Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ludewa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nijaribu kujadili mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa. Moja kwa moja nijikite juu ya suala la Liganga na Mchuchuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Liganga na Mchuchuma ni suala ambalo hata tafiti zake zimefanyika toka mwaka 1929. Serikali imekuwa ikilizungumzia suala hili kwa miaka chungu nzima, lakini tulijaribu kupata faraja hasa sisi watu wa Ludewa pale tulipoambiwa kwamba miradi hii inaanza. Ikumbukwe katika Bunge lako Tukufu niliuliza swali tarehe 19/4 juu ya fidia kwa wale ambao wamepisha hii miradi kufanyika. Tulijibiwa kwamba Juni ndugu zetu wale wa Ludewa wangeweza kulipwa fidia yao na vilevile Bunge liliambiwa mradi ule ungeweza kuanza Machi, 2017. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Ludewa waliaminishwa na sasa wanapiga kelele sana juu ya hili. Nipende tu kutoa taarifa katika Bunge lako kwamba hawa watu wanajiandaa kuja Dodoma kujua hatma yao. Vinginevyo waruhusiwe yale maeneo waliyopisha kwa sababu ni maeneo ya kilimo na ndiyo wanayoyategemea waendelee na kilimo chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mpango Mheshimiwa Waziri anazungumzia sana hili suala la Liganga na Mchuchuma, lakini jinsi ninavyoiona ni kwamba, hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa. Mpango unazungumza hapa kwamba mradi wa umeme wa megawatt 600 unaendelea, sasa najiuliza unaendelea wapi? Mimi sijaona kitu chochote kinachoendelea pale Mchuchuma. Hakuna kitu kama hicho! Labda Mheshimiwa Waziri aje atueleze na alithibitishie Taifa kwamba nini kinachoendelea kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeelezwa juu ya Power Purchase Agreement ndiyo inayosumbua, lakini mpaka sasa hatujui fate yake na mradi utaanza lini? Je, coordination ipoje kati ya Wizara na Wizara na kati ya Waziri na Waziri? Huyu anasema fidia italipwa Juni, sasa hivi tokea Juni ni miezi minne imeshapita hakuna fidia na wala hakuna tamko la Serikali linalosema kitu chochote juu ya fidia hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnapotuaminisha kwenye Bunge sisi tunaenda kuwaambia wananchi Serikali imesema moja, mbili, tatu, nne; sasa leo hii nikienda kule mimi ndiyo ninayeonekana mwongo! Sasa suala la mimi kuonekana mwongo haiwezekani, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje na tamko ili tulichukue na kulipeleka kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nijikite kwenye miundombinu. Leo hii tunasubiri suala la standard gauge kwa reli ya kati, tunaowategemea kuja kufanya hii kazi ni Wachina. Leo hii kitu kidogo kabisa cha Liganga na Mchuchuma tunakaa tukiyumbishana kwa suala la Power Purchase Agreement. Ninachofahamu mkataba huu siyo wa jana wala sio wa juzi, lazima kuwepo na continuity, walipoishia wenzetu sisi tuendelee. Kama pana tatizo basi tujue kwamba hili ni tatizo la msingi na tupeane maelekezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tukiwafuatilia Mawaziri wetu hawana majibu na tunarushiana mpira. Ukienda kwa Waziri wa Madini anazungumza hivi, ukienda kwa Waziri wa Viwanda anazungumza hivi, ukienda kwa Waziri wa Fedha anazungumza hivi, inafika wakati tunakata tamaa juu ya suala hili. Waziri alikuja Mchuchuma Januari na alikuwa anazungumzia hili, sasa haya mazungumzo yanachukua muda gani, lazima tuwe na time frame! Ifike mahali tuseme itakapofika tarehe hii basi hii kazi iwe imekwisha, hapo tutakuwa tunaeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni juu ya miundombinu. Kule kwetu Ludewa tumepakana na nchi ya Malawi, kuna eneo la kilometa zinazokadiriwa kuwa 200, eneo hilo halina miundombinu ya barabara hata moja na hilo ni eneo la mpakani. Nakumbuka juzi juzi hapa wenzetu walikuwa wana-demand lile ziwa na pakawa na kitu kama mgogoro. Sasa najiuliza, eneo la mpakani lenye urefu wa kilometa 200 halina miundombinu ya barabara, halina mawasiliano ya simu, hakuna umeme, je, likitokea la kutokea defense yetu ipoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kulieleza Bunge lako, wananchi kule wameamua kuchukua hatua kulima barabara kwa mikono. Tumeshalima kilometa 40 kwa jembe la mikono na sururu. Sasa kutokana na umuhimu wa eneo hilo kiulinzi na kiusalama na kiutalii Mheshimiwa Waziri aliweke kwenye mpango. Ziwa letu lina matatizo makubwa. Hivi ninavyozungumza wiki iliyopita watu watatu wamefariki kwa sababu ya usafiri na huwa linachafuka halitoi taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kuchukua fursa hii kuomba Serikali iwasaidie wale watu ambao wameamua bila kulipwa kulima barabara kwa kutumia mikono yao. Eneo la Ziwa Nyasa, eneo kubwa ni eneo la Ludewa kuliko Kyela, Mbinga na Nyasa. Kwa hiyo ni lazima hawa watu tuwape kipaumbele. Tuna vijiji vinavyokadiriwa 20 hakuna mawasiliano ya simu kabisa yaani ukishazama huko umeshazama, taarifa zako huwezi kuzipata. Kwa hiyo, ifike kipindi watu hawa tuwaonee huruma na Serikali itu-support kwenye hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la elimu, mpaka sasa Ludewa ina deficit ya Walimu 521 lakini tunapangiwa Walimu 40. Tumejaribu kulipeleka kwenye Idara na Wizara husika watusaidie. Sasa Mheshimiwa Mpango aliweke kwenye mpango wake kwamba Ludewa tuna uhaba wa Walimu na hata ukiangalia performance imeshuka sana kwa sababu hiyo. Kuna shule kama nane (8) hivi zina Walimu wawili au watatu, maximum ni Walimu wanne na tuna shule za misingi 108. Kwa hiyo, hivi vitu ni lazima tuviweke kwenye mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la afya, kweli Ilani ya Chama cha Mapinduzi inazungumzia vituo vya afya kila kata na pia inazungumzia zahanati kila kijiji. Labda tuzungumze sasa hapa wajibu wetu sisi kama Wabunge ni nini? Wabunge ni wahamasishaji wa maendeleo na vilevile tuna wajibu wa kukusanya nguvu na ku-mobilize watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.