Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Riziki Shahari Mngwali

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na ardhi aliyetujaalia sisi sote uzima na afya na akatupa upendeleo maalum kutuweka kwenye jengo hili tujadili kwa niaba ya Watanzania mamilioni kile ambacho kina mustakabali mwema kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nisome tafsiri ya maandiko matakatifu kutoka kwenye kitabu wanachofuata Waislamu cha Qurani na kiongozi wao Mtume Muhammad (SAW). Kuna hizi aya mbili, moja wapo nakumbuka nilishawahi kuisema hapa lakini nitairudia tena, ya kwanza iko katika Sura inaitwa Sura Hajj ni aya 46 ambayo inasema; “Hivi hawatembei katika ardhi, wakawa nyoyo ambazo wanafahamu kwa nyoyo hizo? Au masikio wakasikia kwa masikio hayo? Kwa hakika yanayopufua si macho bali ni nyoyo zilizomo ndani ya vifua.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kuna aya nyingine iko kwenye Sura Araf na ni aya ya 179 hii inasema; “Hakika tumeumba moto wa Jehanum kwa ajili ya watu wengi na majini pia kwa sababu...” wataalam wanasema pale kiunganishi “...kwa sababu wana nyoyo lakini hawafahamu kwa nyoyo hizo, wana macho lakini hawaoni kwa macho hayo, wana masikio lakini hawasikii kwa masikio hayo, hao ni sawasawa na wanyama bali wao ni wapotevu zaidi kuliko wanyama kwa sababu hao ni wenye kughafilika.” Hadithi ya Mtume (SAW) ikasema; “mapambano yaliyo bora zaidi ni neno la haki mbele ya mtawala jeuri.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mtawala ana ngazi, tunaweza kumzungumzia Rais, mkuu wa utawala wa muhimili mmoja naweza kuwa Spika na wasaidizi wake muhimili mwingine, anaweza kuwa Jaji Mkuu na wengine wanaomsaidia. Lakini pia kwenye ngazi za Mawaziri na wote ambao kwa pamoja wanatengeneza utawala. Katika wazungumzaji mmoja jana alisema; “Aah! nina wasiwasi kama vile hatuelewi tunachotakiwa kufanya kwa sababu kila anyesimama analalamika,” hatulalamiki, ndiyo tunachangia! Na ile inakuja kwa sababu ya hali halisi. Tulisema mwaka huu huu tukipitisha, tukijadili bajeti kwamba jamani mbona hapaoneshi kwamba kuna integrated system ya haya tunayo yajadili? Wa viwanda akisimama anaruka ruka, anachachatika, hatuoni viwanda! Akisimama wa Miundombinu na Maji utadhani maji yatatoka kesho kwenye mfereji wanasema jamaa zangu, hakuna kitu! Akisimama wa usafiri ATC imefufuliwa, Bombardier zimenunuliwa, ziko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa Mafia siku chache kabla ya kuanza vikao vya Kamati nikawapigia simu watoto wangu nyumbani hebu harakisheni ATC mkanifanyie booking ndege ya Dodoma. Wakaniambia mama hazijaanza kwenda! Aaah! Mimi nilidhani ndiyo ingekuwa kituo cha mwanzo hapa! Wateja tupo wengi wa uhakika, haipo. Lakini hii Mpango unasema tena kufufua ATC watu wanapiga makofi, watu wanashangilia, jamani hebu tuone kwa nyoyo zetu kwa sababu ni hizi nyoyo ndiyo zilisimama pale zikaapa. Kila mmoja wetu na katika kiapo kile tunaweka ahadi na huyo mwenye mamlaka zaidi na pia ndiyo tunakubali kwamba hayo mamlaka yapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kupitia kwako hebu tuzingatie ile sala tunayoomba hapa kila asubuhi, lakini pia kupitia kwako hebu jengeni mazingira ya kuwa tunamkumbuka Mwenyezi Mungu kila wakati, labda itatujengea hofu na kusema kweli tuna dhima kubwa hapa ndani ya jengo hili, isiwe ushabiki tu! Tunasema jamani haya mambo yako so broad! Yaani ni mapana kiasi kwamba inasikitisha hata kusoma, alisema msemaji hapa kwamba huu ni mwaka wa pili na ni mwaka mmoja, kulikuwa na mwaka kabla yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, laiti tungepata assessment ya mwaka ule japo miezi michache tu ile ndiyo ikawa msingi sasa wa kufanya huu mwaka huu, humu background information nadhani kuna majedwali mengi hapa ukurasa wa 18 mpaka 24; hivi unapozungumzia mpango wa mwaka mmoja tu mwaka wenyewe ni 2017/2018 unapotoa data za mwaka 2013 ambazo wala hazisaidi hata ule Mpango wenyewe wa miaka mitano ambao mkubwa ndiyo ukatolewa huu mdogo. Sasa nikasema huu ni mpango wa mwaka huu au ni nini na tatizo ni nini? Ndiyo hiyo copy and paste au ni kwamba taarifa tu ilimradi buku lijae iletwe? (Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, nadhani hatutendei haki, tuletewe mpango ambao ni mahsusi na niliposema hapa kikao kilichopita kwamba mbona hamna kile wanachoitwa wataalam measurable targets yaani tukiangalia hapa tunasema hapa tumesema mwaka huu tutatoka point moja twende point mbili. Niliguswa zaidi wakati ule na suala la afya na nikasema mahsusi suala la vifo vya akina mama linalotokana na uzazi, wakati ule kulitokewa na figure pale, sijui 400, kati ya watu 100,000, nikawauliza jamani sasa kwa mwaka huo mmoja mmepanga kitu gani hapa? Mbona ni namba tu ambayo haina mwelekeo wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aliposimama mjibu hoja, akasema jamani kweli hamna humo tena kwa ile sauti yake kama vile kaonewa au mtu anasema uongo, sasa mara hii ndio limekuja broad kabisa, katika ukurasa 54 mpaka 55 kipengele 6.4.2 afya na ustawi wa jamii wanasema kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi basi mara hii hata namba hamna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifo vyenyewe peke yake viko aina chugu nzima hivyo vifo vya uzazi viko aina chungu nzima, kwa mwaka huu ni vifo gani mnavitarajia kuvifanyia kazi, na kutoka vingapi mpaka vingapi huu mwaka mmoja tu, mbona haya mambo yanakuwa hivi jamani halafu mnasema tunapanga na kuna wanaosema maneno wanasema if you fail to plan, you plan to fail. Tukishindwa kupanga ina maana tunapanga kufeli au kushindwa, hivi kweli Taifa hili tunakaa watu mamia humo tumeacha mambo mengine yote kuja kujadili hili, jamani hebu tuitendee haki nchi hii, hebu tuwatendee haki wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu haukubali kwamba hali ya uchumi umeshuka jamani kwa ukweli wa dhati ya mioyo yenu hivi kweli Watanzania wangapi sasa hivi wana purchasing power ambayo inafanana kidogo tu na ile ya mwaka jana, yaani ule uwezo tu wa kumiliki yeye maisha yake mwenyewe kwa kile kipato anachokipata kuanzia mama ntilie mpaka maprofesa wa chuo kikuu, ni wangapi kweli purchasing power yao ni kweli inawawezesha hawa kuishi maisha ya kuaminika au maisha angalau kidogo yanampa mtu ahueni, akasema nina mshahara, nina kazi, nina kibarua, nina kipato cha kuaminika. Tunafanya uigizaji sekta isiyo rasmi kila mtu ajiajiri, sekta isiyo rasmi inajengwa na sekta iliyo rasmi. Viwanda vinaeleweka, wafanyakazi idadi fulani inaeleweka, mshahara wao unaeleweka kwa hiyo tunajua kiasi fulani cha pesa kitaingia kwenye mzunguko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuweki mambo tu hivi hivi, na ndio maana hata huu mpango wenyewe wote ukasimama wanasema wasemaji matofali ya barafu ambayo wala hayajengi nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa mambo yanayotajwa kwamba ni msingi ambao mpango huu umesimamia ni amani, usalama, utulivu ndani ya nchi kweli. Nchi hii ina amani? Wataalam wa amani wanasema peace is not the absence of war yaani kukosekana vita sio kwamba mna amani, lazima kuwepo na mifumo mizuri ya kijamii ambayo ina mhakikishia kila mtu haki yake inampa utulivu, inamhakikishia maisha yake ya kila siku, nani nchi hii leo hii, Mbunge hana uhakika kama nikitoka hapa Dodoma nitafika Dar es Salaam bila kukamatwa na askari, nitadaiwa pesa isiyokuwa na mbele wala nyuma.
MWENYEKITI: Ahsante.