Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru sana Mungu kwa kutupa nafasi nzuri kabisa ya kujadili juu ya huu Mkataba wa EPA. Vilevile sina budi nichukue fursa hii katika Bunge hili kumpongeza sana Profesa Kabudi kwa namna alivyotufumbua macho. Profesa Kabudi ni moja ya Watanzania wenye uwezo wa walichonacho kuwasaidia na wengine waweze kuelewa. Hilo ni jambo zuri sana na kwa kweli tunajivunia sana kwamba elimu yako inawafaa wengi na inaifaa nchi. Hongera sana Profesa Kabudi.
Mheshimiwa Spika, ni ngumu sana kusimama hapa kuutetea huu mkataba na ndiyo maana unaweza kuona kuna baadhi wanaojaribu wanapata shida sana. Hauna namna yoyote ya kuuzungumzia uzuri wa Mkataba huu, hata kama umeandaliwa au umejiandaa; ni jambo gumu sana. Ndiyo maana umeona hata waliojaribu kufanya hivyo, wamejikuta wao wenyewe wakipata shida sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Khatib, ameonyesha kwamba isiyo kongwe haivushi, kwamba ukongwe wa CCM ni jambo zuri na inaendelea kuvusha nchi hii. Amesema chama hiki ni kikongwe. Ukishasema kikongwe, maana yake hicho ndicho chenye uwezo wa kuvusha baadhi ya mambo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama umewasikiliza wazungumzaji wachache waliotangulia, nataka niungane nao kwamba hata kuchukua muda mwingi kuujadili mkataba huu ni kutumia tu fedha za Watanzania vibaya, huu mkataba haukustahili hata kufika huku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huu ni moja ya mikataba mibovu kabisa ambao pengine nimsaidie hata mzungumzaji aliyepita, kwa nini Kenya wamesaini? Wamesaini bila kuutafakari kwa makini. Wangetafakari kwa makini; na nikubaliane na Mhesimiwa Zitto kwamba wamesaini kwa ajili ya kufanya biashara ya maua, siyo kwa ajili ya usalama wa mkataba wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 140, hakiruhusu nchi moja kujitoa baada ya kuingia. Mimi nataka niseme, Jumuiya yetu ya East Africa, kama kuna jambo mmetuangusha ni katika jambo hili. Kwa nini msingekaa wenyewe kwanza mkaupitia huu mkataba? Secretariat ya Jumuiya ya East Africa mkakaa mkausoma kwa pamoja kabla ya kuruhusu nchi moja moja kwenda kujisainia yenyewe? Kwa hiyo, hapa tunaanza kona kuna problem kwenye Jumuiya yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lazima Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki iwe inakaa pamoja kwenye mambo ya muhimu na mazito kama haya, leo tusingeona aibu ya Kenya kutangulia kusaini kama mngekaa pamoja mkashauriana, kwamba jamani hivi unaingiaje kwenye mkataba ambao unakuchagulia rafiki? Unaingiaje kwenye mkataba ambao unakulazimisha kushirikiana na adui? Huu mkataba kadri unavyousoma, kuna sehemu unakuchagulia rafiki wa kufanya naye biashara na kuna sehemu unakulazimisha kukaribiana na mtu ambaye wakati huo humhitaji.
Mheshimiwa Spika, ukitazama kwa makini mkataba huu wa EPA, ni sawa sawa na mzee wangu pale kijijini kwenda kupelekewa zawadi ya kuku halafu akachukuliwa ng‟ombe wake kumi; kitu ambacho hakiwezi kukubalika!
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni moja ya mikataba mibovu kabisa. Nasi tunapoukataa mkataba huu na kuitaka Serikali, isiusaini, tunaukataa ili kuwaonesha Jumuiya ya Ulaya kwamba Afrika sasa inao wataalam, wanajitambua na wanaweza kufanya biashara huria na mtu yeyote. Sisi sio watu wa kupangiwa na kuletewa mikataba ya namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niishauri Serikali; kwa mkutadha huu, huu mkataba haufai kusainiwa hata kidogo kwa sababu una vipengele vingi vinavyodhalilisha Afrika.
TAARIFA...
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, namshukuru na namheshimu sana Mheshimiwa Millya, lakini ni mmoja wa watu wachache ambao wamerubuniwa na wazungu. Hawa wazungu waliokuja wamemwona Millya. Maana hapa hatutakiwi kutafuna maneno; kuna baadhi ya Wabunge wamewaona, inawezekana na Mheshimiwa Millya akawa ni mmojawapo kati ya waliowaona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama hukatazwi, unawezaje kutoa notice halafu mwaka mzima ukaendelea kubaki mle? Unabaki humo kwa sababu zipi? Khah, maana wewe mwenyewe unasoma, halafu unajijibu. Bahati nzuri wewe mwanasheria na pengine unaelewa zaidi, lakini umepata majibu kwamba ukishatoa notice, mwaka mzima unaendelea kubaki mle. Ukifanya nini kama unao uhuru wa kutoka moja kwa moja? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nirudie, hili ni jambo letu wote kama Bunge, tusianze kushindana humu. Tukubaliane kwamba mkataba huu haufai, maana ndani una vi-package vya ushoga, una vitu vya ovyo ovyo vimefichwa humo, Watanzania watatushangaa sana.
Mheshimiwa Spika, sisi hatuwezi kuburuzwa na nchi yoyote, sisi ni Taifa huru! Iwe wamasaini nchi nyingine ambazo pengine wao wanavutiwa na ushoga, sisi hatuvutiwi nao. Kwa hiyo, hatuko tayari kukubaliana na jambo hili.
TAARIFA...
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, hiyo itakuwa imetusaidia wote, lakini zaidi sana, Mheshimiwa Millya ameelewa kwamba ni ile block ndiyo inatakiwa kuomba kutoka lakini siyo nchi moja ambayo imezuiwa na mkataba huu.
Mheshimiwa Spika, tuseme tu kwa kifupi, mkataba huu haufai. East Africa wawe makini na mikataba ya namna hii, waipitie wao wenyewe kama Sekretatieti na wao na uchungu na nchi zao kabla ya kuangalia manufaa watakayopata. Kwa sababu wakati mwingine kuna hadithi moja; watu waliwahi kushangilia kwenda kufanya kazi kwa Mfalme, wakati huo huo kulikuwa kuna agizo kwamba ili ukafanye kazi kwa Mfalme, ni lazima uhasiwe kwanza ndiyo uruhusiwe kufanya kazi kwa Mfalme. Kuna watu wakashangilia, walipofika pale kukuta masharti, yakawa magumu kwao. Kwa hiyo, kila mikataba ya kimataifa inapokuja, tuwe na Sekretarieti zinazotazama kwa makini, siyo kukurupuka! Tutakuja tuingie kwenye matatizo makubwa na tuziingize kwenye shida kubwa. Tutakuja kupata adhabu ambazo hazina msingi. Maana kadri unavyousoma unakutana na sehemu inasema EU inaweza kuchukulia hatua.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unaweza kuona ambayo tunaweza tukaingia kwenye matatizo makubwa ya kuchukuliwa hatua na uhuru wa nchi zetu ukawa unatekwa bila sisi wenyewe kuelewa.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono mkataba usisainiwe.