Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia mjadala ulioko mbele yako sasa. Awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, mwingi wa neema kwa kunijalia uzima na afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa pole kwa Watanzania wote, familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba uliotufika wa kuondokewa na Spika Mstaafu, Marehemu Mzee Samuel Sitta. Enzi za uhai wake aliweza kutoa mchango mkubwa wa maendeleo katika Taifa hili hivyo basi hatuna budi kumuunga mkono na kumuenzi kwa vitendo vyake vizuri. Tunamuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, Amina. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na umuhimu wa Halmashauri katika kuleta maendeleo ya Taifa hili bado kuna ubadhirifu mkubwa wa watendaji wa Halmashauri katika usimamizi na utekelezaji wa miradi na hii husababisha miradi kutokukamilika kwa wakati na mingine kuvunjika kinyume cha mikataba. Ukitazama kitabu hiki cha taarifa yetu, ukurasa wa 8 utaweza kuona baadhi ya mifano ya miradi ambayo haijakamilika au kutekelezeka. Mfano, mradi wa maji katika Kijiji cha Kayenze Jijini Mwanza wenye thamani ya shilingi milioni 618.7, mradi huu haukutekelezwa. Mradi wa maendeleo wa shule ya sekondari wa ujenzi wa bweni wenye thamani ya shilingi milioni 94.2 katika Kijiji cha Ndogosi na shilingi milioni 100.13 katika Kijiji cha Ruanda katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambao haujakamilika na mifano mingine inajionesha hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe katika Kamati ya LAAC. Katika utekelezaji wa majukumu yetu, tumebaini mambo mengi hayako sawa katika Halmashauri zetu kwani kuna ubadhirifu mkubwa wa rasilimali za umma pamoja na matumizi mabaya ya fedha ambayo yanakinzana na sheria na kanuni za fedha za Serikali za Mitaa. Hapa naishauri Serikali kuweka sheria kali na kuzisimamia kwa uwazi ili watendaji ambao wanakwenda kinyume na matarajio ya Watanzania na kinyume na dhamira safi ya Mheshimiwa Rais wetu ambaye anataka kuona nidhamu katika rasilimali za umma washughulikiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mara kwa mara tunakaa hapa tukiwajadili watendaji wabadhirifu wa mali za umma wakati sheria zipo kwani hawa watendaji wana pembe? Kwa nini wasishughulikiwe kikamilifu? Nini commitment ya Serikali juu ya jambo hili? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati mwingine Serikali inahusika kwenye udhaifu huu kwa kuwaacha watendaji wa Halmashauri kwenye kituo kimoja kwa muda mrefu. Hii humfanya mtendaji kujisahau au kufanya kazi kwa mazoea na wakati mwingine watendaji wengine kukaimu nafasi zao kwa muda mrefu. Kama wana uwezo kwa nini wasithibitishwe? Kama hawana uwezo kwa nini wasiondolewe katika nafasi hizo ili tuweze kuwabana vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumebaini Halmashauri nyingi hazizingatii Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011, aidha, kwa makusudi au kwa matakwa yao binafsi. Tulibaini baadhi ya Halmashauri zinafanya manunuzi ya bidhaa na huduma nje ya bajeti husika wakati kanuni zinazitaka kufanya manunuzi kulingana na bajeti zilizoidhinishwa. Katika Halmashauri nyingine hakukuwa na kamati za manunuzi hivyo kutokudhibiti ubora na idadi ya bidhaa kulingana na thamani ya pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tulibaini baadhi ya watendaji hutoa zabuni kwa wazabuni ambao hawana sifa wala vigezo vya kupewa zabuni hizo na kusababisha mikataba mingi kuvunjika kabla ya utekelezaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali iendelee kuwabana watendaji ambao hawazingatii kikamilifu Sheria ya Manunuzi ya Umma ambao mara nyingi wamekuwa wakiitia hasara Serikali na kusababisha upotevu wa fedha za umma. Kwa upande mwingine naiomba Serikali kupeleka pesa za miradi ya maendeleo kwa wakati kwani kwa kufanya hivyo wataweza kuondoa mianya ya kupanda gharama za miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto nilizozitaja hapa juu naongea kwa masikitiko makubwa juu ya jambo hili, Halmashauri zetu nyingi zimekuwa hazipeleki 10% kwenye Mfuko wa Wanawake na Vijana na hii imesababisha vijana kutokupata fursa za kujiajiri au kufanya miradi ya maendeleo. Fedha hizi zingekuwa zinapelekwa kwa wakati zingeweza kusaidia vijana kujiajiri au kujikwamua kiuchumi. Mbali na watendaji kushindwa kupeleka 10% kwa vijana na wanawake lakini pia wameshindwa kupeleka 20% za fedha zinazotoka Serikali Kuu kwa vijiji kana kwamba pesa hizo ni za hisani na siyo lazima. Kwa hiyo, naiomba Serikali, kwa kuwa hakuna sheria za kuwabana watendaji kupeleka kwa wakati 10% kwa vijana na wanawake na 20% kwa vijiji itunge sheria ili kuhakikisha agizo hili linatekelezwa kwa wakati na kwa mtiririko unaofaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamezungumzia mengi, kwa haya machache naomba niishie hapa. Ahsante kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.