Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Konde
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nianze kwa kusema kwamba, wakati tuna msiba mkubwa uliolipata Taifa kwa kuondokewa na kipenzi chetu, nasikitika kwamba tunaletewa tena msiba mwingine ambao ni mkataba usiofaa hata kuujadili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili jambo leo nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu, nimesimama hapa kama mzalendo wa Tanzania. Katika mambo ya kinchi, katika mambo ambayo yataleta tija au hasara kwa nchi hii, na mimi nakubaliana, lazima tuwe wamoja. Naupongeza sana uongozi wa juu wa chama changu kwa kuliona hili na kutuletea mawazo ambayo siyo lazima, lakini kutuelekeza katika njia ya kwenda katika mjadala huu ambao ni hasara kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimejaribu kutafuta nondo zangu hapa, kila nilivyoangalia sizioni, lakini nina wasiwasi ndugu yangu Mheshimiwa Zitto Kabwe kazichukua. Kwa sababu yale niliyopanga kuyasema hasa, ndiyo yale ambayo ameyawakilisha. Hongera sana Mheshimiwa Zitto Kabwe. Ametupa somo na funzo zuri ambalo tunafika mahali kama Taifa lazima tukubaliane katika mambo ya msingi kama hili ambalo tunalo sasa hivi mbele ya meza yetu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, binafsi kuna kipengele katika mkataba huu kinachosema kwamba tutakaposaini mkataba huu hatutakuwa tena na uwezo kama nchi kuwa na ushirikiano na nchi nyingine, hii ni aibu! Hii ni aibu kwa sababu Tanzania ni Taifa huru. Hautakuja mkataba wowote ambao utatuzuia kuwa na ushirikiano wa kibiashara, ya kiuchumi au ya kisiasa na nchi nyingine, mkataba huo ukawa na una manufaa kwa nchi hii, haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna kifungu kingine kinasema kwamba tukishaingia katika mkataba huu, suala la kupandisha kodi kwa bidhaa itakuwa halina tena nafasi.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu hii kila mwaka unaona kodi zetu ni hizo za sigara, bia, vilevi na kadhalika. Hizo ndiyo kodi; revenue kubwa inatokana na hayo. Leo tukisaini mkataba huu, hayo mambo yatakuwa hayapo. Kuingiliwa uhuru wa nchi yetu kwa namna yoyote ni janga ambalo mzalendo wa ukweli haifai kulishabikia.
Mheshimiwa Spika, isionekane kwamba wapinzani ni watu wa kukataa kila kitu. Niwahakikishie, likija jambo lenye maslahi tutakuwa pamoja na hatutaangalia chama, lakini niwatahadharishe wenzangu, hasa upande huo, likija jambo la ovyo ovyo kama vile ulivyokuwa Muswada wa Habari, tutaukataa mpaka mwisho wa kiama. Tuambiane ukweli, mkileta lenye manufaa ni kama mnavyotuona, lakini mkija na mambo ya ovyo hatutakuwa pamoja, lazima muone mawazo yetu na muelewe kwamba sisi tupo kwa ajili ya Tanzania yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina mashaka sana. Jamhuri ya Kenya ni watu ambao wakati mwingine sijui wanatuona sisi Watanzania tukoje. Wamekuwa ni watu wa ku-beep, beep tu. Hii Afrika Mashariki haikuja kwa lengo la kunufaisha nchi moja katika Afrika Mashariki na nchi nyingine ziwe mashahidi, haiwezekani. Leo wenzetu Kenya kwa sababu katika mauzo ya nje wana karibu asilimia 90 na kitu, kwa hiyo, wao ni haraka sana kusaini katika hili; na wamekimbilia sana katika hilo, lakini hawatuangalii sisi. Nao ni miongoni mwa zile nchi zilizojifanya wako tayari katika kila jambo. Kwa hiyo, kama hili wako tayari, watakwenda peke yao, sisi bado. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Spika; Mheshimiwa Spika, umekuwa mtoro sana siku hizi mpaka tunakusahau. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, Kenya hao hao tuliokaa nao katika makubaliano ya single custom territory, ndio hao wametuacha kwenye junction. Sisi tumekwenda, wao wamechomoa. VAT on transit goods, hao hao Wakenya tulikubaliana, wakati wa kusaini, sisi tumeingia kichwa kichwa, wao wamechomoa. Mpaka lini Kenya watatuona sisi ni watu ambao ni kama wa kututumia rubber stamp ya kuendeleza mambo yao na sisi kutuacha nyuma. Haiwezekani, lazima tujiangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii inatupa funzo moja kubwa sana. Waheshimiwa, Serikali hii ya CCM hebu sasa fikirieni, dira na sera zetu za kiuchumi zinatuelekeza vipi? Haya ndiyo matatizo makubwa tunayoyapata; kuna mjuvi wa maneno mmoja au mjuaji wa kusema mmoja, alisema kwamba nahodha bora ni yule anayejua bahari anayokwenda. Kwa nahodha asiyejua bahari anayokwenda, hakuna upepo utakaokuwa muafaka katika safari yake, hakuna. Kwamba nahodha ni yule anayejua nchi yangu hii Tanzania, Serikali yetu; sera zetu za kiuchumi zinapelekea sasa wenzetu kuweka mikataba hii na kutuletea kuona kwamba sisi kwa sababu ya dhiki zetu, kwa sababu ya njaa zetu, wao watuletee lolote na tutakubali.
Mheshimiwa Spika, sasa tunasema kwamba ni afadhali tufe na dhiki zetu kuliko kukubali mikataba ya ovyo ovyo kama hii. Hatutakuwa tayari kufungiwa ngulai na kwa sababu eti ni nchi maskini tuendelee kukubali. Sasa umaskini huu ni lazima tuwaulize watawala wa miaka 50 mlioitawala nchi hii, kwa nini nchi yetu inaendelea kuwa maskini wakati sera nzuri na mambo mazuri mnayataja kwenye mikutano, lakini kwenye utekelezaji tunakuwa zero? Why? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lazima sasa mtimize wajibu wenu. Nakiomba sana chama kizee cha CCM, wengine wanaposema chama kizee wanaona kama ni kejeli; uzee ni busara.
Mimi ninapokiita chama kizee, naamini kuna busara. Niliwaambia bahati nzuri sana Bunge hili asilimia karibu 60 ni vijana na wengi ni ninyi, tusifike mahali tukaona wale wazee waliokuwemo kwenye Bunge hili ni bora kuliko vijana ninyi mlio na mawazo ya kizee kupita kiasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.