Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia, ingawa umeniwahi sana, lakini nitajitahidi tu kuweza kuchangia yale ambayo naweza nikachangia kutokana na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa ya Mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo naomba nilizungumzie ni suala zima ambalo ndiyo imekuwa kama nguvu kubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano katika mwaka huu mmoja na ndani ya bajeti hii ya kubana matumizi. Ni hatua nzuri kubana matumizi kwa sababu inasaidia kupata rasilimali fedha za kutosha kuzielekeza kwenye miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana hapa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi ametupa takwimu za watumishi hewa ambao wameondolewa kwenye payroll ya Serikali na hivyo kupelekea Serikali kuokoa shilingi bilioni 19 kila mwezi kutokana na suala zima la watumishi hewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate ufafanuzi kutoka kwa Waziri wa Fedha. Taarifa ya gharama za watumishi tunazipata kupitia taarifa ambayo kila mwezi Benki Kuu inaitangaza; inaiweka kwenye tovuti yake na kuigawa pia (Monthly Economic Review).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Monthly Economic Review ya mwezi Agosti mwaka 2015 inaonesha kwamba wages and salaries ambazo Serikali ililipa mwezi Juni, 2015 zilikuwa ni shilingi bilioni 456. Monthly economic review ya mwezi Agosti mwaka 2016 inaonesha kwamba wages and salaries ambazo Serikali imelipa kwa mwezi Juni mwaka 2016 ni shilingi bilioni 534; kwamba kuna nyongeza ya gharama za mishahara ya kila mwezi ya shilingi bilioni 78. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Utumishi jana ametuambia wanaokoa shilingi bilioni 19 kila mwezi kwa kuondoa watumishi hewa. Taarifa ya Benki Kuu inaonesha kwamba toka Serikali hii imeingia madarakani gharama za watumishi kwa mwezi zimeongezeka kwa shilingi bilioni 78 Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi hewa wameondolewa, ajira mpya hakuna, nyongeza ya mishahara imesimamishwa, lakini gharama za wages and salaries zimeongezeka kwa bilioni 78. Haieleweki! Kuna mmojawapo kati ya hawa wawili anadanganya umma. Ama zoezi la watumishi hewa ni publicity stunt au Serikali inatumia fedha kwa matumizi mengine halafu BOT inasema ni mishahara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nipate maelezo ya Waziri wa Fedha kuhusiana na jambo hilo, kwa sababu ni jambo ambalo umma ni lazima uelezwe na liweze kueleweka tunapopanga mpango kuelekea katika mwaka ujao wa fedha ambao unakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni Higher Education. Jana nimepitia Mpango wa mwaka jana 2015. Mwaka jana tulichelewa kidogo tukaupitisha mwezi Januari. Serikali inazungumzia kuongeza idadi ya vijana, wanafunzi wanaopata mikopo kwenye elimu ya juu. Mpango pia wa mwaka huu unazungumzia hilo hilo na imeongeza; inasema, kuimarisha Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili kuongeza uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wengi zaidi wanaokidhi vigezo, kuendelea kupanua matumizi ya TEHAMA na ukarabati, upanuzi na ujenzi wa Vyuo Vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunapozungumza, idadi ya wanafunzi ambao wana uwezo wa kuingia kwenye Vyuo Vikuu hapa nchini na wanao-qualify kwa mikopo ni takriban 65,000. Watoto waliopata mikopo ni 20,000 tu. Nini ambacho kinaandikwa na nini ambacho kinatendwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hapa napata tatizo kidogo la coordination ndani ya Serikali. Waziri wa Elimu alikuja kwenye Kamati. Kamati ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii ili-dedicate siku nzima na kujadili tatizo la mikopo. Wizara kwa maana ya Serikali kwa kupitia Wizara ya Elimu na Kamati tukakubaliana, kuna mambo yanayopaswa kwenda kuangaliwa upya kuhusu suala zima la financing higher education ili tuweze kutatua tatizo hili la mikopo la muda mrefu. Hata hivyo, ukisoma Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo hukuti jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa maelekezo ya Kamati kwa Waziri ni kwamba by mwezi Februari tutakuwa tuna utaratibu mpya. Wakati huo huo, wiki ijayo tuna mabadiliko ya sheria tunakuja kuyafanya ya mikopo ya elimu ya juu. Katika Miscellaneous Amendment kuna vipengele ambavyo tunaenda kuvibadilisha kwenye mikopo ambavyo vinabana upanuzi wa kupata mikopo zaidi. Sasa nashindwa kuelewa, kuna mazungumzo ndani ya Serikali kabla ya Serikali kuja ndani ya Bunge kuwasilisha Mpango kama huu? Baraza la Mawaziri linakaa ili kuhakikisha kwamba kila Waziri anaeleza new development ambayo imetokea kwenye sekta yake ili jambo linalokuja Bungeni liwe ni lile ambalo limekubalika ndani ya Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya jambo tulilozungumza ni kwamba, ukisoma Mapendekezo ya Mpango kuna kipaumbele kimewekwa kwenye masomo maalum; gesi, gesi asilia, sijui nishati, uhandisi na kadhalika. Kwenye vigezo vya mikopo vya mwaka huu vimetolewa ni kwa wanaosomea Udaktari, Uhandisi, Gesi Asilia na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni nchi gani duniani ambayo haina scholarship programs kwa watoto wake? Kama ninyi mnataka kujenga nchi ya viwanda, mnahitaji Wahandisi kadhaa; mnahitaji wahandisi wa mitambo kadhaa; mnahitaji wataalam wa mafuta na gesi kadhaa; si ni wajibu wa Serikali kutoa scholarship kwa watu hao ili mweze kuwapata hao wataalam? Halafu ili eneo la mikopo, bajeti ambayo mmeitenga kwa ajili ya mikopo ibakie kwa ajili ya watu wengine wote waweze kupata mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwaulize Waheshimiwa Wabunge wenzangu, mnaweza mkasomesha Wahandisi wengi sana; mnaweza mkasomesha Madaktari wengi sana; hivi niambieni, kuna kiwanda hakina Afisa Utumishi? Kuna kiwanda hakina Mhasibu? Kuna kiwanda hakina Wachumi? Mnawezaje mkasema kwamba mwaka huu tutasomesha hizi hard sciences tu? The best way to do that, mnatoa scholarship kwa hizo priorities, hao wengine wanaendelea kupata mikopo kama kawaida. Hayo ndiyo mambo tuliyokubaliana kama Kamati na Wizara ya Elimu. Siyaoni kwenye Mpango; sasa hili ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, jana Mheshimiwa Bashe amezungumzia Kurasini na Kariakoo. Tunafahamu kabisa kwamba suala la Kurasini limeongelewa muda mrefu; lakini wakati tunaongea suala la Kurasini hatukuwa na nguvu hii tunayoongea kuhusu viwanda. Niliwahi kusoma makala moja aliandika Mheshimiwa Dkt. Mpango wakati yuko Tume ya Mipango, ilichapishwa na jarida la REPOA kuhusiana na suala la staying the course, kwamba mmepanga kitu hakikisheni mnakifanya na sequencing. Alitoa mambo kama manane na moja nitalizungumza mwisho kabisa ambalo ni la kumsuta kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kurasini inaenda kuwa ni ya biashara. Kama mnataka kujenga viwanda, kwa nini mnaruhusu uchuuzi huo kama lengo ni la viwanda? Kama kuna transition ambayo nakubali, lazima kuwe na transition; kwa nini tusiitumie Kariakoo kama hiyo transition? Kwa nini tuwaue Waswahili, wafanyabiashara ambao wameanza kukua na kukuza mitaji yao kwenda kuimarisha viwanda vya China na wafanyabishara wa China kuleta bidhaa zao Kariakoo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tusiifanye Kariakoo kuwa ni free trade area; chochote kinachoingia Kariakoo kisitozwe kodi na kinachotoka kitozwe kodi? Kwa sababu Kariakoo Wazimbabwe, Zambia, Malawi, Congo wananunua pale, kila sehemu wananunua pale. Hili jambo naomba liangaliwe upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri sasa hivi, kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati ya Bajeti, mwekezaji yule wa Kurasini ameshaondoka, hayupo tena. Kwa maana hiyo basi, tutumie hii opportunity tuweze kuona namna ya ku-link; na kuna matatizo makubwa pale Kariakoo. Maana yake sasa hivi TBS wameongeza viwango vya tozo na faini na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wadogo wa Kariakoo wanahangaika sana, lakini tunapoenda kwenye transition ya kuelekea viwanda, hawa ndio watu ambao wanapata entrepreneurial skills through biashara zao baadaye waweze kuja kuwa na viwanda. Lazima tuone namna gani ambavyo tutawasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, katika lile jarida moja ya jambo ambalo Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango wakati ule akiwa Katibu Mkuu wa Mipango, alisema lazima uongozi ujenge chini ya ushindi, kama atakuwa anakumbuka mwenyewe; a winning coalition ambapo kila mtu anaongea jambo moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi. Serikali na Bunge hatupo pamoja katika utekelezaji wa mikakati ya nchi. Ama sisi Wabunge hatuielewi Serikali au Serikali haiwaelewi Wabunge; ni either of the two. Pia Serikali yenyewe miongoni mwa Mawaziri wenyewe, bado hawaelewani. Ndiyo maana kumekuwa na matamko ya kila mtu kwa kila kinachotokea utafikiri Serikali inakimbizana kupata front pages za magazeti. Nadhani kuna haja ya kuwa na cooling of period, tuweze kukaa soberly kabisa, Waheshimiwa Wabunge na Serikali tujiulize, wapi tunaenda sawa na wapi hatuendi sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wanalalamika na wananchi wanalalamika kwamba hali ni mbaya. Mimi naelewa na any development economist anaelewa kwamba mnapopiga hatua fulani ya maendeleo lazima kuwe na maumivu. Ndiyo maana kuna dawa za maumivu; lazima kuwe na palliative measures, yale maumivu mpaka mfikie ile hatua ambayo mnayotaka kufika, hatuendi hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba through Mpango tupate nafasi tukae kama viongozi, tuweze kuona nchi inakwenda vipi. Pale ambapo kuna matatizo tukubaliane, matatizo haya ni ya lazima lakini tutayaepuka namna hii. Sivyo hivi ambavyo tunakwenda; tutanyoosheana vidole, tutarushiana madongo na hatutakwenda. Hali ya wananchi sasa hivi malalamiko ni makubwa sana. Ahsante sana.