Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana nami kupata nafasi hii ya kuchangia jambo hili.
Awali ya yote, pamoja na kuwa muda ni mchache nitumie pia fursa hii kuwapa pole wananchi wa Mafinga hasa pale Jambeki kutokana na lile janga la moto na pia janga la moto lililowakumba pale stand ya Mafinga, nawapa pole sana! Na ninawatia moyo kwamba Serikali itaendelea na jitihada za kututafutia gari la zimamoto.
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo, baadhi ya wachangiaji wamesema kwamba tunalalamika tu, tumekuwa watu wa ku-complain. Mwingine amesema tunagombana na EU, tunagombana Kenya, tunagombana na Uganda. Mimi niseme jambo moja kwanza, hatulalamiki, pili, hatugombani na yeyote isipokuwa tunalinda maslahi ya Taifa letu. Mwingine amesema kwamba tumechukua muda mrefu sana ku-negotiate jambo hili, ndiyo negotiation zilivyo za Kimataifa. Kuchukua muda mrefu wala siyo tatizo leo hii Uturuki bado inaendelea ku-negotiate na EU ili iweze kuingia. Pia kushiriki negotiation na kutosaini ni mambo ya kawaida katika masuala ya Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano, Mkataba wa Roma huu ulioleta ICC, Marekani alishiriki lakini hakusaini, kwa hiyo, siyo dhambi kutosaini, wala sisi siyo watu kwanza. Pia hata katika negotiation kwanza kuna stage ya kwanza una-negotiate, pili, unarudi je, tume-achieve katika ile negotiation? Baada ya pale ndiyo unaamua usaini au usisaini. Sasa watalaam wame-negotiate wamekaa chini wameona kwamba katika mkataba huu hatujakidhi matarajio ya yale ambao tunajarajia ku-achieve, wameshauri tusisaini. Haya ni mambo ya kawaida kabisa katika taaluma za mambo ya Kimataifa na mambo ya mikataba ya kibiashara.
Mheshimiwa Spika, pia kuna kitu kingine ambacho watu wengi wameshindwa kukitazama; kuna kitu kinaitwa EBA, kirefu cha EBA ni Everything But Arms. Sasa Everything But Arms ni nini? Kwa lugha nyepesi katika EU-EBA inasema kwamba The EU will offer quarter and duty free market access to all products originating from the LDCs with the exceptional of arms, everything but arms. Sisi ni LDCs - Less Developed Country. Maana yake ni kwamba with EU-EBA mpaka hapa tulipo tunaweza kuingiza chochote katika Soko la EU, isipokuwa silaha, lakini free of duty. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wenzetu Kenya, wao tayari wameji-pronounce kwamba ni middle income country, chochote wanachofanya kule wanachoingiza kule katika Soko la EU lazima wachajiwe ushuru usiyo pungua asilimia 10, sisi with EPA, without EPA kwa yule EU-EBA tayari tunayo hiyo haki ya kuingiza chochote kule bila ushuru. Sasa ndiyo maana tujiulize kwa nini wenzetu wamesaini? (Makofi)
Mheshimiwa Zitto amesema hapa kuhusu maua. Kenya wanauza maua yasiyopungua thamani ya dola 500,000 kwa mwaka, pia export ya Kenya katika EU pamoja na UK ambayo imejitoa kwa mwaka ni wastani wa 1.5 billion USD. Sasa kwa kuwa wanalazimika kulipa ile asilimia 10 wanalipa siyo chini ya milioni 100 kwa mwaka kama ushuru wanapoingiza zile bidhaa. Lakini ni nani anayemiliki maua, ile industry ya maua katika nchi ya Kenya? Kenya tofauti na Tanzania hapa hata mimi Mtoto wa Mama Cosata leo hii ni Mbunge, in Kenya that cannot be possible. Mtoto wa malalahoi ukaja kuwa Mbuge kama tulivyokuwa sisi humu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, industry ya maua ya Kenya wanao-dominate ni ma-giant ambayo ni ma-ruling class na ndiyo maana haraka haraka wame-ratify huu Mkataba ili kusudi uwape hiyo favour. Kwa hiyo, haya mambo ndugu zangu tunapojadili kama alivyosema Ndugu yangu Khatib maslahi ya kitaifa tuyatazame mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la pili kwa nini tunakataa kusaini? Mimi nampongeza Mheshimiwa Rais na ninaipongeza Serikali kwa kuitika wito wa kuleta jambo hili hapa na sisi tuseme lolote. Kwa nini tunakataa? Madhara yake moja, tutapoteza ushuru,ambao mpaka sasa tunatoza hizo bidhaa wanazotuletea. Tukipoteza ushuru maana yake ni nini? Kupitia ushuru huo ndiyo tunatarajia tujenge nchi yetu, tuhudumie watu wetu, tufanye elimu bure, tulipe mikopo ya wanafunzi, tujenge zahanati na kadhalika, sasa hicho tunakiondoa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, tukikubali jambo hili ita-damage jitihada zetu za kujenga uchumi wa viwanda. Kwa sababu tutakubali sasa tuwe tu ni soko.
Mwisho, tujiulize kwa nini wenzetu tunasema jambo hili lazima tusaini as block wao wamesaini, tumeshasema mfano huo wa maua Mheshimiwa Zitto amesema. Pia tuendelee kutafakari kwa kina tunapojadiliana na wenzetu ndani ya East Africa, unafiki huu mwisho wake nini na nini hatima ya East Africa Community na kwa mwenendo na trend ya unafiki wa namna hii?
Kuna watu wamekuwa na mashaka kwamba kwa kutusaini ita-damage mambo mengi, mojawapo wanasema Foreign Direct Investment (FDI) kwamba tutakosa kupata kuvutia mitaji kutoka EU, siyo kweli. Mheshimiwa Hawa Ghasia ametoa takwimu hapa katika FDI nchi ambazo zinaongoza mpaka sasa hivi kuwekeza mitaji yao hapa kwetu ni China, India, Kenya ikifuatia na nyinginezo. Katika nchi 10 ni mbili tu ndizo zinatoka EU, huu mkataba ukisaini maana yake ni kwamba una-discourage FDI kutoka kwingine. Je, tuna uhakika gani hawa watu tukisaini nao kweli wataendelea kutuletea mitaji, ambapo hadi sasa hivi ni nchi mbili tu kati ya 10 ambazo zinaleta hapa hiyo FDI? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine watu wengine wana mashaka kwamba ita-damage mahusiano yetu ya kidiplomasia, siyo kweli. Hii siyo dhambi kutosaini. Leo hii Norway haiko katika EU kwa sababu inalinda maslahi yake. Uturuki inataka kuingia kwa sababu inadhani itanufaika zaidi, Norway haitaki kuingia kwa sababu inalinda maslahi yake, hata Sweden imeingia mwaka 1995 pia kwenye ile Euro Zone kwa maana ya currency hawapo kwa sababu wanalinda maslahi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nini way forward, katika biashara yoyote kitu muhimu ni soko na ndiyo maana tumeleta Jumuiya ya Afrika Masharika, ndiyo maana tuna SADC, lakini pia ndiyo maana tunafikiria kuangalia namna gani tutaunganisha COMESA, SADC na Afrika Mashariki ili tuwe na soko kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia hata katika Afrika tunajadili sasa hivi kuwa na continental free trade area ili tupanue soko. Kwa hiyo, ushauri wangu wakati tunajadili haya naipongeza Serikali, lakini naendelea pia kushauri wakati tunakataa kusaini Mkataba huu na tuendelee kuboresha mazingira yetu ya kuwezesha kuvutia mitaji ili dhana ya kujenga uchumi wa viwanda iweze kutimia.
Mheshimiwa Spika, mwisho, ninashauri, tupende kujihabarisha Waheshimiwa Wabunge. Mkasome ile article ya Mzee Mkapa, ina some details kwa lugha nyepesi sana. Tutaweza kujifunza na kuona, lakini na kuwaelimisha watu wetu huko nje, kwa nini tumekataa kusaini, madhara yake ni nini?(Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na kuipongeza Serikali kwa kutosaini. Ahsante.