Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili kuweza kuzungumzia mpango wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetulinda ametuleta tena kwa mara nyingine mahali hapa, tunaendelea kuomba neema yake na rehema yake atulinde mpaka tumalize Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya kwa ajili ya kupigania nchi yetu na maslahi ya Taifa zima. Naomba nipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ambazo kwa muda mfupi kwa muda wa mwaka mmoja wameweza kuzifanya.
Leo hii naomba nimpongeze Rais wangu kwa kazi nzuri na maamuzi magumu ambayo ameyafanya kuhamia Dodoma, leo hii Serikali inahamia Dodoma ni mafanikio makubwa kwa sababu ilikuwa inazungumzwa kwa muda mrefu na miaka mingi leo Awamu ya Tano imeweza kufanya leo hii Serikali imehamia Dodoma.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaomba niipongeze Serikali, ingawa bado pesa hizi hazijatoka za kwenda kila kijiji shilingi bilioni 59.5, tuna mategemeo Serikali hii ya Awamu hii ya Tano hizo hela zitafika kwa wananchi wetu kwa ajili ya uchumi wa Tanzania hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kununua ndege mbili mpya. Leo hii tunajivunia Serikali ina ndege, alama yetu ya twiga ipo ilikuwa haipo lakini leo sasa ipo kutokana na malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano yameendelea kuwa mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite sana kwenye masuala ya dawa. Ninaomba sasa Waziri wetu aweke mpango mkakati wa ujumla ili wananchi wetu waweze kupata dawa. Dawa ni kitu muhimu sana kwa wananchi wetu wa Tanzania. Ninaomba mikakati mikubwa ichukuliwe sasa hivi, ufanywe mkakati maalum kwa ajili ya dawa ili hospitali zote zipate dawa. Ninajua Serikali ya Awamu ya Tano ni sikivu, mipango inayopanga sasa iweke mikakati ili tuweze kupata dawa kwa ajili ya wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; lazima sasa tufanye mikakati ya kujenga vituo vya afya kila Kata ili wananchi wetu waweze kupata huduma za ukaribu. Tukiweka mipango mizuri na mikakati mizuri kila Kata iwe na kituo cha afya akina mama wengi wataende kufanyiwa operation ndani ya kata zetu na maeneo yetu husika, hiyo mipango iweze kupangwa. Mimi najua Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu, mipango yote tunayomweleza Waziri wetu ataifanya na ataitenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji; bado maji hatujawafikia wananchi vizuri husasan maji mijini bado kuna maeneo ambayo maji hayajawafikia wananchi vilevile maeneo ya vijijini, lazima sasa hivi tuamue kuweka mipango mikakati.
Kuna Mbunge hapa amezungumza kama sisi tunapakana na maziwa, mfano Ziwa Tanganyika li-supply Mkoa wa Katavi inawezekana, kwa sababu kuna mipango iliyopangwa nyuma. Leo hii Mwanza, Shinyanga wanapata maji kutoka Ziwa Victoria, tunaomba na sisi tunaokaa Katavi, Mkoa wa Rukwa na maeneo mengine kama Kigoma yale maziwa yetu yaweze kunufaisha maeneo husika, vijijini pamoja na mijini, mpango ukikaa vizuri nafikiri tutaweza kufanikiwa vizuri sana upande wa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu; ninaomba mipango mizuri ifanyike kwenye elimu. Tunajua Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi nzuri ya kutafuta madawati, leo hii tuna madawati mengi. Vilevile kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano imefanya elimu imekuwa bure, kutokana na elimu bure sasa hivi wanafunzi tumekuwa nao wengi ndani ya shule zetu. Sasa tunaomba Serikali ipange mpango makakati wa kujenga madarasa ili watoto wote waweze kuenea ndani ya madarasa. Kwa sababu madawati, mpango umekwenda vizuri hakuna sehemu sasa hivi watu wanalalamika kuwa mtoto anakaa chini, tunaomba bajeti hii inayokuja tuweke mikakati ya kujenga madarasa nchi nzima ili watoto wetu wote waweze kukaa madarasani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa ardhi; leo hii tunawaleta wawekezaji, lakini kuna matatizo kidogo ndani ya maeneo yetu husika. Leo hii migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na wananchi imekuwa mikubwa mno. Ninaomba Serikali sasa kwa sababu tuna lengo zuri la kuweka mikakati mizuri ya wawekezaji nchini na vilevile tunaendelea kuwaleta wawekezaji ndani ya nchi yetu, kwenye upande wa ardhi tujipange vizuri na Watanzania tumeongezeka, lazima sasa hivi Serikali ipange mikakati ya kuongeza ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu nyingine tumeweka mipaka, mipaka ile tuipanue ili wananchi sasa pamoja na wawekezaji wakae sehemu nzuri. Wawekezaji wengine wanatukimbia kutokana na migongano kati yao na wananchi. Ninaomba Serikali iweke mipango mizuri, mikakati mizuri ili wananchi na wawekezaji waweze kukaa vizuri na waweze kujenga viwanda vyao ndani ya nchi yetu ili vijana wetu wapate ajira, mama lishe zetu wale wanaohangaika waweze kupata ajira kwa ajili ya mipango mizuri ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mikopo ya akina mama. Akina mama wengi bado hatujawafikia kwa elimu. Tunapenda akina mama wapate mikopo, tunapenda akina mama waweze kuinuka, lakini bado hatujawafikia ili waweze kupata elimu nzuri waweze kutumia hayo mabenki tunayoyasemea leo hii mambo yamekuwa siyo mazuri, akina mama tukiwafikia tukiwapa elimu nzuri wakiweza kujikomboa wao kama wao, tukiwawekea mikakati mizuri ninafikiri Taifa hili ukimwezesha mwanamke, tumewezesha jamii nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kilimo; bado Watanzania tunalima asilimia 80 ni wakulima, asilimia 20 ni wafanyakazi. Mpaka leo hapa tulipo wananchi kule hawajapata mbolea na hili lazima tuliwekee mikakati mikubwa na mipana ili kipindi cha mvua kabla hakijafika wananchi hawa waweze kupata mbolea kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa katikati tulikuwa tuna mawakala, leo hii hiyo mipango ya mawakala tumeitoa na wale mawakala ambao tuliowatoa bado hatujawalipa wanatudai na mpaka sasa hivi hatuna mawakala wala hatuna nini, wananchi wameilewa. Hatujui hiyo mbolea itauzwaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali ichukue jukumu ambalo sasa kupanga mikakati mizuri na mipango mizuri ili wananchi waweze kupata manufaa kupitia Serikali yao kwa ajili ya kilimo kwa sababu upande wa kilimo ndiyo uwekezaji upo mkubwa sana kuliko upande mwingine, ninaomba Serikali hii sikivu mipango hiyo iweze kupangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepanga mipango mingi, tunaongea mipango mingi, lakini kuna watu ambao ni muhimu sana ambao tukiwajengea uwezo na tukiwafanyia mipango mizuri, mikakati mizuri wanaweza wakakaa vizuri zaidi. Hapa mara nyingi tunawasahau sana askari wetu na sehemu nyingi ukienda unakuta askari hawana sehemu ya kuishi, lazima sasa Serikali ichukue jukumu la kuweka mpango mkakati wa kuwajengea askari nchi nzima ili hawa askari wanaotulinda wananchi wawe na sehemu nzuri za kukaa ili nchi yetu iweze kuwa na amani na utulivu kama tulivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima sasa tuwawekee mikakati mizuri na mipana ili kila sehemu nchi nzima, nyumba za askari, nyumba za manesi, nyumba za walimu ziweze kuwekewa mikakati mikubwa na mipana zaidi ili sasa nchi yetu iweze kutulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la utalii, kwetu Mpanda nilishasema kipindi kilichopita tumejengewa uwanja mzuri. Naomba nirudie kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ambayo ilifanyika kununua ndege mbili. Ninajua sasa uchumi wa Tanzania na uchumi wa Mkoa wangu wa Katavi utazidi kuongezeka, ninajua sasa ndege itatua Mpanda, Katavi kwa ajili ya kuleta watalii ili uchumi wa Katavi uweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, ninaomba niunge mkono asilimia mia kwa ajili ya mpango huu mzuri.