Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujaalia sote nafasi na tukaweza kukusanyika katika Bunge hili Tukufu na kuweza kutoa michango yetu katika hoja iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili naomba niwashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu mizuri ambayo mmetupatia sisi Wizara ya Fedha na Serikali yetu ya Awamu ya Tano. Ni imani yangu kubwa kwamba, tumeyasikia mengi mliyoyasema na tutayafanyia kazi, na ninaamini tutakapokuja na mpango kamili mpango huo utakuwa ni mpango mahiri na bajeti yetu itakuwa ni bajeti ionayoonesha michango yenu yote Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nichukue fursa hii niweze kuchangia hoja chache sana kulingana na muda wetu tulionao ili tuweze kuahirisha Bunge muda utakapofika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja moja ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wameisema ambayo ningependa kuichambua katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ilikuwa ni kwamba mpango wetu umesahau mambo ya msingi ikiwa ni pamoja na mambo ya kuinua kilimo, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini Waheshimiwa Wabunge wanakazi nyingi wana mambo mengi, lakini mpango wetu umeeleza vizuri sana kuhusu sekta hii ya kilimo, mifugo na uvuvi. Tukienda katika ukurasa wa 56 mpaka 59 umeongelea vizuri sana katika sekta hii ambayo na sisi tunaamini bila kilimo hakuna viwanda Tanzania, bila kilimo Mheshimiwa Mwijage hawezi kugawa viwanda kama alivyofanya hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunathamini sana naomba tusome ndani ya kurasa hizo section ya 6.5 na vipengele vyake, 6.51, 6.52 pamoja na 6.53, vyote hivyo vimeelezwa pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hii ya kilimo.
Kwa hiyo naomba tusome pale, na bado tunaendelea kuandaa mpango wetu mtakapokuwa mmesoma kama bado mnahoja tunaomba muendelee kutuletea hoja zetu ili tuweze kuandika mpango wetu vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili au hoja ya pili ambayo ningependa kuitolea maelezo kwa ufupi ilikuwa ni kwamba maisha ya wananchi yanakuwa duni wakati mapato yanaongezeka.
Waheshimiwa Wabunge, naomba niseme kwamba Serikali inakubaliana na hoja hii na hasa iliwasilishwa na Mheshimiwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha tunakubaliana naye kwamba mapato yanakuwa, lakini si kwamba hali ni duni kwa wananchi kule, hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuimarika kwa hali ya maisha ya wananchi naomba tufahamu jambo moja, haitegemei mapato peke yake, bali hutegemea pia kuimarika kwa huduma za jamii ambazo Serikali yetu ya Awamu ya Tano imekuwa ikizipigania na tukiendelea kutekeleza na ambacho ni kipaumbele chetu kikubwa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rai ya Serikali yetu kuwa pamoja na jitihada tunazozichukua kama Serikali tunaomba pia wananchi watumie muda wao mwingi katika shughuli za kiuchumi kwa ajili ya kuboresha maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna maendeleo yanayokuja wala hakuna mabadiliko yanayokuja kwa kuletewa lazima sisi wenyewe tukubali na sisi kama wawakilishi wa wananchi hawa Waheshimiwa Wabunge tuweze kuwaelekeza wananchi wetu nini cha kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimshukuru na nikampongeza ndugu yangu Mheshimiwa Riziki alipotoa aya za Mwenyezi Mungu kutoka katika Kitabu Kitukufu cha Qurani.
Mimi naomba niseme kwa kumjibu katika aya hizo hizo za kitabu cha Qurani kwamba Mwenyezi Mungu anasema hawezi kubadili chochote katika maisha yako mpaka wewe mwenyewe uamue kubadili mwenyewe maisha yako.
Kwa hiyo, hilo ni jambo la msingi sana hatuwezi kuendelea kulaumu Serikali, kulaumu Waheshimiwa Mawaziri, sisi wenyewe tumefanya nini katika kujiletea maendelea ni jambo la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ningependa kuitolea ufafanuzi ambayo imesemwa kwa nguvu sana, na namshukuru Mheshimiwa Profesa Mbarawa ameweza kueleza nayo ni kuporomoka kwa mizigo ndani ya bandari yetu ya Dar es Salaam. Kwa upande wa Wizara ya Fedha ziliongelewa hoja tatu; ya kwanza ilikuwa ni single customs territory, ya pili ni VAT kwenye transit goods na ya tatu ilikuwa ni wingi wa check points.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge watutendee haki, wamtendee haki Mheshimiwa Rais wetu. Alipoingia tu madarakani aliondoa check points zote na zimebaki chache sana. Kwa hiyo, katika check points hizi tumtendee haki Mheshimiwa Rais, mtutendee haki na sisi tunaomsaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi tumekuwa tukiyafanyia kazi na haya machache yaliyobaki ikiwemo single customs territory pamoja na VAT on transit goods tunafahamu faida zake. Kutoka katika ethical point of view siamini sana kama wewe unaweza ukafurahia nyumbani kwako uko salama na kwa jirani yako hakuko salama, haiwezekani. Naamini ilikuwa ni lengo jema la Waheshimiwa Rais wawili, Rais wetu mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo walipokaa na wakajadili pamoja changamoto hizi na tukaja na hii single customs territory.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kuwa imepigiwa kelele kwa muda mrefu na sisi kama Wizara ya Fedha hatujakaa kimya tayari timu yetu ya utafiti ipo kazini tutakapokamilisha kuifanya tafiti hii tutawaletea hapa na kwa pamoja kwa sababu tuliipitisha hapa Bungeni tutaleta ili tuoni ni nini cha kufanya. Serikali ni sikivu imesikia na tutalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nisemee suala moja, naona kengele imegonga, nayo ni kuhusu TRA kwamba, kwa sasa inakusanya madeni na arrears na siyo kwamba hatukusanyi kodi tunayoistahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo moja, katika hili pia niwaombe Waheshimiwa Wabunge, tunasema no research, no right to speak, kama huna utafiti usiliongelee jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa ambazo zipo na sisi tunazo kwa sababu ndiyo watendaji katika Wizara hii, tunafahamu kabisa ukusanyaji wa kodi ni suala endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha robo ya kwanza Julai hadi Septemba 2016 TRA wamekusanya shilingi bilioni 3,463.8 katika hizi ni shilingi bilioni 90 tu ambazo ni arrears. Sasa mtutendee haki mnapokuwa mnaleta hoja zenu hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka shilingi bilioni 3,000 tuna shilingi bilioni 90 tu ambazo ni arrears na arrears ni kawaida katika maisha yetu hakuna mtu asiyedaiwa, na sisi tunawapa nafasi ya wafanya biashara wetu wanadaiwa muda umefika wa kulipa wanalipa, kwahiyo tulete tu taarifa ambazo ni sahihi tusiwadanganye wananchi wetu kule walipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa maneno machache kwamba Serikali yetu ina nia njema kabisa na Taifa letu na maendeleo ya watu wake. Mheshimiwa Rais wetu ana nia sahihi kabisa na njema na sisi wasaidizi wake tuna nia njema kabisa ya kumsaidia kuhakikisha Tanzania ya viwanda inapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejiandaa vizuri, tulichokifanya tumebadilisha tu spending ya Serikali, wanasema the government has shifted its spending pattern from non-productive activities to productive activities ndiyo maana tunapiga kelele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo tulizoea kuona watumishi wakisafiri hata sisi Waheshimiwa Wabunge tukisafiri, na pia namheshimu sana Mheshimiwa Keissy aliyekuwa akisema safari hewa hizi ndizo tulizofuta. Ukifuta hivi vitu lazima tutalalamika, lakini vitu vya msingi, vitu vya kiuchumi, vitu vya kukuza uchumi wetu tunaendelea kuvifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezoea kuona Taifa letu likiendeshwa na kodi za wafanyakazi, tumesema hapana. Taifa litaendeshwa na kodi za wafanyakazi pamoja na kodi za wafanyabiashara katika sekta binafsi. Sekta binafsi imesahaulika muda mrefu, alisema vizuri Mheshimiwa Bashe, kwamba kama yalifanyika makosa hivi sasa ni sahihi tuendelee na makosa hayo? Hatuwezi kufanya hivyo. Ndiyo kile nilichosema kutoka kwenye kitabu kitukufu lazima tuwe tayari kujibadilisha sisi kama tunataka na Mwenyezi Mungu atukubalie tunayotaka kubadilisha, hilo ni jambo la msingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika haya mabadiliko ninaamini Mheshimiwa Waziri wa Fedha ataongea kuhusu mdororo katika sekta ya mabenki. Lakini naomba niwaambie jambo moja mabenki yetu wamekuwa wavivu, benki zote ziko Dar es Salaam, benki zote ziko sehemu zile ambazo kuna taasisi za Serikali, hivi mbona benki hizi haziwafuati wananchi kule walipo? Kule ndiko pesa zilipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaambie mabenki haya, Serikali imechukua pesa yake, Serikali ilikuwa ni mteja kama wateja wengine imechukua pesa zake ili i-invest katika productive economic activities sasa kwa nini tunalalamika? Mdororo uliopo ni ule mabenki yetu yalikuwa mavivu kwamba tunamkopesha mteja wetu hatujui anaenda kufanyia nini pesa tunayomkopesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajidanganya pesa za Serikali ndani ya benki zetu, Serikali imechukua kama mteja mmojawapo. Wateja wale kwa kuwa walikuwa hawafuatiliwi na sasa hawalipi ndiyo maana tunaona Waheshimiwa wabunge mnasema CRDB ime-register hasara, ni kwa sababu sasa zile pesa walizozoea kutumia zimekwenda kwa mwenyewe na zile ambazo wamekopesha hawana uwezo wa kuzikusanya. Hilo ni jambo la msingi tuseme ukweli, tujitendee haki kama wananchi, tujitendee haki kama Watanzaini na tutaifikisha Tanzania hii salama ndani ya nchi hii na uchumi wa kati tutafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.