenyewe. Ukiangalia hali halisi ya kiuchumi ilivyo, ukitembelea maduka mitaani, wafanyabiashara mbalimbali wanalalamika na hata sisi wenyewe Wabunge tunalalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana imeelezwa kwamba imefikia hatua hata kwenye Kamati za Bunge unapewa maji moja ndogo kuanzia asubuhi mpaka jioni. Pia ukipewa chakula kimepangwa unasimamiwa usije ukazidisha vipande vitatu ni viwili tu, maana yake inawezekana ukizidisha utashikwa mkono. Hiyo maana yake inaashiria hali ya kiuchumi ni ngumu lakini kwenye vitabu wataalam wetu Mheshimiwa Dkt. Mpango na wenzake wanasema hali inaimarika na huduma za kijamii zinaboreshwa. Kwa hiyo, naomba hata atakapokuja kuhitimisha hoja ambayo mimi siungi mkono, basi atueleze angalau kinaga ubaga na kwa lugha ambayo tutaweza kuelewa anamaanisha kitu gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niunge mkono hotuba nzuri sana ambayo imetolewa na Kambi ya Upinzani Bungeni. Niseme Waziri yeyote makini tukitoa hotuba hapa ni muhimu akapitia kile tunachokisema kwa sababu takwimu ambazo zinatolewa na sisi upande wa Upinzani hatuzipiki sisi bali zinatoka kwenye nyaraka mbalimbali Serikalini humohumo. Kwa hiyo, tunapotoa hotuba hapa siyo kuibeza na mimi ningekuwa ninyi ningekuwa mjanja sana kwa sababu mngekuwa mkisema naenda kuyafanyia kazi ili next time mkose hoja. Badala yake mnaweza kukaa hapa miaka mitano mnaambiwa mambo yaleyale ukirudi unatoa siasa, unapiga story, unapiga porojo, miaka inaenda na huboreshi. Kwa hiyo, kimsingi unakuwa hufanyi lolote lile. Hoja ikitolewa iangalie na kama ina ukweli ifanyie kazi na kwa kufanya hivyo utakuwa unalisaidia Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kupitia hiki kitabu, mimi nitajikita kwenye kitabu hiki kilichoandikwa, ukurasa wa 66 – 67, Waziri mwenye dhamana amezungumzia utawala bora na utawala wa sheria, lakini nilipoangalia utawala bora alioandika hapa alikuwa anaandika kuboresha majengo na kuongeza polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoelewa utawala bora angeeleza hapa kwamba mpango wa Serikali ni pia kuheshimiana katika maeneo yetu ya kazi. Kwa sababu kwa utawala huu ambao mnauita utawala wa Awamu ya Tano na mnakwepa kusema utawala wa Chama cha Mapinduzi mnataka watu waamini kwamba miaka inatofautisha matendo yenu, ndiyo maana mnahimiza sana utawala wa Awamu ya Tano, sema Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Watanzania wajue ni ileile hakuna jipya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika hali ya sasa ambayo unataka kuboresha elimu lakini Mwalimu huyu ambaye anadai na hapa katika kuboresha elimu sikuona unaboresha namna gani, wapo Walimu ambao wanadai madai yao tangu mwaka 2012 mpaka leo. Ili uboreshe elimu lazima Walimu walipwe madai yao, wapandishwe vyeo, walipwe likizo na malimbikizo yao ili migogoro iishe. Huwezi kuboresha elimu kwa maana ya majengo wakati Walimu wanadai na Walimu haohao Wakurugenzi ambao mnawateua makada wa CCM wanawaambia wapige deki mbele ya wanafunzi halafu unasema unataka kuboresha elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unazungumzia utawala bora mahali ambapo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu anaagiza eti kuanzia leo Walimu wote nimewashusha vyeo, huo ndiyo utawala bora kweli? Sasa hapa hamzungumzi, mnazungumza habari ya kujenga majengo, haya mambo lazima tuzungumze ukweli. Sasa mnapotuandikia, sisi siyo wajinga, tunaweza kusoma mnachoandika na kuchanganua, lazima mtueleze utawala bora maana yake ni nini? Sasa hivi hali iliyofikia watu hawaheshimiani yaani unakuta Rais ameagiza kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya watumie ile Sheria ya saa 48, kwa hiyo, Mbunge kwenye eneo lake, Diwani kwenye eneo lake, Mwenyekiti wa Halmashauri au Mstahiki Meya anaweza akaambiwa kamata weka ndani, unasema huu ndiyo utawala bora halafu unataka upewe ushirikiano katika eneo hilo. Kwa hiyo, nashauri wahusika wa haya mambo lazima waangalie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kuhusu utawala wa sheria, sasa hivi kinachotawala Tanzania wala siyo sheria ni amri mbalimbali, sheria wala haifuatwi. Bahati nzuri Waziri wa Utawala Bora ndiyo alikuwa mpiga kura kule Kinondoni kwenye uchaguzi wa Meya, walikuwepo hawa. Katika hali ya kawaida inawezekanaje unafanya uchaguzi ambapo unajua idadi ya UKAWA ni nyingi kuliko Chama cha Mapinduzi na Naibu Spika ambaye ni mwanasheria tena alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amehusika kuchakachua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria inasema wateule wa Rais hawatazidi watatu katika Halmashauri lakini mlichokifanya mlipeleka watu wanne pale Kinondoni. Sheria inasema ni lazima mahudhurio yaandikwe, akidi ni mbili ya tatu (2/3), haikutimia hakuna mahudhurio. Watu wa CCM mlikuwa 18, tena viongozi mmekaa pale mkapiga kura mkajiapisha halafu unaandika makaratasi hapa utawala bora wa kitu gani, unamdanganya nani hapa? Huu ndiyo utawala bora kweli, huu ndiyo utawala wa sheria? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wasomi, Mawaziri, Maprofesa, Wanasheria, Naibu Spika na wenzenu, Mawaziri wazima hata aibu hawana, tena Waziri wa Elimu ambapo Waziri wa Elimu alikuja kupiga kura Ilala. Mimi ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mheshimiwa Profesa Ndalichako mama yangu na mtani wangu ambaye namheshimu sana alikuwepo ameletwa kujiandikisha kupiga kura Ilala halafu tena akakubali kubebwa mzobemzobe anashinikizwa kuja kupiga tena kura Kinondoni, wewe unafanya kitu gani kweli? Hata aibu hamuoni?
Aibu sana kwa Chama cha Mapinduzi, chama kongwe, ndiyo maana mnaitwa chama kizee.
Hata busara na hekima inapotea. Sasa hapa utawala bora mnaozungumzia ni kitu gani? Tangu mmeanza kufanya uhuni katika nchi hii mimi kwa kweli nimekuwa confused.
Ndiyo maana mnachofanya hata hapa kwenye elimu ni maigizo, tumegundua mtaji wenu katika nchi hii ni ujinga.
Ndiyo maana mnavuruga elimu makusudi. Rais amewaambia Watanzania yeye hatakubali mtoto wa maskini asiende chuo kikuu atawakopesha, Waziri anasema ataangalia bajeti ilivyo sasa nani mwenye kauli?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza habari ya afya hapa, Makamu wa Rais anasema dawa hakuna Waziri anasema dawa zipo tele na jana Naibu Waziri amethibitisha, akasema tumwonyeshe, tumemwambia tumpelekee nyumbani kwake akakataa. Sasa haya mambo ukisoma kwa kweli, mimi vitabu vyenu huwa navisoma sana, nipo tayari nisilale usiku lakini navisoma sana, lakini mnatuchanganya sana, kwa nini msiandike ukweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akija hapa Waziri wa Viwanda atapiga ngonjera zake utamwona huyu ndiyo mwanaume ametoka Bukoba wengine hawapo kabisa. Akiimba hapa ngonjera zake utashangaa, sasa nenda kwenye hali halisi, yote haya hamna. Anafukuzwa na Kamati yake kwamba mzee umeandika makabrasha mengi, pesa hakuna, Kamati ya Viwanda inasema hujafanya lolote, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda acha kuimbia watu ngonjera. General tyre mpaka leo haijaanza, watu wanataka kuona mnaleta tena story zilezile. Kwa kweli hii habari inatusumbua sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme kuhusu hii habari ya mifugo, Wabunge wengi wanakaa Jimbo la Ukonga na Dar es Salaam kwa ujumla, hata kama mtu hakai ana kibanda pale lakini Dar es Salaam hakuna machinjio ya kisasa. Kuna machinjio ndogo kweli kweli pale Vingunguti na yale mazizi ni ya mtu binafsi siyo ya Serikali. Pale Zingiziwa kuna ekari zaidi ya 120, kama mkiweka mifugo pale na kuna mnada wa Kimataifa wa Pugu ambao kimsingi na wenyewe ni jina, ni mnada lakini ni kijiwe cha ng‟ombe, hakuna maji, hakuna chochote pale, ukiboreshwa utasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam ndiyo kuna Mawaziri, ndiyo ipo Ikulu lakini hakuna nyama safi, watu wanaweza kuchinjia vichochoroni wakauza mitaani, sijui kwa nini hampangi haya na maeneo yapo, hapa sikuona chochote kwamba mnaboreshaje suala hili. Dar es Salaam kuna watu wengi na wageni pia lakini suala hili haliwekewi mipango. Mbona mmesema tupande miti ili Jiji lipendeze Wazungu wafurahi, tengenezeni basi na mazingira mazuri ya kuchinjia nyama kwa afya zao. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme habari ya maji. Watu mikoani wanalia, lakini nawaambia hata Dar es Salaam kule Jimbo la Ukonga katika kata 13 ni kata moja au mbili zinaweza zikawa na uhakika wa maji na visima vingi zaidi ya asilimia 90 ni watu wamechimba wenyewe. Mheshimiwa Dkt. Mpango anakaa Zingiziwa pale Nzasa, yeye ni mpiga kura wangu kule, tupange siku moja aende Zingiziwa aone wale watoto na wazazi wa pale maji ambayo wanakunywa, Dar es Salaam acha kule kwao Kigoma, Dar es Salaam, maana anavyoandika hivi vitu twende kwa ushahidi aende aone, hajaandika chochote hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, afya; Jimbo la Ukonga lina wapiga kura zaidi ya laki sita na kata 13. Watu wote wale kutoka Zingiziwa, Chanika, Msongola, Mvuti, Uwanja wa Nyani wanakuja Amana. Tuna eneo kubwa ekari 45 kwa ajili ya kujenga hospitali na tangu mwaka jana niliwaambia kwamba ile hospitali ikijengwa itasaidia mpaka na Kisarawe mpaka Mkuranga. Halmashauri ina uwezo wa kutenga shilingi milioni moja kwa mwaka na gharama yake ni shilingi milioni 26 maana yake Halmashauri ikiachiwa ijenge itatumia miaka 26 watu wanasubiri huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda anapopanga zahanati, kituo cha afya na hospitali ataje majina ili Mbunge ajue zamu hii ni ya Msigwa, zamu ijayo itaenda labda Kwimba na sehemu nyingine, tuwatajie, asiweke kwenye bracket hapa. Aseme anataka kujenga hospitali ipi, zahanati ipi ili tujue kama siyo zamu yangu nisubiri mwaka ujao na akiandika atekeleze, aache kutuimbia ngonjera hapa. Mlishatuambia tutaisoma namba, tutaisoma wote pamoja, bahati nzuri hatuisomi wenyewe na nyie mnaisoma sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Shirika la Ndege amelizungumzia, nataka nihoji hapa, tuna taarifa kwamba Chato kwa Mheshimiwa Magufuli pale nyumbani kwao Chato unajengwa uwanja wa ndege, mbona kwenye mipango hapa hiyo hela haipo? Bajeti iliyopita haikutajwa na hii hapa haijatajwa lakini unajengwa uwanja wa ndege kule Chato. Tunaomba tujue hiyo bajeti ya kujenga uwanja huo iko wapi mbona hapa kwenye mipango hamuutaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mtuambie, hivi Chato kujenga uwanja wa ndege, sawa kweli wale ni watani na wakwe zangu, hivi kule Chato mtafanya biashara gani, projection ni nini pale? Yaani mnataka mjenge uwanja wa ndege ili Mheshimiwa Magufuli akitaka kupumzika aende na ndege nyumbani kwao? Kujenga uwanja wa ndege ni lazima kuangalia economic zone kwamba biashara itafanyika kwa sababu population ni kubwa na vitu vya namna hiyo. Haya hata hapa hamuonyeshi, sasa hiyo siyo siri tunajua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kumekuwa na malalamiko ya ndege mlizonunua, mimi siyo mtaalam, ndege zenyewe ni Bombardier?
Wanasema mikataba duniani mnalipa kwa advance nyie mmeenda kulipa kwa bei ya jumla. Mmechukua hela zote mkaenda kununua ndege kwa mbwembwe, eti mnazindua kununua ndege, hivi kweli nyie mnaumwa, unazindua kununua ndege? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, karne ya 21, Serikali ya Chama cha Mapinduzi zaidi ya miaka 50, umri wa mtu mzima yaani miaka ya chama chenu inanizidi mimi Waitara, Mbunge wa Ukonga hebu niangalie halafu mnasherehekea kununua ndege. Muangalieni mwenzenu Kagame, ndege ya kwanza aliyonunua na mambo anayofanya. Ameleta ndege ambayo inaendesha kwa mitambo, shabash, nyie mnapiga makofi hapa! Wabunge wanasimama hapa hoja ambazo hazina maana eti anaunga mkono ili asisahau maana wamezeeka halafu wanalalamika, mambo gani haya bwana? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme. Mimi ni Mbunge wa Ukonga, ukienda Kata ya Msongola, robo tatu ya kata hakuna umeme. Kivule ina mitaa minne, mitaa miwili ndiyo ina umeme. Ukienda Zingiziwa kuna mitaa nane ni mtaa mmoja tu wa Mheshimiwa Waziri wa Fedha ndiyo kuna umeme. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Chanika kuna mitaa nane, miwili ndiyo ina umeme. Ukienda Pugu kuna mitaa mitano, mitatu ndiyo ina umeme miwili haina umeme. Ni Dar es Salaam hiyo sikutaja majimbo mengine ya Kigamboni na kadhalika na mnasema ule ndiyo mji ambao una population kubwa, ndiyo mji wa kibiashara, ndiyo Rais yuko pale lakini umeme ni shida. Kule mnatoa matamko kushughulikia watu kwenye vikao, kupindishapindisha na kuiba kura za Kinondoni, mnatangaza Meya hewa, mmeleta Meya hewa pale wakati nyie mnatafuta wafanyakazi hewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu Waziri anayehusika ashughulikie suala hili ili umeme isiwe wimbo Dar es Salaam. Watu wanakaa Dar es Salaam kwa maana ya majina lakini akimwambia mtu amtembelee anamzungusha mjini anamkimbia kwa sababu akienda nyumbani kwake hatafanana na mbwembwe alizokuwa anasema. Kwa hiyo, tunahitaji suala hilo lishughulikiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara muda wako umeisha tafadhali naomba tu ukae.
Haya basi siungi mkono hoja mimi.