Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kutuzawadia uhai na kwa huruma yake tuko salama na tuko ndani ya Bunge hili kwa sababu ya kujadili Mpango wa Maendeleo wa Serikali 2016/2017 na 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, nataka nichukue fursa hii ndugu zangu kwa unyenyekevu mkubwa sana kutoa pole kwa wananchi wenzangu watatu watafiti kutoka Chuo cha Seliani waliouawa katika Kijiji cha Iringa-Mvumi, katika Wilaya ya Chamwino, nawapa pole sana familia. Vilevile nitoe pole sana kwa wananchi kadhaa wa Kijiji cha Mvumi Mission pamoja na Kata ya Manda na Kijiji chenyewe cha Iringa-Mvumi kwa familia ya Tatu ambaye naye pia aliuawa wiki moja kabla ya wale watafiti kukumbwa na kadhia hiyo. Naomba Mungu azipumzishe roho za marehemu wote mahali pema peponi, lakini niitake Serikali kuchukua hatua madhubuti kuwatafuta watu waliokimbia ambao kwa kweli kwa kiasi kikubwa wanatajwa kuhusika na mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, nina mambo machache ya kuzungumza. Jambo la kwanza, naomba niipongeze sana Serikali kwa kazi nzuri. Ndugu zangu nataka nirudie tena maneno ambayo nimekuwa nikiyasema mara nyingi kwamba katika kazi rahisi duniani, hakuna kazi rahisi kuliko kupinga, kupinga jambo lolote ni kufanya kazi rahisi sana. Maana mtu anajenga nyumba kwa gharama kubwa wewe unatumia dakika mbili tu kumwambia nyumba yako mbovu. Kwa hiyo, unaweza kuona namna ambavyo kupinga ni kazi rahisi sana na inayoweza kufanywa na mtu yeyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango, maneno mengi mazuri ameyaandika katika kitabu chake, mojawapo ni kukua kwa uchumi ambapo sasa hivi umekua kwa 5.7% na unategemewa kukua kwa 5.9%. Tatizo tulilo nalo Dkt. Mpango ni namna gani tunahusianisha kati ya ukuaji wa uchumi kwenye vitabu na hali halisi kwa wananchi wenyewe. Hapa ndiyo inatakiwa sasa mtusaidie ku-link kwa sababu tunavyoelewa ni kwamba uchumi unapokua ni lazima uguse baadhi ya wananchi au pengine wananchi wengi zaidi hasa wanaoishi maeneo ya vijijini. Huko bado tuna matatizo makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia viwanda vidogo vidogo, nashauri Serikali tujikite zaidi kwenye viwanda ambavyo vitainua kilimo. Tujikite kwenye viwanda vya mazao yanayolimwa na wananchi. Kwa mfano, kwa Mkoa wa Dodoma ukianzisha kiwanda kwa ajili ya kuinua zao la zabibu utakuwa umetusaidia zaidi kuliko tukiwa tunazungumza ukuaji wa uchumi wa point za kwenye karatasi ambao hauakisi wananchi wenyewe wanainukaje kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niyaseme haya maana imeonekana kwamba Wabunge wa CCM tuna uoga wa kumshauri Rais, lakini leo nataka nitamke kwenye Bunge hili, Rais anafanya kazi nzuri sana na aendelee kuifanya. Bahati nzuri tumekuwa na Rais kama Mbunge mwenzetu kwa miaka 20, anatujua Wabunge, anaijua nchi, anajua namna ambavyo tuna tabia za kuzusha, hawezi kubabaishwa na maneno yanayotoka humu. Katika nchi yetu kwa miaka mingi sana tumekuwa na malalamiko kwamba Serikali yetu inalindana, mtu anaharibu hapa anahamishiwa hapa, mtu anaharibu hapa anapelekwa hapa, tunataka mabadiliko, amekuja Rais wa mabadiliko, ukiharibu unakwenda kupumzika nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu nataka niwaambie wala hakuna mtu anayetisha wala hakuna mtu anayeshindwa kumshauri. Ila nataka niwapongeze sana, mimi mara chache sana huwa nawapongeza Wabunge wa Upinzani lakini safari hii nataka niwapongeze, nawapongeza kwa sababu wamejitoa mhanga. Wanaposimama kusema Serikali imefilisika msifikiri wanaisema Serikali, hapana, wana sehemu wanayolenga kwa sababu ili ujue kwamba huyu mtu amefilisika kuna vielelezo. Cha kwanza, lazima ashindwe kulipa madeni, mtu akishindwa kulipa madeni ujue amefilisika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wabunge wa Upinzani acheni uoga, badala ya kusema Serikali imefilisika, Serikali inayolipa mishahara, Serikali inayowalipa nyie, Serikali inayosomesha watoto bure, tamkeni wazi kwamba Mbowe umefilisika maana umeshindwa kulipa madeni. Tamkeni wazi, hakuna sababu ya kuzungukazunguka unapiga kona ooh mimi nitakamatwa, sasa unatuambia sisi tuje tukuwekee dhamana, ukikamatwa ni kwa makosa yako. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais ameteua Wakuu wa Mikoa wengi wazuri, lakini wachache nitawataja hapa, wa kwanza Mrisho Gambo, nampongeza sana. Wa pili Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rugimbana Jordan nampongeza sana. Wa tatu, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, nampongeza sana Mongella anafanya kazi nzuri. Rais anawajua watu wake, anapowapanga anajua kabisa nani anaweza kufanya kazi wapi. Big up sana Dkt. Magufuli, endelea kufanya kazi ukiamini kwamba nyuma yako wako watu wanaokuombea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie msamiati mgumu sana. Ni bora mtu ufe mawazo yako yabaki hai kuliko mtu uwe hai halafu mawazo yako yawe yamekufa, ujue wewe umepotea kabisa. Hatuwezi kuogopa kuchukua hatua. Leo hii tunasimama ndani ya Bunge hili tunasema utumishi ni uti wa mgongo, kwenye utumishi haitakiwi kuingiza siasa inakuwaje mtu aliyefikia level ya kuwa mtu mkubwa mpaka Katibu Mkuu leo Mbunge wa CHADEMA, alianza lini? Lazima alianza akiwa huko huko katika Utumishi, ndiyo maana lazima tufukue kila sehemu kuangalia tunao watumishi au tunao watu wanaopiga porojo za siasa badala ya kufanya kazi, lazima tusimamie nidhamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna mtu anafikiria kwamba eti tutakuwa na Taifa ambalo halina mabadiliko, haiwezekani! Tumeyaomba sana mabadiliko, tumelala tunasisitiza kwamba tunataka mtu atakayekuja kubadilisha. Kama kuna mfanyakazi anaenda kazini akiwa hana hakika kwamba ajira yake ipo, sawasawa, yeye akachape kazi. Kazi peke yake ndiyo itasababisha ajira yako iendelee kuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusidanganyane hapa. Tunasimama hapa na kuanza kusema ooh kwenye kikao cha chama cha Wabunge wa CCM wamepewa hela, aaah, wamepewa hela na nani? Mbona ninyi mnachangishwa kila siku hapa? Wabunge wanachangishwa kila siku milioni moja moja, wengine wanakuja wanalia wanasema Lusinde angalia meseji hii tunatakiwa tutoe milioni moja moja kwa ajili ya kesi, mbona sisi hatuyasemi yenu? Sisi tupewe pesa na nani? Wabunge wote tulipewa fursa ya kwenda kukopa, kila Mbunge kakopa, wengine wamekopa 200, wengine 300, leo hii uje upewe milioni 10 ili iweje, ni kutudhalilisha tu.
Msichukue fursa hiyo kutudhalilisha, Wabunge wa nchi hii wote wa Upinzani, wa CCM tulipewa fursa, tumekopa hela nyingi, hakuna Mbunge wa kuhongwa milioni 10 wala wa kupewa milioni moja. Ndiyo maana nyie mnachukua hela zenu kukichangia chama chenu, hakuna mtu anayewazungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sana wakati huu ambapo tunazungumzia mpango, baada ya kuwa nimeshawapa dawa kidogo, ni vyema tukajikita kwenye sekta binafsi. Serikali imeambiwa uti wa mgongo ni sekta binafsi. Rais amekwenda kufungua kiwanda kuna watu wanapiga kelele tena, mnaenda kwa Bakhresa, katika sekta binafsi kuna mtu mjasiriamali jamani katika nchi hii anayemfikia Bakhresa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bakhresa akimuita au akimuomba Rais kwenda kufungua kiwanda chake, uharamu wake uko wapi? Au Bakhresa kuacha kuwachangia wapinzani ndiyo imekuwa nongwa? Maana nashangaa unaanza kumlaumu eti kwa nini Rais kaenda kufungua kiwanda cha Bakhresa kampa na ardhi, kuna vivutio vya kuwafanya wawekezaji wa ndani nao waweze kuwekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri Mpango kelele anazozisikia uchumi wa ndani una booster yake. Booster yake ni kuwalipa wadeni wa ndani, ukiweza kuwalipa wadeni wa ndani hela itaonekana mtaani na hizo kelele zitapungua. Mnapokumbuka madeni ya nje ni sawa, lakini kumbukeni na madeni ya ndani. Kuna wazabuni mbalimbali waliofanya kazi kwenye Serikali, hawa wakipata pesa mzunguko wa pesa ndani ya nchi nao utaonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawashauri Serikali muangalie pande zote. Mnaposomesha bure tunaona, mnaponunua ndege tunaona, tunajua yatasemwa mengi lakini endeleeni kufanya kazi kwa sababu hata Mungu angeleta majadiliano na wananchi hicho kikao kisingekwisha. Ndiyo maana ukaona akakaa mbali akaamrisha kama ni mvua, mvua, kama jua, jua. Mwambie Rais tunamuunga mkono, kazi anayofanya ni njema, tumepata Rais wa kunyooka, akinyooka na jambo linaenda kama alivyopanga na ndicho tunachokitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanalalamika hapa ooh Rais anafanya kazi yeye mwenyewe. Halafu mimi nashangaa hawa jamaa wanasema halafu wanajijibu wenyewe. Wananikumbusha Sauli kwenye Biblia alipokutana na kibano cha Mungu Sauli alisema, ni nani wewe Bwana? Yaani aliuliza swali halafu akajibu kwamba huyu ni Bwana, ndiyo hawa! Huku unasema Rais anafanya kazi zote, huku tena unabadilika unasema Rais anawatisha watumishi. Mtu anayewafanyia kazi zote atawatishaje sasa wakati kazi zote anafanya yeye mwenyewe. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Rais ananyooshe hii nchi na tuna uhakika Magufuli nchi hii atainyoosha kutoka pale ilipokuwa imeishia kwenda mbele zaidi. Nawaambia moja ya vitu ambavyo nataka Watanzania watusaidie 2020 nchi zetu za ulimwengu wa tatu hizi kuwahi kila kitu nalo ni tatizo, hata kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi tuliwahi ndiyo maana mnaona hoja zenyewe…..
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Nimalize? Sasa unaingiaje Bungeni kujadili kaptura ya Mfalme wa Morocco hiyo ina uhusiano gani na matatizo ya wananchi? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.